The Chant of Savant

Thursday 1 August 2019

LAITI WOTE TUNGEIPENDA AFRIKA NA KUWAZA KAMA RAIS MAGUFULI!


Rais John Pombe Magufuli anaweza kuwa rais pekee wa Kiafrika aliyeamua kukataa kuaminishwa kuwa Afrika ni bara maskini. Naungana na msimamo huu kama nilivyouandikia kwenye vitabu vyangu vingi vya kiada kuwa kinachochelewesha bara la Afrika kufikia maendeleo au ulinganifu na nchi au mabara mengine ni ile hali ya:-
Mosi, kuwa-defined, sina neno la kiswahili, na watu wengine hasa wale walioitawala na wale wanaolenga kuinyonya na kuendelea kuiibia na kuidhalilisha.
Kinachofanya hali hii kuwa ngumu ni ile hali ya viongozi wengi wa kiafrika kuamini katika definitions kama vile ulimwengu wa tatu, nchi maskini na nyingine nchi zao zinazopewa. Hawahoji wala kuzikaidi kama anavyofanya Magufuli.
Pili, ni ile hali ya kuaminishwa kuwa Mwafrika hana uwezo wa kufikiri sawa na wengine, hivyo, hawezi kufanya kitu chochote bila msaada wa wafadhili ambao wengi wao ni weupe au wakoloni wetu wa zamani toka nchi ya magharibi. Hii ndiyo maana Afrika ina demokrasia aghali ya kuazima toka nchi za magharibi ukiachia mbali serikali nyingi za kiafrika kuwa tegemezi kwa viinchi vingine vidogo kama vile Ubelgiji, Uholanzi na vingine vingi vilivyopata utajiri wake kwa kuliibia bara hili.
Tatu, ni ile ya kubaguliwa kulhali na kuaminishwa kuwa Mwafrika ni tegemezi wakati ushahidi wa kihistoria unaonyesha kuwa Afrika haikuwahi kuishi kwa misaada kabla ya kuja kwa ukoloni ambao uliwezeshwa na dini na mawakala wake wengine. Sambamba na hili, Waafrika wamekubali kutumika kueneza ujinga huu kwa kusalitiana hata kutawalana kijinga jambo ambalo Magufuli anaonekana kuliasi taratibu kwa vitendo.
Nne, ni ile hali ya Mwafrika kubaguliwa na kila kitu chake tokana na msigi mbovu uliojengwa na dini ambazo ziligeuza kila kitu cha kiafrika cha kishetani huku wakitukuza kila kilicho cha wenye dini husika.
Magufuli, kama kiongozi na Mwafrika, ameamua kuanzisha vuguvugu jipya la kimapinduzi kifikra kwa kutaka Waafrika wakengeuke na kubadili msimamo na kuanza kujiona kama matajiri na wenye uwezo sawa na watu wengine.  Hiki ndicho unaweza kukiita mapinduzi ya kifikra yenye lengo moja tu, yaani kuasi mfumo kandamizi, superstructure, ambao umeendelea kuidhalilisha, kuihadaa na kuinyonya Afrika tangu kuanza kwa ukoloni na utumwa. Kwa wale ambao tumejikita kwa muda mrefu kwenye dhana ya decolonisation au uhurishaji, hili ni jambo jema sana.
Kimsingi, anachofanya Magufuli ni kuanzisha mchakato wa ukombozi wa kimawazo sambamba na walivyojaribu kufanya waanzilishi kama vile Julius Nyerere na Kwame Nkrumah ambao waliacha urathi mkubwa wa mawazo na harakati za ukombozi wa kweli wa Afrika. Wao waliweka msingi wa kinadharia, theoritical foundation. Magufuli, kama atapata waungaji mkono, anaweka msingi wa kivitendo, practical foundation ambao kama viongozi wengi wa kiafrika wakiufuata wanaweza kuzikomboa nchi zao tokana na ukoloni mamboleo na utegemezi na utumwa wa kujitakia utokanao na kutojiamini. Kama nchi za kiafrika zitafanya hivi, hazitakuwa zikiogopana kiasi cha kushindwa kuuungano na kujiondoa kwenye minyororo ya mkutano wa Berlin 1884 ulioligawa bara la Afrika kwenye viinchi vidogo na dhalili ili kuendelea kunyonywa na viinchi nyemelezi vya ulaya.

No comments: