The Chant of Savant

Wednesday 2 July 2008

Ufunuo wa Mpayukaji

WIKI ile ya kupokea ufunuo nilikatizwa na kushtuka toka usingizini. Baada ya kuutafuta usingizi kwa saa tatu na kuupata niliendelea kuota.

Siku hizi nimeamua kuota. Hakunigharimu kama bangi na gongo. Hakuna awezaye kunikamata kwa kuota.

Nikiwa ndiyo nimejiweka vizuri kwenye kiti changu cha enzi za usingizi, mara sauti ile niliyoisikia na kukatisha ujumbe wake ilianza.

"We jura wa majura, sakarani wa limbukeni, umesahau ulivyokuwa ukijitembeza kwa wajoli wangu ukitafuta kibali chao uvishwe hilo joho?

"Umesahau mara hii ulivyokuwa ukikesha ukizunguka mabonde na nyika, milima na visiwa ukiwahadaa ungekuwa mshitiri safi si mumiani! Ama kweli hamnazo mna mambo! Yaani mara hii umesahau!"

Nikiwa nasikiliza mara lepe la usingizi liliniiba nikaanza kukoromea kitini. Mara sauti ilinistua kwa ukali.

"Ewe Maliki wa Junaa, tega sikio upate salama yako." Nilishangaa maana mie si Maliki ni Nabii Mpayukaji (MAN).

"Nimeona mahuluti. Ni tumbusi, vipanga, mbwa mwitu na nyoka. Naona mbwa mweupe uliyekuwa umemfuga akilia huko nyikani kaskazi. Ana manyoya meupe mwili mzima kama mvi.

"Ni mbwa mnono lakini mwenye sifa ya udokozi. Ana siha mwilini lakini amekonda moyoni. Namuona mbwa mwingine akilia kwenye nyika za kati. Huyu ana baka kubwa paji la uso wake.

"Ni mbwa mwenye ngozi iliyonawiri, lakini kiwiliwili kilichokonda. Naye ananung’unika baada ya kutupiwa mawe na wajoli wako.

"Naona mbwa wengine wazee wamekuzunguka wakitikisa mikia uwatupie mapupupu, jengelele na mabufulu ya vichwa vya wajoli wangu.

"Pembeni naona mafisi weupe wamejaa kwenye mashimo wakifukua panya. Siyo panya ni makaburi, wanafukua vichwa vya watu.

"Wananyang’anya na kukimbilia kwao porini mbali ulikowatoa. Uliwateleta waje kuwekeza kwenye mashimo walimo.

"Uliwaleta wakusaidie kuwala wajoli wangu badala ya panya! Huwatisha na kuwatafuna wajoli wangu."

Sauti iliendelea... "Ewe mwenye utukufu wa kuazima na sifa za kuangamia, sikiliza sauti hii. Tazama nikuonyeshayo. Unawaona wajoli wanaokulinda? Umewakondesha kama mbwa aliyezaa asilishwe.

"Unaowana wanaokubeba? Ni wagonjwa japo hawajui. Unawaona wanaokuletea minofu ya nyama ya wenzao, maskini hawajui zamu yao! Tazama umeilaani ardhi. Imekosa kutoa chakula cha kutosha kuwalisha watu wake.

"Umelaani bahari. Umesababisha laana katika nchi. Namba yako ni 122005. Hii ni alama ya machukizo kwa wajoli wangu. Kwani ndiyo tarehe walinajisi kiti hicho walipokukweza wewe."

Nikiwa natafsiri maana ya namba hii ya pili baada ya ile 521977 ya wiki ile, mara tazama ilitokea picha ya morani wa Kimasai akiwa ameshika ngao.

Nilimuona mpaka ndani ya kifua chake akiwa na moyo mkubwa mithili ya simba. Mara ghafla nikaona yule morani akichomwa mkuki na juha mmoja aliyekuwa kaandamana naye.

Punde si punde ngao yake ilipokwa na juha mmoja aliyevalia kimorani. Jina lake lina E na Sa. Naye niliangalia kifuani mwake. Alikuwa na moyo mdogo tena wa mbwa! Sikuelewa nilichokuwa nikikiona.

Mara ghafla nikaoana mzee mwenye tabasamu la ajabu. Alikuwa na mvi akiwa amekaa kwenye kiti cha enzi huku watu wake wakifurahi naye. Aliitwa Mwema. Na kweli alikuwa huru kweli. Hakuwa na minyororo wala migogoro.

Ghafla alitoweka. Ndipo nilimuona Musa akiwa amebeba kinyago chenye sura ya binadamu. Nilipigwa na butwaa! Mara nilijisemea. "Kulikoni Musa kachanganyikiwa hadi anabeba kinyago asijue yaliyowapata Waisraeli walipoabudia kinyago cha ndama? Ni hekima gani hii? Nilijiuliza.

Mara ghafla niliona kile kinyago alichobeba Musa kimegeuka jitu jeusi lenye sura isiyopendeza. Ndipo Musa alianza kuuambia umati: "Japo hiki ni kinyago, lakini ni safi kama theluji." Nilizidi kupigwa butwaa nisijue maana ya maono haya.

Maono yaliendelea. Musa alibeba kinyago chake na kukizungusha nyika na nyanda huku akiwashawishi wana wa Mungu wakiamini kingewavusha bahari ya Sham.

Punde si punde niliwaona wana wa Mungu wakipiga kura kwa vijiti. Kile kinyago cha Musa kilishinda wanaume wengine wawili!

Kinyago mtu kiliapishwa kukalia patakatifu pa patakatifu. Lahaula kinyago si mtu ni kinyago! Baada ya Musa kumaliza kukiuza kinyago kwa wana wa Mungu alikata roho.

Kinyago kiligeuka kinyago. Kilianza kuleta vinyago vingine vya fisi, mbweha, kunguru, nyoka na mamba vilivyopata uhai na kuwa viumbe hai. Ghafla kinyago mtu aliyeaminishwa na Musa alianza tabia nyingine.

Nayo ni kuwanyonya damu wana wa Mungu! Kinyago kile na kile chenzie cha kike vilianza kula nyama za watu! Si mtoto si mke wala rafiki. Vinyago vyote vilianza kula nyama za watu!

Nikiwa natafakari maono ya kinyago, mara niliona kiza kikuu kikiingia. Kinyago na vinyago vya wanyama vilivyopata uhai kutokana na kunywa damu vilitimka kimya kimya na kwa kuinamisha vichwa. Mara wakatokea wapiga tarumbeta wakisema vinyago vilikuwa vimetafuna karibu nusu ya watu!

Ghafla niliona kahaba wa makahaba aliyevutia kama mbaramwezi akijinadi kwa wana wa Mungu. Alipendwa na kuaminiwa sina mfano.

Alishirikiana na yule morani mwenye moyo mdogo tena wa mbwa kutangaza ufalme wake. Kutokana na kuliwa na kinyago na vijinyama vyake, wana wa Mungu walifanya kosa jingine.

Walimuamini yule kahaba wasijue mwisho wao. Hawakujua yeye na kinyago lao lilikuwa moja. Wote ni wala watu na wanywa jasho na damu.

Ajabu kubwa ilitoea. Mara niliona yule kahaba kageuka kuwa mimi! Nilijisachi sehemu za siri kujua kama kweli mimi ndiye yule kahaba.

Ajabu nilikuwa na zana zangu zote kama kawaida ila mwenye sura ya kahaba yule wa machukizo! Mara kahaba alianza kutumbuiza kwa nyimbo nzuri zenye nakshi na misamiati mizuri.

Watu walivutiwa na nyimbo za yule kahaba. Walifurahi kiasi cha kusahau kila kitu. Siku zilienda. Kahaba akiwa na wapiga zumari nyoka mbwa na fisi walizidi kutumbuiza.

Mara njaa ilianza kuingia kwenye matumbo ya watu wa Mungu. Walianza kulalamika kuwa wasingeshiba kwa nyimbo.

Mara yule morani mwenye moyo wa mbwa alipigwa kibao na kijana mmoja jabari aitwaye Viwembe. Mara kahaba alianza kuhaha akitafuta la kushika asilipate.

Morani alipotimka mara na mbweha wengine wenye sura za watu wakafuatia huku wengine wakimlilia kwa vile alizoea kuwapa mapupu.

Alikuwa yule mbwa mweupe niliyemuona akikimbilia nyanda za kati. Pia alikuwapo fisi aliyejitupa kwenye ziwa kubwa akaogelea kuelekea kwao! Ni mbwa mwenye kipara. Nani aliwahi kuona mbwa mwenye kipara?

Nilipokuwa nikijaribu kujigeuza, mara nikaona nyufa kwenye kiti changu. Mara nikaona mchwa wakiguguna kiti changu. Walianza kunishambulia kwa kasi nikastuka! Kumbe naota.

Source: Tanzania Daima Julai 2, 2008.

No comments: