Vyombo vya habari viliripoti hivi karibuni kuwa kampuni tata ya Independence Power Tanzania Limited inayotuhumiwa kuliibia taifa zaidi ya shilingi bilioni 200 ilifungua mashtaka mahakamani kutaka Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) akamatwe. Tuseme mwanzoni kabisa kuwa hatutaki kujadili kesi zilizoko Mahakamani. Hivyo , tunachojaribu kudurusu hapa ni dhana nzima ya kuchezewa kama taifa huku wakubwa zetu wakiendelea kujifanya hawajui wala hayawahusu.
Japo kwenda kutafuta haki mahakamani ni haki ya kila mtanzania, hali ilivyo ni kwamba mahakama zetu zinaanza kutumika kama nepi ya mafisadi hasa ikizingatiwa kuwa zinaanza kutumiwa vibaya. Rejea kufichuka kwa taarifa kuwa mwezeshaji mkuu wa IPTL kwenye kashfa ya Escrow James Rugemalira alitembeza fedha hata kwa majaji. Majaji wawili profesa Eudes Ruhangisa na Aloyce Mujulizi walitajwa kunufaika na “ukarimu) japo wa kutia shaka wa Rugemalira. Je majaji kama hawa wanaweza kutoa haki au haramu?
Kitendo cha IPTL kutaka kumtisha kila anayejaribu kutimiza wajibu wake hakiwezi kuvumiliwa. Bila shaka wengi wanajiuliza huyu IPTL ni nani na ana nini na serikali ambayo inaonekana kumgwaya na kumuengaenga huku umma ukiendelea kuumia?
Mwanzoni, watanzania hawakujua nani yuko nyuma ya kampuni hii kidhabi zaidi ya kuwadi wake Rugemalira ambaye anaelezewa kama mtu mwenye kila aina ya utata. Lakini baada ya kujitokeza mhindi ambaye hivi karibuni aliukana uhindi wake japo hawezi, Harbinder Sethi Singh, wengi walianza kupata nuru ya kujua IPTL ni nani? Hata hivyo, wengi bado wanajiuliza: Huyu singasinga amekuwaje kigogo bila ya kuwa na vigogo wa kisiasa hasa kwenye serikali? Je Singh ni ncha ya mlima wa maji mgando (tip of an iceberg)? Je Singh ni kielelezo cha undumila kuwili wa watawala wetu na mfumo wao mbovu au utoto wa mjini?
Haiwezekani Singh mtu asiyejulikana japo anadai yu mtanzania aliyezaliwa Iringa wakati muda wake mwingi aliutumia Kenya anakoshutumiwa kuhusika na ujambazi wa Goldenberg kashfa iliyotaka kufilisi taifa hili, anakuwaje maarufu na mwenye ushawishi ghalfa bi vu kama si uhuni na utoto wa mjini wa wanaomtumia? Je Singh ni ufufuko wa Chavda mwingine ambaye tunaambiwa anaendelea kutesa kwenye maeneo ya Upanga wakati anatafutwa na mahakama butu iliyowekwa mfukoni isifurukute? Je hapa tatizo ni Singh au Chavda au wakubwa zetu wenye sura mia kidogo?
Wengi wanaogopa kutathmini na kufafanua kinachoendelea nchini kwa sasa ambapo ufisadi umehalalishwa huku wakubwa wakichekelea ingawa wana mshipa wa kutuaminisha kuwa watapamana nao wakati wanaupamba na kuushiriki. Kwa wasiochelea lolote, kinachoendelea ni uhuni wa kitoto ambapo taasisi za umma zinageuzwa nepi za mafisadi. Je imekuwaje turuhusu taifa letu kuchezewa na matapeli wawe wa kukodishwa toka nje au walioko madarakani? Je tuwalaumu hawa wahalifu au wananchi wanaowalealea huku wakiendelea kuumia?
Hata ukiangalia maazimio ya Bunge ya hivi karibuni lilipoamua “kuwawajibisha” watuhumiwa wa kashfa ya escrow, utagundua kuwa Singh na Rugemalira hawakuguswa. Je ni kwanini? Je kuna vigogo wa serikali hata chama wanaowatumia? Je ni kwanini umma hautaki kusasambua mfumo huu habithi na wa kijizi wakati wao ndiyo waathirika wakuu? Je huu nao si uhuni kuacha kushughulikia wahalifu umma ukabaki kunung’unika vipembeni wakati hadharani ukijifanya kutojua wala kujali lolote? Je kuna Singh wangapi ambao hawajafunuliwa ukiachia mbali escrow?
Hebu tujiulize. Kama IPTL wanataka Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato akamatwe, kesho watashindwa kutaka mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) hata Mkuu wa Polisi (IGP) wakamatwe kwa vile hawataki kugeuzwa nepi ya kuliibia taifa? Je baada ya kufanya hivi watashindwa kusema kuwa hata rais akamatwe? Je hapa tutakuwa na nchi au upuuzi? Wengi wanaweza kuona kama hii ni kuongeza chumvi, ukweli ni kwamba hawa wahalifu ukiwakaribisha ujue umeumia. Kuna mifano mingi ambapo matapeli kama hawa wamezamisha serikali nyingi. Nani mara hii amesahau jinsi chama tawala cha zamani cha Kenya cha Kenya African National Union (KANU) kilivyoangushwa na kashfa ya Goldenberg huku watuhumiwa wakubwa wakiwamo hawa wawekezaji uchwara walioko nyuma ya ESCROW?
Je yote hii ilisababishwa na kuwezeshwa na nini zaidi ya ufisadi, upogo, upofu na kufanya makosa kuwaamini au kuwatumia matapeli hawa uchwara na wa kimataifa wahusika wakidhani wamepata wasijue wamepatikana? Tunapoongelea na kulaani uhuni kitaifa tumaanisha mambo kama haya. Je ni wakubwa wangapi watatia akilini au wanangoja hadi yawakute? Je tutaruhusu uhuni wa IPTL hadi lini wakati mtikisiko iliosababisha kupitia kashfa ya escrow haujatulia? Ama kweli asiyejua maana haambiwi maana!
Tushikwe wapi ndiyo tustuke? Je ni wangapi watakumbwa na uhuni huu wa ESCROW baadaye? Wawe madarakani au nje, wanapaswa kujua kuwa kila chenye mwanzo kina mwisho. Wako wapi akina Kagoda na Richmond? Wako wapi akina Chavda kama si kuishi kwa kujificha kama mende? Wako wapi akina Net Group Solution waliowika zama za Uwazi na Ukweli ulioishia kuwa Ufichi na Uongo tokana na kuendekeza uhuni kama huu tunaoshuhudia? Tieni akilini wahusika kabla hamjaumbuka na kuteseka. Hawa makuwadi mnaotumia hawana tofauti na kahaba ambaye rafiki yake mkubwa ni mfuko wako lakini si wewe. Ukifilisika au kuondoka madarakani anakupiga teke na kuchangamkia wenye nazo au madaraka.
chanzo: Dira ya Mtanzania Leo.
3 comments:
Hivi mwekazaji aliyemakini anaweza kuwekeza katika mazingira hatarishi ya rushwa na nchi uchumi husiokuwa na uhakika katika soko la biashra na uwekezaji. Kimsingi ni kwamba wawekezaji waliopo wengi ni feki inawezekana wanatumia tuu vivuli ili ionekena wamiliki hao tunaowataja kumbe inawezekana waendeshakaya waliopo na waliostaafu ndiyo wamiliki. Maana inayosemekana kuwa Katiba nzuri tuipigie kura haijasema kuwa Kampuni zote wamiliki wake wafahamike na umma, na kiwango cha pesa itakuwa cha juu ili kampuni iwe ya umma. haya ni miongoni ya masuala muhimu katika kupunguza au kuwafahamu kwa kina wawekezaji feki na wanaojificha nyuma ya pazia.
Anon umesema kweli. Tulio nao ni mawakala wa wakubwa zetu wanafiki na wezi wanaowatumia kuficha madhambi yao. Hukusikia Harbinder alivyokimbia hata kabla ya bunge kuamua? Unaweza kukuta hata hii IPTL ni kampuni ya akina Kikwete na genge lake.Hata hawa akina Rugemalayer tunaohangaishwa nao si chochote si lolote. Si unaona alivyotawanya fedha karibu kwa kila mtu.
KWANI IPTL SI CCM JAMANI
Post a Comment