Ingawa mtia
nia waziri mkuu wa zamani aliyeondoka madarakani kwa kashfa ya Richmond Edward
Lowassa mbunge wa Monduli analaumu wanaomtuhumu ufisadi, anapaswa kujilaumu
mwenyewe. Ndiyo maana tunasema kuwa mchawi wa Lowassa ni Lowassa mwenyewe na
uchawi utakaommaliza si mwingine bali ukimya na kujipa matumaini hata
pasipohitajika kufanya hivyo.
“Nataka
nitumie fursa hii kuwataka wale wote ambao wamekuwa wakinituhumu kwa miaka
kadhaa sasa na kunihusisha na suala zima la rushwa, nawaambia waache mara moja,
kwani hakuna chembe hata ya ukweli wa maneno hayo.” Utetezi wa namna hii licha
ya kuwa mwepesi unaonyesha mwoga wa mhusika. Kwa wepesi na ukosefu wa mashiko
wa utetezi wake, Lowassa licha ya kuwachochea waseme sana, amejionyesha kama
mtu mwoga ambaye hana ubavu wa kuwashughulikia wahusika. Wengi walitegemea
wasikie akisema kwenda mahakama kuwashitaki wahusika. Kusema kuwa waache tu
hakuna uzito wowote hasa ikizingatiwa kuwa yumo kwenye mbio za kisiasa.
Kama wanaomtuhumu wanasema uongo basi yeye
angekuja na ukweli badala ya jibu la mkato kuwa hakuna ukweli bila kuonyesha
uongo wa wanaomtuhumu. Lowassa alisema kuwa amechoshwa na majungu asijue
majungu haya anayosema anayasababisha yeye kwa kukalia kimya shutuma
zinazomkabili.
“Natoa
changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo za kipuuzi, autoe na
aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme nimechukua lini, kwa nani,
kwa lipi na kiasi gani?” Anachopaswa kufundishwa Lowassa ni ukweli kuwa
mahakama ya kisiasa si sawa na ya kisheria. Na isitoshe, watu wanaweza wasiwe
na ushahidi kama anavyoutaka lakini mazingira yakawa ushahidi wa kutosha.
Kwanza, kwanini azushiwe yeye? Jibu ni jepesi kuwa lisemwalo lipo kama halipo
laja. Ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwa –kama anavyokiri Lowassa
mwenyewe–alianza kutuhumiwa zamani. Hivyo, madai ya ufisadi wa Lowassa si suala
la siasa za kuchafuana au mbinu ya wapinzani wake kummaliza kisiasa. Kama
anakiri kuwa ametuhumiwa kwa miaka mingi hata kabla hajaingia kwenye
kinyang’anyiro anategemea nini sasa? Mbona hili jambo ni jepesi kuelewa?
Pili, Lowassa
ni mtu mwenye bahati ingawa bahati haiji mara nyingi. Kama ametuhumiwa miaka
mingi iliyopita, hata kupewa uwaziri mkuu ilikuwa ni bahati. Wengi wanajua
jinsi marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alivyokatiza mbio za Lowassa na
Jakaya Kikwete mwaka 1995 baada ya kudai walikuwa wamepata wapi pesa ya
kukodisha ndege kwenda na kurudi Dodoma kuchukua fomu. Nyerere wala
hakuzungusha. Alikaririwa akisema kuwa wengine wamejilimbikizia utajiri ambao
wasingeweza kuutolea maelezo. Tangu Nyerere afyatue kimondo hiki kiligeuka
kongwa kwenye shingo ya Lowassa. Anachopaswa kujiuliza Lowassa ni kwanini
maneno ya Nyerere yalitafsiriwa kuwa yalimlenga yeye wakati walikuwa wawili
kama hakuna namna? Jibu ni simpo kuwa Nyerere aliwalea akina Kikwete na
Lowassa. Hivyo, alikuwa anawafahamu vizuri sawa na wanachama wenzake Lowassa
wanaosema wazi wazi kuwa hana udhu.
Hivyo, lazima
tusema kuwa utetezi wa Lowassa ni dhaifu na unaonyesha kama kuna kitu anaogopa
kukigusia kwa sababu ajuazo mwenyewe. Kimsingi, asipofanya maamuzi magumu
atazidi kuandamwa. Aige mfano wa Barack
Obama. Alipotuhumiwa kuwa aliwahi kuvuta bangi alikiri na kuomba msamaha na
mambo yakaisha akaendelea kuwa rais.
Japo
hakuwataja wanaomsema, wapo wanajulikana kuwa wengine ni wanachama wenzake na
watia nia wenzake wanaomfahamu fika. Sikumbuki kama ameishakwenda Butiama
kutafuta kuungwa mkono na familia ya Nyerere kama wenzake walivyofanya. Nadhani
wengi wanajua sababu ya Lowassa kutofanya hivyo.
Lowassa
ameshindwa kujitofautisha na watu kama Nazir Karamagi, Andrew Chenge na
Ramadhani Madabida ambao mazabe yao yanajulikana kwa watanzania walio wengi! Je
anajenga picha gani? Je kwanin Lowassa hataki kuongelea kashfa iliyomtoa
madarakani tena kwa hiari yake baada ya kupewa kitanzi ajimalize naye akachagua
kujitundika kuliko kutundikwa? Je anadhani kuwa doa la Richmond anaweza
kulifuta? Sidhani kama waathirika wa ujambazi wa Richmond walishasahau migao na
kulanguliwa umeme. Je Lowassa anashindwa kuelewa kuwa kujitokeza kwa watia nia
wengi chamani mwake tena wasio na doa ni ushahidi kuwa CCM ina wigo mpana wa
kuchagua mbeba bendera yake? Sijui wanaomshauri Lowassa ni akina nani
wasiomuonea huruma. Maana, kwa wataalamu wa mikakati, anachofanya Lowassa ni
kuzidi kutumia fedha zake kwenye mradi ambao matokeo yake yanajulikana kuwa
hauna faida.
Lowassa
anahangaika na wanaomtuhumu ufisadi chamani mwake wakati wapinzani wanaojua
kila kitu hawajafungua midomo. Sijui hata kama anaweza kuwazidi kete CCM akapita
kwenye chujio, atafanya nini atakapokutana uso kwa uso na wapinzani ambao
kimsingi ndiyo walioibua kashfa nzima ya Richmond na wakaisimamia pamoja na
vitisho vyote walivyowekewa? Nadhani hata CCM nao hawawezi kuwa wazembe kiasi
hiki wakaja na mtu ambaye atakuwa soft target ya wapinzani kutokana na kujua
madudu yake. Hapa ndipo mchawi wa Lowassa anapozidi kuwa Lowassa.
Tumalizie kwa
kumpa ushauri wa bure Lowassa kuwa kama anataka wanaomwandama kwa uongo wakome
basi aanike ukweli ili wananchi waamue wenyewe badala ya yeye kukaa kimya
akisema wasemayo si ukweli wakati ukweli wenyewe hauweki wazi. Kama hatafanya
hivyo, basi Lowassa afahamu kuwa mchawi wa Lowassa si mwingine bali Lowassa
mwenyewe.
Chanzo: Dira Julai 6, 2015.
4 comments:
LOWASSA KASEMA KWELI "kwani hakuna chembe hata ya ukweli wa maneno hayo."KAMA KUNA USHAHIDI UTOLEWE SIO KUROPOKWA TUU FULANI HIVI NA VILE
MNA USHAHIDI JAJI ANASEMA TOA USHAHIDI LAKINI NYIE HAMNA USHAHIDI NI CHUKI ZENU BINAFSI
HUYO NDIE LAIS WA WATANZANIA MKITAKA NDIE HUYO NA IKIWA HAMUTAKI NDIE HUYO
Anon umesikika japo rais wa Tanzania hajajulikana. Kama Lowassa ni lais wa Tanzania hakuna anayepingana na hilo na aendelee na ulais wake japo urais hatapata kwa maneno makali ya vibaraka au wapenzi wake.
Kutokana na maoni ya anon...hapo juu. Sasa naamini na nimekubali kweli sisi wananchi ni majuha na tunasahili kupata malais majuha na siyo marais makini na wazalendo wasiohitajika kupakwa rangi ili kuondoa alama za makovu ya uhalifu.
Anon 10:32 umenena vyema. Naamini wahusika wameipata na wamesikia. Shurani sana.
Post a Comment