HAKUNA ubishi. Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lina kibarua kikubwa hasa wakati huu baadhi ya wanasiasa wasio makini wanapolitumia kama mhuri kuhalalisha ajenda zao chovu, chafu na za kichochezi.
Ajabu jeshi lenyewe limekaa kimya au kukwepa linapodhalilishwa, kuhusishwa na mambo ya kipuuzi hata kutumiwa vibaya. Jeshi hili hili limekuwa mstari wa mbele kuwasumbua wananchi wadogo pale wanapofanya makosa kama vile kukatiza kwenye maeneo yake au kuvaa magwanda yake.
Ajabu ya maajabu wanasiasa wanapotangaza mambo ya ajabu ajabu kwa kutumia jeshi, lenyewe limekaa kimya huku mkuu wake akiulizwa na kukwepa kana kwamba halitumiki kisiasa.
Imefikia mahali kujengeka dhana potofu kuwa jeshi letu ni mali ya chama fulani au kikundi fulani cha watu. Lengo la makala hii si kulishambulia wala kulituhumu jeshi wala kulihusisha na tuhuma za kizembe kama madai kuwa litachukua nchi kama wananchi wataridhia mfumo wa serikali tatu.
Hata hivyo, kama taasisi inayoheshimika, jeshi linapaswa kujitenga na upuuzi huu ukiachia mbali hata kuwakaripia hata kuwaadhibu wanaodiriki kulitumia kwenye siasa zao uchwara. Vinginevyo itajengeka dhana potofu kuwa jeshi limeamua kujirahisisha na kutumiwa na wanasiasa.
Hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera. Uratibu na Bunge), William Lukuvi alikaririwa akiwa kanisani akiwatisha wananchi kuwa kama wataamua kuwa na serikali tatu basi jeshi litachukua nchi.
Hii si kauli nyepesi na aliyeitoa si mvuta bangi wala mnywa gongo wa mtaani. Je ni kweli jeshi linaandaliwa kuhujumu katiba ya wananchi kama hawatakubaliana na usanii wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)?
Je kama jeshi litaendelea kukaa kimya halioni kuwa litaonekana kuwa nyuma ya mpango mzima japo hauwezi kufanikiwa hasa wakati huu wa sera za kidemokrasia dunia nzima?
Watanzania wanangoja kwa hamu kusikia sauti ya jeshi lao likiwaaminisha kuwa ni lao na bado ni safi na lisolofungamana na chama wala kundi lolote.
Japo kukaa kimya kisheria si kukubaliana na tuhuma, kwa watu wa kawaida kitendo hiki ni kukubaliana na yaliyodaiwa hata kama ni potofu na ya uongo kiasi gani. Hii nchi ni ya watanzania na si ya CCM wala jeshi wala nani.
Lukuvi alikaririwa akisema, “Unajua jeshi haliwezi kukaa na bunduki bila fedha. Hiyo Serikali ya tatu ambayo jeshi litakuwa chini yake haina vyanzo vya mapato vya kueleweka, sasa hao wanajeshi watalipwa nini? Wenye mitutu watakubali kuishi bila fedha?”
Wenye kujua neema iliyojaliwa nchi yetu waliona kauli hii kama ya kivivu na uongo. Mbona wananchi wamekuwa wana uwezo wa kuiendesha serikali inayolinda ufisadi na kugawa mali zao kwa wawekezaji kupitia misamaha ya kodi na kusaini mikataba mibovu ya kijambazi?
Kwanini Lukuvi asione kuwa ni bora kuwa na serikali nyingi lakini tukazuia mianya ya ukwepaji kodi na wizi wa mali na fedha za umma?
Au ni kwa vile chini ya kiini macho cha serikali mbili akina Lukuvi wameweza kuiba hata kughushi bila kushughulikiwa? Hivyo ikija ya tatu wana wasi wasi madudu yao yatafichuka.
Pia ikumbukwe kuwa jeshi husika lipo kwa matakwa ya watanzania wanaokatwa kodi kuliendesha kwa ajili yao na si kikundi cha watu wala chama.
Kauli ya Lukuvi licha ya kulaaniwa inapaswa kulichochea jeshi kutoa shinikizo awajibishwe ili liwe somo kwa yeyote anayelewa madaraka na kuamua kuropoka bila kufikiri.
Kama haitoshi, kapteni wa zamani wa jeshi hilo hilo mbunge wa Mbinga John Komba naye aliongezea uzito wa tuhuma za kuangushwa nchi kwa alipokaririwa akisema kuwa kama Bunge la Katiba litashawishika likapitisha serikali tatu ataingia msituni kupigania serikali mbili.
Je, anazipigania kwa maslahi ya watanzania wapi iwapo watakaopitisha hizo serikali tatu ni watanzania wale wale? Kwa vile ni wajibu wa jeshi letu kulinda mipaka ya nchi yetu na watu wake,linapaswa kumkamata Komba na hata Lukuvi na kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu haraka sana ili lisionekane liko nyuma ya upuuzi na vitisho hivi.
Muungano wetu hauwezi kuishi kwa kutegemea vitisho, utashi wa jeshi wala mitutu ya bunduki wala utashi wa watawala bali nguvu na utashi wa wananchi wenye nchi yao.
Anayeshindwa kulitambua hili anapoteza muda wake na anajidanganya tu. Mhalifu wa namna hii hapaswi kuwa uraiani akila kuku wala kuwa kwenye ofisi wala Bunge la umma.
Anapaswa kuadabishwa au hata kukaripiwa na kuambiwa akome kabisa. Jeshi letu ni la wananchi na si la wanasiasa hata wawe na madaraka na fedha kiasi gani.
Ni bahati mbaya sana. Hata amiri jeshi amejiingiza kwenye siasa hizi za kizembe na vitisho bila sababu yoyote ya msingi. Siku moja kabla ya kuadhimisha miaka 50 ya muungano, Rais Jakaya Kikwete alikaiririwa akisema, “Sherehe za kesho ni sherehe za jeshi ambao wamepania kuonyesha watakavyoulinda Muungano na atakayeuchezea atakiona cha mtema kuni.”
Kumbe sherehe zenyewe zimetumia pesa ya umma wakati si za muungano bali jeshi ku-show off? Je hawa akina Lukuvi na Komba wametumwa na Kikwete?
Je, wanawajengea picha gani wananchi? Wamemtukana mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na kuchoka. Sasa wameanza kulitukana jeshi kwa kutaka umma uamini kuwa liko nyuma ya njama zao za kuwalazimisha watanzania kukubali serikali mbili ambazo pamoja na kuwepo kwa miaka 50 zimekuwa chanzo cha matatizo badala ya kuyatatua.
Wanasema serikali mbili zinafaa na kero za muungano zilizosababishwa na serikali mbili zinarekebishika. Ajabu hao hao waliosababisha hayo matatizo wakashindwa kuyatatua wanataka kutuaminisha kuwa business as usual chini ya serikali mbili zinazozidi kuudhofisha muungano ndiko jibu wakati ni tatizo.
Kama walishindwa kwa miaka 50 watawezaje hata wakiongezewa miaka 500 zaidi ya kuongeza matatizo?
Kuonyesha akina Kikwete, Komba na Lukuvi walivyo na ajenda ya siri, Kikwete alikaririwa akisema, “Lazima nikiri kwamba sikufurahishwa hata kidogo na baadhi ya wajumbe kususia vikao, eti wanazunguka kwenda kushitaki kwa wananchi, sijui wanakwenda wapi na kumshitaki nani, huko nje waendako siko, wakati wake bado.
Nawasihi warudi bungeni, hawawatendei haki wananchi wao.” Ebo! Hata Kikwete angekasirika hata kupasuka. Kinachoongelewa hapa si suala binafsi bali la kitaifa kwa maslahi ya watanzania. Akasirike au afurahi hili si muhimu. Muhimu ni wananchi kupata katiba wanayotaka na kuigharimia.
Alitaka wakashitaki kwa jeshi? Mahakama halali ya wanasiasa ni wananchi na si jeshi.
Kikwete na wenzake waje na hoja badala ya vitisho na uongo. Nchi hii ni mali yetu sote kwa usawa na inaendeshwa kidemokrasia na si kijeshi wala kibabaishaji. Kinachopaswa kushindanishwa ni nguvu ya hoja na si hoja za nguvu.
Kama Kikwete anataka lake ndiyo liwe basi hakuwa na haja ya kuunda tume ya Warioba. Hakuwa na haja ya kutupotezea pesa na muda kwa jambo ambalo ana jibu lake.
Tuhitimishe kwa, mosi, kulitaka jeshi litoe tamko na karipio. Pili, kuwataka wanaotaka kutuchonganisha na jeshi letu wakome vinginevyo watakiona hicho cha mtema kuni wanachowatishia wenzao.
Wakumbuke na kutambua: Cheo ni dhamana na wao wapo pale kwa muda tu kufanya tuliyowatuma si yale wanayojituma.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 14, 2014.
2 comments:
Sasa huo upembe wa ndovu unapelekwa wapi Mhango?
Sam,
Unauliza jibu ndugu yangu? Upembe unakwenda market kupiga njuluku. Huoni jamaa alivyoshiba fedha ya ujangili? Je tunao wangapi kama hawa wanaotumia crown kutumaliza? Wana bahati Luteni Kanali Jakaya Kikwete mwenzao yuku ikulu akila kwa mikono na miguu tena bila kunawa.
Post a Comment