Baada ya bi mdogo yule ambaye hajaTulia kuja na mpya kuwa atawanyima wahishimiwa wa upingaji posho za makalio kwa vile makalio yao hayakai kwenye makochi ya Mjengoni na kuwezesha masikio kusikia mipasho ya akina Lushindo na wengine, Kijiwe kinataka–kama mbaya mbaya–posho ya makalio iondolewe. Kwani tishu za chooni na maji yanatosha.
Mpemba leo ndiye analianzisha, “Yakhe memsikia eti huyu bibie asiyeTulia ataka kukata posho za makalio ya wahishimiwa wa upingaji? Kwani yeye makalio yake yalani kiasi cha kutaka kukata posho za makalio ya wenzake?”
“We unashangazwa na kukatwa hizi posho za masaburi siyo! Huyu bi mdogo apaswa kutulizwa; kwani wapingaji mbona walitaka tangu zamani posho za makalio ziondolewe hasa ikizingatiwa kuwa makalio hayapaswa kulipwa posho,” anachomekea Mbwamwitu huku akitabasamu. Anaendelea, “Mwenzenu leo naomba mnivumilie tena sana tu. Kwani nitachonga na kuronga sana japo si kawaida yangu. Hebu jiulizeni; kama makalio yanalipwa posho, hiyo miguu, mikono, macho na mdomo vitalipwa nini? Nadhani hii nayo ni aina ya ufisadi iliyohalalishwa waliozoea kuharamisha vya halali na kuhalalisha haramu.”
Mipawa anakula mic, “Nkwingwa nakubaliana nawe. Hawa wanaolipwa posho za makalio inaonekana wanawakilisha matumbo na makalio yao na si wachovu kama wanavyodai. Sasa nimegundua! Kumbe ndiyo maana wengi wao wana matumbo na makalio makubwa! Ni kwa sababu makalio yao yanalishwa kwa posho ya wanuka jasho. Je na huko ulaya watasha hulipa posho kwa makalio yao au vichwa tu?”
Mijjinga anakwapua mic, “Bheng’we kweli leo umenifikirisha na kukukubali kama daktari na si kilaza kama wale watoto wa chuo cha UdoM. Sasa naweza kujua ni kwanini mjengo uligeuzwa sehemu ya mipasho. Unategemea nini makalio yanapolipwa posho yakashiba na kuumka kama siyo kutoa mipasho tena yenye harufu chafu?”
‘Una maana jamaa wanatumia sana masaburi sana kuliko vichwa siyo; ndiyo maana wanaongoza kwa kuwa mjengo wenye mipasho kila wanapokutana ukiachia mbali kutimuana na kususana?” anauliza Mchunguliaji. “Kumbe sasa! Unauliza chooni kunanuka nini katika mambo ya kimakaliokalio kama haya siyo? Hebu jiulize swali jepesi. Anatokea muishiwa tena wa kuteuliwa na kuwania Umicrophone na anapata unategemea nini? Vingetumika vichwa na siyo makalio kilaza kama huyu anayetegemea kubebwa kibaby baby asingekubaliwa kugombea wala kupewa ulaji mkubwa kama huu unaopaswa kushikwa na wasotaji,” anajibu Mipawa.
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akisikiliza kwa makini anakula mic,”Dokta Mipawa usinikumbushe mambo ya vilaza na kaya iliyokuwa ya vilaza. Hivi unategemea nini makalio yanapolipwa posho? Lazima mwenye makalio ataishia kuwa kilaza kwa vile hana haja ya kujihangaisha hasa ikizingatiwa kuwa analipwa posho nyingi hadi makalio yake yanalipwa. Kiumbe wa namna hii hatakuwa na motisha wala haja ya kutumia bongo kufikiri hata awe na PhD kama sisi. Hivyo, msishangae yanayoendelea mjengoni. Shibe mwana malevya jamani; hasa ulevi wenyewe unapokuwa wa madaraka. Kama watu wangeamua kutumia vichwa kufikiri badala ya makalio basi hii posho ya makalio ingepelekwa mashuleni ambako hali ni mbaya. Kama kulipa posho ya makalio ni dili basi walipwe wanafunzi wanaokaa chini hadi makalio yao yanauma kama siyo walimu wanaosimama hadi makalio yanauma.”
Kanji anakwanyua mic, “Dugu yangu, kama kalio nalipwa juruku kuba mimi iko gombea ingia jengoni ili kalio yangu ipate posho. Kama laza kama ile nasaidia Mr Microphone pewa guvu kuba namna hii lazima yeye iende jengoni na kujenga kalio yake kama vao nafanya.” Kijiwe hakina mbavu jinsi Kanji anavyopania kwenda kujenga makalio yake.
Wakati tukiangua vicheko Kanji anaendelea, “Veve cheka! Mimi fika jengoni taka na posho ya roho, sikio, moyo, na kila kitu yanguni.”
Mbwamwitu anarejea, “Kanji nawe kumbe unatamani kutumia makalio kufikiri ili ulipwe posho ya makalio siyo! Halo halo! Ama kweli Bongo kweli bongolalaland alijisemea profesa Mpayukaji! Sijui kama ingekuwa Bombei mswahili angefikiria hata kwenda kufikiri kwa kichwa kwenye mjengo wa magabacholi wanaotuita sisi abusii au manyani!” ananiangalila huku akitabasamu tokana na kunipa ujiko wa kuwa mwanafalsafa aliyeita Bongo Bongolalaland.
Kabla ya kuendelea nami nachomekea, “Ngojeeni Makalioland inakuja siku si nyingi kama siyo Tulieworld.”
Kanji leo kapania kusema; anakula mic, “Kweli mimi jua kuwa hindi kule Bombei na nyingine hapa jumbani naitwa Swahili jina baya; lakini siyo mimi. Mimi na nyinyi iko dugu moja tena kuba sana dugu yangu. Hapana ona nakuja kunya gahawa hapa kila siku?” anajitetea.
Sofia Lion aka Kanungaembe ameamua kutia guu, “Jamani hawa watu wa mjengoni watukwaza sisi wanuka jasho. Hivi kweli hii ni haki kulipana posho ya makalio wakati umaskini ukiendelea kutukalia sisi bila sababu zaidi ya uroho wao? Nadhani; tufanye mpango tuandamane hadi kwa Dokta Kanywaji kumueleza kilio chetu na namna tunavyopinga makalio kulipa posho. Mie nilidhani ni makalio na manonihino ya vyangudoa yanayolipwa tena siyo kwa kukaa bali kushughulishwa. Hili nalo ni jipu kama yule wa kutulia.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la kidhabu Tuliya. Acha tulimwagie kahawa kabla ya kutaka kumtoa nje na kumramba vibao.
Chanzo: Tanzania Daima, Jumatano
No comments:
Post a Comment