How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 7 May 2014

Muungano wa Tanzania ni kama haujawahi kuwapo

MKINZANO, mtifuano hata harakati tunazoshuhudia kwa sasa kuhusiana na muungano vinafichua kitu kimoja: Muungano wetu kama upo au uliwahi kuwapo basi ni wa watawala lakini si wa wananchi. Tuna sababu nyingi za kuamini hivyo.
Ngoja tuanze kwa maswali rahisi japo yanahitaji majibu magum. Kumetokea utata kuhusu uhalisia wa nyaraka za muungano.  Mwanzoni utatu ulikuwa ni wapi zilikuwa hizi nyaraka (articles of Union) ambazo ziliwasilishwa juzi baada ya kusitasita na visingizio vingi toka kwa watawala.
Wapo waliosema kuwa zilikuwa Umoja wa Mataifa. Wengine walisema zilikuwa bungeni bila kuziendea na kuzionyesha.  Mpaka leo baada ya nyaraka husika kuonyeshwa imekuwa vigumu kujua zilipokuwa na ni kwanini ilichukua muda mrefu kuzionyesha?
Wapo wanaosema kuwa hazikuwapo. Hivyo, kusuasua kulikuwa ni kutoa fursa kuzichonga. Je zimewahi kuwapo au ni yale ya waanzilishi kufanya mambo kienyeji?
Aliyekuwa katibu wa Bunge wakati kinachoitwa Muungano kikifanyika Pius Msekwa alisema kuwa hakuwahi kuona hati za maridhiano ya muungano.  
Je hizi tulizoletewa juzi ni nini? Je muongo kati ya Msekwa na waliotuletea nyaraka zenye kutia shaka ni nani? Msekwa alikaririwa na vyombo vya habari kabla ya nyaraka chongwa kuletwa, akisema, “Ana lengo gani la kutilia shaka, ana lengo gani la kusema imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original ambayo iko ofisi ya Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia mate wakati wino upo?”
Hata hivyo, kuna vyombo vya habari vilivyomkariri Msekwa huyu huyu akisema hajawahi kuziona nyaraka husika bila kukanusha. Ukweli ni upi?
Je, hapa Msekwa anamaanisha hati gani iwapo anasema hajawahi kuiona? Na kama anasema hajawahi kuiona hiyo anayosema ina sahihi yake ni hati ya nini na ya lini na ya nini?
Ajabu ya maajabu aliitwa Msekwa huyu huyu ambaye hajawahi kuona hati za muungano kutoa maelezo ya saini yake na ya marehemu baba wa taifa kuhusiana na zinazoitwa hati za muungano!
Hati zipi iwapo mhusika anasema hajawahi kuziona hati za kuridhia muungano? Je hizo zenye saini za kutia shaka ni hati za nini? Na ni nani alizichakachua na kwanini?
Ni jambo la aibu na hatari kwa taasisi kama serikali inayopaswa kufuata na kusimamia sheria na kuaminika kuja na vitu vyenye kuchakachuliwa.  Je serikali ya namna hii bado ina uhalali wa kuongoza?
Kwa namna muungano ulivyofanyika haraka bila ridhaa ya wananchi, kuna uwezekano ukavunjika kirahisi tu. Maana hata wale waliouasisi hawapo tena. Si hilo tu, wakati wa kuwa na muungano wa wananchi umewadia.
Tuanzie pale walipoanzia na kuachia waasisi na kuufanya muungnao wetu uwe wa kisheria na unatokana na kukubalika kwa wananchi. Vinginevyo, mizengwe, uchakachuaji na ubabaishaji havitufikisha popote.
Kwa namna hali ilivyo, kama nyaraka zilizoasisi na kuridhia muungano zitabainika kuwa feki, hata waitwe magwiji wa propaganda na sheria, muungano utaendelea kuwa batili.
Kwa hali hii tatanishi, siku zote kile kilichodhaniwa kuwa ni muungano ni maridhiano ya viongozi wawili tena ya haraka tu. Hata kama muungano ungetimiza vigezo vyote kisheria bado unaweza kuvunjwa, kurekebishwa au kubadilishwa na wananchi kwa sababu muungano si wa watawala bali wananchi.
Viongozi huja na kuondoka lakini wananchi wapo siku zote. Isitoshe kizazi cha sasa siyo kile cha mwaka 64. Wahusika wanapaswa kujua hili.
Kwa maana hiyo kinachoitwa muungano si muungano bali hisia tu. Kwa hali hiyo basi, nchi husika zinaweza kurejea kwenye uhalisi wake kabla ya dhana nzima ya muungano au kuungana upya kama wananchi wataamua iwe hivyo.
Kama wataamua kuuvunja muungano, hakuna haja ya kuwalazimisha hasa ikizingatiwa kuwa kinachoitwa muungano kimekuwa ni migogoro na cha kulazimishwa tu bila kuwashirikisha wananchi wenyewe.
Kama wahusika wataendelea na ngonjera za “hati ni halisi”, Tanzania itabakia kuwa batili na yote yanayofanyika chini yake. Bila kuwasilisha hati halisi za muungano, kila kitu ni batili.
Hivyo basi, hata hili Bunge la katiba litokanalo na mamlaka ya muungano halipaswi kuwapo. Kwani nalo ni batili. Hata Wazanzibari waliopo bara au wabara waliopo Zanzibar wanapaswa kurejeshwa makwao mara moja na kuomba upya kuingia na kufanya kazi huko kwa taratibu za kimataifa.
Kwa hali hii ushishangae tunachokataliwa wananchi wengine wa mataifa yanayounda Jumuia ya Afrika Mashariki kikawakumba watanzania ambao watakuwa chini ya dhana batili.
Akitokea mjanja, (bila shaka wale wanaopinga muungano wa sasa watafurahi na kuuvunja kirahisi), wanaweza kufungua kesi ya kuzuia kila kitu kinachofanywa chini ya muungan, na wanaweza kushinda kirahisi kutokana na muungano kutokuwa na hati ya kuuthibitisha kisheria.
Hata hivyo, kwa sababu Tanzania ni nchi inayoruhusu kughushi huku wananchi wakivumilia jinai hii, huenda kadhia hii itamalizwa kwa kuletwa kwa hati za kughushi na ndipo hapo wahusika watafunika kombe na mwanaharamu akapita.
Hata hivyo, kwa hali tuliyo nayo kwa sasa hilo linaweza kufanya kazi kwa muda. Baadaye wajanja watasimamisha kila kitu kisheria.
Kama hakuna hati halisi, tungeshauri pande mbili ziache ukale. Kwanza, ziutangazie umma uwepo wa hali hii. Pili, zipitishe kura ya maoni kwa pande mbili kuhusu nia ya kuungana au kutoungana.
Kama umma wa pande zote utaridhia, masharti mapya ya muungano yaandaliwe na kupigiwa kura na wananchi. Kuepuka kutumia pesa nyingi, kura mbili yaani ile ya kutaka kujua kama wananchi wa pande mbili wanahitaji muungano au la na ile ya kueleza namna muungano utakavyokuwa zinaweza kupigwa kwa pamoja.
Tumalize kwa kuwahimiza wananchi kutokubali kupandikiziwa serikali au muungano.  Pia watawala wanapaswa kuelewa kuwa kizazi cha sasa kinataka mambo ya kisasa na si mawazo mgando na ya kale kama ilivyo.
Je, tumewahi kuwa na muungano tunaoutaka? Je hati tulizoletewa ni halisi au za kuchongwa?
Chanzo: Tanzania Daima Mei 7, 2014.

No comments: