Baada ya mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustine Mrema kugeuza kujikomba sera yake na chama chake, juzi alikuja na mpya. Baada ya kujigonga sana kwa rais John Magufuli bila mafanikio katika madai ya ajabu kuwa katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Seif Sharrif Hamad ni mhaini kudharauliwa na kutojibiwa, Mrema ameamua kubuni mbinu mfu ya kuwashambulia wapinzani wote kwa ujumla.
Tokana na kuendelea kuishiwa, Mrema alidai juzi kuwa wapinzani wanamshutumu rais Magufuli udikteta ili kumharibia, kumkwamisha na kuvuruga amani. Sijui kama Mrema anajua dhana nzima ya amani kuwa inatokana na ukweli na si uongo na ubabaishaji kama anaofanya. Kibaya zaidi, Mrema anataka wapinzani wote wageuke vigeugeu kama yeye; waache kutetea maslahi ya wananchi; watetee matumbo yao kama yeye. Sijui kama upinzani unaweza kujirahisi na kujikomba na kuisha na kuishiwa kiasi hiki.
Kwanini Mrema hataki kukubali kuwa ameisha na kuishiwa. Si arejee kijijini kwake akapumzike? Kwanini Mrema hataki kuona ukweli kuwa, kwa sasa, hana nguvu wala akili za kuwa kiongozi wa umma? Je Mrema–kwa hali aliyo nayo–anataka kufa na mtu; au ndiyo kuharibikiwa? Kwa mwenye akili timamu, hawezi kuwalaumu wapinzani kwa kutimiza wajibu wao wa kuikosoa serikali na si kulala nayo kitanda kimoja. Kwanini Mrema hataki kutofautisha upinzani wa Tanzania na ule wa kisanii wa Zaire ya Mobutu aliyekuwa akiwapa fedha vibaraka na waramba makalio yake waanzishe vyama kuwazuga wananchi? Kwanini Mrema hataki kukubali kuwa siasa za uchumiatumbo na usaka tonge hazina nafasi tena katika karne hii?
Ukimtathmini na kumchambua Mrema, unashinda hata pa kumueweka; kwani huwezi kujua kama anatumiwa au anajitumia tokana na kuishiwa kisiasa na kimkakati. Laiti angekuwa amesoma, lau angejifanya refarii kama wale madaktari uchwara wa chuo fulani ambao hujifanya watetezi na wasemaji wa CCm ili wakumbukwe. Ambacho kwa wanaompenda Mrema na kutaka kumsaidia ni kwamba akubali kuwa muda unazidi kumtupa mkono. Unaweza kuliona hili pale Mrema anapoongelea yaliyopita akiishi kwenye kile kiitwacho ukale (golden era) alipokuwa amevishwa mkenge na kupewa cheo cha Naibu Waziri Mkuu bila kuwapo kwenye katiba.
Zaidi, ni vizuri kumfahamisha Mrema kuwa wakati umebadilika. Hivyo, hana haja ya kubadilika kiasi cha kuachana na kuendelea na fikra na mbinu mgando na za kikale bila kuangalia hata tabia ya anayemlenga. Magufuli si dhaifu wa kulewa sifa kama waliomtangulia ambao walikuwa wakisifiwa kidogo wanaingizwa mkenge. Magufuli si mtu wa kujisifu wala kusifiwa kirahisi. Ni mtumbua majipu ambaye anapaswa kumnyamazisha Mrema aache kujigeuza msemaji wake wakati anaye msemaji anayemlipa na mwenye elimu na ujuzi wa kazi hii. Anachofanya Mrema–licha ya kutaka apewa tonge–anamtumia Magufuli kujipatia sifa rahisi asijue janja yake imeishajulikana kiasi cha kupuuzwa na kudharauliwa. Kama Magufuli angekuwa anamhitaji Mrema, asingemwacha aendelee kujivua nguo hadharani hivi. Kimsingi, anachofanya Magufuli ni kumpuuzia Mrema kwa vile anajua anayoongea hayatoki moyoni bali tumboni. Ni njaa tu inayomhagaisha.
Pia wengi wanamjua Mrema kama mwanasiasa uchwara aliyezoea siasa za kibabaishaji ambazo mara nyingi hutumia uongo, utapeli na fitina kwa wanaozifanya kuweza kuishi. Huu si wakati wa siasa za namna hii. Huu ni wakati wa “Hapa Kazi Tu” ambapo Magufuli ametangaza wazi kuwa hana ugomvi na wapinzani wala tofauti za kiitikadi. Mtu wa namna hii si rahisi kumuingiza mkenge hata kidogo. Itakuwa ni jambo la ajabu kwa Magufuli kuingizwa mkenge na mchovu anayedandia kila anayepita ili aonekane anamtetea. Magufuli ahitaji mapambio wala utetezi. Kazi na sifa zake zilizomvusha kwenye siasa za ushindani mkubwa ndani ya CCM zinamtosha; ahitaji msaada. Hata kama angehitaji msaada, basi asingetegemea kuupata kwa wachovu na watu wenye mawazo mgando wanaoweza kujipayukia bila kufikiri kama anavyofanya Mrema. Magufulil anajua ubovu wa Mrema. Alimjua sana siku aliposimama jukwaani jimboni mwake Vunjo kujivua nguo akiwataka wapiga kura wake wasimpe kura mgombea wa chama chake bali wampe Magufuli. Mwanandoa yoyote anayeweza kumpa mwenzie mtu mwingine amtumie hawezi kuaminika na hata hayawani. Kitendo alichofanya Mrema kwa chama chake kwa kumnadi Magufuli licha ya kuwa usaliti na uhujumu wa chama kinamwonyesha kama opportunist anayeweza kufanya lolote ilmradi mkono uende kinywani. Huu kwa lugha nyepesi huitwa uchangudoa wa kisiasa. Mwanasiasa anayefikia hatua hii huwa ameisha na kuishiwa kiasi cha kutorekebishika. Kama ni mgonjwa si wa kupona.
Tumalizie kwa kumtaka Mrema arejee CCM kama anaona sera za Magufuli zinamkuna kiasi hicho. Kwanini Mrema anataka kuendelea kutumikia mabwana wawili yaani upinzani na CCM ambayo–hata hivyo–ahitaji huduma yake hasa ikizingatiwa kuwa kama Mrema alikuwa nyama basi limebakia fupa kavu tu ambalo hata fisi bingwa wa tamaa halitamani wala hawezi hata kulinusa. Kama Mrema anatafuta mtu wa kufa naye, amekosea. Hakuna anayemwelewa wala kumwamini kwa sasa. Safu hii–huko nyuma–iliwahi kumsahauri Mrema aachane na siasa za tumbo na majitaka aende kujitibia. Na kama anataka msaada wa matibabu aseme wazi kwa kuomba msaada achagiwe badala ya kuwachafua wenzake. Wapinzani si saizi yake.
Chanzo:Tanzania Daima Jumapili.
No comments:
Post a Comment