The Chant of Savant

Sunday 3 April 2011

UV-CCM na “Ni zamu yetu kula” na kupayuka


Karipio la hivi karibuni na Umoja wa Vijana wa CCM linafurahisha. Ni kutokana na ukweli lilobeba: limegusa mzizi wa mgogoro ambao umekuwa ukitukuta chini kwa chini hadi kuumka hivi karibuni. Wengi hawakujua kuwa ugomvi wote huu ni juu ya ulaji!

Wengi waliposikia vijana wakihanikiza kuwashutumu wale wanaoowaona kama wanadhoofisha chama, walidhani walikuwa wakifanya hivyo kutokana na mapenzi kwa chama. Kumbe siyo ni ulaji!

Tusiuwekee maneno kinywani UV-CCM.
Haya ni matamshi ya hivi karibu ya UV-CCM yaliyowaudhi magwiji na vigogo kama Fredrick Sumaye waziri mkuu wa zamani na kada wa CCM.

“Lakini kwa kumtukana mwenyekiti hawatapata kamwe kwa kuwa yeye ndiye anayejua ni nani muadilifu, hivyo wasiharibu nchi kwa maslahi yao. Wao wameshiba na sasa wamevimbiwa watuache na sisi tule kama wao.”Mwenyekiti wa UV-CCM, mkoani Pwani, Abdalah Ulega.

Baada ya Ulega kufyatua kombora hilo. Naye Sumaye hakunyamaza. Alimjibu, “Ina maana UV-CCM wana mgombea wao ndo maana wengine tunaonekana kero kwao kwani tunamvurugia mtu wao. Vijana wenye tamaa ya KULA ni hatari kwa taifa.” Fredrick Sumaye.

Anaendelea, “Eti vijana wanataka wamweke mtu wao ili wale? Imenishtua sana!”

Ukiachia mbali hili la kugombe mlo, je UV-CCM wametumwa na rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa CCM? Hili ni swali linaloulizwa na wengi. Swali hili linaulizwa kutokana na sababu kuu mbili. Mosi, kwanini tamko hili litolewe na mkoa wa Pwani anakotokea Kikwete? Pili ni ile hali ya kuwa kila mkutano wenye kuzusha tafrani kuwa Ridhiwan Kikwete nyuma yake. Rejea kuvurugika kwa mkutano wa uchaguzi wa umoja wa vijana uliofanyika Iringa mwaka jana ambapo mwenyekiti wa UV-CCM wa zamani Hamad Masauni alitimliwa kwa kile kinachosemekana na kutokuelewana na Ridhiwani.

Je tunaanza kushuhudia utawala wa akina Saddam Hussein, Muamar Gadaffi na Hosni Mubarak ambao watoto wao walikuwa marais wadogo wakitoa matamko kama tulivyoshuhudia hivi karibuni kwa Seif, Khamis na Saad Gadaffi?

Je wanasukumwa na njaa zao au kuzoea kuwaona wazee chamani wakimohola watakavyo? Rejea kugawiana nyumba za umma na ujumbe wa bodi mbali mbali kwenye mashirika ya umma.

UV-CCM waliwashutumu vigogo wa CCM waliotoa matamko kuhusiana na kulegalega kwa chama. Kosa walilotenda UV-CCM ni kuwashutumu wakongwe kutofuata utaratibu wa chama wa kutoa maoni nje ya vikao. Ajabu na UV-CCM walitoa tamko nje ya vikao kwa kutumia magazeti yale yale. Walipayuka kama ambavyo wanawashutumu vigogo.

Haya yanathibitishwa maneno ya Mjumbe wa mkutano Mkuu wa UV-CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Makonda, ambaye alikaririwa akisema, “Haiwezekani Jumuiya ikatoa maagizo kuitaka Sekretarieti ya CCM itoke madarakani, haiwezekani kuwanyooshea vidole wazee wetu na kuwaambia waache kutoa siri za vikao wakati sisi vijana tabia zetu ndio hizo za kutoa matamko yanayokinzana kila kukicha kwa kuishutumu serikali na chama.”

Kumbe ni mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu!

Kigogo mwingine wa CCM aliyejitokeza kuwajibu UV-CCM ni mbunge wa zamani wa Jimbo la Vunjo na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Aloyce Kimaro, aliyekaririwa akisema, “Leo baada ya mambo kuharibika ndiyo wanajitokeza, hivi jamii itawaaminije kama hawatumiwi na mafisadi? Tungewaona wako makini kama wangekuja na mkakati wa kuiimarisha CCM kabla ya 2015 na siyo kupayukapayuka tu.”

Matamko ya UV-CCM yanaonyesha uchu wa madaraka yaliyojikita kwenye maslahi binafsi ya kimakundi. Hili lilithibitishwa na maneno ya Mrisho Gambo, ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu wa Mkoa wa Arusha, aliyekaririwa akisema, “Nani hafahamu ukweli kuwa Lowassa na Rostam ndio wanaokipotezea mvuto CCM? Wananchi watakuwa na makosa gani wakihusha Dowans na CCM wakati viongozi wake wakubwa ndani ya chama wanahusika na chama hakijawafanya chochote?”

Maneno ya Gambo yanatoa jibu la nini kifanyike badala ya kuendekeza njaa na ulafi. Hata ukichunguza maneno ya Sumaye, yanalenga kuisaidia CCM kujikosoa na kufanya mambo kisiasa badala ya kuendekeza ubinafsi na kutetea ufisadi.

Imefikia mahali UV-CCM kujionyesha kama ina nguvu kuliko chama chenyewe kinachoibeba. Je hili ni somo kuwa CCM imeishiwa na ushawishi na nguvu za kudhibiti wanachama na asasi zake?

Wanaoamini kuwa UV-CCM imetumwa na wakubwa wa chama wanauliza swali moja kuu: kama hawakutumwa, kwanini wakubwa wa chama hawawakemei au kutoa tamko la kupinga namna UV-CCM inavyojifanyia mambo kizembe? Je huu si ushahidi tosha kuwa CHADEMA inazidi kuibomoa CCM?

Tuhitimishe kwa kuushauri UV-CCM kuwa makini. Waache unafiki wa kuona kibanzi kwenye macho ya wenzao wakati wao wana boriti. Hata timming ya matamko yao haikisaidii chama, wao hata yule wanayemtetea kwa kumbomoa.

UV-CCM inapaswa kujua kuwa chama kilichopo madarakani hakipo pale kula au kuneemesha makundi, watu binafsi na familia zao bali kuwatumikia wananchi waliokichagua. Kama ajenda yao ni kula hawana haja ya kuwa madarakani. Huu nao ni ufisadi wa hali ya juu unaopaswa kupigwa vita kulia na kushoto.
Chanzo: Dira ya Mtanzania April 4, 2011.

No comments: