The Chant of Savant

Saturday 28 May 2022

Weusi unapogeuka dhambi ya mauti!

Kwa mara nyingine, tarehe 15 Mei, ilifichua ukaburu, unafiki na uoza wa taifa linalojiita kubwa kuliko yote huku likijifanya mwalimu wa haki za binadamu, usawa na ustaarabu wakati ni taifa la hovyo na ovu, yaani Marekani. Ni pale mbaguzi wa kunuka Payton Gendron, kijana wa miaka 18 mbaguzi na mjinga alipowamiminia watu zaidi ya 20 waliokuwa kwenye duka la Superstore na kuua watu watu 10 nane wakiwa weusi huko Buffalo Marekani ambako alikwenda kwa dhamira ya kuua weusi au watu wasio wazungu ambao anadhani wanachukua nafasi ya wazungu kwa wingi. Hivyo, kutishia maslahi ya weupe huko Marekani.                 Kijana huyu ni mmoja wa wahafidhina wanaoamini katika nadharia njama na uchwara ya replacement theory au nadharia mbadala ambao weupe wanaamini na kutaka kuwaaminisha wengine kuwa watu wa rangi au wasio weupe wanazidi kuchukua nafasi zao kwa wingi kiasi cha kutishia madaraka na ulaji wao wa kujipatia kupitia ubaguzi na ukoloni na mifumo mingine fichi na habithi kama vile ubepari, ubeberu na ukoloni mamboleo. 
        Hawa pamoja na kuwalaumu mahabithi wenzao kama akina Adolf Hitler na Benito Mussolini, wamekuwa wakifanya mambo yale yale wanayolaani kwa kisingizio cha ustaarabu wakati wanachofanya ni ushenzi. Hivi kweli ukoloni na utumwa navyo vilikuwa ni aina ya ustaarabu? Je ustaafrika nao uko wapi hadi Afrika itegemee ustaarabu ambao nao ni matokeo ya utumwa wa kiakili wa kudhani kuwa kuelimika au kusonga mbele kitabia na kimila lazima vipimwe na uarabu.
        Kuonyesha kuwa ubaguzi si wa Marekani tu bali mpango wa wazungu wengi wanaojiona kama ndiyo wenye haki ya kuwa binadamu kuliko wengine, hata hapa Kanada baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vikilipoti tukio bila kutaja jina la muuaji wakati anajulikana kuwa ni Payton Gendron. Hii inakumbusha kisa kimoja nchini Marekani ambapo mswahili mmoja aliua mtu mmoja na kuwekwa ukurasa wa mbele wakati muuaji mweupe aliyeua watu sita kipindi hicho hicho kuwekwa kurasa za ndani tena kwa kichwa cha habari chenye umbo dogo ikilinganishwa na mswahili.
        Hata pale Python au chatu (namuita hivyo maksudi) alipoua waswahili nane, hakupigwa risasi alipojitokeza mbele ya polisi. Angakuwa mswahili au mtu wa rangi, angemiminiwa risasi kwa madai kuwa alikuwa hatarishi kwa jamii na polisi. Siku chache kabla ya mauaji haya ya kibaguzi na kishenzi, mtanzania mmoja Rogers Kyaruzi alionekana, eti akionyesha tabia zenye kutia shaka kwenye maegesho na kuishi kupigwa risasa na kufariki hapo hapo.                     Angekuwa mzungu, angepelekwa hospitalini kuangalia ni kwanini alikuwa anaonyesha tabia zenye kutia shaka. Sitashangaa huyu muuaji mbaguzi Payton Gendron kama hatutaambiwa kuwa ana matatizo ya kiakili au alikuwa na utoto mbaya wa manyanyaso japo nyaraka alizorusha kwenye mtandao zinamuonyesha kama mhafidhina anayechukia watu wasio wazungu.
        Juzi juzi tu majeshi ya Israel yalimpiga risasi na kumuua mwandishi wa Al Jazeera wa kipalestina Shireen abu Akler. Pamoja na kujulikana kuwa muuaji ni majeshi ya Israel, vyombo hivi baguzi havitaji hivyo kwa kuogopa kumuudhi kibaraka wao. Akiuawa mwarabu si habari, japo mwarabu akiua muisrael, ni habari kubwa na tishio kweli kweli.
        Japo waarabu walio wengi, kama wamarekani, wamekuwa wakijitahidi kujionyesha kama wapenda usawa na haki tokana na kunyanyaswa na Israel, nao wanashiriki au kufumbia macho dhuluma, udhalilishaji, unyonyaji na mauaji ya wafanyakazi wa ndani huko Mashariki ya kati. Hii yote inatokana na imani iliyojikita kwenye dini nyemelezi za kigeni ambazo humuona mtu mweusi ima kama aliyelaaniwa au mtumwa wa mtu mweupe japo wengine wanaojiita weupe kama waarabu na wahindi wakija huku nao wanaitwa weusi kiasi cha wazungu kushindwa hata kuwatofautisha. 
        Hivyo, kuwabagua, kuwadharau na kuwanyonya sawa na waswahili wanaowabagua na kuwanyonya nao wakijidanganya kuwa ni weupe kama wazungu. Hivi kweli kuna binadamu mweupe? Kama wazungu ni weupe, maziwa na chaki vitakuwa nini? Haya ni maswali ambayo waswahili wanapaswa kujiuliza na kuyapatia majibu sahihi hata kama kufanya hivyo kunaumiza vichwa. Tuumize vichwa ili tujikomboe na kuachana na ujinga wa kuendelea kutumikia ubaguzi tena kwa kujibagua, kuruhusu kubaguliwa au kubaguana wenyewe.
        Kwa wabobezi wa lugha ya kiingereza ambayo ni lugha ya watu wabaguzi kuliko wote, kila kitu kibaya ni cheusi. Siku ikiwa mbaya utaambiwa black day, black summer, black spirit na mengine mengi. Na kila kitu kizuri ni cheupe katika lugha hii.
        Sambamba na kiingereza, hata kwenye vitabu vya dini kama Biblia, utakuta laana, utumwa na ubaya vyote ni vyeusi. Mfano ukisoma namna watoto wa Ham walivyolaaniwa na kugeuka weusi, utaona mzizi wa kadhia hii inayoanza kuwa tishio duniani. Ham alipolaaniwa alipewa adhabu mbili kuwa mtumwa kama Wamisri, Waethiopia na wahindi na mweusi kama wao.
        Kwenye Quran Surat al Imran (3:106) nayo inasema wale watakaoingia motoni sura zao zitageuka nyeusi na wataulizwa kwanini hawakuamini hadi wapate adhabu ya kutoamini. Kwa watakaoingia peponi, sura zao zitakuwa nyeupe.
        Mbali na dini, hata baadhi ya lugha kubwa za kiulaya kama vile kiingereza, kwake kila kitu kibaya ni cheusi na kila cheupe ni kitakatifu. Utasikia black Friday, black sheep, black summer na mengine mengi. Kujitenga na dhambi ya weusi, usishange kuona watajwa hapo kama vile Waethiopia wakiwabagua wengine huku wahindi wakijiita weusi japo wazungu wanaowaona wote ni weusi au watu wa rangi ambao ni tishio kwa mafanikio na maisha yao.
        Tumalizie kwa kuwahimiza waswahili kujitambua, kuwatambua maadui zao, kujuana, kujaliana na kuthaminiana pia kushirikiana kupambana na huu ubaguzi wa wazi dhidi yao kwa vile ni weusi. Hapa ndipo jibu mujarabu kwa tatizo la weusi kugeuka adhabu tosha ya kifo mbele ya wabaguzi wa kunuka kama ilivyotokea huko Marekani juzi. Tieni akilini.
Chanzo: Raia Mwema jana.

No comments: