How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Monday, 28 July 2008
Muungano au mgongano wa Tanzania?
Kuna kipindi ukiniuliza hiki kinachoitwa muungano wa tanganyika na zanzibar ni kipi kati ya muungano na mgongano,huwa napata jibu moja. Vyote sawa.
Nitatoa sababu.
Kwanza licha ya nia nzuri ya waanzilishi wa muungano, ukweli ni kwamba muungano huu haukufuata utaratibu yaani kuanzishwa na kuridhiwa na wananchi.
Watetezi wa hili watakwambia kuwa wakati ule watanganyika na wazanzibari hawakuwa na uwezo kielimu kuhusishwa kufanya hivyo. Lakini sheria ya mahusiano huwa haiagalii kiwango cha elimu bali utashi, ulazima na kufuata kanuni.
Pia baada ya muungano kuwa umefanyika, hata baada ya wananchi kupata hicho kiwango cha elimu, bado hawakuhusishwa hadi leo licha ya kupiga makelele mengi kutaka wahusishwe.
Tatu, muungano ulioanzishwa na watawala wetu wa kwanza, umeendelea kuwa mali ya watawala huku wananchi wakilazimishwa kuukubali na kuaminishwa kuwa ni kitu bora kuwa nacho. Ndiyo muungano kama ndoa ni taasisi njema na bora. Lakini hiari muhimu. Kuimilki muhimu. Nasema wananchi wamekuwa wakiaminishwa na kulazimshwa kuukubali kutokana na watawala kuutumia kusimikana na kugawina madaraka. Mfano wa karibuni ni kwamba kama siyo kutumia kichaka cha muungano, Amani Karume asingekuwa rais wa baraza la mapinduzi. Maana kwa anayekumbuka uchafu na wizi uliotembezwa na Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi wa 2005 na hata kabla ya hapo hawezi kuona mantiki ya mtu huyu kuwa madarakani.
Hivyo kinachofanyika kwenye kivuli cha muungano, ni chama cha mapinduzi na tabaka la watu wachache kuikalia Zanzibar huku wakiishika mateka.
Muungano umeifanya Zanzibar iwe kikaragosi cha bara. Rejea jinsi Zanzibar ilivyotaka kuwa mwanachama wa OIC,ilivyofurushwa na kukaripiwa kama mkoa badala ya nchi yenye mamlaka na haki zake kwenye muungano.
Pia kumekuwa na mawazo kuwa Zanzibar inabebwa na kuwa zigo kwa bara. Ukiangalia utitiri wa wabunge na wawakilishi ilio nao Zanzibar., utaona ukweli huu. Hebu angalia kijisehemu kisicholingana hata na mkoa wa Kigoma kuwa na wabunge na wawakilishi wengi kuliko Tanganyika. Hii ni nini kama siyo kuwabagua Watanzania kwa njia ya sehemu watokako?
Hata ukiangalia kiwango cha maisha. Wakati bara kipindi cha nyuma tulikuwa tukilanguliwa umeme na TANESCO, Zanzibar walikuwa wanagawiwa umeme wetu bure! Yaani mtu wa Mtera analanguliwa umeme unaozalishwa uani mwa nyumba yake. Lakini mtu wa kilometa zaidi ya mia tatu kisiwani alikuwa akitanua kwa kuufaidi bure.
Kwa ufupi ni kwamba muungano umechakaa unahitaji kufanyiwa marekebisho lakini baada ya kupitishwa kura ya maoni kuona kama wananchi bado wanautaka au vinginevyo.
Kuna sakata la Zanzibar kutaka wabara wabebe vitambulisho wanapokwenda Zanzibar wakati wazanzibari hawafanyi hivyo wanapokuja bara. Hili linachukua nafasi ya paspoti zilizotumika muda mrefu kama alama ya ubaguzi na ukosefu wa ulinganifu na haki sawa katika muungano.
Kuna maswali muhimu ya kujiuliza kuhusiana na sakata hili kuanzia Zanzibar kwenda upande wa pili wa Muungano. Je hii ni tabia ya chako kitamu changu kichungu au ni ile hali ya Zanzibar kuona kama haifaidiki na Muungano? Maana mwanzo wa ngoma lele, kwa wenye akili, tamko hili lina maana na maanawia. Je na Bara ikiwataka wafanye hivyo wataridhika?
Je kutakishana vitambulisho kunaimarisha Muungano au kuudhoofisha? Je huu ni Muungano au Mgongano? Twambieni jamani. Je kama Wabara wataingia kwa vibali huko hao Wakenya au Waganda watakaotokea bara si watahitajika kugongesha upya kwenye pasi zao?
Je ina maana viongozi wa Zanzibar hawajui haki ya usawa kwa Watanzania ndiyo inafanya kila Mtanzania awe na uhuru wa kwenda popote na kuishi popote ndani ya Jamhuri, uhuru ambao Wazanzibari wanautumia kuliko hata hao wabara wenyewe wanaowatakisha vitambulisho? Tunadhani wanajua tena sana.
Lakini waingereza "who will get the cat out of the hat" Je Bara nayo kwa kutaka kuonyesha kuwa inajua kinachoendelea, itawataka Wazanzibari waje na vitambulisho kwa ajili ya usalama wake? Je kwa kufanya hivyo kutakuwa na Muungano tena hapa?
Je huu ndiyo mwanzo wa kuuchoka na kuanza kuupekenyua Muungano ili hatimaye wauvunje? Je Muungano ukivunjika nani atakosa nini na nani atapata nini? Hatujui nani atakuwa wa kwanza kulia! Wakati tukitafakari hayo hebu tuzingatie baadhi ya matukio na hali ambazo zina ukweli na ushahidi wa kutosha juu ya umuhimu wa Muungano, nani ananufaika nao na nani hanufaiki.
Historia ni shahidi kuwa nje ya Muungano. Hakuna mmojawapo kati ya hawa wanaotumbua marupurupu ya ukubwa atakalia kiti alichokikalia. Kwani nje ya Muungano serikali ya Zanzibar itaundwa na Chama cha Wananchi CUF na siyo CCM taka usitake.
Rejea chaguzi tatu zilizopita ambapo Baraza la Mapinduzi na serikali yake vilishapigwa buti na wapiga kura ikabidi bara iingilie kuwaokoa kijeshi. Je wakubwa hawa mara hii wamesahau au kuna sehemu wanatarajia kupata maslahi zaidi nje ya Muungano?
Tujalie hao Wabara nao wakianza choko choko wakaanza kuuliza, hivi Zanzibar ina nini cha mno kutubagua kiasi hiki? Je nani anauhitaji Muungano zaidi ya mwingine?
Je hili siyo changamoto kwa Rais Jakaya Kikwete aliyeahidi kuudumisha Muungano uliokuwa umesahauliwa na Mkapa ambaye kimsingi alibariki kila aina ya ujambazi wa kisiasa visiwani? Je atakubali kuuona Muungano unayoyoma akibakia kuonekana muongo kwa ahadi hii na sifa ya kuwa Rais ambaye chini ya utawala wake ulivunjika Muungano?
Je yaweza kuwa hawa wanaoanza na choko choko ndogo hawana la ziada zaidi ya kuutia nyufa Muungano ili hatimaye uvunjike? Je huku kwaweza kuwa kuchezea moto ambao si rahisi kuuzima? Yakhe tuambizane lau tujiandae.
Kupitia chaka la muungano wakati dunia inapambana na ongezeko la watu, wao hawana tatizo na hilo maana wana mahali pa kupeleka watu wao wa ziada.
Wakati dunia inapambana na wakimbizi wa kiuchumi, Zanzibar hawana hili tatizo maana kuna pa kukimbilia. Si kwa hayo tu, hebu jikumbushe ule mshike mshike wa 1995, 2000 hata wa mwaka juzi,walikimbilia wapi kama siyo Bara?
Hali ya kubebeshana vitambulisho ndani ya nchi moja ni vya ajabu! Je kwa kuwataka Wabara wabebe vitambulisho kwenda Zanzibar hakuwezi kutafsiriwa na Wapemba kuwa nao wawatake Wazanzibari wabebe vyao kuja Pemba? Hapa kweli kutakuwa na Muungano?
Tunakumbuka baba wa taifa Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alionya kuwa, mtaanza kusema sisi ni Wazanzibari nanyi ni Wabara.baadaye mkishatumaliza sisi mtamalizana wenyewe maana mtaanza kuwatafuta Wazanzibari na Wazanzibara miongoni mwenu.
Sie wacha twende mbele zaidi kuwa hata mkishamalizana na Wazanzibari na Wazanzibara bado kutakuwa na Wazanzipemba, nao watawataka msijihusishe nao. Hapo bado makundi ya Wazanziafrika na Wazanziarabu hawajaingia.
Hapa kinachotaka kufanyika ni sawa na kuwasha moto eneo moja la nyika kavu ambayo inaungana na nyumba yako usijue kuwa kitakachoungua si nyika kavu tu bali hata nyumba yako.
Leo waeanza na vibali, Mamlaka huru ya Anga ndani ya nchi moja. Kesho watazusha pesa na baadaye hata uraia huru. Kimsingi kama tukizingatia maana ya Tanzania kuwa ni Tanganyika kujumlisha Zanzibar, hakuna haja ya kuwa na Wazanzibari ndani ya Tanzania maana kuzaliwa kwa Tanzania kuliua utanganyika na uzanzibari.
Kama hali hii itaendelea basi watakuja kurejea Watanganyika. Hapa ndipo Mchungaji Christopher Mtikila anapoona mbali zaidi ya viongozi wetu.
Tunadhani ni wakati muafaka kwa watetezi wa haki za binadamu na mabingwa wa masuala ya Muungano kuingilia kati kuzuia mbinu hizi zisichafue hata kuua Muungano.
Kabla ya kuanza kugawana mbao,ni vizuri ama serikali ya Muungano au ya Zanzibar kutangaza mgogoro wa kikatiba mbele ya Mahakama ya Katiba ili uamuzi utolewe.
Kama siyo kuna haja ya kuepuka mizengwe ambayo badala ya kutatua matatizo ya Muungano huyalimbika ambapo wanaochafua hali ya hewa hutimuliwa na matatizo hubakia pale pale yakizaliana.
Je wakati wa serikali ya Muungano kukubali kutupa mbao kwa kukubali kuigawa nchi baada ya kuchoshwa na kutokubaliana umefika? Ila ni vizuri kukumbuka kuwa shibe mwana malevya.
Lakini kuna haja ya kujua hatima ya nchi hii ambamo kila upande unaona kama unaumizwa na kutumiwa na upande mwingine. Je haya siyo madhara na matokeo ya watu wachache kujichukulia mamlaka na kupitisha maamuzi yanayougusa umma bila kuushirikisha?
Je hii ni changamoto kuwa wakati umefika wa Muungano kupelekwa kwa wenyewe ambao ni wanachi au kuuchinja?
Kwa maana nyingine kinachofanyika ni ishara kuwa maandishi yako ukutani kuwa Muungano una mshikeli. Hivyo basi kuna haja ya kuurudisha kwa wenye Muungano ambao ni wananchi waamue njia yakuchukua kama ni kuuchinja au kuuendeleza, shauri yao maana Muungano ni watu siyo watawala na bendera zao.
Ila tutoe tahadhali kuwa ijapokuwa Muungano ni mali ya wananchi, nao wananchi kwa miaka mingi wameachwa nje ya kufanya maamuzi, wasiuchukulie kama kitu kisicho na faida bali wapewe muda wa kutafakari njia ya kuchukua kuelekea hatima ya Muungano.
Hivyo basi ni vizuri Muungano ukawa wa Watanzania badala ya watawala. Kwani siyo siri kuwa kwa sasa nchi inatawaliwa chini ya Muungano wa watawala unaoitwa Muungano wa Tanzania!
Kuna haja ya kutoa tahadhali hapa kuwa matatizo ya Muungano hayawezi kuachiwa ama kutatuliwa na watu wawili yaani Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar,ambao ni wawakilishi wawili wa Serikali bali Watanzania wenyewe kwa ujumla wao.
Tuwatoe wananchi kwenye kiini macho cha Jamhuri ya Muungano wa watawala wa Tanzania kwenda kwenye Jamhuri ya kweli ya Muungano wa watu wa Tanzania.
Je hii siyo awamu ya pili ya machafuko ya "hali ya hewa" visiwani? Historia inayo tabia ya kujirudia! Je wetu ni muungano au mgongano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?
Source: Kulikoni Julai.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment