Ukiangalia namna mataifa ya Ulaya na Marekani (na dunia) yanavyoshughulikia mgogoro wa Ukraine na Urusi, unashangaa na kusikitika kuona namna yanayowaita wahamiaji haramu wakimbizi wanaokimbia vita kwenye nchi za Kiafrika ambao zimewafungia mipaka huku zikifungua mipaka na mikwiji kwa wakimbizi toka taifa moja la Ukraine kwa sababu tu ni weupe wenzao. Hawa hawa ndiyo wengi wao waliosababisha migogoro barani Afrika ukiacha mbali kufaidika na raslimali na malighafi zinazoibiwa toka nchi husika. Inatia kinyaa kuona mabilioni ya fedha yanayotumika kushughulikia kadhia hii wakati nchi za Kiafrika zinazoendesha dunia kwa raslimali zake zikibaguliwa wazi wazi mchana kweupe nazo zisifurukute japo kidogo lau kwa kulalamika au kulaani.
Mgogoro wa Ukraine umefichua chuki, ubaguzi na unafiki visivyomithilika. Kuliona hili, angalia wakimbizi wanaokimbia ima mifarakano, umaskini na ujambazi wanaotaka kuingia nchini Marekani wakitokea Mexico wanavyozuiliwa mpakani hata kurejeshwa makwao kwenye hatari na vita huku wale wa Ukraine wakifunguliwa mpaka wakihimizwa na kuruhusiwa watakavyo wakati wowote. Hata huko ulaya hali ni ile ile. Wakimbizi toka Afrika na kwingineko wanaojaribu kuingia ulaya hata kwa kuhatarisha maisha yao kwa kupanda vyombo vibovu vya majini kuvuka bahari ya Meditereniani, wanazuiliwa hata kupanga kuhamishiwa Afrika. Je wale wa Ukraine wanapokelewaje? Kwa mikono miwili.
Kwa sasa, wakimbizi toka taifa moja, tena dogo na ambao idadi yao haiwezi kulinganishwa na wale wa kiAfrika na wengine, wameonekana kuwa binadamu zaidi ya wengine ambao ima ni nusu binadamu au wanyama katika macho ya mataifa haya nafiki na baguzi. Hata hivyo, wale wanaojua namna mataifa ya kimagharibi yalivyounda mfumo koloni na baguzi unaoendesha dunia, hawatashangaa kuona kinachoendelea hasa wakijikumbusha namna yalivyosaidia utawala wa kibaguzi wa kikaburu wa Afrika ya Kusini wakati ukiwatesa na kuwaua waafrika tokana na rangi na mali zao au yanavyofumbia macho ugaidi wa Israel dhidi ya wapalestina huku yakijifanya kuhimiza kila mtu duniani kuilaani Urusi kwa kuua waukraine wenye macho ya bluu na ngozi nyeupe ambao kwao ndiyo binadamu wanaostahiki haki za binadamu lakini si wengine.
Eneo jingine linaloonyesha ubaguzi na unafiki vya kiwango cha lami ni misaada ya hali na mali mataifa husika yanatoa kwa Ukraine ikilinganishwa na mataifa mengine yanayokumbwa na kadhia kama hii, tena kwa muda mrefu ukiachia mbali kuathiri na kuua watu wengi kuliko hawa wapendwa. Hivi karibuni, bunge la Marekani liliidhinisha jumla ya dola za kimarekani bilioni 13.6 kusaidia Ukraine kwa mujibu wa jarida la Marekani la New York Times (Machi 18, 2022) mbali na bilioni 33 ambazo rais Joe Biden ameomba zipitishwe haraka ili kwenda Ukraine (New York Times, Aprili 28, 2022). Ukijumlisha pamoja fedha ambazo zitaigia Ukraine hadi mwisho wa mgogoro, zinaweza kuwa zaidi ya nusu au sawa hata zaidi ya pato la taifa hili.
Mbali na Marekani, Umoja wa ulaya hivi karibuni uliidhinisha Euro bilioni 1.2 kwa mujibu wa Reuters (Januari 18, 2022) na kuamua kutoa Euro Bilioni 17 kusaidia wakimbizi wanaokimbia vita huko Ukraine. Zaidi ya hapo, uliitishwa mkutano wa wafadhili uliofanyika Warsaw, Poland na kuahidi kuchangisha dola bilioni 6.5 kwa ajili ya Ukraine ambapo wakati huo huo Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) lilikuwa likihangaika, bila mafanikio, kutafuta dola bilioni 1.2 kwa ajili ya kuhudumia wakimbizi milioni 2.3 wa Sudan ya Kusini ambao ni takriban nusu ya wakimbizi wa Ukraine waliotamalaki katika mataifa ya DRC, Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda.
Kwa wale ambao hawajaona huu ubaguzi na unafiki wa kunuka, wanaweza kupata jawabu toka kwa mkimbizi toka Kameruni Wilfred Tebah aliyekaririwa akisema, “sina cha ziada bali kushangaa nini kingetokea kama haya mamilioni toka mataifa ya ulaya mashariki wangekuwa ni rangi nyingine” (AP News, Aprili 11, 2022). Mbali na majibu haya, taifa la Marekani linaweza kutoa picha safi ya namna ubaguzi huu wa kimfumo na kimataifa unavyoonekana na kufanya kazi. Mfano, baada ya kuanza vita huko Ukraine, Marekani imeahidi kuchukua wakimbizi 100,000 kwa kuanzia ikilinganishwa na wakimbizi 30,000 toka Syria ambako vita imekuwa ikiendelea kwa zaid ya miaka kumi. Kanada ilishaingiza wakimbizi 73,000 toka Syria ikilinganishwa na na maombi ya waukraine 204,000 ambapo 91,500, kwa mujibu wa tovuti ya uhamiaji ya Kanada, yameishakubaliwa ndani ya kipindi cha miezi michache. Je hii ni nini?
Pamoja na Afrika kuwa na migogoro hatarishi na mikubwa tangu miaka ya 60, mwaka 2018, Kanada iliahidi kupokea wakimbizi wa kiafrika na Mashariki ya kati 10,000 huku idadi kubwa wakichukuliwa wa Mashariki ya kati. Hii ni nini kama siyo ubaguzi tena dhidi ya Waafrika?
Ubaguzi huu wa kimataifa unawaumiza sana Waafrika kuliko wote japo bara lina wakimbizi wengi na migogoro mikubwa na mingi kuliko mabara yote. Kwa upande wa Marekani, hali ni mbaya sana. Kwani, kwa mujibu wa mtandao wa Pewresearch.org (Januari 27, 2022), kuna idadi ya watu Weusi, si waafrika 4,100,000 nchini humo idadi hii ikipanda toka wakimbizi Weusi 8000,000 miaka ya 80. Je kama tukizidisha namba ya wakimbizi wanaochukuliwa toka Ukraine kwa miaka 32 tukazidisha na kiwango cha sasa tunapata nini? Kwa ubaguzi huu kama waukraine watapigana kwa miaka 32 na wakachukuliwa kwa kiwango cha sasa, wataingia Marekani wote na kubaki na nafasi sawa ikizingatiwa kuwa Ukraine ina idadi ya watu milioni 43.
Mbali na uchache wa wakimbizi Weusi wanaoruhusiwa kuingia Marekani, kuna juhudi kubwa za kimataifa kutaka kumaliza mgogoro wa Ukraine huku migogoro ya muda mrefu na hatarishi barani Afrika ikifumbiwa jicho. Mfano, hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Manuel de Oliveira Guterres alitembelea Ukraine na Urusi kutafuta namna ya kusaidia kumaliza mgogoro haraka ili kunusuru uharibifu na vifo mbali na Papa Francis aliyeahidi kwenda kule kufanya kazi ile ile. Jiulize, walipouawa Wanyarwanda kwenye mauaji ya kimbari ya 1994 au yale ambayo yamekuwa yakiendelea Darfur, Sudan, hawa viongozi zaidi ya kuwa sehemu ya tatizo, walifanya nini? Wakati Umoja wa Mataifa ukilaumiwa kwa kupuuza maonyo ya kutokea kwa balaa hili, kanisa Katoliki lilishutumiwa kuhusika na mauaji na baadaye Papa aliomba msamaha kwa ushiriki huu. Gazeli la the Guardian (Machi 20, 2017) lilimkariri Papa akisema “dhambi na maanguko ya wakristo viliharibu sura ya Ukatoli.”
Kama haitoshi, muda huo huo wakati yakifanyika mauaji ya kimbari nchini Rwanda sambamba na yale ya Kosovo, Umoja wa kujihami wa Ulaya wa NATO uliingilia kati nchini Kosovo na kumaliza vita huku ukiacha Wanyawaranda wamalizane.
Kwa ufupi, hii ndiyo sura ya ubaguzi na unafiki wa kimataifa inavyoonekana. Je Waafrika tunajifunza nini tokana na jinai hii ya makusudi dhidi yetu? Ajabu ya maajabu, pamoja na kujua ukweli, bado tunaamini watesi wetu kutusaidia kuleta amani na maendeleo wakati wakitubagua, kutuchukia na kutuhujumu wazi wazi? Nani alituroga?
Chanzo: Raia Mwema jana/
No comments:
Post a Comment