Hivi karibuni mke wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Janet, alikaririwa na vyombo vya habari akiwa mkoani Mtwara alikotoa msaada wa takriban shilingi milioni 200 kwa wazee. Hakika hili ni jambo jema japo nyuma yake kuna namna.
Mumewe alipoingia madarakani, binafsi niliandika makala ya kumpongeza kwa kutoanzisha NGO kama watangulizi wake ambao walionekana kuwa wafanyabiashara zaidi ya wenzi na washauri wa rais. Hata hivyo, kutokana na hili la juzi, hali inaanza kubadilika kiasi cha kuchanganya na kutia shaka. Kwa mfano, wengi wangetaka kujua alikopata fedha nyingi kiasi hiki; na nani walimpa na kwanini sasa wakati wazee na wenye shida wamekuwapo nchini hata kabla ya Magufuli kuingia madarakani?
Kwa tunaojua wake wa marais waliopita ukimuondoa mama Maria Nyerere, hawana heshima waliyostahili mbele ya jamii kutokana na kujiingiza kwenye biashara hii kwenye migongo ya waume zao. Hivyo, tutamshauri mama Magufuli mambo kadhaa ili kumuepusha na kashfa, na madhara yatokanayo na biashara hii ya NGO.
Mosi, tungemshauri atumie muda wake kujisomea. Achukue mfano toka kwa mama Tunu Pinda mke wa waziri mkuu mstaafu Mizengwe Pinda ambaye–tokana na nafasi yake na kiwango chake cha elimu–anaweza kuiga mfano mzuri kwake. Mama Pinda alitumia muda wa uwepo wa mme wake madarakani kujiendeleza kielimu hadi kufikia shahada ya pili. Tofauti na yeye, mke wa rais mstaafu Jakaya Kikwete, Salma alipoteza muda mwingi kwenye biashara ya NGO kiasi cha kuendelea na kuwa na elimu haba bila sababu ya msingi zaidi ya kutoona mbali. Mwanzilishi wa hii biashara ya NGO za wake wa marais, Anna Mkapa, aliondoka na sifa mbaya sana ya kumrubuni mumewe aliyekuwa ameanza kazi vizuri kufanyia biashara ikulu hadi kufikia kijimilkisha mali ya umma kama vile Machimbo ya Makaa aya Mawe ya Kiwira ambayo yamegeuka kongwa shingoni mwa Mkapa. Mpaka tunapoandika, Mkapa hana jeuri aliyokuwa nayo wakati akinadiwa na Nyerere au kipindi cha kwanza cha urais wake. Ni mtu anayeishi kwa kutegemea kulindwa na rais aliyeko madarakani kama ilivyotokea wakati wa Kikwete ambaye alisema tumuache mzee Mkapa astaafu apumzike pale baadhi ya watu walipotaka awajibishwe kuhusiana na kashfa ya Kiwira. Huyu naye ni jipu; na hizi NGO ni majipu tu yanayopaswa kutumbuliwa na kuepukwa na mke wa rais anayeonyesha kufanya hii biashara kwa mlango wa nyuma.
Pili, tunamshauri mama Magufuli aachane na biashara ya NGO; itamchafua na kumchafulia mumewe hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi wenye kutia shaka watakuwa tayari kumtumia kwa kisingizio cha kutoa misaada kupitia kwake. Mfano, hivi karibuni mama Magufuli alikaririwa akimsifia aliyemuita Nabii TB Joshua ambaye biashara yake ya kuchuuza roho za watu inajulikana.
Tatu, afahamu na kujiuliza swali jepesi: hawa akina Joshua walikuwa wapi kabla ya Magufuli hajawa rais? Kwani wazee wa Tanzania wameanza kupata matatizo alipoingia Magufuli? Kwanini hawakutoa misaada husika kwa wizara husika kama kweli wana nia njema na mama Magufuli hata hao wazee wanaojidai kuwasaidia? Je wanataka kumtumia kama walivyomfanyia rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda, waliyemhadaa kuwa wangemuwezesha kushinda kwenye uchaguzi wa urais nchini humo akaishia kuangikia pua? Nani anahitaji kushinda kwa maombi kama si upuuzi? Rais anashinda kwa sifa na si miujiza wala maombi. Ni jambo la kutia shaka kwa Magufuli aliyekiri kuwa ni muumini wa kiroma tangu kuzaliwa kuruhusu mkewe, hata naye binafsi, kuyumbishwa na manabii wa uongo kama huyu tapeli wa kinegeria ambaye miaka miwili iliyopita hosteli yake ilianguka na kuua watu wengi waliokuwa wameingia mkenge kuja kuombewa. Pia mamlaka za Nigeria zilikuta kuwa ujenzi wa hosteli yenyewe ulifanyika kitapeli na chini ya viwango. Mhalifu kama huyu kweli anaweza kuwa nabii? Nilimsikia mama Magufuli akimshukuru na kumwita nabii Joshua wakati akijua fika kuwa enzi za manabii wa kweli ziliisha zamani zikabaki na manabii wa uongo alioonya Yesu kuwa wangekuja na kupoteza wengi.
Nne, mama Magufuli anapaswa kujua kuwa si wengi wanaokuja kwa gea ya kumpa misaada wana nia njema naye. Wanaangalia kiti alichokalia mumewe ili kuwa karibu na jungu kuu wapate miradi yao. Mbona Nigeria ina wazee wengi wanaoadhirika? Kwanini Joshua asianze kwao hasa ikizingatiwa kuwa hisani huanzia nyumbani?
Tano, atangaze hiyo NGO anayoonyesha kuiendesha kichini chini. Juzi juzi alitoa misaada ya shilingi za kitanzania milioni 200 bila kutoa maelezo ya ni nani walitoa fedha hiyo. Kwanini wasiitoe kwa wizara husika na wizara itafanya kazi gani kama mke wa rais anaingilia kazi zake? Si lazima kila mke wa rais afanye biashara ya NGO. Tumeona madhara yake na uchafu uliowakumba waliozianzisha kwa tamaa ya utajiri kwa kisingizio cha kuhudumia watu ambao wana wizara ya kuwahudumia tayari. Kama lengo ni kuwasaidia basi mama Magufuli awaambie wanaotaka kumsaidia waelekeze misaada hiyo wizarani.
Mwisho, najua makala hii haitawapendeza wahusika na wale wanaopenda kuwahadaa ili kulinda kitumbua chao mbali na wanaojipendekeza ili lau wakumbukwe. Lazima niseme wazi; naandika kuwasaidia na kuwakosoa badala ya kuwasifia mambo ya kipuuzi. Rais Magufuli aliomba watanzania tumsaidie katika uongozi wake. Hii nayo ni mojawapo ya kumsaidia kimawazo ili asiingie mkenge akapoteza sifa zake njema na kujuta kama Mkapa ambaye kwa sasa anajiishia tu akiomba Mungu asitokee rais mwenye kuchukia ufisadi akafichua uovu alioufanya kwenye uwekezaji ambao umeiingiza nchi kwenye umaskini bila ulazima.
Janet pia anaweza kuiga mfano mwingine toka kwa mama Maria Nyerere ambaye hakujiingiza kwenye biashara yoyote eti kwa vile mumewe alikuwa rais. Mama huyu hadi sasa anaheshimika kwa kumsaidia mumewe kuipusha ikulu kuwa pango la wezi kama ilivyokuja kugeuka pindi tu mwalimu alipong’atuka wakati ruksa na vimemo vya first lady.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili.
No comments:
Post a Comment