Hakuna kitu kibaya kama kuishiwa. Mtu aliyeishiwa hana tofauti na mtu aliyechanganyikiwa hasa kama hakubali kuwa ameishiwa. Hivi karibuni mwenyekiti Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, aliwaacha wengi hoi kama si kuwaudhi alipojigeuza jaji kiasic ha kumtuhumu Katibu mkuu wa Chama cha Wananachi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad, kuwa ni mhaini bila kujua hata ukubwa wa tuhuma kama hizo.
Mrema aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kujivua nguo. Hata hivyo, kutokana na hali yake kiafya, kuna uwezekano; uwezo wake wa kufikiri unazidi kumtupa mkono. Pia, tokana na elimu yake kiduchu, Mrema ameonyesha wazi kuwa hata hiyo shahada aliyodai aliipata Marekani ni feki; na inapaswa kuchunguzwa; ili ikiwezekana atumbuliwe sawa na wengine walioghushi sifa na vyeti vya kitaaluma. Kama Mrema angejua uzito na athari za madai yake, wala asingejivua nguo. Ina maana yeye ndiye anajua sheria kuliko mamlaka zote za Tanzania ambaye ameuona “uhaini” wa Seif ambao serikali imeshindwa kuuona? Kama ni mhaini, kwanini hakamatwi na kufunguliwa mashtaka? Jamani, hata kama ni kutetea mtu au ulaji, angalau wanaofanya hivyo watumia japo akili lau kidogo tu. Hata unapotaka kumnasa samaki, angalau, huweka kitu kidogo kwenye chambo. Kwanini Mrema anataka kupaka rangi upepo au kutaka kuung’ao mbuyu kwa kijiko?
Mrema alimtuhumu Seif kuwa ni mbinafsi bila kujua kuwa naye alichokuwa akifanya pale licha ya kuwa ubinafsi wa kujipendekeza ili akumbukwe lau kwa cheo ni kujidhalilisha na kuchochea vurugu; sijui ili apate nini? Kwanini Mrema hakubali kuwa kwake game is up; na akajiuguze aone mwisho wa hali yake? Pia, Mrema alimtuhumu Seif kuwa anautaka urais kwa gharama yoyote; hata kama ni kwa njia ya kumwaga damu. Madai ya ajabu, hovyo na uongo wa wazi wazi. Inaonekana Mrema hana kumbukumbu tena ya jana tu? Sijui ni kwa kukosa kumbukumbu au makusudi mazima Mrema alishindwa kukumbuka kuwa ni maalim Seif huyu huyu aliyewahamasisha wazanzibari wasifanye fujo tena wengi wa wafuasi wake walipokuwa tayari kuingia mitaani kuitangazia dunia kuwa wamedhulumiwa! Sijui kwanini Mrema hakumbuki kuwa ni Seif huyu huyu–anayemzushia ubinafsi, uhaini na uroho wa madaraka bila kutoa ushahidi–ndiye aliyekutana na rais John Pombe Magufuli ikulu na kumhakikishia kuwa hataunga mkono vurugu. Je huo umwagaji damu anaoongelea Mrema ni upi?
Ajabu ya maajabu ni madai ya Mrema kuwa aliyopayuka yalitokana na uzoefu wake wa kuwa waziri wa mambo ya Ndani wa muda mrefu bila kutaja huo muda mrefu ni miaka mingapi na kwa vigezo vipi? Kwani uwaziri wake wa Mambo ya Ndani ni taaluma? Kwanini Mrema hataki kuwa mkweli kwake binafsi na umma kuwa anasumbuliwa na kusukumwa na njaa kiasi cha kujipendekeza kwa rais Magufuli ili lau amkumbuke kwa cheo lau agangie njaa kali inayomkabili? Ama kweli wahenga walisema; adui yako muombee njaa na mwenye njaa kweli hana miiko. Pia, hili la kutaka apewe lau ubunge wa kuteuliwa nalo linapaswa liangaliwe vilivyo na kwa makini hasa ikizingatiwa hali ya kiafya ya Mrema. Hivi Mrema anadhani Magufuli ni mtu wa kutapeliwa kirahisi hivyo; abugi step amteue mtu ambaye anapaswa kutumia muda uliobaki kujiuguza? Hata kutoka kwenye mkutano wenyewe alikorushia makombora yake alitoka akiwa ameshikiliwa kuonyesha asivyo timamu kiafya. Hivi kwa udhaifu wa kiafya alio nao Mrema, anaweza kufanya kazi gani zaidi ya kutaka ateuliwe ale dezo jambo ambalo nalo ni ubinafsi, ufisadi, upotezaji fursa na matumizi ya fedha za umma ukiachia mbali kuwa ujipu ambao Magufuli akiufanya atakuwa anajipiga mtama? Tunamshauri Seif na Magufuli wampuuzie Mrema. Kwani, inavyoonekana, anataka afe na mtu. Hebu tuwe wakweli kidogo. Unawezaje kumteua mgonjwa; au Mrema anajigonga ili aendelee kugharimiwa matibabu India?
Kwanini Mrema–kama kweli si mbinafsi tena wa kunuka–anaamua kuwapakazia wengine ndiyo apate mradi wake? Kama tukiwa wakweli, kuna mwanasiasa mbinafsi Tanzania kama Mrema ambaye kila alipohamia aliua vyama kwa sababu ya ubinafsi na ukosefu wa usomi na busara na uzalendo? Kwanini Mrema anataka kuwageuza watanzania majuha na wasio na kumbukumbu kiasi hiki; wakati wanajua historia yake iliyojaa ubinafsi, ujanja ujanja, utatanishi ukiachia mbali uchu wa madaraka? Kama Mrema amepoteza kumbukumbu, basi asidhani watanzania wote wamepoteza kumbukumbu kama yeye. Mgogoro wa matokeo ya uchaguzi wa Visiwani si wa kufanyia usanii wala kugangia njaa. Wengi walidhani; Mrema angewahimiza wahusika wakae kwenye meza ya mduara. Bahati mbaya sana, tena sana, Mrema anaonekana kumwaga mafuta kwenye moto. Hata hivyo, kutokana na kuishiwa kwake, sijui kama Seif atapoteza muda kumjibu hasa ikizingatiwa kuwa hamna hoja ya msingi ya kujibu; ukiachia mbali kutaka umaarufu kupitia mgongoni mwake na UKAWA. Je anadhani watanzania wamemsahau Mrema muungu mtu aliyetaka kila tatizo la kitaifa litatuliwe kijijini kwake Kiraracha? Nani hamkumbuki Mrema mpenda makuu? Kama Mrema anataka kurejea CCM, si arejee tu badala ya kuanza kutafuta kuwachafua wenzake? Kwanini Mrema amejigeuza mpinzani wa wapinzani na kwa faida ya nani?
Ni bahati mbaya kuwa Mrema hakutoa hata suluhisho wala m change kwenye tatizo zaidi ya tuhuma za uongo ambazo alishindwa hata kuzithibitisha achia mbali kushindwa kujenga hata hoja. Amekuwa tatizo badala ya kuwa jawabu.
Tuhitimishe kwa kumuuliza Mrema kwanini anashindwa kuwa refa mzuri kwa kuangalia mapungufu ya pande zote? Au ni ile hali ya kuwa njaa inapopanda kichwani basi hubongo huacha kutumika na badala yake utumbo hutumika?
Chanzo: Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment