How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 17 July 2008

Roho mtakakitu alipoibukia madhabahuni

TAZAMA nimelala. Napata maono kama kawaida. Naona genge la watu watatu lifanyalo utatu mtata mtakakitu. Ni utata kweli kweli uliosheheni kila aina ya uchafu na ulafi.

Ni utatu wa baba wa mafisadi aitwaye Janaba Kitwitwi. Yu afanana na ndege kitwitwi. Kwani hakawii kuruka toka tawi hili kwenda lile. Ajiliwaza na kuwaliwaza wamsikilizao kwa nyimbo za kasuku asijue weshazichoka.

Kitwitwi baba wa utatu hayuko peke yake. Yeye ni yote ndani ya yote ingawa si yote katika yote. Tazama naona mwana katika utatu tata mtakakitu huu. Naonyeshwa mtu mwenye kofia nyeupe akiwa amevaa mawani ya mbao ya ufisadi machoni mwake.

Ni fisadi kuanzia unywele hadi ukucha. Ananuka kuliko hata tundu la choo! Ni jamaa asiye mgeni kwangu. Kama namjua. Hapana simjui. Huenda wanafanana. Naye anaitwa Enenda Umelowasasa. Huyu mwana ni kiboko kama baba yake. Ni baba wa tamaa nifaki na majivuno. Silaha yake kubwa ni uongo na ghilba kila namna.

Alikuwa amevishwa taji la baba yake. Bahati mbaya katika kukurupuka na kufanya uchafu wake patakatifu pa patakatifu, wazee wa makuhani walimvua taji na kumtimua kiasi cha kuudhoofisha utatu mtakakitu.

Yupo huyu roho mchafu mtakakitu. Naye ni binadamu usiyemdhania. Anaitwa Azirika Rostitamu. Huyu ni Myahudi wa ukoo wa Isakandali. Ni mjukuu wa Ishmaeli aliyekimbia toka Mlima Parani akaishia kwenye nyanda za kati.

Huyu kimsingi ndiye roho ya utatu mtakakitu. Ni jamaa mwenye sharubu kidogo anayeonekana mcheshi, lakini sumu kuliko hata ya nyoka. Ni mwizi hakuna mfano. Ni bingwa wa kughushi na kulahibu asijue ajulikana kwa wajoli wanaoanza kumuumbua kila uchao.

Hupenda kuabudiwa asijue apaswaye ni mmoja tu aliyeumba mbingu na ardhi! Hajui kuwa utatu wao tata ni dini ya kishetani iliyopo duniani kuiba na kuishia kuchomwa moto!

Huyu pamoja na mwana na baba ndiyo kila kitu. Ni yote katika yote katika kueneza dini iitwayo mizengwe. Dhehebu lake linaitwa Sisimka uibe.

Tazama naona baada ya wazee wa makuhani kumfurusha mwana, huku wakimkemea roho mchafu mtakakitu, namuona ameibukia kwenye mimbari ya madhahabu ya mbwa mwitu wajivishao majoho meupe wakijifanya wanaye roho mtakatifu.

Baba ambaye ni machukizo kwa wajoli, bado yumo nyuma ya pazia akihubiri ukombozi ilhali yu mjumbe na mkuu wa utatu mtakakitu wenye kuleta maangamizi ya halaiki. Jitihada zake si haba.

Utatu mtakakitu umeishakwanyua sadaka takatifu ya wajoli iliyotolewa na washitiri wao, huku ukiirudisha kwa mlango wa nyuma na kupokelewa na vicheche, mbwa mwitu na vinyama vya mwitu vya usiku vilivyosheheni patakatifu.

Amewakamata kama ruba kiasi cha kuwaingiza kwenye dhehebu lake. Amewapa vipande thelathini vya fedha fedheha ili wawasaliti wana wa Mungu.

Tazama naowana hawa mbwa mwitu wenye majoho meupe wakigawana vipande thelathini kwa aibu wakichekelea wasijue wanagawana moto. Naona mmoja akimpongeza roho mtakakitu. Wamekumbatiana wakipongezana wasijue wana wa Mungu waliishawastukia!

Wakati roho mtakakitu akijieneza kwenye majumba ya Bwana, naona baba yake akichekelea huku mwana akijipa moyo kuwa kwa kuwapata mbwa mwitu wajiitao wachunga wa wajoli huenda akatakaswa na kurejea kwenye nafasi yake ili aharibu taifa la Mungu. Naona mwisho mbaya kwa nyamaume huyu mwenye wingi wa uchu kama mbwa kusiri.

Tazama naona malaika anipaye habari akitikisa kichwa kwa hasira na masikitiko, akiniambia niwaambie wajoli waamke na kumpinga roho huyu mtakakitu aliyefunga ndoa na wale wenye kudai wana roho mtakatifu ilhali wana roho mtakachafu na mchafu.

Malaika anahanikiza na kusema: “Wambie wajoli wana wa Mungu mkuu kuwa uchafu wanaojipaka utakuwa mwanzo wa maangamizi yao. Waulize tangu lini kondoo na mbwa mwitu wakalala zizi moja? Waambe na uwaase wajue bwana yu aona yote. Waeleze. Wale wenye uchu siku ya siku utawatokea puani. Kwani wajoli wataamka na kuwachoma moto kama vibaka huku wakiwatimua toka patakatifu pa patakatifu.”

Ananikazia macho huku akitoa machozi ya damu kuwalilia wajoli wa yule aliyemtuma kwangu. Anasema: “Waambie wajoli waelewe kuwa laana itokanayo na hasira zangu kama wataendelea na ukondoo wangu itaviangamiza vizazi na vizazi kama moto uangamizavyo nyika.

“Hasira za Mungu kwa uzembe na woga wao zitawahiliki kama gharika la Nuhu au hata kuwageuza mawe kama kaumu Luti. Wasiruhusu Sodoma na Gomora ya uchukuzi kuihiliki nchi.”

Anaamsha ubawa wake na kuupigiza kwa hasira. Naona mabawa yake na kinywa chake vikitema moto. Anaendelea kusema: “Waamuru wajoli waamke na kupambana na roho mtakakitu na mitume wake. Waambie watoke usingizini wapambane na mhimili laanifu huu wa utatu mtakakitu na mharibifu.

“Wafumbue macho yao. Waambie waache kuota na kuona mauzauza wakiwaachia nyoka na mbwa mwitu wasimamie mayai na vifaranga. Ni yupi mpambavu amkabidhie nyama mbwa au humpa jini damu aitunze? Hakika giza na nuru havichangamanani.”

Ananikazia macho na kuendelea: “Aharibuye kazi uharibu jamii. Hivyo naye hujiharibu asijue maana ni sehemu ya jamii. Je, aliyepanda mwembe au mchungwa na mpera anawalisha wangapi? Anawalisha watu, wadudu hata ndege. Hii ndiyo faraja na faida ya upanzi.”

Upanzi si uchoyo wala ukaburi. Upanzi ni kujitoa kwa ajili ya wengine kama ambavyo wengine walijitoa kwa ajili yako. Je, aukataye mmea si mchawi auwaye vizazi vingi? Heri mchapakazi asiye na kazi kuliko mvivu na mchoyo umpaye kazi aiharibu. Je, utatu huu mchafu mtakakitu utateketeza wangapi kama wajoli wakiendelea kuuabudia na kuuchekea?”

Baada ya kuandika neno ambalo sikulijua chini anaendelea: “Mwewe ana macho makali kuliko binadamu. Lakini hajui kusoma! Nani aliwahi kuhesabu meno ya wadudu, tena wadogo sana? Nyoka hana miguu, lakini hutembea hata kusimama akapambana na adui yake!

“Maji hayana mdomo, lakini hupiga makelele, tena ya kutisha! Maji huzima moto, lakini moto huchemsha hata kuyakausha maji! Je, kati ya maji na moto ni nani mwenye nguvu zaidi ya mwenzie? Tia akili.”



Source: Tanzania Daima Julai 16, 2008.

No comments: