The Chant of Savant

Wednesday 2 July 2008

Bunge tuokoe tumeuzwa na siasa za "maji taka"







Hivi karibuni Tanzania imeshuhudia kuamka na kufufuka kwa ukuu wa bunge.



Hii ni baada ya kutumika kwa muda mrefu kama mhuri wa utawala kupitishia kila aina ya miswada isiyokuwa na faida kwa wananchi. Muhimu ni ule wa takrima. Hata kama imefutwa, hii ni sheria iliyoiweka nchi yetu kwenye mikono michafu kiasi cha kuuzwa kama alivyosema hivi karibuni mbunge mmoja.



Pia ni bunge hili lililotumiwa hata kuliua Azimio la Arusha ambalo kimsingi ndilo chimbuko la kinachoitwa mshikamano na amani ya nchi yetu. Bila Azimio hata hawa wanaouza nchi wasingeliona darasa wala kufika hapo walipo wakitenda kufuru kila aina. Wangefikaje ilhali wazazi wao walikuwa makapuku wasioweza hata kuwapatia lishe ya kutosha?



Sasa bunge limefufuka. Tulipe shime lisiishie lilipo; lilitoe taifa kwenye mikono michafu ya waroho wachache. Ndiyo. Maana rais ameshindwa vibaya sana . Limsaidie kurejesha heshima ya nchi na watu wake.



Mnamo mwezi Februari kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania na bara la Afrika, bunge la Tanzania lilimfukuza kazi waziri mkuu, Edward Lowassa ambaye kikatiba alikuwa ni mkuu wa shughuli za serikali bungeni.



Hii ni baada ya Lowassa kubainika kutenda kosa la ufisadi kwa kuipiga tafu kampuni kidhabu ya Richmond .



Sambamba na Lowassa, bunge liliwatimua mawaziri Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha huku likimlazimisha rais Jakaya Kikwete kuvunja baraza la mawaziri akiwatupa nje vigogo kama Basil Mramba, Zakhia Meghji, Kingunge Ngombale Mwiru, Joseph Mungai na wengine wengi wazito.



Lowassa rafiki na mshirika kwa Kikwete aling’oka baada ya tume teule ya bunge kumkuta na hatia. Kwa usuhuba na mipango ya pamoja, rais Kikwete alikosa ubavu kuthubutu kumkaripia Lowassa na wenzake!



Lakini kwa ujasiri wa ajabu, bunge liliweza kumfurusha mteule huyu kiasi cha kumuacha akiwa uchi akitapatapa kutafuta wa kufana naye.



Hivi karibuni kamati kuu ya CCM, NEC, eti nayo kwa siasa za maji taka ilimsafisha isijue maji taka hata yachujwe vipi bado ni maji taka na kibaka ni kibaka hata akiombewa dua. Huku nako ni kufilisika bila shaka.



Angalia siasa za maji taka zinavyomsumbua spika Sitta. Hizi hapa ni nukuu zake za hivi karibuni kama zilivyonukuliwa na vyombo vya habari akiutaka umma umsaidie kupambana na wanasiasa taka.



"Baadhi ya wale wanaosema haki wanashambuliwa, lakini tutashinda."

Akimnukuu Ayubu wa kwenye Biblia, Spika Sitta alisema. "Lakini mteteaji wangu yu hai, na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi."





Tukiachana na taka taka za siasa za maji taka turejee kwenye umahiri wa bunge.

Mwezi wa tano mwishoni kulitokea kituko ambacho hakijawahi kutokea kwenye bunge lolote duniani. Mbunge ambaye ni waziri wa zamani mwandamizi aliyefurushwa baada ya kubainika amesweka mabilioni nje alikamatwa na kamera za bunge akiwanga bungeni!



Kabla ya hapo Mbunge machachari Aloyce Bent Kimaro wa Vunjo-CCM alimtolea uvivu rais mstaafu Benjamin Mkapa, mkewe, mwanae na swahiba yake Daniel Yona akitaka warejeshe mali za umma walizopata kwa njia za panya walipokuwa madarakani kubwa ukiwa ni mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira.



Hapa hatujaongelea kituko kingine cha mwaka cha waziri wa fedha, Mustapha Mkulo kulipa bunge takwimu za kupikwa zenye makosa kibao!



Katika ya mwezi wa sita, bunge lilishuhudia kitimtim kingine pale mbunge tutakayemwita Ana-Jasiri alipoitolea aibu serikali na kusema lazima irejeshe pesa za umma zilizoibiwa na watu wake kwenye wizi uliolitikisa taifa wa EPA.



Baada ya kusema hayo, mbunge wa kuteuliwa tutakayempa jina la Ana-Fisadi aliamua naye kumtisha Ana-Jasiri akitetea ufisadi kinamna namna kwa mtindo wa kumwaga chozi la mamba huku akiishia kulitukana bunge!



Tukirejea kwenye siasa za maji taka kama neno lilivyobuniwa na spika wa sasa wa bunge Samuel Sitta akiwazodoa mahasidi wake waliotaka kumchafua, inaonekana sasa zimegeuka kuwa siasa za nchi. Hivi inaingia akilini kweli kwa mbunge mwenye uchungu na nchi na watu wake kutetea upuuzi kama EPA? Rejea karipio uchwara la mbunge Ana Fisadi asiyemwakilisha mtu isipokuwa tumbo lake na yule aliyemteau. Hivi mtu kama huyu siyo mzigo kwa mlipa kodi kweli? Analipwa kwa lipi kiasi cha kupewa marupurupu, cheo cha uheshimiwa na shangingi ilhali ni adui wa umma?



Je hadi hapa kuna haja ya watanzania kuendelea na kuwa na wabunge nyemelezi walioteuliwa kulinda uoza wa wakubwa zao?



Je viumbe wa aina hii siyo mama wa ufisadi nchini mwetu?



Siasa za maji taka za mparurano na mchafuano huzaa kujikomba na uchumia tumbo. Hudhalilisha sana . Baba au mama zima, bila chembe ya aibu, linasimama mbele ya kamera kuropoka na kutoa mineno ya kuudhi kama kumkatisha tamaa mbunge wa umma asiutetee! Hizi ni siasa za maji taka zilizopita kipimo.



Bahati mbaya sana Tanzania imevamiwa na siasa hizi za maji taka tangu kuondoka kwa mkongwe Julius Nyerere. Nchi imeishauzwa kama alivyosema mbunge wa Singida Kaskazini-CCM, Lazaro Nyarandu.



Pesa ya umma inaishia kwenye matumbo machafu ya kikundi kidogo cha watu huku kikitunafiki kinaweza kutupeleka Kanani ilhali kinatupeleka Misri.



Wako wapi wezi wa EPA, Richmond ,IPTL, TICTS,Net Solutions, NBC na mbweha wengine? Nani awakamate iwapo aliyepewa kulinda vifaranga ndiye anavila? Rejea kufumka kwa kashfa za bwana mkubwa aliyewahi kutawala nchi hii kabla ya huyu aliyepo ambaye naye anaonekana kuwa sawa na huyu wa kwanza anayemlinda.



Mwalimu Nyerere aliwahi kusema ka nchi kananuka. Wakati ule kalinuka lakini sasa kameoza, kameuzwa na kananuka zaidi ya wakati wa Mwalimu. Majambazi wamejaa kila sehemu. Wapo bungeni. Wapo ikulu. Wapo mahakamani. Wako kila kona.



Pia mwalimu aliwahi kuonya juu ya ikulu kuwa chaka la mafisadi. Tuko wapi iwapo baadhi yao ni wabunge tena wanaotuhumiwa kutumia makampuni yao ya mfukoni na makaratasi ya kughushi kuiba pesa zetu toka benki kuu? Huku siyo nchi kuendeshwa na maji taka kiasi cha kutaka bunge lenye mamlaka ya kutunga na kubatilisha sheria kuingilia?



Tuko wapi na tunakwenda wapi? Hapa ndipo bunge, kwa kutumia staili na ujasiri uliomfurusha Lowassa, linapaswa kurejea kazini na kuhakikisha nchi yetu inarejeshwa kwenye mstari. Hapa ndipo maneno ya mama Ana Jasiri yanapotoa mwangwi ambao unapaswa kutozimwa kwa vitisho au mizengwe. Tumechoka na kuna siku patachimbika bila jembe na patakuwa hapatoshi hata wabunge mataahira na mafisadi watutishe vipi.



Mojawapo ya hatua ya kulitoa taifa mikononi mwa wezi ni kusimama kidete na kuhakikisha pesa za EPA na Richmond zinarejeshwa na wahusika kufilisiwa na kufikishwa mahakamani. Salaam kwa mbunge Chitaahira anayetuhumiwa kughushi vyeti anayetetea mafisadi. Akae chonjo tutamchimba hadi ang’oke.

Source: Dira ya Tanzania Julai 1, 2008

No comments: