The Curse of Salvation

The Curse of Salvation

Monday, 9 November 2026

Wanandoa kuweni kama mende mkutanapo na changamoto


Wengi kama siyo sote tunawajua wadudu mende, wadudu wasumbufu ila wasiokata tamaa wanapotaka lao. Ni wangapi wamewahi kuwachunguza na kudurusu tabia zao hasa linapokuja suala la uvumilivu na ung’ang’anizi katika kutatua matatizo yao hasa kutafuta chakula au malazi? Wachunguze au jikumbushe walivyo wastahimivu na wasumbufu. Vivyo hivyo, katika ndoa, ung’ang’anizi na usumbufu dhidi ya changamoto na matatizo dhidi ya ndoa ni silalha tosha ya kuyatatua bila wawili kushindwa, kutengana, au kuachana.
             Japo hawalimi, hawana mikono wala bongo kubwa kama binadamu, mende wana funzo kubwa la uvumilivu na utatuzi wa matatizo. Mende uhangaikia chakula na maisha yao bila utani. Hawachukulii maisha yao kirahisi rahisi na hawakubali kushindwa hata kama ni majaliwa yao. Hawana mchezo wala mzaha na maisha yao. Hilo, ndilo somo la kwanza toka kwa menda.
             Pili, pamoja na kuwa waharibifu, tabia ya mende ya kung’ang’ania ina somo kwa binadamu hasa wanandoa wenye kukumbwa na changamoto mbali mbali za kimahusiano. Kwa wanaojua ugumu wa kufukuza mende, watakumbuka na kujifunza kitu hapa. Mende, pamoja na udogo wao, ni wasumbufu na wasiokata tamaa hasa wanapodhamiria kufanya au kupata kitu fulani. Ukiwafukuza huku, wanatokea kule hadi wapate wanchokitafuta.
            Kwa wanandoa wanaotaka kudumisha na kufaidi ndoa yao, linapotokea jambo linalotaka kuwachonganisha au kuwatenganisha, wakumbuke mende kwa kuwa na ithibati kama wao. Yaani, msikubali kuachia au kuachana kirahisi au haraka bila kujaribu kutafuta suluhu ya tatizo.
            Wanandoa wajue. Matatizo katika jambo lolote hayaepukiki, pia huwapa fursa ya kujifunza. Wataalamu wa utatuzi wa migogoro huamini kuwa matatizo yaweza kuwa fursa kama yataangaliwa na kutatauliwa kisayansi. Isitoshe, nyinyi siyo wa kwanza wala wa mwisho kupambana na changamoto. Kila ndoa ina changamoto ambazo wahusika hulitatua na kuendelea na maisha.
            Wakati mkitafari tutakayoandika hapa, mjue kuwa duniani, tunaishi mara moja.  Si mende tu. Wadudu wote hufanya kazi kwa bidii na maarifa kwa kujua kuwa maisha yao ni mafupi sana kuliko viumbe wengine wala hawachezi wala kuchezea muda wao. Hivyo, basi, wadudu mende wanatupa funzo kubwa hapa kuhusiana na kugandana hata mnapokabiliwa na changamoto zinazotaka kuwafarakanisha. Kila siku ipitayo haitarudi maishani mwenu. Hivyo, mkilijua hili, mtaachana na imani potofu kuwa kukwepa tatizo ni suluhu wakati ni kulikuza bila sababu.
            Mnaweza kukosana ambalo ni jambo la kawaida kwa binadamu wote. Inapotokea kukosana, tafuteni namna ya kuganda na siyo kubanduka au kutengana. Kumbukeni. Wagombanao ndiyo wapatanao na majembe yalimayo konde moja, hayakosi kugongana. Hata vikombe kadhalika. Hili nivmuhimu hasa mkizingatia kuwa mlipooana, mliapa kuwa ni kifo pekee kitawatenganisha. Mende katika kutafuta riziki, ni kifo pekee kinachoweza kuwazuia kuacha kusaka wanachotaka au kutafuta. Hivyo, inapotokea tatizo, kwanza, jikumbushe kiapo hiki. Pia, mjue, yapo makubwa kuliko yenu kwa wenzenu japo hamuyajui. Wagombanao ndiyo wapatanao. wahenga walisema.
            Tushaeleza sana kuhusu usiri katika ndoa. Siyo baba leo kaja mikono mitupu, mama unaanza kulalama hata kutukana kiasi cha kumuita mwanaume suruali au kumlinganisha na kiatu. Unajua ni wangapi wanalala njaa tena mara nyingi kuliko wewe? Je, unataka aibe achomwe moto, afungwe, au kuletwa kwako mikono nyuma? Tunawajua wengi waliooana maskini na kuishia kuwa matajiri baada ya kushirikiana kama mende na kupambana na changamoto zao. Nanyi mnaweza. Ni suala la kuelewa na kuamua.
            Unapojaribu kuwafukuza mende, huwa wana mkakati mmoja. Hupanga  haraka haraka namna ya kubadilisha mbinu ili kukabili tatizo. Hawa ni viumbe hohehohe na wadogo lakini wenye uthubutu. Takribani wadudu wote wana silka hii. Wanashirikiana pale wanapopata changamoto na kuzitatua pamoja.
            Mbali na ushirikiano, wadudu ni ving’ang’anizi. Huwa hawashindwi kirahisi bila kujaribu.  Hupanga mikakati na kuitekeleza pamoja kwa lengo moja. Sasa, kama wadudu wanaweza, sisi binadamu tunashindwa nini?
            Mwisho, mende ni wadudu hohehahe na wadogo lakini wanaoweza kufanya makubwa kama kung’ang’aniana, kushirikiana, na kustahamili katika kuelekea na kulitatua tatizo. Hivyo, wanandoa igeni na kuweni kama mende mnapokutana na changamoto za maisha na ndoa.
Chanzo: Mwananchi J'pili jana.

No comments: