Mke wa rais Janet Magufuli :Hapa Magabacholi wameishamdaka |
Baada ya kuona namna mambo yanavyokwenda–kiasi cha kuanza kuharibika kama si kuzusha wasi wasi na shaka–nimeamua kuvunja mwiko na kuomba kukutana na mke wa mnene ambaye wengi hupenda kumuita bi mkubwa namba moja utadhani munene ana nyumba ndogo au ana mpango wa kuoa mke mwingine.
Juzi juzi nikiwa zangu Ntwara njini nikipata chamaki nchana na nkojo. Ghafla bi vuu si nikaona bi mkubwa wa murume akipokelewa uwanja wa ndege kama rahis kwa vile ni anachangia uchago na bwana mkubwa. Kwanza, nilijiuliza; nani alimpigia kura ya kula huyu? Sikuamini kuwa Jeni angepoteza muda kutoa misaada kwa wazee walevi ambayo ingeweza kutolea na akina Jeni Muhangama munene wa wizara husika. Pili, machele yanicheza nikasukuti na kujiuliza: huyu bi mkubwa kapata wapi nshiko wa kuwakumbuka waliosahaulika hivi? Je kuna anachotafuta? Je anataka kuwatumia au anatumika? Baada ya kukosa majibu, niliamua kujiandaa kumkabili. Zamu hii nitamkabili na si kumuandikia waraka kama nilivyofanya kwa bi mkubwa mfanyabiashara ya asasi zisizo za kiraia wala kijeshi Salmia Njaa Kaya Kitwitwi ambaye nilimtwanga barua kali alipotangaza kuwa makao makuu ya NGO yake ni ikuu.
Baada ya kukutana na zali la mentali kwa wazee wa Ntwara, kwanza nilidhani huu ni wema tu wa kawaida ambapo mke wa mwenye ulaji alikuwa ameamua kuwasaidia wakongwe hawa waliopigika. Kilichonistua ni habari kuwa kumbe misaada aliyokuwa anamwaga bi mkubwa ilikuwa imetolewa na wafadhili tena matapeli toka Afrika Magharibi kwenye kaya inayosifika kwa utapeli wa kiroho na kimwili. Sijui kama bi mkubwa huyu alijiuliza namna ya hawa wanaomshobokea walivyochanga njuluku wanazomwagia hadi kuwazimia na kuwasifu hata kuwapa majina matukufu. Je walikuwa wapi; na kwanini wamchangamkie leo baada ya murumewe kuukwaa ulaji? Je kwanini asiwaambie hawa wenye mapenzi mema waelekeze hiyo misaada kwa wizara husika kama hakuna namna?
Hakuna kitu kiliniacha hoi kama kusikia kuwa mmoja wa wafadhili waliomwagia bi mkubwa misaada ni Mnigeria. Kwanini huyu kidhabu asiwasaidie wanigeria aje kuwanea uchungu wabongo kama hakuna namna?
Lazima niseme ukweli; simzimii huyu bi mkubwa. Ninayemzimia ni mzee wake ambaye ana tabia kama zangu; si mwoga wala mbabaishaji kama wale vilaza aliowarithi. Kwanza, nafahamu kuwa bi mkubwa–tokana na elimu yake kiduchu–anaweza kurubuniwa kirahisi kama mtangulizi wake ambaye alikuwa akijaribu kubukanya kimombo anatoa jasho utadhani amekwea mlima Kilimanjaro. Hivyo, hoja yangu ya kwanza kwake–tutakapofanikiwa kukutana–ni kumpa laivu kuwa akapige shule badala ya kukimbizana na njuluku.
Pili, nitamtonya akiendelea na spidi hii–licha ya kuingizwa mkenge na kutumiwa na matapeli –atamchafulia mrume wake. Naongea kutokana na uzoefu nilioupata toka kwa Anna Tamaa Makapi Ben Tunituni mzee wa uvivu wa kufikiri nyodo na kujitwalia mimali ya walevi hasa ile ya Kiwila.
Tatu, nitampa laivu kuwa walevi wanachukia hizi NGO za ulaji na za uongo na ukweli zenye kutaka kuwatumia waliopigika kujipatia ukwasi wa haraka. Nitamshauri aangalie Anna Tamaa na murumewe wanavyoishi kwa kuogopa na kukimbia vivuli vyao kiasi cha kustuka usingizini wanapotajiwa jina la munene ambaye anaonekana hana nchezo na vibaka wawe wakubwa hata wadogo. Humuoni wale vibaka wanene na wanono wanavyokimbilia ikuu kila mara kupoza mambo ili wasiishie kunyea debe?
Nne, nitampasha kuwa akiona hawa wanaomchekea na kumzimia asidhani wanamzimia yeye zaidi ya kigoda alichokalia murumewe; wakishatimka toka ikuu wanabakia makapi ambayo hata waandishi wa umbea hawayataki. Nani leo–kwa mfano anaweza kupoteza muda na nafasi ya chombo chake cha habari–kumfuata bi mkubwa wa Njaa Kaya kwenda kupata habari zake? Ni mwandishi gani aliyeishiwa kama kanjanja anaweza kumhoji Anna Tamaa leo zaidi ya kuwinda habari zake mbaya ili kumuanika? Maisha ya ustaafu huwa karaha; na siyo raha ukiondoka ukiwa na mizigo ya kashfa tena zitokanazo na kutoona mbali, tamaa na upuuzi mwingine. Nitamwambie aone bi mkubwa wa mzee Mchonga anavyoendelea kutesa tokana na kujitenga na ufanya biashara ikuu. Jamani, kuna maisha baada ya kustaafu.
Kwa vile sijapewa appointment ya kukutana na bi mkubwa huyu, sitamaliza yote ninayokwenda kutoa moyoni kwake. Cha mno ni kwamba walevi wamenituma nimpe kavukavu kuwa hawapendi tena NGO ya bi mkubwa wa murume kwa vile zilizopita ziliwatumia na kuwatajirisha vidhabu waliojifanya kuwajali kumbe wanatafuta miradi yao uchwara.
Nimalize kwa kusema ukweli–maana msema kweli ni mpenzi wa Mungu–kuwa sitaki kuona bi mkubwa wa munene akijiingiza kwenye kufanya biashara pale Magogoni wala kuruhusu pageuka pango la wezi na matapeli kwenda kupiga dili kama ilivyokuwa.
Tuonane nikitoka kumpa vitu vyake bi mkubwa wa munene Kanywaji.
Chanzo: Nipashe Jumamosi.
No comments:
Post a Comment