How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 10 August 2019

Ajali ya Moto Morogoro Somo kwa Watu Wote

    Image result for ajali ya moto morogoro photos       Ajali ya Jumamosi 10 Agosti ambapo baadhi ya watanzania wapatao zaidi ya 60 walipoteza maisha ima wakiwa wanachota mafuta baada ya gari la mafuta kupata ajali au kuwa karibu na eneo la ajali ina somo kubwa kwetu kama taifa. Pamoja na kutisha na kusikitisha kwa tukio hili lililoacha simanzi nyingi kitaifa, kama taifa na watu, tunapaswa kujisuta na kuthamini maisha yetu. Si jambo jema inapotokea ajali watu kwenda kuiba au kuchukua vitu vinavyokuwa kwenye chombo kilichopata ajali. Hii ni jinai kama jinai nyingine itokanayo na ujinga na umaskini vya kupita kiasi. Kama taifa, kuna haja ya kuanza kuwaelimisha watu wetu kuwa wanavyoona mambo siyo yalivyo. 
          Ni ajabu kidogo kwa watu wenye akili kukimbilia kuchota mafuta huku wengine wakiwa wanavuta sigara ukiachia mbali kutochelea kuwa unaweza kutokea mlipuko na kusababisha maafa kama yaliyoshuhudiwa Morogoro. Pamoja na ujinga na umaskini, pia ujinai na roho mbaya vinachangia kadhia hii. Kabla ya kuchukua hatua ya kwenda kuiba kwenye chombo kilichopata ajali, jifikirie. Je ningekuwa mimi mhanga ningependa nitendeweje? Isiwe mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Ni jambo la aibu kwetu kama taifa kuendelea kuthamini udohoudoho kama huu kiasi cha kuhatarisha maisha ya wengine. Tunatoa mkono wa rambirambi kwa wafiwa tukiomba wawe ni mabalozi wazuri wa kuelezea kadhia hii ya kutumia ajali kama fursa ya kujipatia kipato. Tusiogopane kuambiana ukweli. Kwani kufanya hivyo ni maafa zaidi ya haya tunayoshughulikia. Inabidi, kama taifa, tukemee vikali tabia hii ya maangamizi ya kujitakia.

No comments: