How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Friday, 16 May 2014
Mlevi kuomba kazi sirikalini
Baada ya kugundua kuwa kuchonga na kuirushia sirikali madongo kunanirostisha ilhali mambo niliyosoma au kufundisha yakiwafanya watu kuwa mabilionea wa kutupwa, napanga kuomba kazi sirikalini ili kuchanga njuluku kirahisi.
Kuna kipindi bi mkubwa alitaka kunipa talaka kuhofia kufikwa ujane mapema au kushuhudia la aziz wake nikiozea lupango kwa kusema ukweli mchugu na wenye machukizo kwa wezi walao wenzao.
Nakumbuka maneno yake kana kwamba aliyasema jana: “We baba una nini na kakuroga nani kudhani utakikomboa kizazi cha laana kilichojiangamiza chenyewe?
Sana sana watakukolimba, kukatabaro hata kukumwangosi unitie machungu na ujane bila sababu.” Mwangwi wa maneno haya huniandama kila ninaposhuhudia uoza kama huu uliofichuliwa juzi ambalo limegeuka zoezi la kila mwaka la kutuongezea shinikizo la damu na moyo, nyongo na hata maji mwilini.
Hata hivyo, swali jingine nalo hunisumbua: Kama wote tutaendekeza ulafi na roho mbaya na upogo vizazi vyetu vitashindwa kukojolea makaburi yetu huku vikifukua mafuvu yetu kujua ni wapi tulikuwa tumeharibikiwa? Nikifikiria juu ya hili hofu hunijaa kiasi cha kupuliza mibangi kama sina akili nzuri.
Hakuna kitu kilinitekenya kiakili na kunichochea kusaka ulaji sirikalini kama ripoti ya hivi karibuni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hasara na Ulaji wa Sirikali.
Ripoti hii ilifichua kuwa kuna ngurumbili wanaiba “vizibo” tena mipembe ya ndovu kwenye vituo vya ndata na hakuna anayewakamata wala kuwastukia.
Kwa wasiojua, vizibo ni vizibiti au exhibits kwa lugha ya kinyasa.
Hivyo, baada ya kugundua kuwa undata, uafisa wa ubalozi ambako watu wanastaafu na kuendelea kulipwa huku wakitanua ughaibuni na mazabe mengine yanalipa, naachana na kuchonga.
Sina haja ya kufa kwa ugonjwa wa shinikizo la moyo mapema wakati kuna shamba la bibi kwenda kuhomola. Hata hivyo, inabidi nisukuti sana. Maana nikiangalia kulia na kushoto sioni kuwa na jamaa kwenye sirikali.
Sina baba wala mama wala rafiki zao wenye vifua humo. Na usawa huu wa kujuana ambao wasukuma huita nepotism, bila kuwa na refa wala mshitiri ujue inakula kwako.
Hivyo, kitu cha kwanza ni kughushi vyeti vya kitaaluma na kuonyesha kuwa ima mimi ni mtoto wa Makambae, Kikwetee, Nchimbie, Mwinyie, Mgimwae, Mzindikaya, Malimae au Nnauyee.
Kwa vile kaya yetu imegeuka ya kurithishana, lazima nichonge misheni ya kupata jina kubwa ili nipate ulaji mkubwa chamani au sirikalini. Nisipopata ulaji sirikalini basi nitafungua kampuni ya kukata tiketi za ndege ili niitoze sirikali nauli nitakavyo kama walivyofanya majambazi aliowafichua CAG hivi karibuni.
Hapa lazima nibadilishe jina kuwa Chavda, Patel, Vithlani au Chande kama siyo Manji au Azim.
Usidhani napayuka yote kutokana na gongo na mibangi.
Hasha. Hii kaya ni Bongo boondoogle. Yaani mijitu inajihomolea kana kwamba hakuna mwenye akili wala uchungu hata mmoja!
Kwanini nisijiunge na sirikali hii ambayo inajua kitu moja tu yaani ulaji? Kwanini kufa njaa wakati kuna neema kwenye shamba la chizi?
Najaribu kupiga picha nitakavyokuwa nafanya ujangili wa kutotumia bunduki, yaani kungoja ndata wakamate vipusa mie niende na kubeba na kuuza. Mie mjanja ati.
Sihitaji kwenda porini kupambana na mijoka na walinzi wa mbuga na mibunduki yao wakati naweza kuchukua kiulaini toka vituoni tena kwa kutoa kitu kidogo au kutumia krauni yangu, au vipi? Pia nafikiria kuomba kufanya kazi uwanja wa ndege hasa ule wa mzee Mchonga au KIA ambapo nitakuwa nikiruhusu mibwimbwi kupita na kukatiwa changu.
Kama sitapata kazi hapa lazima ning’ang’anie undata hasa ule wa kitengo cha kuzuia bwimbwi ambapo tutakamata bwimbwi na kubadilisha na unga wa mahindi huku tukiuza mibwimbwi mitaani ili kuzalisha mataahira wengi ambao hawatavuruga wala kubughudhi ulaji wetu. Nikishaukata naanzisha NGO ya kusaidia mateja ili nionekane najali walevi wa kaya hii.
Ikizidi ikapungua naanzisha dhehebu la dini na kujifanya mtu wa God hata kama nyuma ya pazia ni muuza bwimbwi wa kutisha na kunuka.
Kwani hamuwaoni wauza bwibwi wakubwa waliojificha kwenye majoho wakitema cheche kwenye mahekalu? Kunogesha dili nakata kadi ya chama tawala ili nionekane mkereketwa hivyo asitokee kinyangarika wa kugusa ulaji wangu.
Ukereketwa hata kama ni wa kukeketwa unalipa au vipi?
Naona yule anachekelea mipango yangu akidhani ni ya kilevi. Kwenye kaya hii ukijivunga unaliwa badala ya kula. Nani anataka kuliwa?
Heri kula wengine kuliko kuliwa mimi kama wanavyoliwa wadaganyika. Naona yule anazidi kutikisa kichwa na kucheka akidhani hii ni mipango ya Pwagu na Pwaguzi.
Wenzenu wanakula na kunona kama paka wa dukani wakati nyinyi mkikonda kama vijisindano bado mnaona mambo mswano.
Shauri yako na karagabaho. Siku hizi sera ni kupeana na kuhomola. Mnapeana hata kurithishana ulaji walevi wanahanikiza.
Mnajifanya hamnazo wala hamna macho na masikio kusikiliza vilio vyao hata waandike na kutangaza kwenye radio na runinga. Kwanini nami nisitafutie vitegemezi vyangu urithi wa ulaji kama wale wanaotawazana na kurithishana hata viti vya maulaji?
Kama jogoo aliwafundisha vifaranga kupuu ndani kwanini mimi nisiwafundishe vitegemezi vyangu jinsi ya kuchanga njuluku za walevi ambao kwa sasa wamegeuzwa shamba la chizi?
Hivi nitashindwa nini kuukata wakati hakuna hata sheria moja inayonibana kutaja nilivyotengeneza ukwasi wangu kijambazi?
Kwa vile nina usongo wa kuukata kabla shamba la bibi na chizi halijastuka baada ya kuja wenye akili, acha nikapate misokoto kama miwili hivi na gongo niingie viwanja.
Leo salamu zangu ni kwa wavuta bangi wote wanaovuta kwa sababu ya kudai haki. Legalize it now like you did with graft.
CHANZO: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment