The Chant of Savant

Saturday 27 December 2014

Mlevi aomba ateuliwa mwanasheria mkuu


Baada ya jamaa yetu tuliyemtonya kuwa alivyokuwa akifanya sivyo, jaji Freddie We-rema kuachia ngazi kwa aibu na kuzomewa, mlevi anataka kuomba ateuliwe kuziba pengo lake ili aisafishe kaya. Japo huwa mlevi si mpenzi wa vyeo vya kuteuliwa ambavyo mhusika asipoangalia humfanya awe wa kujikomba badala ya kukomboa walevi, ana mpango wa kuomba rungu hili ili awakomeshe wote wanaowahujumu walevi haraka sana iwezekanavyo. Anataka kurejesha heshima ya kaya toka kuwa shamba la chizi kwenda kuwa kaya ya kuogopwa, kuwajibika na kuheshimika.
Nikishaapishwa, nitahakikisha wote waliokwapua njuluku za escrew na nyingine kama vile EPA wananyea debe kwenye magereza yote kayani bila kujali nyadhifa wala mitandao yao. Sitakuwa tayari kuwekwa mfukoni wala kumwangalia nyani usoni. Hivyo, wale wote wanaojijua walifanya monkey biz wajiandae kufia lupango.
Nitahakikisha nafunga yeyote atakayetuma njuluku kwenye akaunti yangu bila kujali ametoa mamilioni au mabilioni.
Nitahakikisha mabenki yanayosaidia wizi na utoroshaji wa njuluku za umma yanafungiwa na kufilisiwa mara moja huku wakubwa zake wakiishia lupango. Nataka nipige kaya msasa na kuanza upya kuanzia chini hadi juu. Jamaa waliozoea kutoroshea njuluku India na Dubai na Uswazi wakae mkao wa kuliwa.
Nitapendekeza kwa dingi watuhumiwa wachunguzwe na watakaopatikana na hatia wanyongwe ili liwe somo kwa wengine waliogeuza kaya shamba la bibi. Pia nitapeleka mswada bungeni kubadili sheria za sasa zinazowalinda majambazi, wauza unga, mafisadi na waharifu wengine wote.
Pia nitapeleka mswada mwingine bungeni kuhakikisha kiongozi yeyote atakayebainika au kuondolewa madarakani kwa vitendo vya kifisadi asilipwe marupurupu yoyote wala stahiki yoyote kwani hakufanikisha kile alichokuwa ameapa kutekeleza. Hivyo, watu kama Were na Eddie Ewassa watakoma kupokea marupurupu. Hivi ni aibu na uzezeta kiasi gani au tuseme ufisadi wa kimfumo kumlipa mtu marupurupu wakati alitenda jinai? Hizi ni akili au matope? Ukiwanyima maulaji na makandokando yake unakuwa umetoa onyo kwa wote wanaofuata kuwa atayakwapua hatapeawa kiinua mgongo baada ya kuibia kaya.
Pia nikiwa mwanasheria mkuu nitahakikisha maadili ya uongozi yanarejeshwa ili kuondoa huu ujambazi wa madili uliochukua nafasi ya maadili. Nitawaomba wahishimiwa warejeshe Azimio la Arusha na kutangaza kifo cha Azimio la kijambazi la Zenj lilipotishwa na wale marehemu mzee Mchonga aliowaita wahuni. Nadhani wote waliofanya hivi wanakumbuka walivyoingiza kaya msambweni kiasi cha kugugunwa na kila matapeli wa ndani na wa kigeni.
Nitahakikisha nawasaka wote waliotoroka kaya kwenda kujificha nje ili wasikamatwe. Nitarejesha wale wanyama waliosafirishwa kwenye Qatari.
Nitapeleka mswada mwingine wa kuwabana wanakaya wote kutangaza mali zao na jinsi walivyozipata. Zoezi hili litafanyika kila mwaka na atakayekaidi kutangaza utajiri hata umaskini wake anafungwa jela miaka kumi.
Kimsingi, nataka nijulikane kama mwanasheria mkuu wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Pia nitahakikisha wale wote wanaotumia fedha na ofisi za umma vibaya wanakiona cha mtema kuni. Tangia nitakapotia mguu ofisini, ziara za hovyo hovyo za wazito kwenda ughaibuni zitageuka historia.
Pia nitahakikisha nashirikiana na mamlaka za Uswizi kurejesha njuluku zote zilizofichwa kule. Kwanza, nitamwomba msamaha balozi wa Uswizi bwana Olivier Chave tokana na vitisho alivyofanyiwa na Were. Baada ya hapo ni kukusanya taarifa za wezi wote na kuhakikisha wananyea debe bila kumwangalia nyani usoni.
Nikimalizana na walioficha njuluku ughaibuni, nawageukia wauza bwimbwi. Nitaanzia kwenye mipaka na viwanja vya ndege kwa kuwakamata maafisa wote wanaojulikana kwa kuruhusu madini na mibwimbwi kupita bila kujali koo zao au mitandao yao. Nitahakikisha nafukuza hata watumishi wa wizara ya mambo ya kaya wanaosifika kuuza pasi zetu za kusafiria kama njugu kwa wauza unga na wazamiaji.
Pia nitapeleka mswada bungeni kubadili sheria ya uchaguzi ili kuondokana na uchakachuaji unaozalisha viongozi wabovu. Nitapendekeza katiba iandikwe upya huku madaraka ya dingi nayo yakipigwa panga. Nitaamuru wote walioshiriki kwenye mauaji ya rasimu ya Jaji Jose Waliobora wakamatwe na kuwekwa lupango huku wote waliohudhuria vigwena vya kupitisha katiba mchakachauo ya kifisadi wanarejesha njuluku zao na kufungiwa kugombea cheo chochote kwenye kaya yetu.
Kuhakikisha mjengoni kunafanyika kazi inayotegemewa na walevi, nitapeleka mswada wa kuwatimua mjengoni na kuwanyang’anya uhishimiwa waishiwa wote watakaolala mjengoni au kutuhumiwa kuomba au kupokea rushwa toka kwa mafisadi kuanzia wale wa serikali za mitaa hadi wachukuaji waitwao wawekezaji.
Mwisho, nitahakikisha kampuni jizi la IpTL, Dowanis, na mengine mengi yanafungiwa huku wakubwa zake wakiozea lupango baada ya kufilisiwa.
Pia napanga kutoa pendekezo la kubadili sheria za ajira ambapo watumishi wa umma wanaotuhumiwa kufanya madudu kama wale walioidhinisha kujengwa kwa mghorofa wa uhindini ulionyotoa walevi wanahukumiwa kifo tena cha kupigwa mawe huku mafisadi ambao kwangu wataitwa mibaka watachomwa moto kama vibaka wafanywavyo.
Kitu kingine ni kwamba nitarekebisha mikataba yote ya uwekezaji hasa kwenye madini na nishati. Hapa wale wote waliowahadaa na kuwatisha walevi kuwa mikataba haiwezi kuonwa na bunge wangoje kitanzi siku nitakapoingia ofisini.
By the way, mmeona iron lady wa vijisenti vya ugolo alivyopigwa teke pamoja na kusema kuwa asingeenda popote utadhani ndiye mwenye ulaji. Tunangoja kusikia atakachosema baada ya kupigwa panga huku wengi wakitaka kujua kama atarejesha uchache wetu au kuishia nao. Pia hili la Muongo na wenzake kuwekwa kiporo kama linakera na kuchanganya. Nani anataka watendaji viporo wanaowekwa viporo ili kuwa re-cycled baadaye? Je Tiba baada ya kuonyeshwa mlango atateuliwa kwenye bodi za ulaji au ubalozi. Let’s wait and see. Nawatakieni Heri ya Mwaka Mpya wenye kila fanaka hasa kujisuta na kubadilika na kuacha kuwa waangaliaji wakati kaya ikiibiwa bali wachachezaji mitaani kama jamaa zetu wa Burkina Faso.
Chanzo: Nipashe leo.

1 comment:

Anonymous said...

Sasa wameanza kupakwa matope watu wa ughibuni kwa kuwatehua wale wa wakilishi wao wa Chukua Chako Mapema (C.C.M) ughaibuni ili kuharibu sifa ya wapenda maendeleo kwa jamii ya kitanzania ili lolote litakalozungumzwa na watu ughaibuni watatumia wasemaje wao katika taasisi zao za siri. na kusema angalia leo huyu Mwanasheria Mkuu ametoka huko huko hawa waandika maoni hapa, hay angalieni madudu yake wakiwajulisha umma wa wa-danyanyika.
Kumbe alikuwa nimwenzao aliyeshindwa kuishi ughaibuni kwa sababu ya kuzoea vya kunyonga akaona maisha magumu akapitia huku wasiopenda kufikiri lakini wakijipatia Madorotoreki, maporofesa ya kumwaga na Tegeta-Escrow,EPA,Radar,Meremeta, Buryanhulu,Ndege ya mkuu wa kaya, na makila kitu ya wizi wa mchana jua likiwaka .