Baada ya waishiwa kulipua kazi ya kuwalipua majambawazi wa escrow, Kijiwe, japo hakikuridhika na hukumu ya waishiwa, kimeamua kusonga mbele kwa kushguhulika na wengine ambao hawajashughulikiwa. Wiki hii Kijiwe kinakaa kushinikiza waliotorosha wanyama wetu wafungwe huku kikitaka wanyama wetu warudishwe.
Mpemba analianza, “Yakhe mwatafsiri vipi hiki kiini macho kiitwacho hukumu ya gabacholi alotorosha wanyama wetu? Je hii haki kuhukumu mtu mmoja tena kuwadi wakati walomtumia wakiendelea kutesa na kuua wanyama wetu?”
Kapende anampoka mic na kuchonga, “Ami usinikumbushe. Niliposikia kuwa Kamlaaniwa yule habithi wa Kipakistani aliyetorosha wanyama wetu amehukumiwa miaka 60 jela wallahi nililia. Hii imenichefua na kunichafua. Inakuwaje wahukumu wakala wa majangili wenye madaraka badala ya mabwana zake wanaojulikana?”
Sofia Lion aka Kanungaembe hangoji leo. Anakula mic kwa usongo, “Watu wengine kwa kupenda kujisemea bila ushahidi, wanakera. Unaweza kututajia hao mabwana zake Kamlaaniwa unaodai walimtumia na hivyo walipaswa kufungwa? No research no right to speak?”
Kijiwe hakina mbavu jinsi Sofi anavyoamua kuonyesha kuumanya ung’eng’e.
Kapende akiwa anamtazama Sofi kwa dharau anakatua mic na kusema, “Kwani wewe huwajui? Unaishi wapi dadangu?”
Sofi anadhani kampata mbaya wake. Anachemka na kusema, “Ninaishi kwenye nyumba. Kwani unadhani naishi pangoni? We tutajie hawa unaowatuhumu kumtumia Kamlaaniwa finish.”
Kapende anacheka na kusema, “Basi kama unajifanya huwajui leo utawajua. Wa kwanza ni mkuu mwenyewe ambaye lisirikali lake limekaa kimya hata bila kutoa maelezo. Rejea alivyomteua aliyekuwa katibu wa wizara ya mali ya kuibiwa na utalii dk Laddie Komba kuwa balozi UG. Kwani hatujui?”
“Kapende acha nikuongezee. Wengine waiotoosha wanyama wetu ni seikai ya Katai ambayo dege lake la kijeshi lilitumika kusafirsha hao wanyama hapo Novemba 24, 2010. Mbona hawa Interpol wanaodanganya wanamtafuta Kamlaaniwa hawataji seikai ya Katai ambayo ni mtuhumiwa na mnufaika nambai wani?” Mgosi Machungi anaamua kutoboa.
“Dada nadhani umeridhika au nikuongezee?” Anasema Kapende huku akimtazama Sofi kwa tabasamu la dharau.
“Kama uhuni basi wote tunaujua. Basi niongezee.” Anasema Sofi kwa kuudhika.
Baada ya Msomi Mkatatamaa kugundua kuwa maongezi yanaanza kuchacha anaamua kuingilia kati akisema, “Da Sofi na wengine wenye mawazo kama yako, hata kama ni haki yenu kuamini mnachotaka, ukweli ni kwamba kila mtu anajua walioshiriki uhujumu huu. Hata ndege wenye ubongo mdogo wanajua fika kuwa dili hili lisingeweza kukamilika bila wanene kujua wala kushiriki. Nadhani hii ni escrow nyingine au tuseme Richmonduli kama siyo EPA nyingine.”
Anakohoa kidogo kutokana na moshi wa sigara kali uliofurumushwa na Mijjinga na kuendelea, “Tatizo la wezi wa kaya yetu ni kudhani sote tu taahira au vipofu kama wao. Hivi inawezekana mnyama kama twiga akamatwe, kusafirishwa tena kuelekea uwanja wa ndege mamlaka yasijue? Hao uhasama wa taifa na ndata wanafanya kazi gani na ni wa nini kama hawawezi kugundua vitu rahisi kama hivi?”
Mijjinga anatupa kipisi cha sigara na kuramba mic, “Msomi usiniambie habari za uhasama wa taifa wala ndata. Hawa lao moja. Wakubwa zao wakikatiwa chochote kidogo wanageuka vipofu wasioweza kuona hata tembo wala twiga pamoja na ukubwa na urefu wao.”
“Usinichekeshe. Kama juzi juzi dege la rahisi wa Uchina linasemekana kuondoka na tani za pembe za faru na ndovu, unataka nini zaidi kujua kuwa hata kwenye utoroshaji huu wa wanyama wanene wamo?” Anazoza Mipawa.
Kanji naye anaamua kula mic, “Siku yote hapana mimi unga kono wazo yako. Siku yote mimi dhani nyinyi chochezi. Leo naona sema kweli mpaka nafungua mimi. Hapa iko namna dugu zangu.”
“Amekufungua wapi na vipi Kanji? Chunga hiyo lugha watakufugua kweli uanze kulalamika bure.” Anatania Mbwamwitu huku akitaka kugongesha mkono na Kanji ambaye anakataa.
“Tuache utani. Danganyika ni kaya pekee chini ya jua ambayo ina wakuu na vyombo vya usalama ambao wanaweza kuruhusu jinai hii. Sijui ni kwa vile wanaishiriki au la. Maana walipotoroshwa hawa wanyama, waziri wa Utalii na Mali ya Asili, waziri wa ulinzi na Usalama, waziri wa mambo ya ndani, waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji na hata lisirikali lote walipaswa kuwekwa kando kuchunguzwa hata kufungwa. Hawa ndiyo walipaswa kuhukumiwa miaka 60 korokoroni. Nani alifanya hili? Watajiwajibisha vipi wakati wachovu walikaa kando na kuangalia kana kwamba hawa wanyama si mali yao?”
Mheshimwa Bwege aliyekuwa akisoma gazeti anaamua kutia guu, “Jamani mliyosema yanachusha na kuhuzunisha. Tuombe Mungu jamaa wamalize ngwe yao ili wenye akili waje huenda watasafisha kaya hii iliyogeuzwa shamba la bibi. Maana haiwezekani wanyama wakubwa vile wasafirishwe bila kujulikana na halafu mtuhumiwa eti awe mmoja tena raia wa kigeni. Huu ni uchavda mwingine. Mnakumbuka skandali ya Chavda alipopewa mashamba akaishia kuyatumia kuchukua mamilioni toka Benki bila kuyaendeleza? Alipobainika wakubwa walifanya nini zaidi ya kumfukuza nchini ili asiwataje? Nalo hili mmelisahau?”
Mgosi anavunja watu mbavu kwa kusema, “Huyu mwizi nilimiona Upanga akitanua na bila shaka analindwa na ndata wetu nilioshuhudia wakihongwa na Harbinger Seti Singasinga hivi kaibuni.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si lakipita shangingi la jaji aliyempa dhamana Kamlaaniwa! Tulimtoa nje na kumfanyia kitu mbaya japo vyombo vya umbea havikuinyaka.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano.
2 comments:
Wanyama hawa waajabu kweli wamepnda ndege wenyewe, kama unavyojua sisi nchi ya miujiza. waakti wetu wa kuvuna unafikia sasa uchaguzi huo wateja wetu ni nani hasa wanaokuja kwenye tunguli?
Anan,
Fumbo lako kubwa kweli kweli. Sijui niite fumbo la imani Nonihino alikufa nonihino alifufuka au nonihino alitumwa na nonihino ni kipenzi cha nonihino?
Post a Comment