The Chant of Savant

Wednesday 17 December 2014

Tunapoadhimisha miaka 53 ya Udhuru!

Kila Desemba 9 kila mwaka Tanzania huazimisha siku ya uhuru wake. Ni siku ya kutafakari tulipotoka, tulipo na tuendako. Kwa wenye kufuatilia historia ya taifa, watakubaliana nasi kuwa uhuru wetu haujakidhi matarajio ya umma. Kwani, bado tu maskini, tegemezi, hovyo na taifa la kifisadi.
Japo watawala wakijisifu kutenda ‘mengi’, wananchi hawaoni la maana lililotendeka, na kama lipo, ni kidogo ikilinganishwa na matarajio yao. Wengi wanahoji hata huu uhuru ambao unaonekana kutoa fursa kwa wachache kuwanyonya, kuwaibia hata kuwahujumu wengi. Rejea kutamalaki kwa kashfa zinazohusisha wizi wa mabilioni ya shilingi huku umma wa watanzania ukiendelea kuwa maskini kila uchao.
Hivyo, katika kuadhimisha miaka 53 ya uhuru wa Tanzania, watanzania wamesherehekea kwa makundi hata matabaka. Kwa mfano, kwa wakulima wanaoendelea kulanguliwa mazao yao na hali zao kuzidi kuwa mbaya hawaoani cha kusherehekea. Maana, uhuru ni kuwa na maisha bora na uchaguzi mpana katika maisha. Ni kuwa na nguvu ya kuchagua. Hatuwezi kujidai kuwa tuko huru wakati polisi wetu bado wanaua raia wasio na hatia, uchumi wetu unaendelea kuwa tegemezi huku bajeti yetu ikitegemea wafadhili kwa zaidi ya aslimia 40.
Hatuwezi kuwa huru bila uwajibikaji na uongozi bora, mipango madhubuti, haki na utawala wa sheria. Kama kuna wanaosherehekea uhuru si wengine bali wale wanaoutumia kujitajirisha ghafla bin vu kama vile watawala, mafisadi na wezi wa fedha za umma ambao hawaguswi. Sijui kama wagonjwa wanaorundikwa kitanda kimoja huku wengine wakiombwa hata rushwa walikuwa nalo la kusherehekea. Sijui kama wajawazito wanaojifungulia ima sakafuni au nje ya zahanati na hospitali walikuwa na la kusherehekea. Wenye ubavu wa kwenda kuangaliwa afya zao na kutibiwa ughaibuni hata baada ya kuvuruga  uchumi na huduma za jamii walikuwa na cha kusherehekea kwa vile wako huru kwenda kutibiwa nje wao na familia zao kwa gharama ya kodi ya makapuku wa taifa hili wana kila sababu ya kunywa na kufurahia uhuru huu wa kufanya watakavyo.
Je wanafunzi, hasa wanaosoma kwenye shule za kata au kukalishwa sakafuni, walikuwa na cha kusherehekea? Sijui kama vibaka wanaochomwa moto huku mibaka ikikingiwa kifua na wakubwa walikuwa na cha kusherehekea. Sijui kama mashahidi wa ufisadi wa kunuka walikuwa na cha kusherehekea. Kama kuna waliosherehekea tena kwa kujisikia si wengine bali wale wachache wanaofaidi keki ya taifa. Wauza unga wanaotajwa na kujulikana wasichukuliwe hatua walikuwa na cha kusherehekea lakini si waathirika wa mihadarati.  Wakubwa walioghushi vyeti vya kitaaluma au kupata fursa ya kuiba na kuficha fedha nje walikuwa na la kusherehekea. Wakubwa wenye hisa kwenye makampuni tunayoambiwa ni ya uwekezaji walikuwa na cha kusherehekea. Wale wote wanaolipwa mafao ya kustaafu hata bila kustaafu wana kila sababu ya kusherehekea.
Hata hivyo, kama ukiangalia takwimu (ambazo mara nyingi huficha uongo) za tulikotoka na tulipo, hasa mchango mkubwa wa serikali ya awamu ya kwanza, kuna baadhi ya mambo ya kujivunia. Mfano, kiwango cha wenye elimu kimeongezeka ingawa ubora wake haukufanya hivyo. Tunazo zahanati na hospitali nyingi alizojenga Mwalimu Julius Nyerere japo hazina madawa wala zana sasa. Kuna barabara japo mbovu na zinazotumiwa na maafisa fisadi wa serikali kupata cha juu. Je ubora wake ni sawa na uhuru wenye umri wa miaka zaidi ya 50?
Tofauti na wakati wa ukoloni, tunayo demokrasia ambapo kila baada ya miaka mitano tunakwenda kwenye uchaguzi ambao hata hivyo si huru na wa haki bali uchakachuaji na matumizi mabaya ya fedha ya walipa kodi. Hata hivyo, bado ‘demokrasia’ yetu licha ya kuwa ya mizengwe, bado inafadhiliwa toka nje. Je namna hii kuna la kujivunia zaidi ya kutafakari?
Ukiuliza wanasiasa watakupa mlolongo wa mafanikio ambayo ukiyaangalia kwa makini hayalingani na umri wa uhuru wetu wala matarajio ya watu wetu. Watu wetu vijijini hawana barabara za uhakika, umeme wala huduma za maji, wanaishi kana kwamba wako kwenye karne ya 17 ukiachia mbali kuwa na vijisimu vya bei nafuu vya mkononi. Je hawa wana cha kusherehekea kwenye maadhimisho ya miaka 53 ya uhuru unaoonekana kuwa udhuru kwao? Sijui kama mwanamke anayeendea maji kilometa tano ana la kusherehekea.
Huwezi kuwa huru wakati tofauti baina ya walio nacho wachache na wasio nacho wengi ikizidi kuongezeka. Uhuru ujengwe kwenye kutatua matatizo ya taifa ambayo yanajulikana kuwa ni ujinga, maradhi, uvivu, ufisadi, dhuluma, ubinafsi, ujambazi, njaa na mengine mengi ambayo yanafumbiwa macho na utawala wetu ambao sana sana unayazidisha. Rejea matumizi mabaya ya fedha za umma ambayo yamesababisha deni la taifa kuumka bila maelezo yenye kuingia akilini.
Tumalizie kwa kusema wazi kuwa wakati wa maadhimisho ya miaka 53 ya uhuru wapo ambao hawakuona cha kuadhimisha wala kusherehekea zaidi ya udhuru kwao binafsi na taifa. Huwezi kuwa na taifa linalohalalisha wizi, uvivu, ufisadi, ukabila, kujuana, kulipana fadhila, uchakachua na hata mauaji ya raia ukasema uko huru. Je wahanga wa jinai hizi ni huru au si watanzania? Tujisute, tutafakari na kujifunza kutorudia makosa au kuendelea na kitu kile kile ambacho waingereza husema ni wehu.
Chanzo: Tanzania Daima leo.

No comments: