MBUNGE wa Bushosa, Samwel Chitalilo (CCM) kwa mara nyingine ametawala kwenye vyombo vya habari. Hii ni baada ya kujaribu bila mafanikio kuwatetea marafiki na mabosi wake wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi.
Akitoa mchango wake bungeni hivi karibuni, Chitalilo ambaye hadi sasa Watanzania wapo kwenye wingu la utata kuhusu tuhuma zake za kughushi vyeti na kuwadanganya wapiga kura kama ilivyothibitishwa na Jeshi la Polisi, alidai kwa sababu Waziri wa zamani wa Miundombinu na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, hakuvunja nyumba ya mtu, hivyo hana hatia! Chitalilo huyo huyo, alikaririwa pia akitoa karipio kwa Watanzania kuacha kuwafuatafuata Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kwani hawakutenda kosa lolote.
Wanaomtetea Lowassa, wawe watu au chama, wanapoteza muda. Hakuna jinsi ya kumerejesha madarakani hata kama wanajidanganya. Hii si nchi ya mabwege kama alivyosema Dk. Harrison Mwakeyembe, na isitoshe mambo yamebadilika sana.
Alilionya taifa na Bunge kwamba linaweza kugeuka sehemu ya majungu. Kinachokera ni Chitalilo kujifedhehesha kama mbunge, ukiachia mbali wapiga kura wa Buchosa.
Kinachokera zaidi ni ile hali ya Chitalilo kulishambulia Bunge. Maana, aliyemtaka Lowassa kuwajibika ni Kamati Teule ya Bunge ambayo kama sikosei aliiidhinisha kama mbunge.
Na isitoshe kamati hii ilifanya kazi kwa niaba ya Bunge. Je, Chitalilo hayajui yote haya? Kama anayajua, ni kwa vipi anaamua kwa makusudi kulidhalilisha Bunge?
Wapo tunaohoji udhu wa Chilalilo kuwasafisha wenzake ilhali naye ni mchafu. Rejea wingu la utata kuhusu tuhuma zake za kughushi ambalo ni kosa la jinai.
Je, wabunge kama Chitalilo wanatufaa kwenye kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na dhoruba za ufisadi? Hivi tatizo la Chitalilo ni nini hasa?
Je, kujitokeza kwa Chitalilo kutoa madai ya hovyo yanayolidhalilisha Bunge, si ushahidi wa kujigamba kuwa hakuna anayeweza kumfanya kitu kwa vile chama chake chini ya dhana nzima ya kujuana na kulindana kimemkingia kifua kiasi cha kuudhalilisha hata mfumo wa mahakama wa nchi yetu?
Hivi Chitalilo angekuwa mbunge wa upinzani na akakabiliwa na shutuma za kutenda jinai hii angekuwa wapi? Je, huu si ushahidi kuwa CCM haipo kutenda haki kwa wasio wanachama wake?
Je, Chitalilo amesahau au ameponzwa na kiwango kidogo cha elimu na uelewa wa mambo? Je, ametumwa na hao anaowatetea? Mbona wamekosea kwa kumchagua kondoo mwenye madoa asiyeweza kujitetea! Je, haya si yale ya kisa cha boriti na kibanzi? Maswali ni mengi bila majibu.
Kwa bahati nzuri Mbunge wa Kyela Dk. Mwakyembe (CCM) kwa ukali na stahiki yake amejibu utumbo wa aina hii ya wabunge nyemelezi waliopo bungeni kulinda ufisadi badala ya waliowachagua na kuwatuma.
Ingawa Dk. Mwakyembe amejibu na hata kutishia kujiuzulu kama upuuzi huu utaendelea, kuna haja ya kulishinikiza Bunge litoe adhabu kwa wabunge aina ya Chitalilo.
Mbona Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA) alipopatikana na kosa dogo alipewa adhabu mara moja? Je, Chitalilo ni nani? Au kwa vile yeye ni CCM na CCM ina wenyewe, hasa mafisadi?
Hapa Spika Samuel Sitta, ana changamoto ya kupambana na wabunge wanaotumika kudhalilisha Bunge. Tunangoja kuona ni hatua gani za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya Chitalilo na wengine wanaolidhalilisha na kuhujumu Bunge.
Hakuna ubishi ufisadi unaanza kuimeza na kuibinafsisha nchi yetu na taasisi zake nyeti, hasa baada ya mafisadi waliopata madaraka kupitia takrima kujipenyeza kwenye taasisi za umma.
Bila kutunga sheria ya maadili kuanzia ya ubunge na mtu binafsi, nchi yetu itajikuta pabaya, hasa inapokuwa na wabunge wa hovyo wasiotambua utukufu wa chombo ambamo wao ni wanachama.
Kwa mtu anayejua ukali wa Jeshi la Polisi la Tanzania bado anashangaa kama hakuna rushwa ya kichama kwa Chitalilo kuendelea bila kukabiliwa na mashitaka ya jinai kama ilivyothibitishwa na polisi wenyewe.
Je, Jeshi la Polisi limezuiliwa na CCM kumfungulia mashitaka Chitalilo? Mbona wale wabunge wa Arusha waliodai kusakiziwa na aliyekuwa kigogo wa serikali ili washtakiwe kwa rushwa walishtakiwa haraka huku jeshi hili hili likimfumbia macho Chitalilo anayeweza hata kuvuka mipaka na kulishambulia Bunge na wananchi?
Kama Chitalilo angekuwa mbunge wa kuteuliwa kama mama fulani aliyejivua nguo hivi karibuni, tungesema ana kiburi kwa kukingiwa kifua na aliyemteua kumfanyia kazi za hovyo.
Kwa nini Bunge lisimpe adhabu kali Chitalilo ili hili liwe somo kwa wengine wenye mawazo mgando na utapiamlo wa fikra, wanaopanga kulichafua Bunge kwa maslahi binafsi, tena uchwara?
Kama Bunge litazidiwa ujanja na CCM na akina Chitalilo, basi tumwambie mbunge huyo na wenzake wenye matatizo kama yake wasome alama za nyakati.
Wajue haya wanayofanya na kusema tunayalimbikiza. Kwenye uchaguzi ujao kama ilivyodhihirishwa na baadhi ya wabunge wanaoona mbali, wapiga kura watawaadhibu kama wanavyowaadhibu leo kwa kushindwa kuwawakilisha ipasavyo.
Kama Chitalilo anaona wateule wake wanaonewa, awashauri waende mahakamani kunakotolewa haki. Afanye hivi haraka badala ya kuvunja katiba kwa kujifanya hakimu. Pia afuate maneno ya Yesu kwamba ‘kila mmoja ataubeba mzigo wake mwenyewe siku ile ikifika’.
Tuhitimishe kwa kuwashauri wananchi wa Buchosha kuweka nukta kwenye aibu wanayosababishiwa na mbunge waliyemchagua kwa bahati mbaya baada ya kuwadanganya na kuwaonyesha vyeti vya kughushi kuhusu elimu yake.
Pia tunamshauri Chitalilo kuiga mfano wa Dk. Mwakyembe aliyefikia hata hatua ya kutaka kuachia ubunge kama atabainika kutenda kosa kwenye majukumu aliyokabidhiwa na Bunge kama mwenyekiti wa kamati ya kuchunguza mchakato na mkataba wa upatikanaji wa zabuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond dhidi ya serikali kupitia Shirika la Umeme (TANESCO).
Kamati hiyo ilimpiga teke Lowassa na wenzake Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha huku matokeo yake yakimlazimisha Rais Jakaya Kikwete kuvunja Baraza la Mawaziri.
Source: Tanzania Daima Julai 5, 2008
No comments:
Post a Comment