The Chant of Savant

Thursday 12 May 2022

Wabunge Igeni Mfano wa Mhe. Mpina, Ujasiri, Ukweli na Uzalendo

Akichangia hoja  bungeni hivi karibuni, kwa uchungu na uzalendo vya wazi, Mheshimiwa Luhaga Mpina ( CCM-Kisesa) aligusia jambo ambalo wengi hawapendi kuligusia kwa kuchelea kupoteza maslahi yako au kugusa wakubwa pabaya. Mhe. Mpina, kwa lugha inayoeleweka na kushawishi, aliwatolea uvivu wafanyabiashara wanaopandisha bei za vitu huku serikali ikiangalia kana kwamba haina uwezo wa kuwashughulikia au kuwazuia wakati inao uwezo na kila sababu. 
Katika makala hii nitajikita kwenye ugumu wa maisha unaotengenezwa na watendaji wetu walioko kwenye ulaji––––kama alivyosema Mhe. Mpina bila kificho, kupindisha wala woga. Niliwahi kumwandikia Mheshimiwa Rais juu ya nchi ya Kanada–––kama mfano wa nchi zinazoitwa zimeendelea zinavyotumia vizuri pesa zao––––kwa kubana matumizi na kuepuka kuwaumiza wananchi wake.  Katika barua na ushauri wangu kwa Mhe. Rais, nilimwelezea namna maafisa wa serikali hapa wanavyochapa kazi. Muhimu, niligusia namna wanavyotumia nafasi zao kwa kujitegemea–––bila kutegemea au kunyonya kodi za wananchi kama ilivyo nyumbani ambapo kila mkubwa ni mnyonyaji wa kawaida kama tutalinganisha na wenzao hata wa juu yao hapa Kanada.
Naomba nirejee tena ushauri huu––––huenda ukafanyiwa kazi kipindi hiki kigumu cha maisha ili kuepuka kuongeza chuki ya makapuku dhidi ya serikali na wakubwa zake–––kama kweli tumeamua kujikomboa na kuwatumikia vizuri wananchi wetu tunaodai kuwawawakilisha na kuwaongoza. Hapa Kanada, mawaziri karibia wote hujiendesha. Hawana walinzi wala wasaidizi kama ilivyo kwetu kwenye nchi maskini na ombaomba. Ukiachia mbali mawaziri, majaji na maafisa wengi wa serikali wanajiendesha wenyewe na hawana walinzi.  Je hali ikoje nyumbani? Mkuu wa wilaya, wizara, mkoa, jaji, hakimu, na maafisa wengine wadogo eti wanawekewa madereva na wengine wabunge hata walinzi na watunza bustani. Wanalipiwa kodi ya pango.
Nilihoji kiasi cha fedha serikali inapoteza kwa kugharimia mambo ambayo wafanyakazi wengine hawapewi. Je huu ndiyo usawa tunaofundishwa na kuhimizwa wakati tunabaguana kwa vyeo? Kwanini watu wanaolipwa mishahara mikubwa, mfano, wanaishi kwenye nyumba bure wakati hawa wadogo wakikamliwa kidogo wanachopata kwa taabu? Kuna haja gani, kwa mfano, waziri au mkuu wa mkoa au mkuu wa idara kulipiwa kodi ya nyumba lakini si mwalimu? Je hapa kuna tofauti gani kati ya utawala mkoloni na nchi huru ambapo wakubwa wanajigeuza wakoloni weusi? Nimo kwenye kukamilisha kitabu kiitwacho Africa Must Deal with Blats for Its True Decolonisation: Africa’s Unclothed Truth about Internalised Internal Colonialism, yaani Afrika lazima ishughulike na wanaharamu na kupambana na ukoloni mtupu uliosimikwa na kukubalika.
Mbali na Mpina kuwamulika wafanyabiashara wanaojiona kama wao ndiyo serikali, aligusia mikataba ya hovyo akitaja wazi wazi ule wa Symbion ambao alitaka kujua nani yuko nyuma yake na namna unavyohujumu nchi huku ukipigiwa chapuo na wabunge ilipwe mabilioni bila kueleza iliingiaje, ilikwepa kodi kiasi gani na mengine kama hayo ambayo mbunge anayajua kuliko mimi na wewe. Je serikali imechukua hatua gani kumhoji Mheshimiwa Mpina lau aipe usaidizi kwa kutoa ushahidi na vielelezo alivyo navyo kuhusiana na kadhia husika?
Japo Mpina hakwenda mbali zaidi, tangu afariki Hayati Dkt John Pombe Magufuli, tumeona namna ya wale watuhumiwa wa ufisadi wa kutisha walivyoachiwa kwenye mazingira yenye utata. Japo nimekuwa mshauri na shabiki mkubwa wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, naona kama mambo yanakwenda ndivyo sivyo. Leo, kwa mfano, ukiiuliza serikali ni vipengee vipi na utaratibu gani vilitumika kuwaachia watuhumiwa wa Escrow, Habinder Singh na James Rugemalira na vipi maslahi ya taifa yalilindwa au kuhujumiwa na kwa faida ya nani? 
Mpaka naandika makala hii, niliudhika baada ya kusikia kuwa serikali iliamua kufuta mashtaka dhidi ya watuhumiwa wa uhujumu wanaojulikana. Mfano, wale wanaoona kama kulikuwa na sababu za kisheria au kimsingi au hata zinazoingia kwenye akili ya kawaida, ilikuwaje baadhi ya watu, tena maarufu, waliokuwa wamepokea fedha toka kwa mtuhumiwa kama vile Rugemalira, mfano, mawaziri wa zamani, Prof. Anna Tibaijuka na William Ngeleja na Askofu Methodius Kilaini. Je kama mhusika hakuwa ana shitaka, ilikuwaje vigogo hawa, tena wajuvi wa mambo, waliamua kurejesha fedha walizopewa na mtuhumiwa kama hakuna namna? Je ilikuwaje awamu ya tano iliendelea kuwashilikilia chini ya sheria za uhujumu uchumi lakini ghafla, baada ya kuingia awamu ya sita, wakaachiliwa haraka bila maelezo yanaoingia akilini wala kushawishi akili? Je hapa kunani? Je nani walioko nyuma ya Escrow?
  Tukija kwenye kashfa ya Symbion, tunajua wazi ilivyotingisha serikali ya awamu ya nne baada ya kuwagusa viongozi wa juu   hadi waziri mkuu wake Edward Lowassa akalazimika kujiuzulu baada ya kubanwa na ushahidi au kuhofia kuumbuliwa? 
Je kati ya awamu ya tano na sita, ni ipi ilikuwa/ina ukweli juu ya kashfa hizi? Je awamu ya tano ilikosea au ya sita ndiyo imekosewa zote zikuhusishwa na awamu ya nne ambayo viongozi wake wakuu, karibia wote isipokuwa Makamu wa Rais waliguswa moja kwa moja na kashfa husika ukiachia mbali awamu ya pili ambayo ndiyo iliasisi kashfa husika huku waliokuwa mawaziri wake waliokuja kuwa wakubwa kuhusishwa moja kwa moja?
Nafahamu wazi. Wachambuzi, hata waandishi na wakereketwa wa ndani wanaoogopa kugusia kashfa hizi. Je nani asiyejua kuwa kuna rafu inachezwa?  Nani asiyejua kuwa baada ya kufariki kwa Magufuli, kuna mambo yanafanyika ndivyo sivyo mfano kashfa ya Escrow ukiachia mbali baadhi ya watuhumiwa wakubwa wa ufisadi kuanza kutesa kwenye ulaji? Nani alitegemea, kwa mfano, baadhi ya wanachama wa CCM waliozuiwa hata kugombea ubunge tokana kukumbwa na kashfa kubwa, kurejea kwa kishindo kama wawekezaji wakubwa? Kama tutakuwa wakweli kwa nafsi yetu kama wananchi na wenye nchi, nani asiyejua mfano aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo moja mkoani Tabora alivyozuiwa kugombea ubunge tokana kukumbwa na kashfa ambaye siku hizi amejitokeza kuwa mwekezaji mkubwa kwenye mawasiliano? Je ni miujiza gani imefanyika akatakaswa bila kukutikana bila hatia na mahakama? Je hapa nani anamdanganya nani? 
Nimalize kwa kumpongeza Mhe. Mpina kwa ujasiri, ukweli na uzalendo wake. Kuna falasa kuwa unaweza kuwadanganya watu wote kwa wakati fulani,watu fulani kwa wakati wote lakini si watu wote kwa wakati wote. Wenye madaraka tieni akilini mkijua kuwa hata hayo madarka yenu yana mwisho kama ilivyokuwa kwa watangulizi wenu. Nyie ni wa kupita lakini si taifa wala ukweli. Tieni akili ili lau mtende haki. Mhe. Mpina ametimiza wajibu wake kwa watu wake na taifa lake. Kazi kwenu kueleza upi ni ukweli na upi ni urongo na kwanini.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: