
Mbali na kutambua mchango wa Kiswahili na Tanzania, Kiswahili kitakuwa lugha pekee ya Asili ya Afrika na ya Ukombozi kutumiwa na nchi wanachama. Hii ni njia sahihi ya kujikomboa (true decolonisation) ukiachia mbali kuondoa sumu ya ukoloni (detoxification). Mbali na SADC, Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) ishakiridhia na kukitumia ukiachia mbali nchi kama vile Rwanda na Sudan ya Kusini kukitambua umuhimu wake huku Afrika ya Kusini, kwa kutambua mchango wa Kiswahili na Tanzania kwenye ukombozi wake kuamua kifundishwe mashauleni. Tunaamini. Kuna siku Kiswahili kitakuwa si lugha ya EAC wala SADC tu bali lugha ya Afrika. Na hili likitimia, Afrika itakuwa imeanza kupiga hatua kwenye ukombozi wa kweli.
Ukiachia mbali na kuwa lugha ya asili ya Afrika, Kiswahili, kitawafanya Waafrika kujifunza na kukijua kirahisi kutokana na asilimia kubwa ya Waafrika kuwa na lugha zenye kufanana kitabia na kimuundo. Pia Kiswahili, kinaweza kuleta manufaa ya kiuchumi kwa Afrika kwa maana kwamba, fedha nyingi zinazotumika kutafsiri kwenye mikutano ya Kiafrika zitatumika kwenye maeneo mengine. Hata gharama ya kufundisha Kiswahili si aghali kama vile lugha za kikoloni ambazo bado Afrika haijazimanya vilivyo. Hivyo, kutegemea wageni kuwafunza watu wake wanaoshughulikia masuala mbali mbali. China, Japan, Urusi hazikufikia kwenye maendeleo yake kwa lugha za kikoloni. Korea pia kadhalika. Kwanini Afrika isiweze?
No comments:
Post a Comment