Gazeti hili la tarehe 28 Novemba lilitoa ripoti ya utafiti juu ya kutamalaki kwa rushwa ya ngono kwenye taasisi za elimu ya juu. Utafiti huu ulivitaja vyuo vikuu viwili vya umma kimoja kikongwe na kingine kikubwa nchini. Kama kweli hali iko hivi, kwanza hii ni aibu. Na pili ni kielelezo kuwa mfumo wetu wa elimu una matatizo yanayopoaswa kushughulikiwa bila huruma kama ilivyokuwa kwenye kadhia ya vyeti vya kughushi na ajira na wanafunzi hewa. Tatu, udhaifu na uoza huu utumike kama fursa ya kurekebisha mfumo mzima ili uweze kuwa wajibikaji na kuzaa matunda tarajiwa.
Leo, tutatoa baadhi ya mapendekezo ya kupambana na kuondoa aibu na kadhia hii kama ifuatavyo:
Mosi, tujenge mfumo wenye uwazi katika uendeshaji taasisi zetu na utendaji kazi ambapo lazima kuanzishwe mfumo wa utathimini wa walimu na wanafunzi sawia na sambamba. Hapa ni kwamba, walimu wawatathmini wanafunzi na wanafunzi wawatathmini walimu wao. Hapa Kanada, mwalimu anamfanyia mwanafunzi tathmini na kadhalika–––kila baada ya kumaliza somo–––wanafunzi hupewa fomu za kuwatathmini walimu wao bila kuweka majina yao. Utaratibu, licha ya kuleta uwajibikaji na ushindani, unajenga imani kwa wanafunzi na walimu. Hapa hakuna kuchezeana wala kupunjana. Ukisoma unasoma kweli kweli vinginevyo, utatafuta la kufanya kama hufai.
Pili, tuanzishe utaratibu wa walimu kuwajibika kisheria kuwa na sera ya mlango wazi ambapo kila kinachofanyika ofisini kinaonekana. Hili usaidia si kuleta uwazi tu bali hata kuheshimiana na kuwajibika
Tatu, Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ihakikishe inaweka mashushu wake vyuoni kwenye ngazi zote kuanzia wanafunzi hata wafanyakazi na uongozi. Hili, licha ya kubaini tatizo na kulishughulikia vilivyo mapema, litajenga hofu na mazingira ya uwazi na uwajibikaji si kwa walimu tu bali hata wanafunzi wanaotaka kupata shahada za dezo bila kustahiki au kuzihenyekea.
Nne, wasomi wajiepushe na kujichafua na kuwaharibia maisha wanafunzi. Msomi aliyeelimika vilivyo anapaswa kujua mipaka yake. Kutumia elimu au mamlaka kujipatia rushwa ya aina yoyote ni Ushahidi tosha kuwa mhusika–––licha ya kutokuwa muadilifu–––hajaelimika ipasavyo na vilivyo. Watu wa namna hii wanapaswa ima kufukuzwa kazi au kurejeshwa darasani ili wasome na kuelimika.
Tano, wale wanaopatikana na hatia wapewe adhabu kali ili liwe somo kwa wengine wanaotarajia kujihushisha na jinai na uchafu huu. Hapa lazima adhabu iwe kwa wote, yaani mtoa na mpokea rushwa. Wanafunzi wanaoruhusu kuchezewa wanakuwa washirika wazuri. Kwanini wasiripoti kadhia hii ili kuanzisha mgogoro ambao mamlaka zitaushughulikia ili kuepuka kupatilizwa au kuonewa? Maana bila kufanya hivi, wanafunzi watakaolipoti uchafu huu, wanaweza kuonewa ima na wale waliowatuhumu au marafiki na washirika wao. Lazima kuwepo na namna ya kuwalinda wanafunzi watakaotoa malalamiko ya kuombwa rushwa. Pia hapa lazima tuwe makini wasitokee wanafunzi wakatumia fursa hii kuwakomoa wabaya wao ambao ni walimu wao. Ifikie mahali hata mwanafunzi akipendekeza kutoa rushwa ya ngono kwa profesa, mhusika naye amripoti ili kutenda haki kwa wote. Maana rushwa mara nyingi, ni makubaliano baina ya mtoaji na mpokeaji.
Sita, wanafunzi nao waache njia za mkato. Mfano, hapa Kanada, hakuna namna ya kupata shahada bila kuihangaikia. Mfano, shahada za kwanza, humjengea mwanafunzi uwezo wa kujitafutia maarifa huku za uzamivu zikimpa changamoto ya kuweka maarifa yake kwenye vitendo huku za uzamili zikimpa changamoto mwanafunzi kuyazalisha na kuyatumia maarifa na ujuzi wake. Huwa nashangaa kuona maprofesa au madaktari ambao licha kuficha tasnifu zao, hawachapishi. Huwezi kuwa mwanataaluma aliyeiva kweli kweli ukashindwa kuchapisha. Usipofanya hivyo, unahatarisha ajira yako. Kwani kazi ya profesa siyo kufundisha tu bali kuzalisha elimu mpya kwa njia ya utafiti na machapisho. Hii humsaidia mhusika na taasisi yake kutoa mchango kwa jamii yake kitaaluma.
Saba, kuna umuhimu wa kuanzisha elimu ya kupambana na rushwa kwa jamii ili wahusike wajue madhara yatokanayo na maamuzi ya kuomba au kutoa rushwa. Kama ilivyo kwa magonjwa ya kutisha, rushwa ichukuliwe kama janga ambalo dawa yake ya kwanza iwe ni kuielimisha jamii juu ya madhara yake na yatokanayo na kujihusisha nayo.
Nane, tujenge mfumo wa kushukiana na kutoaminiana. Hapa Kanada, kwa mfano, hakuna cha kuaminiana kienyeji. Kila mtu anajua haki zake; anajua mipaka ya mamlaka na haki zake. Ukijenga jamii ya namna hii, licha ya kutenda haki, unakuwa na jamii makini na yenye ushindani na kuheshimiana. Jamii ya namna hii lazima itaendelea. Hii ni kwa sababu kila anayepewa jukumu, licha ya kujua wajibu wake, anakuwa ameiva kweli kweli kulitekeleza huku akijua madhara ya kulala kwenye usukani kama wasemavyo huku.
Tusiangalie rushwa ya ngono tu. Tuangazie na rushwa nyingine ambazo huwafanya watu wasiostahiki kuwa na ukwasi usiokuwa na maelezo ya kueleweka. Mfano, hapa Kanada, huwezi kulala maskini ukaamka tajiri kama ilivyokuwa nyumbani. Kila mtu hujaza taarifa zake za mapato kila mwaka. Hivyo, kipato cha kila mtu kinajulikana na hivyo ndivyo anavyopaswa kuishi. Hakuna njia za mkato au mission town kama nymbani ambako mtu anaweza kulala maskini akaamuka tajiri bila vyombo vya sheria kumshika, kumhoji, kumtaka maelezo na kumchukulia hatua pale anapogundulika kuwa na kipato kisichoweza kutolewa maelezo. Utaratibu huu huondoa mazingira na motisha wa wananchi kujiingiza kwenye jinai ya aina yoyote kama njia ya kujiongezea kipato.
Tumalizie kwa kuhimiza kuwa lazima tufanyie mfumo wetu wa elimu pamoja na mingine maboresho na marekebisho makubwa ili kuweza kupata matokeo tarajiwa.
Chanzo: Nipashe Jumapili.
No comments:
Post a Comment