How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 24 May 2022

Turasimishe na Kuthamini Vyetu Vyote si Gongo tu

Uploading: 3717120 of 5928360 bytes uploaded.

Japo si wengi waliomwelewa––––na sijui kama ameeleweka vilivyo­­­­––––Mbunge wa Chomba, Mheshimiwa Kondesta Sichalwe. Japo si wa kwanza kufanya hivyo––––amewafumbua macho wenye akili na kujithamini huku wakishuku uhohehahe na uhovyo na uoza wa mambo na mifumo yetu tuliyorithi na kupwakia bila kufirikiri toka kwa mabwana zetu na watesi wetu waliotutawala na kuendelea kufanya hivyo kwa visingizio mbali mbali. Kwa fahari na ushufaa, tunaongea lugha zao na kupwakia kila ujinga wao tokana na upumbavu wetu huku tukizikimbia na kuzidharau na kuziogopa zetu tuzijuazo vilivyo. Tunaabudia imani na miji yao kana kwamba hatuna vitu hivi. Tunaita miji na nchi zao takatifu kana kwamba zetu ni chafu. Ukiuliza wapi ni mahali patakatifu, utaambiwa ima Jerusalemu, Makka au Roma wakati hakuna utakatifu wowote zaidi ya longolongo na propaganda za kijamii tokana na ukoloni wa kimila.

            Baya zaidi, hata mamlaka na serikali zetu zilichaguliwa na watu wetu (washenzi), zinaapishwa kwa kutumia dini na imani za kigeni huku tukijiumiza kwa kudharau, kudhalilisha na kuhujumu vilivyo vyetu. Je serikali zinazoapishwa na kuamini kwenye imani za kigeni zinaweza kututumikia kweli bila kutuuza? Viongozi ima wanaapa kwa Biblia au Kurani. Je nini nafasi ya imani zetu na viongozi wake wa kimila? Hili linaweza kuonekana kama jambo dogo na jepesi tena chokonozi na la kuudhi, linatuvua nguo na kuaonyesha utumwa wa kiakili na kiimani hata kiutawalatulivyo navyo kwa maangamizi yetu na vizazi visivyo na hatia vijavyo.

Tumegeuzwa mabunga na mazuzu kwa kupewa maneno matamu. Hatujui tofauti kati ya halali na haramu (japo yote ni maneno ya kuletewa na kupandikizwa bila kuyachunguza maana na undani wake. Tunadharauliana kwa dini za kuazima. Tunaitana majina ya hovyo kama vile makafiri, waliopotea, wasiookoka, wasio wastaarabu na mengine mengi ya kishenzi, majina ambayo tuliitwa na kupewa na watesi wetu nasi tukayaamini na kuyapwakia bila kuhoji. Wengine wanatoa kafala ya binadamu wakati sisi ni wanyama. Na wengine wakitoa wanyama kama sisi wanatwamba ni matoleo kwa Mungu. Je sisi­­­­––––kabla ya ujio wao na dini zao––––tulikuwa tukitoa kafala gani zaidi ya wanyama?  Tunaongelea ustaarabu ila si ustaafrika. Tunaongelea pepo za kigeni huku tukiita amali zetu kama mila vitu vya motoni na udhambi. Tunaahidiwa madangulo na kwaya kwa kisingizio cha pepo. Tunashindwa kuitambua leo tukiifia kesho ya kitapeli japo tunajua kuwa wahenga walisema mla kala leo kesho kalani! Tunatenda dhambi ya kujibagua, kubaguana, kudhalilishana na kujidhalilisha wenyewe kwa wenyewe huku mabwana zetu wa kila aina wakicheka na kutushangaa nani alituloga. Tumeahidiwa pepo na upuuzi wa kila aina ili tujipeleke kwenye majili (kinyongeo) yetu ya kujitakia. Lini Waafrika tutakengeuka na kukua kutambua na kujithamini huku tukiamini na kuamini na kupenda vilivyo vyetu?

Tunasifia na kutukuza lugha na mila za kigeni tukidhalilisha zetu.  Msomi lazima aongee kiingereza kana kwamba kiingereza ndiyo usomi. Tunaona aibu kuongea lugha zetu huku wengi––––hata wasiojua kitu––––wakihangaika kutuaminisha kuwa wamesoma wakati ni wajinga wa kawaida. Ukiwasikia wakiongea, wanachanganya kimombo na kibatu (Kiswahili). Tunashindana kuibiwa na kuharibu watoto wetu kwa kuwapeleka kwenye shule za kizungu huku tukiua zetu. Ukifanya kitu cha maana wanasema ni uzungu. Ukifanya kisichostahiki wanakwambia ni uswahili.

Vyakula bora vinaitwa vya kienyeji au kishenzi huku majank ya kigeni yakiitwa vyakula bora. Utasikia ‘kuku wa kizungu na kuku wa kienyeji’ japo sisikii bata wa kizungu.’ Waonje uone yupi mtamu na mwenye viini safi kati ya hawa wawili. Hichi ndicho kiini macho na utapeli wa kujaza maduka ya vyakula vya hovyo na majunk kama vile Burger King, KFC, MacDonald (yote ya kigeni) kati ya mengi yanayoanza kutapakaa Afrika bila sababu ya msingi zaidi ya ujinga hata upumbavu mbali na ulimbukeni. Yako wapi maduka ya vyakula safi na tamu vya kiafrika? Ni bahati mbaya hata wasomi na wanasiasa wetu ima hawajui au hawataki kutwamba ukweli. Kwa wanaofikiri sawa sawa, wajikumbushe kitabu cha Tendehogo kinachochamba ujinga huu wa pamoja au collective imbicilization.

 Tunapwakia gongo ya kigeni iitwayo konyagi, brand, au whisk huku tukiita pombe zetu tunazojua formula na siri za utengenezaji wake kwa kukumbatia na kutukuza ulevi ule ule wa kigeni. Tunapenda na kununua vitu vya kigeni na kutajirisha wageni huku tukiua uchumia wetu. Tukizidiwa, tunaenda kule kule kuomba pesa ile ile tuliyoibiwa kimila!  Tunachukia vyakula vyetu na kupenda vya kigeni bila kujua vimezalishwa wapi na vipi na nani.  Tunajenga viwanda vya wenzetu na kubomoa na kufilisi vyetu!

Walevi wetu wanatajirisha wengine huku wakijifilisi na kujigeuza ombaomba na kopa kopa wakati Mungu aliwajaalia kila kitu! Je hili linahitaji wafadhili kulienga na kuelewa?

Tumedhalilishwa, kujidhalilisha na kudhalilishana na kuijikimbia kuanzia kukana majina yetu tukikumbatia ya kigeni bila kujua hata maana wala sababu zake, kutukana mila zetu na kukumbatia na kushambikia za kigeni kwa visingizio mbali mbali kama dini na ustaarabu wakati vyote ni mila. Tunaona fahari kuitwa John au Yahaya huku tukikimbia majina yetu.  Tumepewa utambulisho bandia huku tukikimbia ule wa asili yetu. Tutashindwa kujikana na kujitukana wenyewe? Adui yetu ni sisi wenyewe. Tunahitaji kukombolewa dhidi yetu wenyewe. Ajabu, ukombozi huu unategemea ubongo na mila na mifumo ya kigeni. Je tunamkomoa nani kama siyo sisi wenyewe? Tunaabudu miungu ya Israel na Kiarabu huku tukitukana na kukana yetu! Nani atusaidie kama siyo sisi wenyewe?

Tunafungishwa ndoa za kigeni huku tukiita zetu za kimila kiasi cha kutozitambua hata kisheria. Tunapewa vyeti kana kwamba upendo unahitaji na kutegemea karatasi. Muafrika akioa wanawake wengi kwa imani ya mila yake anaambiwa ni ndoa za kienyeji zisizotambulika kisheria wakati muislamu akiona wengi hao hao anaambiwa ni amri ya Mungu. Je huyu Mswahili anaona kwa amri ya nani kama siyo Mungu huyo huyo? Ni wangapi wanajiuliza maswali chokonozi na tunduizi kama haya japo yanaudhi?

Sheria zetu zinatungwa na watu wetu na kuandikwa kwenye lugha za kigeni kana kwamba hatuna lugha zetu adhimu. Hatujiamini wala kuaminiana. Tunadharauliana badala ya kuheshimiana. Tunachukiana badala ya kupendana. Tunahujumiana badala ya kujumika pamoja na kusaidiana. Mabwana zetu wa kiakili, kimila na kisiasa wametugeuza vikaragosi na askari wa kujimaliza wenyewe.

            Tunapwakia maji machafu ya chupa huku tukikimbia maji matamu na safi toka kwenye chemichemi zetu alizotujalia Mungu. Tunaletewa maji ya ‘baraka na upako’ toka nje au yale yale na matapeli wachache kana kwamba yetu si maji! Tukitaka kula au kulala tunaomba miungu ya kigeni itulinde kana kwamba kabla ya ujio wake tulikuwa hatarini.

Kwa ujinga wa maksudi na upogo, tumeua na kuchukia, kuua na kutelekeza elimu na ujuzi wetu kwa kuamini na kupwakia wa kigeni. Mtu akisoma nje anaonekana msomi kuliko yule aliyesomea nyumbani.anayesoma shule za English media anaonekana kuukata kuliko yule anayesomea shule za kata. Je viongozi wetu waliotukuka na kutukomboa au kutupigania walisoma shule na English media au nyumbani schools?

Leo sisemi mengi. Muhimu, kwa kuangalia ujasiri wa Mhe. Sichalwe, niseme––––bila wasi wasi–––tuanze kujiamini, kuaminiana, kujitathmini, kutathminiana, kujithamini, kuthaminiana, kujihoji, kuhojiana na kuhoji kila kitu na kujitambua na kutambuana bila mawenge wala miwani ya kikoloni. Bila shaka, wakati wa kuramisha, kutambua, kuthamini na kutumia vilivyo vyetu ni sasa. Saa ya ukombozi wa kimila na kulhali ni sasa.

Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: