How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 31 July 2024

Sir God Ameniamuru Nilete Dini ya Ukombozi

Baada ya kugundua kuwa mafyatu wake wengi wameharibikiwa na kuchanganyikiwa kiasi cha kufyatuliwa na kudhalilishwa na kila tapeli, Sir God ameniamru nilete dini ya Ukombozi. Hii ni baada ya kuona kuwa matapeli wengi wanawafyatua mafyatu waliogoma kuelimika wakawafyatua wanaowafyatua. 
        Nimeona mafyatu wangu wakiuziwa kila upuuzi kuanzia maji tena machafu, mafuta tena ya kishirikina, notebooks, kalamu, leso tena chafu, wengine wanavuliwa hata nonihino na kushikwashikwa vyote ukiwa ni utapeli kuwaibia wajinga ufanyawao na wajinga wenzao waavivu wa kufikiri na kubuni mambo ya manaa. Ni ujinga pande zote matapeli na wanaotapeliwa. Wengi hata hiyo elimu hawana. Wala hawana ubunifu wa kubuni vitu visivyo vya kikumbaff kama hivi. Wote wanahitaji ukombozi utakaoletwa na dini ya Ukombozi. Mafyatu wanadhalilika hakuna mfano. Wanahitaji Mkombozi ambaye ni mimi na ukombozi ambao ni dini ya Ukombozi. Wale uliotegemea wawazindue, wanawafyatua au kushirikiana au kuwafumbia macho wanaowafyatua.Wahenga kweli walisema wajinga ndiyo waliowao.
            Kwa vile imemfurahisha Sr God nipambane na jinai hii kwa kunishushia dini yake, msishangae mkisikia naongea lugha msizoelewa. Hata hivyo, hamtashangaa. Kama matapeli toka kaya nyingine wanakuja na kuwafyatua, kwanini mnishangae mie ninayewashangaa? Hamjawasikia wanaokuja na kujianzishia madhehebu ya kinyonyaji na kitapeli huku wakiuwauzia ujinga na woga? Naona yule anatikisa kichwa akishangaa sirkal iko wapi? Kwani wawili hawa wana tofauti? Kazi ya sirkal si kuwafumbua macho mafyatu. Kazi yake ni kuleta wachukuaji, sorry, wawekezaji waje wafaidi vinono vya kaya yetu. Tena nimekumbuka. Dini ya Ukombozi itawasaidia hata wanasiasa wanaotaka kushinda uchaguzi. Nawashauri waje niwaombee ilmradi walete mbuzi na ng’ombe na kutembelea Chegama.
        Kuanzia sasa nitaitwa Daktari, Genero, Papa, Mtakatifu,  Mtukufu, Mwenye maono, Mponyaji, Muota ndoto, Mtabiri Dk, Alhaji, Mhashamu, His Excellency, His Eminence, HH etc. Fyatu Mfyatuzi bin Mfyatuaji bin Mfyatukage wa Mfyatulizi mwana wa Mfyatukizi mjukuu wa Fyatuafyatua mwana wa Mfyatuizi kijukuu cha Mpayukaji Msemahovyo Msemakweli.
        Kijiji changu cha Chegama, kuanzia sasa, ni sehemu takatifu kuliko zote duniani. Hapa ndipo Mafyatu tulipotua tulipotoka mawinguni na kuanza kuijaza dunia. Mafyatu wote duniani walitokea kijiji hiki ambacho wao huita Bustani ya Edeni. Tokana na utukufu wake, Mafyatu wote duniani wanaamriwa kuja kutembelea sehemu hii takatifu mara tano katika maisha yao bila kujali ni makapuku au wakwasi.
        Nyumba nilimozaliwa, kuanzia sasa, ni hekalu la Sir God pia sehemu ambapo mafyatu watakaokuja kuonyesha utii wao watazunguka na kubuni lolote la maana watakalo na kulipata hapo hapo.
        Kwa vile Sir God amenipa madaraka ambayo hajawahi kutoa kwa yeyote isipokuwa mie,  kuanzia sasa, picha zangu zitasambazwa dunia nzima na mafyatu watakuwa wakiziweka kwenye sehemu maalumu za ibada. Kila picha itauzwa kwa dolari za Kiamerikani elfu tano. Itabidi kila kijiji kuchangishana na kuhakikisha wanakuwa na picha yangu kama mwakilishi wa Sir God aliyeniamuru kuleta dini ya ukombozi.
        Kuanzia sasa, kila fyatu atapaswa kutoa kafara ya mbuzi au ng’ombe jike kulingana na maelekezo yangu anapotembelea sehemu takatifu ya Chegama. Hawa wanyama watatunzwa hadi siku ya mwisho watakapochinjwa kwenye karamu ya mafyatu wote duniani. Hivyo,  nitaiamrisha sirkal kupanua eneo la kijiji ili kuweza kutunza zawadi hizi za Sir God mwenyewe.
        Kuanzia sasa sitatembea kwa miguu. Sir God ameniamuru niiambie sirkal kunijengea hekalu kila kaya, kuninunulia mashangingi idadi nitakayo, mashua na ndege ili kuniondolea msongo wa mawazo nna kuweza kuizunguka dunia haraka na kwa raha nikitangaza ukombozi wa mafyatu wote duniani. Nitatumia mahekalu yangu matakatifu kwa ajili ya kuwakirimu watakaokuja kuonyesha heshima yao Chegama. Mashangingi na ndege vitanisaidia kutembelea duniani nikionyesha utajiri wa Sir God na upendo wake kwa mafyatu wanaoibiwa na matapeli wanaomtumia.
Kuonyesha kuwa mie si mganganjaa, msakatonge, tapeli au jinga kama wale, kuanzia leo nitakuwa nafanya muujiza mkuu ambao ni kutoa mhadhara kuwa hakuna miujiza duniani bali ukumbaff na ujinga. Kupitia ufyatukaji, nitakuwa nikifungua vichwa vilivyogandishwa na woga wa uvivu wa kuchapa kazi. Nitawaelimisha mafyatu namna ya kufyatua wezi wanaowaibia ili waweze kutajirika badala ya kutegemea kuombewa.
        Nitafanya miujiza ya kuwafyatua mafyatu waache ukumbaff. Mfano, wote wanaotegemea waganga wa kienyeji au wachunaji waitwao wachungaji walewe kuwa ni wakumbaff. Kwani hawapo? Ni wangapi wanawajaza mafweza wanganganjaa na wachunaji eti wapate utajiri bila kufikiri wala kuchapa kazi? Ni akina mama wangapi walioishiwa kimaadili wanakimbizana na kudhalilishwa kwa waganga wa kienyeji eti wakitafuta dawa ya mapenzi wakati hakuna? 
        Siku hizi wameanza kuua zeruzeru kutafuta bahati wakati ni ukumbaff. Wangapi wanaamini kwenye ukumbaff wa kutoana kafara ili watajirike? Wangapi wakiwaona mataahira kwenye jamii fulani tajiri zinazosifika kuoana ndugu kwa ndugu na kuzaa mataahira wakadhani eti hao mataahira ndicho chanzo cha utajiri wasijue chanzo ni kuoana ndugu kwa ndugu? Kwani hayapo haya?  Hili ndilo lengo la kuanzisha dini ya Ukombozi. Semeni hamna.Hivi kumeishakucha?
Chanzo: Mwananchi leo.

Monday, 29 July 2024

For and in the memories of Hugh Masekela and Tebogo Modingoane

https://www.youtube.com/watch?v=7StGJtI7SSI

Mwenye mapenzi anaona tena sana


Kuna imani au tuseme usemi kuwa mwenye mapenzi haoni. Je kweli mwenye mapenzi haoni hata kama macho anayo? Je ukweli ni upi haoni au anaona tena sana? Ingawa “mwenye mapenzi haoni” ina tafsiri nyingi kutegemea na hali yaliyomo mapenzi, ukweli ni kinyume. Tutatoa sababu zifuatazo:
        Kwetu mwenye mapenzi lazima aone na aone kwelikweli. Utawezaje kuujua uzuri na mvuto wa mwenzako kama kweli mwenye mapenzi haoni? Ingekuwa hivyo, watu wengi wenye changamoto za aina mbalimbali za ulemavu ambazo ni kazi ya Mungu wasingenyanyapaliwa, kukataliwa, na wengine kutoolewa kabisa au kuachika tokana na changamoto ambazo siyo matokeo ya kazi wala utashi wao. Pia, ukitaka kujua mwenye mapenzi aone, jiulize ni visa vingapi wanandoa waliopeanda haswa walipoachana au kuuana baada ya mmojawapo kumtendea mwenzie mabaya? 
            Kuna kisa cha wanandoa wawili ambapo mke alikuwa si mzuri wa kuvutia ikilinganishwa na mumewe ambaye alimpenda mkewe vilivyo. Hata hivyo, kwa kujua anapendwa, mke alipata msukosuko wa ndoa akatembea na mganga wa kienyeji. Pamoja na mapenzi makubwa yaliyovutia wengi, mume alimuacha mkewe bila hata kumpa nafasi ya kujitetea. Kwa ufupi ni kwamba mwenye mapenzi anaona tena mambo mengine ambayo katika hali ya kawaida huwezi kuyaona wala kudhania yanaweza kuonekana. 
        Kisa kingine ni cha jamaa tunayemfahamu mwenye ulemavu wa macho. Ndugu zake walimtafutia mke toka nchini kwao kuja Kanada bila kumwambia ukweli kwa vile aliwahakikishia kuwa anampenda yule Bwana. Kufanya mambo kuwa magumu zaidi, walimuonyesha picha ya mdogo mtu badala ya muoaji mwenyewe wakiamini akifika Kanada, atazubazwa na uzuri na hali nzuri ya maisha. Pamoja na kuwaonya kuwa walipaswa kumueleza mchumba mtarajiwa kuwa ndugu yao alikuwa na changamoto ya kutoona, hawakufanya hivyo wakiamini mtarajiwa akifika asingeweza kumwacha mtu aliyemfadhiri kuja Kanada. Waliogopa kumwambia wakiogopa kuwa mtarajiwa angeweza kutumia fursa hii kujia Kanada kama ambavyo wengi wako tayari hata kuzama bahari au kudhalilishwa na wasafirishaji binadamu ilmradi wafike majuu. Na kweli, huyu bibie alipata fursa kuingia Kanada kama ilivyotokea. Jamaa akiwa amefurahi kuwa amepata jiko na ndugu zake kadhalika wakifurahi wamemhifadhi ndugu yao, mama alipofika, alilala siku mbili. Kwa sababu mwenye mapenzi anaona, yule mama alishangaa na kuchukia baada ya kugundua kuwa kumbe yule aliyeonyeshwa hakuwa mtarajiwa wake. Alikaa kimya ili lau ajipe muda wa kupokea hali ile iliyomfadhaisha sana.
         Siku ya tatu alisema bila aibu wala kumuogopa Mungu kuwa hawezi kuolewa na kipofu! Je hapa tatizo ni nini? Kuna matatizo mawili. Kwanza, yule mama alikuwa akitarajia mumewe angekuwa mwenye kuwa timamu kwa sababu hakuambiwa kuwa alikuwa na changamoto au tuseme ulemavu wa macho. Pili, yule mama alikuwa na matarajio tofauti na hali aliyoikuta. Alifichwa ukweli ili kuamua kama alikuwa tayari kuishi naye au la pamoja na mapungufu yake.
Kufupisha hadithi ndefu, tunapoandika, hatujui huyu bibie aliishia wapi zaidi ya kujua kuwa alikataa kuishi na mumewe licha ya kumdhanimi kwa matarajio kuwa wangeungana kupiga maisha majuu. Alichoacha ni sononeko kwa yule mume na nduguze.
Turejee kwa mwenye mapenzi haoni. Anaona. Hebu jiulize. Ulipokuwa ukimtafuta au kutafutwa na mwenzako ni vitu gani ulikuwa unaangalia kwa vile ndivyo vilikuwa vigezo vyako vilivyokuvutia? Mwenye mapenzi anaona tena sana. Wakati mwingine anaona visivyoonekana. Vinginevyo wafitini wasingevunja au kuyumbisha uchumba hadi Waswahili wakaja na busara kuwa ficha uchumba na kutangaza ndoa kwa kuhofia mambo yanayoweza kuzushwa na wafitini na yakapewa umuhimu hata kama ni fitina na uzushi. Ndiyo maana tuna sifa na vitu vya kupatikana kwenye yule unayetaka kuoana naye. Ingekuwa hivyo basi kusingekuwapo na kuwahusisha jamaa kumuangalia na kumpima mtarajiwa wako. Unawaonyesha ili iweje kama siyo kutaka kusikia wanamuonaje? 
J            amaa mmoja nchini Saudia aliona picha ya msichana mrembo wa kimisri aliyekuwa anatafuta mchumba mtandaoni. Alimpenda na kuridhika na sura yake kiasi cha kutoa mahari dola za kimarekani laki tano. Kitu ambacho msaudia hakujua kuwa kumbe yule msichana aliyekuwa ameweka picha yake kwenye mtandao alikuwa na dada yake mwenye makengeza ambaye hakuwa amebahatika kuolewa kutokana na mwonekano wake. Jamaa baada ya kulipa mahari ilifika siku ya kwenda Misri kuchukua jiko. Alipofika akiwa na hamu ya kumuona mkewe, alionyeshwa dada mtu. Jamaa alipomuona, aliruka futi mia na kusema yule aliyeonyeshwa hakuwa yule aliyemuona na kumpenda. Kufupisha hadithi ndefu, jamaa alitaka arudishiwe fedha yake haraka. Wake walitia ngumu. Jambo hili lilifikishwa serikalini baada ya Saudia kutishia kuvunja uhusiano na Misri kama raia wake asingerudishiwa fedha yake. Je kama mwenye mapenzi haoni, si huyu Msaudia angebeba alichopewa?
        Mwisho, je mpaka hapa, bado unaamini mwenye mapenzi haoni au anaona sana tu? Kwa ufupi, mwenye mapenzi anaona sana tu. Siyo kila usemi unapaswa kuchukuliwa bila kufikiri hata kuhojiwa kama ilivyo dhana hii potofu kuwa mwenye mapenzi haoni wakati anaona sana.
Chanzo: Mwananchi Alhamis iliyopita.

Ndoa inahitaji maandalizi kisaikolojia

Kama ilivyo kwenye uanachama wa chama au taasisi yoyote, anayefanya hivyo lazima, kwanza ajielimishe aweze kujiunga na chama au taasisi inyomfaa kutokana na uchaguzi, malengo, na matarajio yake. Kufanya hivyo, mhusika anapaswa kumjua anayetaka au kutarajia kumuoa au kuolewa naye. Tofatuti, mwanachama wa vyama vingine au makundi tofauti na ndoa, anaweza kuondoka wakati wowote na kujiunga na vingine. Kwenye ndoa ni tofauti. 
        Wengi huingia wakitarajia maisha yenye furaha na mafainiko hadi kifo kiwatenganisha. Hata hivyo, ambao hushindwa na kuachana jambo ambalo mwanzoni mwa kuingia mahusiano haya huwa si moja ya malengo wala matarajio ya wahusika. Hili linaweza kuepukika kama wahusika watafanya utafiti wa kutosha na kujielimisha kuhusu wenzi japo na majaliwa yana nafasi yake. 
Lazima wahusika wajue ubora na udhaifu wao, welewa hata ujinga wao kama binadamu kwenye safari hii yenye milima na mabonde na misukosuko lukuki. Kuyajua haya hutoa fursa kwa wahusika kujiandaa kisaikolojia na kulhali kuishi pamoja wakifundishana na kuelimishana somo la maisha.             Nani anaajiriwa bila kutakiwa kuonyesha taaluma, akili, uzoefu, na uwezo wa kufanya kazi anayomba? Tusikubali kuingia au kuingizwa kwenye ndoa bila maandalizi na utayari. Wahusika wasikilize roho zao na sauti zao za ndani bila kulazimishwa au kushawishiwa na yeyote kwani ni wao watakayoyaishi maisha wanayoingia.                         Tunasema hivi kutokana na kuzuka mtindo kwa baadhi ya wazazi kuwalamisha watoto wao waolewe au kuoa watu fulani kwa kuangalia vitu kama vile mali na wadhifa wa familia watokazo wasijue vinaweza kuwa chanzo cha maanguko kama wahusika hawakuchagua wenyewe. Hili ni muhimu kwa sababu ndiyo wao watakaofurahia au kuumia mambo yakienda yalivyopangwa au ndiyo siyo. 
        Kama tulivyosema hapo juu, tofauti na chama au taasisi nyingine ambako mhusika anaweza kuhama na kujiunga bila kuumia au kusababisha matatizo kwake binafsi na wengine, ndoa ni tofauti kabisa. Ikishindikana au kutofanikiwa, huleta hisia hafifu kuwa ndoa ni kifungo au ndoana.
         Mfano wa pili, huwezi kununua gari na kuanza kuliendesha kabla ya kujifunza namna ya kufanya hivyo. Hii hutokana na hatari ima ya kuiparamia gari na kusababisha ajali hata kifo au kununua bovu ukaambua hasara. 
            Kwa Waafrika walio wengi, kabla ya kuoa au kolewa au kuoana kama wasemavyo siku hizi, kulikuwa na kipindi maalumu cha kujifunza taasisi hii, nini vinahitajika, havihitajiki, mbinu na miiko ya kuifanikisha na kuifaidi. Pia, kulikuwa na kipindi cha mhusika na wanafamilia yake kumchunguza mtarajiwa ili kujiridhisha kama anakidhi matarajio na viwango vyao. Kwenye jamii nyingi, walichunguza vitu hatarishi vya kifamilia kama magonjwa ya kuambukiza, tabia mbaya kama uchawi, ulafi, kujinyonga, na vingine kama hivyo kulingana na kabila au jamii wanamotoka wahusika. Kwa Waswahili, kulikuwa na jando kwa wanaume na unyago kwa wanawake. 
        Tunaposema Waswahili, hapa tumaanisha Watanzania ambao lugha yao ya taifa na kitambulisho ni Kiswahili au Waafrika kwa ujumla kwa vile tunafanana kisura na kimila ukiachia mbali kuwa Kiswahili ndiyo lugha kubwa pekee ya Kiafrika inayoongelewa zaidi Afrika na ulimwenguni. Hivyo, dhana ya Waswahili inaweza kumaanisha Watanzania hata Waafrika kwa ujumla kulingana na anayeitumia na anavyokubaliana nayo.
        Kitu kingine muhimu ni kujua historia, tabia, sura, umri, na utayari wa anayetaka kufunga ndoa. Kisheria, kuna umri unaoruhusiwa kufanya maamuzi. Hivyo, wahusika wasifichane umri wala tabia zao. Vitu hivi unaweza kuvificha kwa muda. Baadaye vitafichuka hasa ikizingatiwa kuwa unaingia kwenye uhusiano wa kudumu. Kuna kisa cha mwanandoa mmoja aliyemdanganya mwenzie umri wake. Walifunga ndoa na wakaishi kwa furaha tele japo kitambo. Tatizo katika kuficha umri, mhusika hakuwaambia au hakuwa na uwezo wa kuwaambia wote wanaomfahamu. Siku moja wanandoa hawa wakiwa hawana hili wala lile, mwanandoa aliyemficha mwenzie umri alipatikana. Mara nyingi, umri huwa tatizo kwa wanawake kuliko wanaume. 
        Mume wa mhusika akiwa kazini, aliajiriwa mwanamke mmoja akiwa mfanyakazi mwenzao mpya. Katika kutamjitambulisha kwa wafanyakazi wenzake, alisema kuwa anatokea sehemu fulani ambacho kilikuwa ni Kijiji cha mke wa mwanandoa huyu. Baada ya kumaliza utambulisho wa kiofisi, mwanandoa huyu alimwendea yule mfanyakazi mpya. Walisabahiana kwa uchangamfu na akamuuliza moja kwa moja, “unamjua fulani?” Yule mfanyakazi mpya alijibu, “fulani, alimtaja jina. Namfahamu tumesoma wote. Na isitoshe tumetofautiana siku mbili kuzaliwa.” 
              Mwanandoa alimuuliza, “una maana ulizaliwa tarehe” alitaja tarehe. Yule mfanyakazi mpya aliyeonekana dhahiri kuwa mkubwa ikilingaishwa na mkewe alijibu. “Ndiyo, wote tulizaliwa mwaka” aliutaja. Yule jamaa alitabasamu ingawa aligundua kuwa mkewe alikuwa mkubwa miaka sita zaidi ya umri aliokuwa amemwambia. Alianza kujiuliza “je amenificha mangapi na kwanini?”
            Kukatiza kisa kirefu, mwanandoa alimkabili mwenzie na kumuuliza. “Hivi una cheti cha kuzaliwa?” Mwenzake aliuliza, “unataka cheti cha kuzaliwa cha nini?”
Tumalizie. Ndoa inahitaji maandalizi kisaikoloji, kiakili, na kulhali.
Chanzo: Mwananchi jana.

Sunday, 21 July 2024

Mwenye mapenzi anaona tena sana

Kuna imani au tuseme usemi kuwa mwenye mapenzi haoni. Je kweli mwenye mapenzi haoni hata kama macho anayo? Je ukweli ni upi haoni au anaona tena sana? Ingawa “mwenye mapenzi haoni” ina tafsiri nyingi kutegemea na hali yaliyomo mapenzi, ukweli ni kinyume. Tutatoa sababu zifuatazo:
        Kwetu mwenye mapenzi lazima aone na aone kwelikweli. Utawezaje kuujua uzuri na mvuto wa mwenzako kama kweli mwenye mapenzi haoni? Ingekuwa hivyo, watu wengi wenye changamoto za aina mbalimbali za ulemavu ambazo ni kazi ya Mungu wasingenyanyapaliwa, kukataliwa, na wengine kutoolewa kabisa au kuachika tokana na changamoto ambazo siyo matokeo ya kazi wala utashi wao. 
            Pia, ukitaka kujua mwenye mapenzi aone, jiulize ni visa vingapi wanandoa waliopeanda haswa walipoachana au kuuana baada ya mmojawapo kumtendea mwenzie mabaya? Kuna kisa cha wanandoa wawili ambapo mke alikuwa si mzuri wa kuvutia ikilinganishwa na mumewe ambaye alimpenda mkewe vilivyo. Hata hivyo, kwa kujua anapendwa, mke alipata msukosuko wa ndoa akatembea na mganga wa kienyeji. Pamoja na mapenzi makubwa yaliyovutia wengi, mume alimuacha mkewe bila hata kumpa nafasi ya kujitetea. Kwa ufupi ni kwamba mwenye mapenzi anaona tena mambo mengine ambayo katika hali ya kawaida huwezi kuyaona wala kudhania yanaweza kuonekana. 
        Kisa kingine ni cha jamaa tunayemfahamu mwenye ulemavu wa macho. Ndugu zake walimtafutia mke toka nchini kwao kuja Kanada bila kumwambia ukweli kwa vile aliwahakikishia kuwa anampenda yule Bwana. Kufanya mambo kuwa magumu zaidi, walimuonyesha picha ya mdogo mtu badala ya muoaji mwenyewe wakiamini akifika Kanada, atazubazwa na uzuri na hali nzuri ya maisha. 
            Pamoja na kuwaonya kuwa walipaswa kumueleza mchumba mtarajiwa kuwa ndugu yao alikuwa na changamoto ya kutoona, hawakufanya hivyo wakiamini mtarajiwa akifika asingeweza kumwacha mtu aliyemfadhiri kuja Kanada. Waliogopa kumwambia wakiogopa kuwa mtarajiwa angeweza kutumia fursa hii kujia Kanada kama ambavyo wengi wako tayari hata kuzama bahari au kudhalilishwa na wasafirishaji binadamu ilmradi wafike majuu. Na kweli, huyu bibie alipata fursa kuingia Kanada kama ilivyotokea. 
            Jamaa akiwa amefurahi kuwa amepata jiko na ndugu zake kadhalika wakifurahi wamemhifadhi ndugu yao, mama alipofika, alilala siku mbili. Kwa sababu mwenye mapenzi anaona, yule mama alishangaa na kuchukia baada ya kugundua kuwa kumbe yule aliyeonyeshwa hakuwa mtarajiwa wake. Alikaa kimya ili lau ajipe muda wa kupokea hali ile iliyomfadhaisha sana.
         Siku ya tatu alisema bila aibu wala kumuogopa Mungu kuwa hawezi kuolewa na kipofu! Je hapa tatizo ni nini? Kuna matatizo mawili. Kwanza, yule mama alikuwa akitarajia mumewe angekuwa mwenye kuwa timamu kwa sababu hakuambiwa kuwa alikuwa na changamoto au tuseme ulemavu wa macho. Pili, yule mama alikuwa na matarajio tofauti na hali aliyoikuta. Alifichwa ukweli ili kuamua kama alikuwa tayari kuishi naye au la pamoja na mapungufu yake.
Kufupisha hadithi ndefu, tunapoandika, hatujui huyu bibie aliishia wapi zaidi ya kujua kuwa alikataa kuishi na mumewe licha ya kumdhanimi kwa matarajio kuwa wangeungana kupiga maisha majuu. Alichoacha ni sononeko kwa yule mume na nduguze.
        Turejee kwa mwenye mapenzi haoni. Anaona. Hebu jiulize. Ulipokuwa ukimtafuta au kutafutwa na mwenzako ni vitu gani ulikuwa unaangalia kwa vile ndivyo vilikuwa vigezo vyako vilivyokuvutia? Mwenye mapenzi anaona tena sana. Wakati mwingine anaona visivyoonekana. Vinginevyo wafitini wasingevunja au kuyumbisha uchumba hadi Waswahili wakaja na busara kuwa ficha uchumba na kutangaza ndoa kwa kuhofia mambo yanayoweza kuzushwa na wafitini na yakapewa umuhimu hata kama ni fitina na uzushi. Ndiyo maana tuna sifa na vitu vya kupatikana kwenye yule unayetaka kuoana naye. Ingekuwa hivyo basi kusingekuwapo na kuwahusisha jamaa kumuangalia na kumpima mtarajiwa wako. Unawaonyesha ili iweje kama siyo kutaka kusikia wanamuonaje? 
        Jamaa mmoja nchini Saudia aliona picha ya msichana mrembo wa kimisri aliyekuwa anatafuta mchumba mtandaoni. Alimpenda na kuridhika na sura yake kiasi cha kutoa mahari dola za kimarekani laki tano. Kitu ambacho msaudia hakujua kuwa kumbe yule msichana aliyekuwa ameweka picha yake kwenye mtandao alikuwa na dada yake mwenye makengeza ambaye hakuwa amebahatika kuolewa kutokana na mwonekano wake. Jamaa baada ya kulipa mahari ilifika siku ya kwenda Misri kuchukua jiko. 
        Alipofika akiwa na hamu ya kumuona mkewe, alionyeshwa dada mtu. Jamaa alipomuona, aliruka futi mia na kusema yule aliyeonyeshwa hakuwa yule aliyemuona na kumpenda. Kufupisha hadithi ndefu, jamaa alitaka arudishiwe fedha yake haraka. Wake walitia ngumu. Jambo hili lilifikishwa serikalini baada ya Saudia kutishia kuvunja uhusiano na Misri kama raia wake asingerudishiwa fedha yake. Je kama mwenye mapenzi haoni, si huyu Msaudia angebeba alichopewa?
        Mwisho, je mpaka hapa, bado unaamini mwenye mapenzi haoni au anaona sana tu? Kwa ufupi, mwenye mapenzi anaona sana tu. Siyo kila usemi unapaswa kuchukuliwa bila kufikiri hata kuhojiwa kama ilivyo dhana hii potofu kuwa mwenye mapenzi haoni wakati anaona sana.
Chanzo: Mwananchi leo.


Watufilisio wamefilisi, tumefilisika wamefilisika!

“Kufilisika kubaya. Jamanini kufilisika kubaya. Heri ufilisike mali kuliko akili. Heri ung’atwe na dogi kuliko kung’ata dogi.” Hayo ni maneno ya wimbo nilioutunga zamani nikakosa vifaa ukaishia kwenye makabrasha. Tuachane na mistari ya dhahabu ya zama za dhahabu. Naami mafyatu wote mnajua maana ya kufilisika. Niwasaidia wasiojua. Ni kuishiwa kitu chochote iwe akili au njuluku hata sera. Leo nitaongelea namna mafyatu wanavyofilisiwa na wanaowafilisi wanaopaswa kuwafilisi ili sote tufilisike na watufilisio wakiwamo ngoma droo ili kutenda haki.
Kunyaka mantiki ya somo, nitafudisha kupitia maswali kama ifuatavyo:
Mosi, je unapoteua cahawa kuwa mlongaji wa chata lako huligeuzi chata kuwa Chata cha Machawa (CcM)? Niliwaonya tusifanye mchezo na waharifu mafyatu wakadharau. Yako wapi sasa? Si tuliweka kikaragosi kikafyatufyatuka kikitaka kutubomoa eti kwa kujijenga baadaye eti kichukue ulaji wangu kama rahis wa mafyatu. Yametukuta mafyatu. Juzi katika kijiwe chetu cha uongozi si tukapendekeza fyatu mmoja aliyewahi kupatikana jinai ya kuteka na kuua mafyatu wenzake. Jamaa huyu chawa na changu kisiasa alijipenyeza, akapenya, na tukapenyeka tukamteua kuwa mlongaji wa Chama Cha Mafyatu (CCM). Naomba msichanganye CCM letu na nambari one ya twawala. Huko sipo. 
        Kufilisika nifundishao hauwahusu hao, kwani, walifilisika zamani machawa yalipowanyonya hadi wakaonda hata upstairs hadi wakawa wanalindwa na mbwa aliyekonda utadhani makondakonda sorry makandokando ya mikweche ya akina Daodi, Alubati, na Buushit.
Pili, unapofungulia mbwa, tena mwenye kichaa cha dog akawang’ate mafyatu usijue anaweza kukung’ata hata wewe, unategemea nini? Je hapa hujafilisika kisiasa? Je ulishajiuliza itakuwaje dogii akiamua kufilisika kama mwenyewe na kukung’ata wewe umfugaye? Hii huitwa mbwa kula mbwa kwani mbwai mbwai. Je unajua kuwa hizi ni baadhi ya dalili za kufilisika pale mwenye mbwa unapotegemea mbwa akulinde na kukuhakikishia usalama hata kukubalika kwako kwa mabavu wakati mbwa ni mbwa atabwabwaja na kufanya uumbwa? 
        Je unaambua nini kwenye ushauri huu wa bure toka kwa gwiji Dk, Profesa, Alhaji, Mhashamu, His Excellency, His Eminence, HH etc. Fyatu Mfyatuzi bin Mfyatuaji bin Mfyatukage wa Mfyatulizi mwana wa Mfyatukizi mjukuu wa Fyatuafyatua mwana wa Mfyatuizi? Naona yule anashangaa na kutikisa kichwa. Hujui naweza kutaja majina elfu na ushei ya kizazi changu kama kilivyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu ingawa lilibadilishwa likawekwa la ka jamaa toka Mashariki ya nonihino? 
        Tatu, wewe unayeendelea kufanya makosa kuendekeza mbwa ukidhani atakuletea amani na usalama hata kwa kuwang’ata wachapakazi wako? Huku ndiko kufilisika kunakoongelewa hapa. 
        Nne, unapompa bangi mbwa mwenye kichaa tayari kung’ata wabaya au wapingaji wako  kwa sababu ana uzoefu wa kung’ata, kwanini nao wasijitoe akili wakamng’ata ikawa habari halafu wakakufyatua nawe na jibwa lako fyatu? Huku ndiko kufilisika kunakotufilisi kwa kufilisiwa na hawa waliofilisika wakatufilisi nasi.
        Tano, ili kuonyesha hawajafilisika, kwanini mafyatu wasinyongelee mbali hili jibwa ili wasing’atwe na kuendekeza madogiii? Huu si wakati wa madogii kutuchezea na kutung’ata kama kipindi kile walipokuwa wakibweka na kung’ata huku aliyewafuga akizidi kuchekelea na kuwanenepesha tena kwa njuluku na mamlaka ya mafyatu wafyatuliwa na kufilisiwa.
        Sita, mafyatu walipoona wanene tumempitisha huyu dogi, walisema wazi kuwa kipindi hiki ang’atwi fyatu hata mmoja. Badala yake mafyatu watang’ata hata mbwa mng’ataji. Hivi unapowaletea mafyatu mbwa, ina maana mafyatu wamekwisha au ni ile hali ya kuzidiwa na kunyonywa na chawa au kufilisika?
Saba, hivi inawezekanaje mbwa kuwazidi akili mafyatu tena wakubwa kiumri na kimaulaji? Je hapa mbwa na fyatu ni yupi au mmebalishana baada ya kufyatuka na kufilisika hadi mkaruhusu mbwa awafyatue na kuwafilisi? Je mfupa uliomshinda fisi nyinyi mtauweza?
Nane, inakuwaje mbwa anaendekezwa ili ang’ate mafyatu waliokwishafyatuka wakati tunao wanyama kibao na mabaki kibao kwa wale wanene wanaokula nyama? Kwanini wasimtupie mabaki ya milo yao badala ya kutaka awang’ate mafyatu wasio na noma na yeyote?
Baada ya kumaliza kuuliza maswali ambayo sitegemei kuletewa majibu ili yachapishwe kwa vile fyatu anayenihariri na kuruhusu hii kitu itoke hewani mafyatu wasome hataruhusu. Naye kuna siku nitamfyatua. We acha tu. Ukisoma hii, soma kimya asisikie akanifyatua nikashindwa kuwafyatua mafyatu wanaotufyatulia mimba itufyatue wasijue usawa huu, tutaifyatua kama mbaya, mbaya. Kwani mbwai mbwai kwa kimombo.
        Je tuko tayari kuendelea kung’atishwa majibwa tena yaliyochoka baada ya kujaribu hata kuwang’ata waliowakota majalalani? Inakuwaje mbwa koko anaendekezwa kiasi cha kuwazidi mafyatu wakati ananenepa kwa njuluku zao? Je kinachoendelea ni mbwa kugeuka chawa au chawa kula akanenepa na kugeuka mbwa?
Nimalizie. Kweli wametulifisi mali nao wakafilisika mawazo! Du! Kwani niko wapi?
Chanzo: Mwananchi Jumatano iliyopita.

Friday, 12 July 2024

Mwapambana na ‘Machangu’ Wapi?

Kama mwanasharia na msomi, najua madhara ya kujadili jambo ambalo ni sub judice yaani lililoko mahakamani. Hivyo, nitaongelea kasheshe la baadhi ya mafyatu wanene kunyaka, kudhalilisha, na kuwapeleka kwa pilato dada wachovu eti kwa vile ni machangu. Pamoja na kutokuwa na ushahidi wala mashiko, niseme wazi. Uchangu si kosa kisheria bali aibu. Kama madada wanauza maungo yao, matatizo au mateso gani mafyatu tunaupata ikilinganishwa na wale wanaotuibia au kutuuza jumlajumla? Nani ananunua hizo laana zao? Naona yule anatikisa kichwa. Sitetei uchangudoa. Kinachogomba nikafyatuka kwa hasira na usongo ni kubaguana, kudanganyana, kudhalilishana na kuoneana.
Kamusi ya mafyatu inafasiri. Changudoa wako aina mbili, changu na changudoa (changu mwenye madoa) wapatikanao kwa wingi baharini kuliko wengine. Ni wa kike na wa kiume kama ngurumbili walio machangu. Tofauti, samaki si malaya wala wakware, wanyonyaji, wajinga, na wachafu kama chawa. Kosa lao ni upatikanaji wao kirahisi kama changu mafyatu.
Kwangu, changu ni fyatu yoyote asiyeaminika na mchumiatumbo ahiariye kutweza hata kuuza utu wake ilmradi apate tonge. Uchangu hauna unene, unono au unyonge. Hauna usomi wala ujinga. Ni fyatu aliyeishiwa akili hata ubunifu kiasi cha kujidhalilisha ili kujaza tumbo. Changu anaweza kuwa murume au jike. Anaweza kuuza mwili wake hata watu wake. Anaweza kuwa wa kijamii au hata wa kisiasa hata kiuchumi. Kimsingi, vyangu wote ni mafyatu wa kujidhalilisha kwa kushindwa kuheshimu utu wao. Machangu na machawa hawana tofauti. Tofauti iliyopo ni kwamba machawa ni machangu wa kisiasa na vyangu ni wa kijamii. Pia,wa kisiasa huwaonea wa kijamii.
Kwanini nafyatuka kwa hasira leo? Kama nilivyofyatua hapo juu, nilishika kichwa hadi tama, nilipoona mafyatu wazima, wanene, tena machawa, sorry, machangu, sorry, wenye ulaji wakiwakamata na kuwadhalilisha machangu wenzao wachovu. Wote, kifyatu, ni machangu. Tofauti yao ni waliposimama. Huwezi kumtofautisha changu wa kisiasa kama yule aliyetimika juzi na kwenda kuramba matapishi yake na hawa wakamatwao na kudhalilishwa. Nimesemaje? Nimesema Pita yule aliyemkana Tunda Lishe, sorry, Yesu? Message sent. Pita Msigwer ni shabiki wangu. Siwezi kumuita changu japo kwenye siasa kuna uchangu unaonekana kuhalalishwa na kuheshimika wakati ni uchangu kama uchangu wowote. Wala siwezi kusema ameramba, kubwia, na kupwakia marapishi yake. Si ndiye alisifika kuiponda Fisiemu akiwa Chakudema? Yethu na Maria. Nini hii la hawla wa la quwwata illa Billah.
Turejee dhana ya uchangu. Changu awezafanya chochote asijali madhara wala utu ilmradi apate atakalo. Anaweza kutoa mwili wake ale. Anaweza kuwaibia  wamtumiao, wakware au wanasiasa kama ambavyo mtashuhudia msimu huu wa usanii na uchawa kuelekea kwenye uchakachuaji. Mtawaona mafyatu wanene msiowezawadhania wakifanya uchangu kisiasa kwa vile ni halali kisheria. Kama nilivyofyatuka hapo juu, uchangu ni uchangu uwe wa kisiasa, kisanii, au kingoni. Changu avaaye vimini na avaaye suti au Tshirt za vyama wote vyangu. Changu atembea pekupeku na yule apandaye mashangingi na mashankupe wote vyangu. Nakazia. Changu ni changu awe mnene au mnyonge. Uchangu ni kama magonjwa mengine. Hayabagui. Tofauti ni kwamba uchangu ni ugonjwa wa kujitakia sawa na ujinga au imani kibubusa.
Uchangu ni kujiuza wewe na utu wako. Uchangu una sura nyingi tena mbaya. Unaweza kuunganisha uchangu na ukosefu wa maadili au upigaji madili. Wasomi wenzangu wanaoingia mikataba hatarishi kweli si machangu kimaadili na kiuchumi? Je hawa wanaotuibia kila uchao si machangu walio tayari hata kuumiza wenzao kama changu anavyoweza kumtilia mteja madawa ya usingizi kwenye kinywaji amfyatue uchache na rununu na kuishia? Hata wanaoahidi wasiyotekeleza na kupata kura ya kula ni machangu kisiasa. Wale wanaoruka viama kama daladala ni machangu tu. Heri uwe fyatu kuliko kuwa changu. Heri uwe fyatu kuliko kuwa chawa.
Natoa ujumbe mahsusi kwa wanaopoteza njuluku na muda vya mafyatu kuwinda na kukamata machangu. Waache uchangu. Kama watakamata basi wakamate machangu wote wa kimaadili na kisiasa. Uchangu ni uchangu. Unapaswa kushughulikiwa kwa namna na nguvu sawa bila kubagua wapi wa kukamata na wapi wa kukaribisha hata kuandalia halfa na kutangaza kwenye runinga wasijue nao ni uchangu tu. Nashauri, kuanzia leo, kuwe na usawa katika uchangu na ushughulikiwavyo. Mfano, penye machangu wa kike wapo wa kiume kwani wanafanya pekee. Dhana ya ukahaba vivyo hivyo. Kahaba ni wanawake na wanaume. Huko leo siendi japo ukahaba na uchangu ni mapacha. Tofauti ni matumizi yake hasa usawa huu wa kushitakiana hata kunyamazishana. 
Tumalizie kwa kuuliza. Mwapambana na changu wapi kulingana na mchanganuo huu? Woooi! Kumbe sijaenda baa sorry, ofisini, sorry, sokoni, sorry, Sinzer kuona vyangu!
Chanzo: Mwananchi Alhamis


Ndoa Zote Zina changamoto


Ndoa zote, sawa na taasisi yeyote ihusishayo binadamu zina chagamoto. Kinachotofautisha mafanikio na maanguko ya ndoa ni namna ya kuzikabili na kupambana na changamoto. Zinapotokea changamoto, jambo ambalo haliepukiki katika ndoa na maisha kwa ujumla, lazima wanandoa, kwanza wazikubali. Pili, wasisome na kuzielewa ili kuzitafutia majibu na ufumbuzi sahihi na kwa wakati. Tatu, wasione kama ni kitu kipya au cha ajabu. Hawa wote mnaona kama wamefanikiwa ima kitaaluma, vyeo, hata mali, bado ndoa zao zina changamoto sawa na binadamu wowote.
         Hivyo, changamoto katika ndoa ni jambo la kawaida na la lazima. Malkia wa Uingereza Elizabeth alisifika kwa ukubwa na hadhi ya mamlaka yake licha ya kuwa na changamoto katika ndoa yake. Changamoto ya kwanza ilitokana na mumewe Philip kupenda vimwana. Pili, changamoto nyingine ilitokana na kuvunjika kwa ndoa za watoto wake wote wa kike na kiume mbali na kashfa zilizowahusu. Cheo, mali au mamlaka ya mtu havifanyi awe na ndoa iliyofanikiwa. Hivyo, hata rais, profesa, milionea, wote wana changamoto katika ndoa zao. 
        Mfano, jarida maarufu la Marekani la the Washington Post (Desemba 25, 2017) https://www.washingtonpost.com/news/retropolis/wp/2017/12/16/fact-checking-the-crown-is-prince-phillip-a-total-jerk/ lilifichua kuwa Mwana wa mfalme. Philipo ambaye “hakuwa mwaminifu katika ndoa wa kiwango chake. Kwa miaka mingi, alikuwa akihusishwa na wanawake mbalimbali.” Je changamoto za ndoa ya Malkia zilijificha vipi?       
        Kwanza, malkia hakuwahi kulalamika au kutangaza mgogoro kwa kujua madhara yake kwake binafsi na cheo chake. Alitunza siri. Pili, waingereza wanasifika kwa unafiki na usiri wao. Hivyo, hawakutaka kumuaibisha kiongozi wao.
Mbali na Malkia wa Uingereza taifa linalojidai kufuata taratibu za kimila kwa kiwango cha juu, Ghengis Khan (1162–1227) anasifika kama mfalme aliyejenga himaya kubwa na yenye nguvu kuliko zote zilizowahi kutokea duniani. 
        Hata hivyo, alikuwa na udhaifu kingono. Mpaka anakufa, kuna taarifa kuwa alikuwa na watoto 44 aliowazaa na wanawake mbalimbali tena kwa kuwabaka. Kwa kuwazaa watoto wengi tena kwa njia hii, mke wake Khan aliyeitwa Hö’elün, unadhani alikuwa na changamoto kiasi gani hasa ikizingatiwa kuwa aliyekuwa akimkosea wakati wa uhai wake alikuwa na mamlaka kuliko mtu yeyote? Je ni wangapi wenye fedha, taaluma, na mamlaka wenye udhaifu huu? Ajabu, viumbe dhaifu na wadogo ukilinganisha nao kama vile njiwa, wanawazidi ufanisi katika hili. 
        Una habari kuna wanyama ambao wakioana ndo wamemaliza hadi watenganishwe na kifo wakiwa na mapenzi na uaminifu wao? Mjusi wapatikanao huko Australia waitwao shingleback au bobtail or Australia sleepy Lizards wanasifika kwa kuwa waaminifu kiasi cha kuishi na kufa bila kuchepuka. Basi, tuwapeni maua yao. Mbali na mijusi hao, kuna samaki waitwao diploozoom paradixum ambao nao wanaishi pamoja hadi kufa kwa sababu wawili wanapoamua kuwa kitu kimoja hubaki hivyo hadi kifo kiwatenganishe. Wengine ni tumbusi weusi waitwao kwa kimombo coragypas atratus. Hawa jamaa ni po asana. Katika kuzaa na kulea husaidiana kwa usawa tofauti na wanadamu na viumbe wengine waliolewa mfumo nyonyaji dume.
        Kwa ufupi, uzinzi na ukosefu wa uaminifu katika ufalme wa Uingereza, sawa na wengine waliofanikiwa kifedha, kimamlaka, na hata kitaaluma ni kitu cha kawaida. Unaweza kukuta tajiri mkubwa akiyumba katika ndoa huku maskini hata walemavu wakitanua na kuifaidi ndoa. Ndoa haina daktari, rais, profesa wala mwanasayansi. Ni taasisi ambayo imewakwaza wengi na kuwaenzi wachache. Helen Sirleaf na Mary Banda marais wa zamani wa Liberia na Malawi mtawalia, pamoja na urais, mafanikio na ukubwa wa nyadhifa zao waliachika. Pamoja na kuwa kiongozi mwenye nguvu sana duniani na anayeogopewa, Rais wa Urusi, Vladmir Putin alishindwa na ndoa kiasi cha kuishi kiseja bila kuta. 
        Kadhalika Rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi, aliishi bila mke kwa muda wote aliokuwa madarakani. Hapa hatujagusia watu maarufu na wenye ushawishi sana duniani waliooa na kuacha baada ya taasisi hii kuwapiga chenga tokana na sababu mbalimbali zilizo wazi na za siri. Ngugi wa Thiong’o (Kenya) na Wole Soyinka (Nigeria), pamoja na umahiri wao katika liwaya na uandishi walitaliki. waliachika. Wole Soyinka (Nigeria), watangazaji wa kimataifa kama vile Larry King (CNN), Dana Bash, Christiane Amanpour (CNN), matajiri kama vile Bill Gates, Elon Musk na wengine walivyoshindwa katika ndoa zao pamoja na kufanikiwa kifedha na kiuchumi. 
        Hili linatufundisha kuwa ndoa ni taasisi ya ubinadamu inayopaswa kuukubali na kuushughulikia ubinadamu na udhaifu wake. Hakuna wanandoa ambao ni malaika. Wapo hata walioogopa kuoa kama Plato, baba wa falsafa wa Kigiriki, Ludwig Beethoven, bingwa wa kupiga piano, Nicola Tesla mvumbiuzi wa kimarekani na William James Sadis aliyeaminika kuwa na kiwango kikubwa kiakili, pamoja na umahiri wao, waliishi na kufa wasera. Ndoa haina tajiri wala maskini, ukubwa wala udogo, uzuri au ubaya. Ndoa siku zote ni ndoa na lazima itakuwa na changamoto hata iwe imefanikiwa kiasi gani. Bill Gates, Elon Musk, Jeff Bizos, Reginald Mengi, pamoja na ukwasi wao, walishindwa hadi kutalakiana na wenzi wao.
          Tumalizie kusema kuwa kila ndoa ina changamoto yake iwe ya mkubwa au mdogo. Muhimu ni kupambana nazo kiakili na kwa usiri ili kulinda ndoa husika.
Chanzo: Mwananchi.

Wednesday, 3 July 2024

Mkimbinafsisha Bi Mkubwa Wangu Naua Mjue


Mtukufu Dk. Rahis, msikivu, mwenye maono, ndoto, uthubutu, ukimya, nk., naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, rahis, du! A’udhu billahi min ash-shaytaan-ir-rajeem. Nimemsahau Mtume! Naona yule anshangaa. Kwani nazusha? Wanagapi, sijui chawa, sijui kunguni, wakianza kuchonga wanafanyahivyo kwa maangamizi yao na mafyatu wao?
Nasikia kila mara rahis akisifiwa kuwa na ‘maono’ tena yasiyooneka. Kupitia maono, amegawa, sorry, binafsisha bahari, bandari, barabara, mbuga za waanimo, n.k. kama ni kweli. Hii inantisha kwelikweli. Naomba leo nifyatue kitu. Hivi huyu Bi Mkubwa ni Mungu, muungu, malaika, hata ntume? Hakosei? Je hizi sifa za kweli au kupakana mafuta kwa ngongo wa chupa au uchawa na ukunguni wa kutumia matumbo kufikiri badala ya vichwa ili kujaza matumbo?
Nasikia Bi Mkubwa ametenda ‘maajabu.’ Je ni maajabu kweli katenda au ni ajabu kusema katenda? Kamwaga njuluku. Mafyatu wanazipata? Kamwaga kiasi gani na kwa yupi?  Nasikia. Kamwaga pikipiki. Tunahoji ni za nini na hiyo njuluku ameitoa wapi au kuipataje na anategemea kupata nini na kwanini sasa tunapoelekea kwenye uchakachuaji wa uchaguzi? Ananunua nini? Ajabu, wakati rahis akitoa pikipiki kwa kila nkoa bwerere, akina maza wenzake wajawazito wanajifungulia nje ya zahanati! Mwe! Kwani hajui adha ya ujauzito na machungu ya kujifungua? Hayo tuyaache.
         Je rahis ni tajiri kiasi gani na nini chanzo cha ukwasi, ‘huruma na upendo’ hivi, ni vya nini, na anategemea kupata nini? Mafyatu tukienda hospitali tunaandikiwa dawa tukanunue! Maji ya mgao! Je hizi njuluku za pikipiki zingesaidia wajawazito, mafyatu, hata upatikanaji wa maji kiasi gani? Je hii njuluku ingeondosha michango ya hovyo na tozos kiasi gani? Je mikoa yetu inahitaji pikipiki wakati pesa inayopata tokana na bajeti ni kiduchu? Kwanini hatangazwi mmojawapo wa mabilionea wa kaya? Inakuwaje anakwenda ughaibuni kukopa na kubomu wakati ana ukwasi kiasi hichi? Kaya yake inashindwa hata kuendesha mangwalangwala ya mwendo kinyonga, sorry, kasi?
Tunapaswa kuwa wakweli. Pia, naye awe mkweli kwake na kwa mafyatu. Hizi pikipiki ni za nini kama hakuna namna ya kuhongana, sorry, kuchanganyana, kuelekea kwenye uchakachuaji mwakani? Kwanini sasa na si jana wala juzi? Je huyu bilionea wa sirini analipwa nshahara kiasi gani? Tukiuliza haya, mengine, na mengineyo tunakosea?
Turejee kwenye uwekezaji ambao wapingaji wanauita uchukuaji kama siyo uchakachuaji na uhujumu uchumi uliohalalishiwa na kufanywa na wanene tena kwa mlango wa nyuma. Bandari, tumewekeza. Juzi tuliona magawio la madafu 153.9 bilioni sawa na dolari za Kijoji Kichaka milioni 80! Kiduchu hichi kwa mwaka! Je waliingiza kiasi gani tujue kama kweli ni gawio au zenguo? Tunapaswa tujiulize na kuwauliza wamepata nini na wanatupa nini na nini tulipaswa kupata kisheria na kimakadirio. 
        Tusifanye magawio kuwa hisani bila kujiridhisha kuwa tunachopata ndiyo sitahili yetu badala ya kujiruhusu kupigwa na kufyatuliwa kijiiinga tu.  Fine. Je kwa namna bandari inavyotema njuluku kweli tulichopewa ni stahiki au chenga la mato? Mwaka 2016, bandari iliripoti mapato ya shilingi trilioni 13.37 (Mwananchi, Julai 6, 2016). Je kwa gawio hili walipata kiasi gani? Je walifikia, kutofikia, au kuvuka malengo? Je hiki ndicho tulichoahidiwa na kutegemea baada ya kugawiwa, sorry, kuuzwa, sorry, kubinafsishwa bandari kwa watasha wa Do Buy?
        Barabara tunawekeza baada ya kuunguza njuluku ndefu za mafyatu kuzitengeneza ili kuwanufaisha wachache? Nafyatua maswali yote haya na mengine kuepuka kuuziwa goat kwenye gunia tunajiona.
        Bahari, tumebinafsisha. Natamani na visiwa vibinafsishwe uone wazenj watakavyocharuka na kudai uhuru. Natamani hata makaburi yabinafsishwe. Bado milima na mito. Tukimaliza yote haya, tunabinafisha na machawa. Sijui nani atakuwa tayari kuwanunua wamkondeshe kama mafyatu. Tukimaliza vyote kweli kesho hamtabinafsisha hata hewa? Je Bi. Wakubwa zetu watanusurika? Wallahi, ikifikia kubinafisishana na mkamgusa Bi. Mkubwa wangu––––tate nane tate nane––––nakufa na fyatu. Hata hivo, kabla ya kumfyatua fyatu, nitamwambie Bwa. Hafith amwambie Bi Nkubwa wake ajibinafsishe kwa wamanga aone inavyouma na kuumiza. Nimesemeje? We koma!
Najua Ngolongolo akina Yero weshabinafsishwa na kuhongwa, sorry, kujengewa vibanda kule Msomea. Ukisikia maono ya maza na wamanga ndiyo haya. Si juzi niliowaona wakiwa wameishakubuhu kukata vikalio utadhani walizaliwa Tangamano. Huo nao uwekezaji au siyo. Soon, nitawaona wamanga wamepiga migolole ya kiyero wakipambana na lion. Nao ni uwekezaji au siyo.
Nimalizie. Hata kama mnatuaminisha hata kutufyatua kuwa uwekezaji ni muhimu kama kweli ni uwekezaji kama siyo uchukuaji, basi wekezeni kwa busara, tushirikishe, msituhamishe na kutuchuuza kama ilivyo sasa. Pia, wajibikeni na kueleza mnavyotumia njuluku zetu na zenu kama mnazo kama kwenye skandali ya pikipiki. Hivi Bi Nkubwa wangu bado yu salama kwa sera hizi? Hivi niko wapi? Kama naota!
Chanzo: Mwananchi leo.