The Chant of Savant

Friday 13 May 2022

Barua ya Wazi kwa Waziri Mkuu Juu ya Ufisadi

Mhe. Waziri Mkuu, nakusalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni mara yangu ya kwanza kukuandikia barua ya wazi. Kuna clip nilitumiwa ilyozagaa kwenye jukwaa la WhatsApp unapoonyeshwa na kusikika ukilalamikia manunuzi na matumizi mabaya kwenye madawa na vifaa tiba ambapo bei zimeongezwa bila maelezo ya kitaalamu wala ya kuingia akilini. Unaonyesha uchungu namna ya watendaji wa umma walivyopaisha bei za vifaa tiba kinyume na ukweli wa bei halisi za vifaa husika pamoja na kusomeshwa na kutengenezwa kwa fedha ya umma ili wahudumie badala ya kuuhujumu. Hili ni jambo jema, kuchukizwa na kulaani vitendo kama hivi japo njia zilizotumika si sahihi. Hata hivyo, tokana na ukweli wa mambo, ukiachia mbali unyeti wa suala husika, linaacha maswali mengi kuliko majibu tokana na namna ulivyolishughulikia. Je kulikuwa na sababu ya haraka wakati ukijua madhara yake?
          Mhe. Waziri Mkuu, naomba niulize maswali. Mepesi japo ya msingi yafuatayo: mosi, kwanini usikamate wathumiwa kwanza ndipo umwage mtama? Pili, je uliwasiliana na wataalamu wa uchunguzi kabla ya kusema uliyosema lau kupata maoni yao juu ya faida na hasara za kufanya hivyo? Tatu, je kama wewe mwenye unalalamika hivyo, sisi wachovu tufanye nini? Nne, je hii ndiyo njia ya busara ya kawaida na kisayansi ya kushughulikia tatizo kubwa na nyeti kama hili? Tano, je umefanya uchunguzi kwanza kabla ya kupasua mbarika lau ujue mzizi na historia ya kadhia? Sita, je haraka ni ya nini wakati ukijua kuwa kufanya hivyo kunaweza kutoa mianya kwa wahalifu kuficha uchafu wao hata kukimbia nchi kwa wale waliopewa tenda ambao si watanzania au ni watanzania wa mguu ndani mguu nje? Saba, je hili lina tija gani kwa taifa? Nane, najua wengi wa wanufaika wa tenda na ufisadi huu si watanzania wa kweli tokana na historia ya ubadhilifu katika taifa letu Je hii ndiyo staili yenu ya uongozi ambayo, kimsingi, inaweza kutafsiriwa vibaya kuwa hamko makini japo mko makini?
            Mhe. Waziri Mkuu, kama nilivyosema, maswali ni mengi kuliko majibu. Tisa, je kusema kwako kabla ya kuwakamata wahusika huoni unawasaidia watoroke au kufuta nyayo zao?
Kumi, je waliokula hiyo fedha ni maafisa wa umma tu wapo wakandarasi ambao wengi ni wageni wanaoweza kukitoa kabla ya kutiwa nguvuni? Kumi na moja, je hukujua madhara ya kusema kabla ya kuthibiti? Kumi na mbili je huu ni mchezo wa kwanza? Ni uchunguzi gani wa kina umefanywa? Kumi na mbili, je inakuwaje unawaambia wezi warejeshe fedha badala ya kuwaweka ndani na kuwafilisi kwanza ndipo sa uwatake wategemezi wao kusema ukweli wote?
            Mhe. Waziri Mkuu, japo mie si mshauri wako wa kuajiriwa, naomba nitoe ushauri ufuatao. Isitoshe, nimekuwa nikotoa ushauri wa bure kwa bosi wako Mhe. Rais ambaye mara nyingi ameufanyia kazi. Hivyo, unapata ushauri toka kwa mtu mwenye kufaa asiye na makundi wala maslahi yoyote kisiasa. Nasema haya kuepuka kuonekana na kushambulia. Kama inatokea ofisi yako au wewe binafsi unapokea tips kuhusiana na ubadhilifu kama huu, hakuna haja ya kukurupuka kutangaza badala ya kuwastukiza na kuwaweka ndani watuhumiwa ili kuepuka kuwa sehemu ya tatizo badala ya suluhu. Naomba niongeze maswali. Mosi, je una habari kuwa ukipasua mbarika kabla ya kukamata unawasaidia watuhumiwa kukimbia nchi au kuharibu ushahidi na kuwa tatizo badala ya suluhu? Tabia hii inaweza kutafsiriwa vibaya kama kuwapa mwanya wahusika kutoroka kwa wale ambao si raia au raia wenye makazi nje. Hili halihitaji kuwa na shahada katika uchunguzi na upelelezi. Historia ya ufisadi nchini ina mifano mingi ya watu waliotoroka baada ya kustuliwa na wakubwa mfano mkubwa ukiwa ule wa Chavda. Inahitaji akili ya kawaida, umakini, na uzalendo kupambana na kadhia kama hii. Nineshauri tuwe makini ili kwenda mpaka kwenye kiini cha kadhia hii si kwenye idara moja bali zote za serikali. Mbili, je ni madudu mangapi kama haya yameishafanyika bila kugundulika na kuchukuliwa na hatua? Tatu, je tatizo ni tabia za watu binafsi kuhusiana na tamaa au mfumo wetu mbovu wa manunuzi ukiachia mbali mazingira kuruhusu baadhi ya wenzetu kutuibia na kufaidi chumo la wizi? Haya ndiyo maswali muhimu kujiuliza na kutafutia majibu mujarabu.
Mhe. Waziri Mkuu, hapa Kanada huwezi kufanya hivyo ukapona kwa vile kila mtu kila mwaka hutoa taarifa ya mapato na matumizi yake. Inapotokea ukuwa fedha, mapato au matumizi yasiyo na maelezo lazima uchukuliwe hatua. Kama una fedha au mali zilizozidi, hukamatwa hadi utoe maelezo yanayoridhisha kwa serikali.  Je, kama kweli mnamaanisha msemacho juu ya kupambana na ufisadi na wizi wa fedha za umma, mnashindwa nini kuanzisha mfumo huu unaohakikisha usalama wa fedha na mali za umma?
            Mhe. Waziri Mkuu, kwa ujuzi na uzoefu wangu, ingeleta maana kama ungetangaza na kusema uliyosema baada ya kukamata na kuweka ndani watuhumiwa ili haki itendeke. Baada ya kumwaga mtama, usishangae wahusika kupeta nasi kubaki tukiwalaumu bure wapelelezi kwa kushindwa kuwaweka hatiani wahusika kutokana ushahidi utakaokusanywa. Huwezi kuinama kuokota jiwe halafu ukalaumu kwa kunguru au ndege kuruka kabla ya kumtwanga jiwe. Je haraka ni ya nini? Je kulikuwa na ulazima?
            Mhe. Waziri Mkuu, naomba nimalizie kwa kuomba uupatie umma majibu ya maswali kama ishirini niliyoibua hapo juu huku ukifuata utaratibu wa kufanya kazi na uchunguzi kwa usiri badala ya kutangaza kabla ya kuchukua hatua za kuwakamata na kuwahifadhi wahusika. Kila la heri.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: