How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 7 May 2014

Kijiwe chalaani vitisho ufujaji na urushi

BAADA ya Joni Kombo kuchafua hewa kwa kutishia kwenda msituni kupigania upuuzi, kijiwe leo kimekaa kama kamati ya kulaani upuuzi huu.

Pia kinalaani kauli mbili za Njaa Kaya za kudai kuwa maadhimisho yaliyopita ya muunganiko yalikuwa ni kwa geshi kutishia wachovu na ubabaishaji na ufujaji wa njuluku za umma zilizotumika kwenye ushufaa uchwara wa maadhimisho ya vitisho.
Mpemba anaingia akiwa anavuta tasbihi yake huku akiwa amenuna kama vile ameletewa habari mbaya. Analianzisha, “Yakhe mmesikia hizi tambo baada ya mipashoo ya wajivuni na walevi wa madaraka?”
Kapende anadakia, “Kaya hii ni ya tambo, mipasho, ubabaishaji, mitusi na michosho. Unaongelea tambo na michosho ipi au ni ile ya Bunguu la Katiba?”
“Yakhe hiyo mipasho ya Bunguu la ulaji tushaichoka kiasi cha kuizoea hata kama yakera wallahi. Mie naongelea hii mpya ya Joni Kombo kusema eti atakaenda mwituni kupigania sirikali mbili kama tatu zitapita na ule uongo wa Njaa Kaya kusema eti apewe majina ya wanaoruhusu bwimbwi kupita viwanja vya ndege awashughulikie.” Anajibu Mpemba huku akisogeza kahawa yake vizuri kwenye meza.
Mipawa anadakia, “Huyu tushamzoea. Hana sera wala jipya bali kuishiwa na kutaka ujiko. Hakuna aliponiacha hoi kama hayo madai ya kutaka majina mapya ya wavusha bwimbwi wakati yale ya wauza ameyaatamia miaka nenda rudi.
Kama anataka majina ya wauza bwimbwi akawaulize akina Rei C na mateja wengine anaowatumia kujifanya ana huruma na vijana wakati ameacha waharibiwe na mibwimbwi yao.”
Msomi anampa gazeti Mchunguliaji na kunyaka mic, “The guy is bust and fraught.”
Kabla ya kuendelea mzee Maneno anamuonya, “Msomi lugha hiyo.”
“Samahani. Huwa nikipandisha mzuka naongea ukameruni kuonyesha kuwa nimesoma na si kughushi kama akina Lukuvii na wenzake. Hata mimi kusema ukweli jamaa aliniacha hoi hasa pale alipodai kuwa maadhimisho ya juzi yalikuwa yanalenga kututisha ili tukubaliane na sera mfu za kuimeza Danganyika. Jamaa angejinyamazia afunge virago na kutuachia balaa lake la miaka nenda rudi akimaliza ngwe yake.”
Mijjinga aliyekuwa akizozana na muuza kahawa kwa kumjazia sana anaamua kukwanyua mic, “Wote waseme hata kifutu Joni Kombo naye. Eti anasema atakwenda msituni kudai sirikali mbili.
Kwa nguvu ipi wakati amefura. Kama kwenda msituni ni deal aende gymn akapungeze unono. Hata kuimba kwenyewe hawezi tena zaidi ya kukoroma baada ya kufakamia ulaji na kunona utadhani anataka kujaa kwenye ramani ya kaya.”
Kijiwe hakina mbavu kwa jinsi Mijjinga anavyomkandia Joni Kombo anayetoa mawazo ya kimakombokombo.
Mgosi aliyekuwa kimya akibofya ki-tablet chake kipya anaamua kutia guu, “Hata mimi niicheka sana kusikia eti Joni Kombo naye anataka kututishia nyau kama Ukuvi na Njaa Kaya. Wameishiwa hawa.
Wamemtukana mzee Wayoba na kuishiwa sasa wanaanza vitisho vya kitoto na kijinga. Hakuna kitu kimeniuma hadi nikasusa kushiiki huu upuuzi kama pae Njaa Kaya aliposema eti wanaadhimisha vitisho na si muungano.
Hawa jamaa wana roho mbaya sina mfano. Yaani sisi tinakufa kwa ukapa wao wanafuja mabiiyoni kwenye kututisha! Walaaniwe wote.”
Bi. Sofi Lion aliyekuwa amefura baada ya kumnong’onezea jambo Kanji anaamua kuonyesha unazi wake, “Jamani tuseme mara ngapi muelewe? Hivi kusema kuwa geshi linaadhimisha muunganiko kwa kuonyesha zana na misuli yake ni dhambi hivyo? Mlitaka asemeje iwapo kazi yake ni kulinda kaya?”
“Dada Sofi kubali umeishiwa. Sasa kuonyesha misuli na muunganiko wapi na wapi? Kama hakuwa na la kusema si angejinyamazia kuliko kujivua nguo? Hata hivyo, hatishiki mtu. Hivi mchovu kama Joni Kombo anaweza kumtisha nani iwapo mwenyewe hajiwezi?”
Mijjinga anakwanyua mic tena, “Mie jamaa aliniacha hoi aliposema eti wanamuenzi mzee Mchonga. Wameuenzi kwa lipi wakati wamejilimbikizia mimali ya wizi? Huyu Kombo anadhani mambo yake na alivyotumia pesa ya wamalawi kujipatia shule zake hatujui?”
Kabla ya kuendelea Kanji anaingilia kati, “Sasa Jinga ongopa sana. Veve nadhani kuita shule Bakili Muluzii diyo iba pesa Malavi?”
Mijjinga anajibu, “Kama si pesa ya Maravi kwanini hapana ita shule yake mzee Chonga kama yule gabacholi Saabodo ambaye yeye naenzi yeye kwa kutengeneza juluku. Hii hapana enzi yeye. Nasanifu yeye kama ile toa nishani feki wakati iko fuja zuri yote Chonga naacha.”
Kijiwe hakina mbavu jinsi Mijjinga anavyomuigiza Kanji.
Mpemba anarejea tena, “Wote waongo wallahi. Wawezaje muenzi mzee Nchonga kwa kufuja njuluku zetu huku wakitutishia nyau? Kama vitisho mali, wakawatishe wake na mama zao hatishwi ntu hapa.”
Mgosi Machungi anaamua kuongezea, “Ami hapo umisema. Hatishwi mtu hapa. Mimi nazani tiwabane watiambie ni kwanini wanachezea njuuku zetu kwa kuzitumia kwenye mambo ya hovyo badaa ya mambo ya maana. Hatiwezi kueendeea kufumbia macho upuuzi huu. Wamekuwa wakizurura. Timevumilia. Wametitishia timevumilia. Hili sasa halivumiiki jamani. Tifanye kitu kieeweke.”
Msomi anakohoa kidogo na kunywa kahawa yake na kupoka mic, “Kama alivyosema mzee Waryuba, hawa jamaa wameishiwa hoja sasa wanataka kutumia nguvu kwa kuogopa kuondoshwa kwenye ulaji na kufichuliwa mazabe yao. Waache waendelee kujidanganya. Kila chenye mwanzo kina mwisho. Kuna siku wataishia lupango kwa walivyotuibia, kuchezea na kuibaka kaya yetu.” 
Mchunguliaji anampa gazeti Kapende na kunyakua mic, “Mmesikia kuwa Lukuvii ametimkia ugabacholini kwenda kutibiwa baada ya kijiwe kupanga kumfanyia kitu mbaya? Bahati yake. Asingekimbia, nilikuwa na mpango wa kwenda kumshikisha adabu. Huyu Kombo niachie. Nitamtafuta nimfanyie kitu mbaya sana ili liwe somo kwa wengine.”
Sofi haridhiki, “We acha rongo rongo. Huna ubavu wa kumshikisha adabu mtu. Mkeo mwenyewe anakushikisha adabu.”
Mchunguliaji anaamka kwenye benchi akimwendea Sofi. Anasema, “Ngoja nikushikishe wewe adabu ili ukawaambie walevi wenzako wa maulaji. Siogopi mtu ati.”
Baada ya kugundua kuwa Mchunguliaji hatishii tunaamua kumzuia na kila mtu anaondoka kwa njia yake kuepuka zegele ambalo lingetuletea ndata.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 5, 2014.

No comments: