How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 8 July 2008

Je ni mwisho wa fungate ya mabwege?

wasomaji nadhani mnakikumbuka kisa cha Dan Nganyika aliyeoa mwaka juzi. Alioa kwa sherehe ya aina yake iliyotumia mamilioni ya shilingi. Pia katika kumpata Mchumba wake wakati ule,Jackie Kikwekwe ambaye kikwetu ni kizuri. Alioa karibu sana na Krismasi mwaka juzi.


Nganyika au maarufu kama Danganyika alioa mwanamke mrembo ,mweupe na mwenye ustadi wa kuimba. Lakini mkewe Danganyika anao udhaifu mmoja au tuseme kasoro. Pamoja na kusifika kwa urembo na ulimbwende wake na ustadi wa kughani, bado ni mvivu. Utajionea mbele ya safari inshallah.

Kinachomsaidia Bi. Danganyika hadi sasa siri yake ya kuwa mvivu kutofumuka, ni ile hali ya kujaliwa nyota jadidi tena ya jaha ya kukubalika nyumbani kwa Bwana Danganyika ingawa nyota imeanza kuchafuka tena sana.

Kwani tunavyoandika imekatika miaka mitatu; bado wawili hao wako kwenye fungate.

Uzuri wa Kikwekwe,sawa na wa tausi haukosi kasoro maana hata tausi mwenyewe ukimchunguza,licha ya kuwa mvivu ana miguu mibaya tu. Hivyo doa hili la "tausi" katika haiba na uzuri wake huenda likafumka na kuvuruga kila kitu.

Pamoja na sifa za Bibie tulizozitaja hapo juu analo lake. Lipi hilo? Waweza kuuliza. Japo ni miaka tangua aolewe,licha ya kumhudumia bwana na nduguze kwa mipasho hakuna la maana alilokwisha fanya!

Hajawahi japo kuwapikia na kuwatengenezea japo togwa waonje fani yake jikoni! Danganyika na nduguze wanalilia lau wapate pishi tuvu lenye wingi wa manjonjo ya jikoni kama vile tui bubu na makando kando mengi. Lakini wapi!

Kweli kipya kinyemi japo kidonda! Ingekuwa kwenye kabila jirani, washamstukia na kumtimua zamani gani. Ila wahenga walisema ivumayo haidumu; kuna uvumi kuwa watu wameanza kuhoji na kulaumu. Watu weshaanza kusema mbona mambo si mambo tena kwa mshangao na mghafiriko si haba.

Nao wapambe kama ada,wanazidi kusifia umahiri wa mipasho na sauti ya bibie! Ebo watu watakula sauti? Hata kama ni uzuri kwani waliwa? Wenye unywanywa na ithibati wanauliza pasina kuhofu hata kama ni kwa kunong’ona.

Kila upuuzi afanyao bibie wapambe yao ilikuwa ni "marahaba" ilmradi atawapa mabaki ya akiba ya Bwana. Si unawajua wapambe walivyo nuksi?

"Mwe! Tutakula mipasho na ulimbwende wa bibie?" Ndugu wanauliza. Bibie hajibu kwani hujifanya hajasikia. Lake ni kuongeza unywanywa na ziara za ngomani!

Hali ilivyo kwa sasa Danganyika si Danganyika tena bali Danganyuka. Maana ashaanza kutia shaka. Anapanga jinsi ya kulikabili tatizo ila mahaba na urembo vinamkwaza.

Yote yanatokana na sifa yake ya uvumilivu. Maana ni mwaka juzi tu alitaliki jakazi moja jeusi liitwalo Benadetta Walia Makapu alilokuwa kaozwa na Marehemu Baba yake Mzee Nyenyere wa Nyungu nyungu. Wakati akilioa hilo jakazi jeusi, baba yake alilisifia kuwa linaaminika licha ya ubaya wa sura yake. Maskini hakujua kwapuzi la kutupwa!

Hujasikia: uzuri wa mwanamke tabia? Danganyika aliambiwa na marehemu mzee wake maskini asijue mambo si mambo bali kuuingia mkenge!

Marehemu alimuaminisha kuwa jakazi lile lilikuwa safi hakuna mfano. Kumbe mzee kutokana na uzee hakuwa ameona vizuri. Maana janajike lile licha ya kiburi,uroho na udokozi,halikuwa na uaminifu katika ndoa. Licha ya kuwa kichwa ngumu na limbukeni,lilikuwa na shetani wa kugawa mali za bwana.

Lilithamini ndugu zake huku ndugu wa mume likiwachukia!

Lilijaliwa majigambo na kujisifu hakuna mfano! Lilijaliwa lugha ya mafumbo na vijembe si haba. Pia lilikuwa limesoma si haba.
Tokana na sifa zake chafu,chumvi,sukari na hata baadhi ya suti za bwana lillizigawa kwa hao watu wake na ndugu zake.
Hamadi! Daganyika kutahamaki,nyumba ishafilisika! Mali ishahamishiwa kwa ndugu wa jamaa! Lahaula!

Tumrejee Bi Chaurembo mke mpya wa Danganyika. Pamoja na sifa zote za ushufaa tangu aingie ndani,jikoni paka wamelaliana, "mapanya" bado yanasomba mali za mumewe!

Kwani tokana na kuwa bize na mipasho na kutafuta sifa,bibie karithi mapanya yaliyomtia mwenzie doa. Hakupata muda wa kuyafurusha na kuisafisha nyumbaye maskini! Yeye kakalia mipasho na ulimpyoto!

Hata wapambe na mashoga ni wale wale aliowaacha aliyemtangulia. Wengi ni akina Uvuruge mwana wa Karukarange. Wanauma na kupuliza,wanatabasamu usoni na kulia rohoni.

Kwani Bwana Danganyika si haba ni mkwasi pesa anazo. Karithishwa ,mashamba,mifugo na miradi mikubwa ya biashara.

Waswahili wana mambo tena makubwa sana. Mambo yanaharibika wao wakusifia. Lakini vipembeni wanalalama kukunanga na kukulamba uchogo tena kwa kukuanika si haba.

Hujawasikia wakilalama? ‘Njaa jamani njaa. Jama mke si mke bali pambo" Toba!

Walalamika. Kila siku hadithi huku jiko limenuna na nyumba imeliwa na kiza. Nyumba bado ni chafu imesheheni mipanya na mende na huku mali za Bwana zikizidi kusombwa!

Maskini Bibie Chaurembo hajagutuka wala kukengeuka kuwa mambo yanaanza kuchacha huku watu wakichachamaa! Sijui tumwambe lipi na vipi ajue amechelewa na alio nao hawako naye?

Wakwe wanasema wanataka matunda si maneno. Zimeishasikika nong’ono. Wakwe wanasema nyumba si nyumba tena maana kila kitu kiko hovyo hovyo na mali zinapungua.

Bado wana hasira na lile jakazi. Lakini tusishangae siku moja,kama bi Chaurembo hatajirekebisha akafanya yampasayo,watu waweza kulikumbuka jakazi lile yarabi!

Danganyika hana bahati maskini. Yeye bado kapiga moyo konde akiishi kwa matumaini kuwa huenda bibie atabadilika. Lakini lini iwapo muda ndiyo huo unakimbia?

Maskini kalewa na kuzuzuliwa na urembo. Lakini si Kosa Lake. Hujasikia kuwa mwenye mapenzi haoni?

Wawapendao wawili hawa kwa dhati hawasiti kusema, "Jamani achaneni na fungate muanze maisha halisi" Je wahusika watasikia na kuelewa? Pamoja na ukwasi wa Danganyika,watu wanauliza,fungate gani ya miaka tena mitatu?

Yetu macho, mwanzo wa ngoma lele. Huenda huu ndiyo mwanzo wa mwisho wa subira za Danganyika na jamaa zake. Huenda ndiyo. Maana kila lenye mwanzo shurti liwe na mwisho. Tumalizie. Je tutakula urembo sifa na mipasho? Je tutakula ngonjera nyimbo na tenzi? Mbona twalishwa mbichi na mbovu ilhali twaona? Je nasi tu mabwege kama bibie kiasi cha kutokengeuka na kuustukia huu mkenge tuliomo? Toba! Amkeni jamani tulikabili bibi hili vinginevyo twafa twajiona.

Twakataka mapishi ya bibie. Tushachoka na mipasho uchwara na laghba za hovyo. Matumbo yatukatua na nyoyo zimejaa sononi kuuingia mkenge mchana kweupe. Bibie nawe stuka waliwa. Stuka kabla ya kufurushwa kama Wa Makapu na Makapi aliyeiba mali za Bwana kiasi cha kukuachia mapanya na kenge wakitafuna kila kitu. Huoni? Hayo macho yako malimbwende yanini? Juzi tumemtimua shoga yako Edwina bado wewe kama hutatia adabu.

Wale wenye sifa za bwana na bibi Danganyika mpo? Tubadilike. Tunawaambia walioko chini wajuu watasikia.

Tunaomba kutoa hoja ya mwanzo wa mwisho wa fungate ya mabwege. Amkeni kumekucha mmeachwa mwadhani mwangojewa. Shauri yenu.
Kalabaho.
Source: Dira ya Tanzania Julai 7, 2008.

No comments: