How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 17 December 2014

Dk., Prof, alhaj Mpayukaji alazwa kuchunguzwa ubongo

Baada ya Prof., Dk., Alhaj, Sheikh, Kanali, Ustaadh, Mtukufu, Maulana Mpayukaji Msemahovyo kukabiliwa na hasira, sononi na mfadhaiko vilivosababishwa na kashfa zilizotamalaki kayani, amekutikana na ugonjwa wa sononi kiasi cha kulazwa kwenye hospitali ambayo ni siri kubwa eneo la Manzese. Ugonjwa huu si wa miaka mingi. Umegunduliwa juzi juzi tu hivyo kufanya apangiwe miadi na daktari tayari kumtibu ili aendelee kunywa na kuvuta bangi bila usumbufu.
Kwa vile Prof Dk Mpayukaji ni mwanadamu aliyeumbika kwa maji, chumvi, hydrogen, nyama na makemikali mengine na anayemcha na kumuogopa Mungu na wale anaowaongoza, muwazi na mkweli, ameamua kutangaza ugonjwa wake tofauti na wale waliofichia kwa miaka nenda rudi hadi maradhi yakawaumbua.  Kwani hamjaambiwa kuwa mficha maradhi kilio humfichua? Sasa mbona hamjifunzi kiasi cha kuendeleza upuuzi ule ule utadhani mmeumbika kwa nuru kama Malaika.  Wako wapi akina Cobra Sata walioficha wakaumbuliwa na vilio? Hata hivyo, tusiwalaumu sana wale walioua huduma za jamii wanaopenda kutibiwa ughaibuni kwenye hospitali za kisasa na za bei mbaya hasa ikizingatiwa kuwa walichowafanyia akina Dk Steve Ulimboka hakiwaruhusu kutibiwa Manzese.  Wanajali nini iwapo hawalipii matunuzi yao wala makosa ya kuharibu na kuvuruga huduma za jamii ambazo wamezigeuza hujuma za jamii? Mnawatuma akina Rama Igondhuz kuwatesa madaktari halafu mjipeleke kwao siyo. Anyways, hayo mie hayanihusu japo yananiongezea ugonjwa wangu wa usongo. Nimelazwa hospitali gani? Niwieni radhi. Sitataja. Ni kwa ajili ya usalama wangu. Si mnajua tena mafisi na mafisadi wanavyoniwinda ili waninyotoe roho niache kuwaghasi. Wanaojua ni washikaji zangu akina Mijjinga, Mgosi Machungi, Msomi, Kapende, Mpemba na Mipawa. Hata washirika zao wa bedroom na akina Kanji na Sofia Lion aka Kanungaembe hawajui.
Nitawaficha nyote lakini si washirika zangu.  Kwa walivyofyatu, ukiwaficha wakagundua au ukakiri baadaye jua ulaji wao umeutema.  Kwa wanywa kahawa hakuna dhambi kubwa kama kuwaficha au kuwadanganya ukidhani wao ni majuha kama wale. Siwezi kula njuluku zao na kutumia kutibiwa halafu nikawaficha.  Isitoshe, wao hawajadhalilishwa kiakili kiasi cha kukubali kila upuuzi kama ufisadi na maigizo tena vikifanywa kitoto na kipumbavu na watu unaoweza kudhani wameelimika na ni watu wazima na timamu kiakili kumbu bure kabisa! Lazima niwaheshimu na kuwathamini Wanywa kahawa. Maana, bila wao mimi si chochote wala lolote. Wao ndiyo mabosi wangu ati, ndiyo wanaolipia matibabu yangu. Isitoshe, mimi ni ngurumbili wa kawaida anayeugua hata kuweza kurejesha namba. Sina ubora wowote kuliko wanywa kahawa wanaoniweka kwenye hii misifa na matanuzi ninayofanya na bi mkubwa kila mara. Kwanza, huwa nachukia mijitu miroho na yenye roho mbaya inayojiangalia yenyewe utadhani haitakufa. Hayo tuyaache.
Nimeamua kutibiwa Manzese badala ya ughaibuni ili kuepuka kupoteza na kufuja njuluku za wachovu. Nina uchungu na wachovu tofauti na wale wanaofuja njuluku za makapuku na wafwadhili tena kwa magonjwa ya kuficha. Pia, nimeamua kufanya hivyo ili kuonyesha usawa kwa Wachovu wote bila kujali cheo wala hadhi ya mtu. Cheo mbona dhamana tu. Ningekuwa na akaunti Uswizi na Uswazi huenda ningelazimika kwenda kule ili kukagua kuna kiasi gani. Hivyo, ninapoandika niko hospitalini kuchunguzwa namna ya kupambana na msongo wa mawazo, sononi, hasira, usongo na ngoa vinavyonisumbua hasa wakati huu wa mazingaombwe ya escrew ambapo wezi wanaombwa watende haki wakati wao ndiyo watuhumiwa wakubwa.
Hakuna kilichodhoofisha afya yangu kama kugundua kuwa mafisadi wa siku zote wanaendelea kuiba njuluku za walevi. Nani alijua kuwa mzee wa vijesenti angeungana na tapeli wa vijisenti ugolo kuwaibia walevi kwa mara nyingine? Nani alitegemea wasomi, tena wenye PhD, kufanya upumbavu na ujinga wa kitoto kana kwamba hawakuona madarasa?
Kitu kingine kilichokaribia kuninyotoa roho ni ile hali ya kugundua kuwa na wachungaji wa kondoo ambao wamegeuka wachunaji nao walishiriki makufuru na ujaumbazi na ukahaba wa escrew. Baada ya kunyaka nyuzi nilitamani nimpigie simu papa Franco lau afanye kweli kutokana na msimamo wake wa kuchukia ufisadi na ufisi.
Hapa nilipo hospitali niko nawasiliana na wafwadhili kuwaambia wasitoe njuluku tena hadi majambazi yote ya escrew yanawajibisha. Hata yale yaliyoingiza jinai hii chini ya Indecent Power Transgression Ltd (IPTL) nayo yashughulikiwe badala ya kupewa jukumu la kuwashughulikia wenzao wakati lao ni moja. Tangu lini kesi ya ngedere ikahukumiwa na nyani? Je nyani wetu hatumuoni wala kumjua?
Baada ya kumaliza kuwasiliana na wafwadhili, nina mpango wa kuwasuta wapingaji ambao wameingizwa mkenge wakahanikiza kupambana na vifaranga wakati jogoo aliyewafundisha kunya ndani akichekelea na kuendelea kunya zaidi kwenye kiota. Hivi mlirogwa na nani nyinyi wapingaji au mmekatiwa chochote kitu? Mbona mmenfanya vitu kama vile hamnazo? Sitajidanganya na kuwahadaa wengine kuwa madaktari wamesema nimepona sononi na mfadhaiko. Nitaponaje wakati uchafu na mazabe ya kuwadhulumu wachovu vinaendelea?  Hata wanaojisifia kupona kansa wanajidanganya. Kwani kansa kubwa waliyo nayo ni ya ufisadi kuliko hiyo nyingine. Hivi yule kunguru kaolewa au ni msela tu?
Chanzo: Tanzania Daima leo.
 
 

No comments: