Kumekuwapo visa vya walinzi kuiba kwenye malindo yao, wafanyakazi wa maofisini kuiba kazini mwao na hata wanafamilia kuibia familia zao. Kinachokera ni kwamba baadhi ya wenzetu wameanza kuukubali na kuuzoea mchezo huu mchafu ambao ni mauti kwa taifa. Kushamiri kwa matukio ya wizi unaowahusisha watu wa ndani ya taasisi si jambo jema kwetu kama jamii. Huu ni ushahidi tosha kuwa mamlaka zinapaswa kupambana na hali hii inayoanza kuzoeleka kiasi cha kuchafua sifa nzuri ya taifa letu.Tukio la hivi karibuni ambapo meneja wa tawi la benki ya Barclays la Kinondoni lililoibiwa pesa hivi karibuni kukutwa alisuka ni ushahidi wa kushamiri kwa jinai hii. Katika wizi huu Sh392 milioni za Tanzania, Dola 55, OOO za Marekani, Euro 2,150 na Paundi za Uingereza 50.
Watuhumiwa wote wako chini ya miaka 40 na idadi yao ni 13 wakihusisha wa ndani ya benki na wan je. Ni jambo la aibu kugundua kuwa hata meneja wa benki husika aliyepaswa kufichua wizi huu alishiriki pamoja na msaidizi wake kama walivyokiri kwa polisi. Ukiangalia kiwango cha fedha kilichoibiwa na idadi ya waliosuka jinai hii, unagundua upogo na ujinga, tamaa na hatari ya wahusika. Je wahusika hawakusoma maadili kwenye taaluma zao kama wanazo? Je tatizo hapa liko wapi kati ya wahusika na mfumo uliowatengeneza? Tujalie kuwa wahusika wangefanikisha wizi wao. Baada ya kugawana sana mwenye kupata nyingi ingekuwa ni shilingi milioni 30. Utazifanyia nini? Hata hivyo, kwa kijana wa miaka 30 ambaye hajafanya kazi kufikisha hata miaka 10 bado pesa hii ni kubwa tu.
Inasikitisha kusema kuwa Tanzania imegeuka nchi ya vibaka kutokana na kutokuwapo na sheria zinazowataka raia wake kueleza walivyopata utajiri wao. Kama viongozi wakubwa wanaopaswa kusimamia maadili, kanuni na sheria wanapata kigugumizi kutaja utajiri wao unategemea nini? Je huu si ushahidi tosha kuwa hawa viongozi nao wameongoza kwenye kushamirisha jinai hii? Je namna hii tunategemea kupungua kwa jinai hii ya kujiibia kama watu binafsi, taasisi na taifa? Je viongozi waliopata utajiri wa haraka kwa njia haramu ya kuliibia taifa wanaweza kusimamia maadili na kuhakikisha kadhia hii inaondoshwa mara moja iwapo nao wanaishiriki? Je wananchi nao ambao kimsingi ndiyo waathirika wa jinai hii wanashindwa nini kuingia mitaani kudai ikomeshwe au hata kuwalazimisha wawakilishi wao kutunga sheria za kupambana na ukosefu huu wa uaminifu, uzalendo na maadili?
Japo tumejiruhusu kama taifa kuendekeza udokozi na ujambazi wa wazi, tujue kuna gharama huko tuendako. Maana kama jinai hii haitaondoshwa, uwezekano wa kuaminiwa kama taifa ni mdogo. Na mkiendelea hivi hata hao wawekezaji mtawakosa au mtajikuta mkilazimishwa kufufua maadili ambayo mliyageuza madili. Hali haiwezi kuendelea hivi bila kudhibitiwa. Hata hili wimbi la ukosefu wa usalama chanzo chake ni hali hii ya kubariki wizi wa wazi wazi ambapo mtu analala maskini na kuamka tajiri. Hiki ndicho kichocheo cha kushamiri kwa ujambazi, ujangili, mihadarati na kila aina ya jinai.
Hali ni mbaya. Imefikia mahali hata taasisi za umma zinachochea vitendo vya uhalifu kama huu. Hivi karibuni, kwa mfano, Shirika la Nyumba (NHC) lilitangaza kuuza nyumba zake. Ukiangalia masharti yaliyotolewa kwa wanaotaka kununua, unagundua jinsi taifa letu linavyogeuka taifa la kijambazi. Hili linahitaji Makala ya pekee kuonyesha jinsi taasisi za umma kama NHC zinavyosaidia kuchochea wizi na ujambazi.
Nadhani ni Afrika tu ambapo mtu anaweza kuchuma mali bila kutakiwa kisheria kueleza alivyochuma ukiachia mbali hata kutoulizwa kama mali husika inalipiwa kodi. Matokeo yake ni kwamba tunao watumishi wa umma waliotumia nafasi zao kupata utajiri haramu wa haraka bila hata wasi wasi. Hiki ndicho chanzo cha kushamiri biashara ya madawa ya kulevya, ujambazi, wizi, ufisadi, rushwa, uzembe, ubabaishaji, utapeli na jinai nyingine nyingi. Vyote hivi vinashamiri kutokana na kuwapo mazingira mazuri ya kumilki utajiri uliotokana na jinai bila kutakiwa wala kuandamwa na mamlaka kueleza mhusika amepata utajiri vipi. Hiki ndicho chanzo cha magenge ya kijambazi ya kimataifa kupenda kuja kuwekeza Tanzania. Wanajua watafanya kila watakavyo kuvunja sheria na kuchuma na hakuna atakayewagusa wala kuwashughulikia. Hali hii inaondosha sifa ya kuwa taifa. Sana sana tunaelekea kuwa taifa lililoshindwa kutokana na kubariki jinai na kuendekeza upogo, uroho, ubinafsi na jinai.
Hali ni mbaya sana. Kumekuwapo visa vya baadhi ya polisi wasio waaminifu kushirikiana na majambazi. Kuna visa ambapo mawaziri wamekuwa wakiingia mikataba ya kijambazi ya uwekezaji baada ya kukatiwa chao. Matokeo yake tumekuwa nchi ya kulalamika na kutofanya vizuri kiuchumi. Mifano na matokeo ya ujambazi huu wa kimfumo ukiachia mbali tukio la waajiriwa wa benki tawi la Kinondoni kujiibia. Makampuni kama IPTL, Symbion (Richmond ya zamani) na mengine mengi yaliyoingia mikataba ya kuzalisha nishati kifisadi yanaendelea kuingiza nchi kwenye maafa ya kiuchumi. Nchi imetekwa kiasi cha kuwa majeruhi wa mafisadi papa wanaoshirikiana na viongozi wakubwa tu. Mfano, hakuna mtanzania asiyejua kuwa IPTL imekuwa ikitulangua umeme ukiachia mbali kuchafua mazingira. Pamoja na hatari yote hii, wakubwa zetu wamekataa kuendeleza vyanzo vingi vya umeme tulivyojaliwa na Mungu kwa kuogopa kupoteza maslahi yao ya kijinai. Tumegeuka taifa la hovyo kama Nigeria ambayo hivi karibuni ilifichuka kashfa ya wauza jenerata wanaoshirikiana na watawala kuzuia nchi hii kuwa na vyanzo huru na imara vya umeme kwa kuhofia kuingilia maslahi ya wauza jenereta. Ni aibu kiasi gani kwa taifa kuweka mifukoni mwa wahalifu? Je haya tunayoandika ni uongo au uzushi?
Mifano ipo kila mahali iwe midogo au mikubwa ya sasa na ya zamani. Tubadilike kabla hatujaliangamiza taifa kwa sababu za uroho na upogo.
Chanzo: Dira Mei 2014.
2 comments:
Mwalimu narekebisha kidogo hapo Ulipoaandika Richmond ya Zamani, nadhani maelezo sahihi ni kuandika Richmond alimzaa akina Dowans akamzaa Symbion. Kifupi wote ni ndugu hao(kama mkulima wa bangi akipanda anavuna bangi kamwe haitatokea kuwa mchicha)
Anon shukrani sana ujumbe wako umefika nitaufanyia kazi siku nyingine nikiandika kuhusiana na zengwe na jinai hii. Ubarikiwe sana na karibu tena na sana kibarazani.
Post a Comment