The Chant of Savant

Sunday 6 December 2020

POLENI KAIRUKI, KIGWANGALA, MAKAMBA, MAKONDA, NNAUYE, NA MWAKYEMBE

 


Hakika, kutangazwa kwa baraza jipya la mawaziri kumewaacha wengi vinywa wazi ingawa ilitarajiwa kutokana na kutokuwa rahisi kutabiri hatua ambazo rais John Pombe Magufuli angechukua. Nani alijua vigogo kama Hamis Kigwangala wangekosekana kwenye baraza la mawaziri? Wapo ambao walitegemea huruma ya bosi kama vile Dk Harrison Mwakyembe, Angela Kairuki na Kangi Lugora ambao waliangukia pua kwenye uteuzi wa ndani wa chama. Mfano, Kingwangala alisifika kwa utendaji kazi wake. Hata hivyo, hatuwezi kujua alikuwa ametimiza matarajio kiasi gani. Lugora, alipoteuliwa waziri wa mambo ya ndani aliingia na mikwara kibao kiasi cha wanaojua mambo ya uongozi kutabiri kuwa mbio zake zingekuwa za sakafu kama zilivyokuwa. Alitumbuliwa na kutokomea kwenye kaburi la sahau haraka sawa na Paulo Makonda ambaye, kwa kiasi fulani, madaraka yalimpanda kichwani hadi akafikia kudharau ushauri wa bosi wake wa kumtaka achape kazi na kuachana na tamaa za kisiasa bila kusikiliza. Naye, kama Lugora ametokomea kwenye kaburi la sahau haraka sana. Kwa upande wa Mwakyembe, alianza kuonyesha kupwaya pale alipopewa wizara yake ya mwisho akiondolowa kwenye ya kwanza iliyokuwa ikimfaa kama mwanasheria. Kairuki amepotea tokana na kushinda kufuzu kwenye mbio za ndani ya chama.
        Ukiachia hao hapo juu, wapo walioshinda kwenye mchakato tena wengine bila kupingwa kama vile Januari Makamba na Nape Nnauye lakini wakakwama kuteuliwa. Wanaojua mwanzo na mwisho wa kupanda na kushuka kwa wawili hawa, watajikumbusha walivyomkosea adabu bosi wao kiasi cha kuwavua uwaziri. Japo waliomba msamaha, ufa ukiishaingia umeingia hasa kwenye dimbwi lenye samaki wengi ambapo mvuvi anaweza kumvua yeyote.
Ukiachia hao hapo juu, wapo walioibuka kidedea tokana na sababu mbali mbali ikiwamo utendaji na umakini wao kama vile Philip Mpango waziri wa uchumi, Profesa Kitilya Mkumbo na Profesa Palamagamba Kabudi bila kuwasahau Ummy Mwalimu, Seleman Jafo, Juma Aweso  George Simbachawene na Dotto Biteko mbali na wapya kama vile Dk Dorothy Gwajima, Elias Kwandika,  Leonard Chamuriho, Mwambe Alphonce, Probas Katambi, David Silinde na wengine ambao nyota zao zimechomoza ghafla.

No comments: