Kwa hali iliyo, ni dhahiri. Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa mwenyekiti wake, rais Jakaya Kikwete, kimeanzisha, bila kujua, safari ya kulikomboa taifa toka kwenye mikono michafu ya utawala mbovu na fisadi. Najua unayesoma makala hii unafanya hivyo kwa mshangao. Unajiuliza: CCM iliyozamisha taifa hili inawezaje kulikomboa tena dhidi ya nani zaidi ya CCM yenyewe.
Kama tutaangalia utendaji mbovu wa serikali za CCM kuanzia awamu ya pili, tutakubaliana kuwa CCM imejenga mazigira mazuri ya kutupwa nje ya madaraka kwenye uchaguzi ujao. Hili linategemea mwamko wa wapiga kura na jinsi wanavyochambua na kuona madudu yanayoendelea. Pia inategemea uoni wa umma juu ya umuhimu wa kutumia njia ya kidemokrasia kuondoa utawala mbovu ambao hauna cha kujivunia zaidi ya kulinda na kutenda maovu. Rejea kutamalaki kwa wizi wa fedha za umma na uhujumu wa taifa kwa ujumla kupitia ufisadi.
Kama watanzania hasa wapiga kura wataamua kujikomboa, bila shaka, watapigia kura upinzani ili kuiunga mkono CCM katika kuiondoa madarakani kwa njia ya kuinyima kura a kutoiruhusu kuendelea kuchezea chaguzi zetu kupitia mtindo iliouasisi na kuuzoea wa uchakachauaji. Matokeo ya hivi karibuni ya uchaguzi wa serikali za mitaa ni kiashiria kuwa kama umma ukiamua unaweza tena kwa siku moja tu. Pamoja na ushindi mwembamba wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ikilinganishwa na tulikotoka ambapo CCM ilizoea kushinda asilimia tisini ya viti vyote, si haba, tunasonga mbele. Muhimu, tusiridhike na huu ushindi kidogo bali tuuendeleze kwa kuzidi kuinyang’anya CCM viti vingi hasa kwenye ubunge ili tuwe na Bunge linaloweza kuiwajibisha serikali wakati wowote.
Kama tulivyosema hapo juu, CCM, tangia awamu ya pili haina cha kujivunia zaidi ya utiriri wa kashfa zenye kuendelea kuwafanya watanzania kuwa maskini pamoja na kujaliwa raslimali lukuki. Je kikwazi ni nini? Je tuendelee kuilamu CCM iliyokwishajichokea na kuonyesha wazi kuhitaji kupumzishwa au ujinga wa wapiga kura kuchagua kitu kile kile wakitegemea matokeo tofauti? Hakika, hapa ndipo ilipo sababu ya kusema kuwa CCM isaidiwe katika kulikomboa taifa, ipigiwe chini kama wasemavyo watoto wa mjini. Inashangaza na kuchukiza kuona chama ambacho kimeiweka nchi kwenye mifuko ya mafisadi na wezi kila aina kuendelea kushinda. Je kwa kuipa kura CCM hatushiriki jinai zote inazotenda? Je hapa nani alaumiwe hasa ikizingatiwa kuwa hakuna serikali inaweza kuwa madarakani bila ridhaa ya serikali?
Rais Kikwete, kwa makusudi au bahati mbaya, kwa kukosa uwezo au kutojua, ameruhusu serikali yake, kwanza, kuridhi uchafu wa serikali iliyotangulia. Na pili, ameruhusu serikali kuwa mshirika wa maovu wakati ilipaswa kuyapiga vita. Rejea kashfa ya EPA ambapo fedha ya umma iliibwa na kutumika kuwahonga wapiga kura na kuingiza awamu hii. Nani anabishia hili? Rejea kutuhumiwa kwa rais Kikwete na Benjamin Mkapa kuwa nyuma ya EPA na kitendo chake cha kutotaka kuongelea tuhuma hizi.
Tukio la kuonyesha wazi kuwa CCM imeasisi ukombozi wa taifa ni kashfa ya escrow ambapo shilingi bilioni 400 ziliibwa toka kwenye fedha ya umma. Baada ya kufichuliwa jinai hii, Kikwete wala hakuhangaika kutoa maelezo wala kuchukua hatua hadi wafadhili walipoamua kumtolea uvivu wakatoa shinikizo awawajibishe watuhumiwa ingawa hajafanya hivyo zaidi ya kumtoa kafara waziri wake wa zamani wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka kwa kosa la kukatiwa shilingi bilioni 1.65 huku wanaotuhumiwa kusomba fedha husika kwenye viroba na maboksi akiendelea kuwaweka kiporo. Hii ni nini kama siyo kuwaonyesha wananchi kuwa ameshindwa na hivyo wamwajibishe na chama chake?
Bahati mbaya sana, pamoja na Kikwete na serikali na chama chake kutoa taarifa rasmi ya kushindwa, Bunge lilifurukuta likaishia kujiaibisha baada ya kushindwa kushughulikia serikali nzima na badala yake likashupalia maajenti wake. Baada ya kuhitimisha uchunguzi na mjadala hata kwa kumtaka Kikwete awawajibishe hao wachache waliotolewa kafara serikali yake, Kikwete aliendelea kupuuzia kutekeleza maazimio ya Bunge akijaribu kungoja wafadhili watulize hasira zao aendelee na utamaduni ule ule wa kulizamisha taifa. Rejea matamshi yake ya hivi karibuni alipokaririwa akisema, “Kimsingi fedha hizi ni za IPTL, katika swali pesa za nani, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipoulizwa na Kamati ya Bunge alisema humu yawezekana zipo za umma pia zipo za IPTL.” Bunge limesema fedha hii ni ya umma, Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) imesema fedha ni ya umma na Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa fedha za serikali (CAG) amesema fedha ni ya umma. Kikwete anapata wapi jeuri ya kusema fedha ni ya IPTL ile ile anayotuhumiwa kuiingiza nchini na kuiruhusu iendelee kuliibia taifa kama siyo kuwatukana watanzania matusi ya nguoni? Je watanzania hasa wapiga kura wanataka watukanwe vipi au kuguswa wapi ndipo wastuke, kuchukia na kuifurusha CCM ili kulikomboa taifa? Je hapa bado tunailaumu CCM kwa kutuonyesha uovu na uhovyo wake au kujilaumu kwa kushindwa kuitimua madarakani? Je hili nalo linahitaji wafadhili au kuamua kujikomboa vilivyo?
Tumezidiwa akili na wenzetu wa Kenya ambao waliitimua KANU madarakani tena kwa sababu ya kashfa moja ya Goldenberg tofauti na sisi ambapo tuna kashfa lukuki? Wengi walitegemea angalau umma uingie mitaani kulazimisha serikali iondoke kama walivyofanya wenzetu wa Burkina Faso hivi karibuni. Hili halikuwa tokana na woga wetu na kudanganywa kuwa hii ni nchi ya amani. Amani gani wakati wachache wanaiba watakavyo huku umma ukiendelea kusikinishwa na jinai hii? Je hapa tuilaumu CCM au tujilaumu?
Chanzo: Dira Desemba 29, 2014.
No comments:
Post a Comment