The Chant of Savant

Thursday 5 May 2022

Uraia Pacha Tanzania Upo Barua kwa Rais Samia Suluhu Hassan

Mheshimiwa Rais, nakusalimu kwa jina la JMT na kukupa pole kwa safari ndefu ya kutoka hapa kurejea nyumbani. Ni kipindi tangu tuwasiliane. Yalitokea mauzauza nikagoma kuandika. Hayo tuyaache. Naomba niende kwenye pwenti moja kwa moja. Kumekuwa na shinikizo kwa Tanzania kuridhia uraia pacha kwa wananchi wake walio nao. Pia, kumekuwa na sintofahamu hata longolongo kuhusiana na suala hili wakati uraia wa kuzaliwa hutolewa na Mungu na si binadamu. Juzi nilikusikia ukiwa Marekani ukisema kuwa suala la uraia pacha so far halipo bali hadhi maalumu. Je wenye uraia pacha watakubali katazo hili? Kama wanaipenda sana Afrika, kwanini wasichukue uraia mwingine kwenye nchi za kiafrika zinazoruhusu uraia pacha badala ya kubembeleza kupewa kilicho chao?
        Mhe. Rais, serikali haitaki kuridhia uraia pacha ingawa inafurahia fedha walioko nje wanazotuma nchini. Ama kweli Baniani mbaya kiatu chake dawa! Na penye udhia penyeza rupia. Je kuna faida au hasara kukubali au kuukataa uraia pacha? Je kweli Tanzania hakuna uraia pacha? Kwa wanaojua ukweli, uraia pacha upo. Waulize wazanzibari nawe ukiwamo. Je wanaitwa wazanzibari badala ya watanzania kwa utaifa na uraia upi kama siyo pacha? Mzanzibari yeyote ni mzanzibari kwanza na mwisho mtanzania. Je mtanzania au tuseme mbara kashikilia utanzania na kusahau utanganyika! Nani hapa anamdanganya nani? 
    Mheshimiwa Rais, je kwanini watanzania wanachukua uraia wa mataifa mengine? Jibu ni rahisi, dhiki. Wakihitaji kusoma au kufaidi baadhi ya haki na huduma ambazo mtu asiye raia hapati, wanajilipua si kwa kupenda bali kulazimika. Je hili kosa lao au uchovu na umaskini wa Tanzania uliowalazimisha kukimbilia nje kutafuta riziki? Nani huyo mpumbavu anayekimbia nchi yake wakati mambo yake ni mazuri au anayekubali kuteseka kwenye nchi yake wakati kuna fursa nje? Yesu alipotishiwa maisha, wazazi wake waliachana na uzalendo na kuokoa uhai wake kwa kumkimbizia Misri. Mtume Mohamad (SAW) alipoona vita inazidi, aliwatuma watu wake Ethiopia.
         Mhe. Rais, ungekuwa ombaomba na ukapata fursa nje ungeshikilia ‘uzalendo’au kwenda nje kuboresha maisha yako? Je mafisadi wengi wanaojulikana nchini wana uraia pacha? Badala ya kuamua bila kuvaa viatu vya watu wenu walioamua kuchukua uraia wa nje badala ya kuhukumu kama miungu, vivaeni mjitendee na kuwatendea haki. Mna bahati wanabembeleza badala ya kuchangamkia uraia wa nchi nyingine za kiafrika zinazoruhusu uraia pacha. Nimesoma, kwa mfano, namna uraia wa Kanada unavyotolewa. Anayeomba uraia wa Kanada hana haja ya kukana uraia wake wa kuzaliwa wala kuuacha kwa sababu uraia wa kuzaliwa huondosheki. Je kwanini Tanzania tunashindwa kuliona hili wakati nchi tajiri zina uwezo wa kuwazuia maskini kuchukua uraia wao? Hapa mnaposema eti wenye uraia wa nchi nyingine wamekana uraia wa kuzaliwa, mnatumia vigezo gani? Hawakani uraia. Wanabaki na uraia wao.
            Mhe. Rais, Tanzania inaruhusu uraia pacha. Rejea namna wazanzibari, ukiwemo wewe mheshimiwa rais, mnavyojiita wazanzibari kwanza na watanzania baadaye kulingana na manufaa mnayopata toka kwenye utanzania. Inakuwaje wazanzibari mnakuwa na uraia pacha, wa Zanzibar na Tanzania na bado mnapata jeuri ya kuwaambia wengine kuwa wana uraia pacha ndani ya Tanzania huku mkisema wazi wazi kuwa uraia pacha hauruhusiwi Tanzania? Tanzania kuna chuki na wivu na upogo. Inakuwaje akina Chavda, mafisadi wa kunuka, waliweza kukimbilia India haraka walipobanwa kama wasingekuwa na uraia pacha? Kwa taarifa yako dadangu, wapo wengi nchini wenye uraia pacha na wengine wako serikalini. Fanya utafiti. Mfano mdogo ni mwaka 1994 pale RPF ilipoingia madarakani Rwanda. Wengi waliokuwa wakidhaniwa ni watanzania akiwamo mchumi maarufu Donald Kaberuka aliyekuja kuwa waziri wa fedha wa Rwanda na mkuu wa Benki ya maendeleo ya Afrika ADB, alikuwa akijulikana kama mtanzania kabla, walienda kuindeleza Rwanda baada ya kusomeshwa na Tanzania. Hapa Tanzania ilipata hasara maana Kaberuka alisomea UDSM na akaenda kuifaidisha Rwanda tofauti nasi tuliosomea nje na kutaka kuleta ujuzi wetu nyumbani na bado mnatukataa. Ili iweje?
        Mhe. Rais, najua woga ni kwamba wenye uraia pacha––––tokana na exposure yao–––wanaweza kuingia kwenye siasa na kuwafunika wanaojiita wazalendo wakati siyo. Je hili ni kosa? Mbona huku wenye uraia wa hapa wa karatasi wanaruhusiwa kuingia kwenye siasa. Mfano, kwa sasa Kanada ina mawaziri wenye asili ya India watatu ambao ni Harjit Sajjan, Navdeep Bains na Bardish Charger. Pamoja na kutoka nchi maskini kama India ikilinganishwa na Kanada, hakuna anayewazuia kuingia kwenye siasa. Huku mtu akichukua uraia wao haambiwi kuukana wake wa kuzaliwa, kwa mujibu wa waafrika waliochukua uraia wa hapa wasemavyo. Nyumbani mnaogopa nini? Marais, Barak Obama (Marekani) na Nicholaus Sarkozy (Ufaransa) wangekuwa waswahili wasingeweza kuwa marais wa mataifa yao tokana kwamba wazazi wao hawakuzaliwa kwenye nchi walizoongoza. Hata mwasisi wa Zanzibar, hayati Abeid Karume, asingekuwa rais wa Zanzibar kama ingekuwa sasa kwa vile alizaliwa Malawi na si Zanzibar ukiachia mbali aliyemfuata, Hayati Abood Jumbe Mwinyi aliyezaliwa Juba, Sudan ya Kusini. Hata hayati Kenneth Kaunda asingekuwa rais wa Zambia kama angekuwa mtanzania sasa ukiachia mbali Robert Mugabe ambaye naye, kama Kaunda, baba yake alikuwa mmalawi.
        Mheshimiwa rais, shukuru Mungu wewe ni mtanzania. Ungekuwa kwenye nchi za kiarabu–––ambazo bado zina mawazo ya kikale–––usingekuwa rais kwa sababu tu ya kijinga na kipumbavu kuwa wewe si mwanaume bali mwanamke.  
        Nasema haya kwa uchungu. Nataka niwe mkweli kwako hata kama hatujuani wala kuhusiana. Tunajiangusha kwa ukale wetu. Niandikaye, siombi fadhila. Niliomba kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam kusomea sheria sikukubaliwa. Hapa nilikubaliwa na punde nitapata shahada yangu ya uzamivu. Isitoshe, wapo watanzania mafisadi mliowasomesha na wanaibia Tanzania. Ajabu mnawakataa waliochukua na si kukana uraia wao kwa sababu walipewa na Mungu waliojisomesha au kusomeshwa na mataifa yao wakati wapo mliowasomesha wanaoliibia taifa letu lililowasomesha. Hapa bora ni nani kama tutakuwa wakweli? Hebu jikumbushe orodha ya mafisadi wanaojulikana waliowahi na wanaoendelea kulitesa taifa. Je nao wana uraia pacha?
        Mhe. Rais, mie ni kati ya waandishi na wasomi wachache wa kiafrika ambaye nimejitengeneza na kuandika vitabu zaidi ya 20 vikiwemo vya mtangulizi wako Hayati John Pombe Magufuli, Kudos to John Pombe Magufuli na kingine cha Magufulification new Concept that will Define Africa's Future and the Man who Makes Things Happen nilichoandika pamoja na rafiki, kaka na mentor, spika mstaafu mhe. Pius Msekwa. Nani ajuaye? Huenda siku moja nitaandika chako.
        Mhe. Rais, sitaki nikupotezee muda. Naomba nimalizie kwa kukushauri uangalie suala hili kwa mbali badala ya ukale. Inakuwaje majirani zetu wauridhie na kuendelea kupata faida za uraia pacha sisi tuendelee ukale ili iweje wakati kuna ushahidi kuwa kuna watanzania wenye uraia pacha ukiwamo wewe kama mzanzibari? 
Chanzo: Raia Mwema leo

No comments: