Mpendwa na mheshimiwa sana mzazi wangu mama Salma Kikwete,
Nakusalimia kwa heshima zote na taadhima. Leo sipayuki naongea. Naongea nawe shufaa mzazi wangu.
Sikuwa nimepanga wiki hii kuongea nawe kwa njia hii. Hata hivyo sina jinsi. Sina uwezo wa kukutana nawe ana kwa ana tukiwa tunacheka na kutongoa.
Kilichonisibu kukuandikia waraka huu mtuvu ni maneno ya chama cha NCCR-Mageuzi juu ya NGO za wake za wakubwa.
Maneno yao ambayo sitaki kuyarudia yameniingia na kunitia hamasa, chuki na mshawasha lau niseme bila kumung’unya.
NCCR-Mageuzi wanasema hizi NGO ni vichaka vya wizi wa pesa ya umma na mianya ya pesa chafu toka kwa watu wachafu wasiolitakia taifa letu mema kuhalalishwa na kusafishwa. Je walijua hili mama yangu? Kama hulijui basi ngoja nikuibie tena kwa utuo.
Baada ya kuibuka sakata la mtangulizi wako kupitia kampuni iliyo na hisa zake kuwalangua walimu maskini, mengi yamesemwa. La mno nawe kwa njia moja au nyingine umeguswa.
Najua mama huna unachokosa. Mumeo ni mwenye nchi hii toka mashariki magharibi kusini hadi kaskazini. Ana mshahara na marupurupu lukuki. Akicheka analipwa. Akinuna analipwa. Mkisafiri ughaibuni mnalipwa. Kila mnalofanya au kutofanya mnalipwa.
Kwa hiyo mama, sitaki ulaumiwe kama mtangulizi wako ambaye sasa zinaanza kumtokea puani asipate hata pa kuweka uso wake.
Mama yangu mzazi wangu, watu wanasema huu mchezo wa kuanzisha NGO ni ufisadi. Wanauliza ni kwanini mngoje hadi waume zenu waingie madarakani ndipo iwajie huruma ya kuwasaidia hao mnaodai mnawasaidia? Pia wanahofu wanaowachangia na jinsi mnavyoziendesha hizo NGO.
Kwa mfano NGO yako iitwayo WAMA au maendeleo na wanawake imejikita kwenye kusaidia akina mama. Hili ni jambo bora. Lakini bora zaidi ni kuiachia wizara ya masuala haya ifanye hiyo kazi adhimu.
Nikukumbushe mama yangu. Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliyepigania na kuleta uhuru wa nchi hii ambayo wale ambao hawakuipigania wanaifaidi na kuitapanya hakuruhusu mke wake bibi yangu Mama Maria kujiingiza kwenye kadhia hii. Nani kama Nyerere muhula huu?
Alijua watu watasema na kushuku. Wapo wanaosema kuwa NGO hizi zinamtia kishawishini rais. Kwani jina na ofisi yake vinatumiwa na wafanyabiashara mbwa mwitu kujipatia hisani zisababishazo madhara kwa walio wachagua. Na hii ni kweli. Tuliona jinsi NGO iliyopita ambayo siku hizi imedoda ilivyokuwa ikipeleka misaada kenye mikoa ya mama, mumewe na rafiki yake waziri mkubwa. Huu ni ufisadi hata kama unatendwa na wakubwa. Sitaki nawe uhusishwe na upuuzi kama huu.
Wengine wanahoji taarifa zenu za hesabu na uongozi mzima wa kampuni. Juzi mke wangu aliyekuwa akilalamika kuwa anatumiwa aliniambia kuwa NGO za namna hii ambazo yeye huziita nyemelezi zinamilikiwa na wake wa wakubwa watupu. Mama Mpayukaji muathirika hapewi nafasi ukiachia mbali misaada.
Najua una nia nzuri na akina mama. Lakini nia nzuri hugeuka kuwa mbaya hasa inapotimizwa kwa njia mbaya. Wengi wape hasa wenye nchi yao. Sasa wanasema NGO hizi ni vichaka vya ufisadi ulafu na wizi. Mimi sisemi hivyo ingawa naanza kushawishika hasa nikiyaona ya bi Nonihino aliyepita.
Naona aibu kwa mama wa taifa kuwa machinga kisa? Tamaa ya pesa chafu itokanayo na watu wachafu kulhali.
Nachelea kusema hivyo hata hivyo mama. Lakini wataalamu wa falsafa husema heri kusikia lawama za mwenye busara kuliko wimbo wa sifa na pambio za mpumbavu. Najua kwa sasa wapambe na wapumbavu watakusifu wapaswapo kukukanya na kukulaumu kwa vile una mamlaka. Yakishakutoka wanakunanga. Na isitoshe mama, madaraka ni tunda la msimu. Ni nguo ya kuazima ambayo haisitiri manonihino.
Pia wapo wanaosema kuwa hata kuwa kwako kwenye kamati za chama ulizoshinda hivi karibuni si jambo jema kwako mumewe na familia kwa ujumla ukiachia mbali chama na taifa. Wanasema hii inaweza kutafsiriwa vibaya kama kupenda madaraka na kurudisha ufalme usio rasmi kwa mlango wa nyuma.
Kama wapambe na washauri wako na mumewe wanakuogopa ili wasitie kitumbua mchanga, wacha mie asiye na cha kukosa nikwambie kwa mapenzi mazito mzazi wangu.
Mama,
Kwa sasa mumeo analaumiwa kwa kushindwa kuwakamata na kuwashughulikia mafisadi waliotamalaki kwenye serikali yake. Kuna balaa linaitwa EPA. Najua linamnyima usingizi kwa vile hajui aanzie wapi. Kuna hizi ahadi alizotoa za kuwapeleka watu Kanani. Sasa wanasema anawakimbizia Misri!
Nilimsikia juzi kule Muheza akisema watu wafunge mkanda na kuvumilia matatizo. Lakini matatizo hayavumiliki. Alisema ugumu wa maisha unasababishwa na kupanda kwa mafuta. Lakini mbona ulianza hata kabla ya bei za bidhaa hii adimu na aghali kupandishwa bei?
Kwangu naona ufisadi ndiyo unaofanya maisha yawe mawe. Hivi Bilioni 133 zilizoibwa na vibaka wajiitao wakubwa zingepunguza machungu haya kwa kiasi gani? Na zile zilizokuwa zikitolewa kwa kampuni la kitapeli la Richmond na mdogo wake Dowans zingetusogeza hatua ngapi?
Sikusomea uchumi ila najua uchumi. Uchumi hauhitaji maneno marefu ya Mstaafu Mkulu. Hata ndege anajua kuwa nchi yetu ina vibaka na majambazi wengi waitwao waheshimiwa.
Hivyo nisikuchoshe mama yangu. Naomba kwa taadhima kabla ya kukuaga nikushauri ingawa mimi siyo mshauri wako. Achana na NGO ambazo umma unaziona kama ufisadi. Achana nayo. Tulia ulee watoto wako na umhudumie mzee.
Pia kuna jambo moja nilitaka kusahau. Wapo wajinga wanasema eti unapenda sana kuandamana na mumeo ughaibuni kutumbua. Wanasema hii nayo inasababisha maisha magumu kwa wale wanaowagharimia yaani walipa kodi maskini.
Pia naomba umshauri mzee aanze kutimiza ahadi alizotoa akijitenga na watu fisidi na wanafiki wanaotaka yamkute yanayomkuta nonihino. Maana walimchagua yeye peke yake na mambo yakiharibika ni yeye atawajibika.
Hata huu utawala wa nyuma ya pazia unaoitwa NGO siku umma ukitaka maelezo ataumia aliyechaguliwa siyo wale waliojichagua kwa sababu wanalala naye nyumba moja.
Naomba niwasilishe kwa heshima na taadhima.
Source: Dira ya Tanzania Julai 29, 2008.
No comments:
Post a Comment