How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 5 December 2020

Mnaichafua Tanzania Kupata Nini Jamani?

Kumekuwa na kampeni za makusudi za kupotosha ukweli baada ya kuisha uchaguzi mkuu wa 2020 za kuichafua, kuihujumu na kuisingizia Tanzania. Naseme hivi tokana na wahusika kutotoa ushahidi wowote unaoingia akilini zinaoendeshwa na  baadhi ya watanzania walioshindwa kwenye uchaguzi uliopita pamoja na mashabiki wao wa nje ya nchi. Mfano wa hivi karibuni, nilihudhuria mjadala kupitia zoom juu ya mashambulizi ya kigaidi huko Mtwara yaliyofanywa na magaidi toka Msumbiji. Tofauti na mijadala niliyowahi kuhudhuria, huu ulionyesha wazi namna ya waliouandaa walivyolenga kulaumu serikali kwa “kutoshughulikia” kadhia hii jambo ambalo, hadi sasa, sijui kama lina chembe ya ukweli–––ikizingatiwa kuwa Tanzania haijawahi kuacha kuwalinda wananchi wake. Isitoshe, madai yaliyotolewa ni makubwa mno kuwa magaidi walichoma vijiji na kuua watu ukiachia mbali kuingiza silaha za kivita nchini. Katika mjadala husika, waandaji walijigeuza wajuaji na wasemaji wa kila kitu huku wengine tukiachwa. Nilishangaa walivyokuwa wakiteua waulizaji na wajibuji maswali. Yupo mmoja, kiongozi wa chama cha upinzani, aliyetoa paka kwenye kapu. Alisema “ni mimi (alitaja jina lake) nataka kuuliza swali.” Aliruhusiwa kuongea alivyotaka akitupa madongo yake kwa serikali bila chembe ya ushahidi kiasi cha kutuacha wengi vinywa wazi.

 Kuonyesha upande mmoja, hapakuwapo na msemaji wa serikali wala ushahidi kuwa waliitaarifu ikakataa kutoa maelezo au kutuma msemaji wake.

Kwa watu hawa, madaraka hayana maana; wala demokrasia haileti maana bila ya wao kuwa kwenye ulaji. Ama kweli mvunja nchi ni mwananchi! Kama tutakuwa wakweli, watanzania–––hata kabla ya kufanya uchaguzi–––walionyesha kuridhishwa na uongozi wa awamu ya tano ambao, kwa kipindi hiki, wamechagua chama tawala kiasi cha kuufuta upinzani, kwa kuazima maneno toka kwa rafiki yangu Mzee Pius Msekwa. Kama nilivyowahi kusema huko nyuma, hii inatokana na serikali kujibu karibu kero zote zilizowasumbua watanzania tangu kupata uhuru–––kimsingi, ushindi huu haukusababishwa na kuiba kura au njama yoyote zaidi ya utendaji uliowaridhisha wapiga kura. Pamoja na ukweli huu kujulikana, bado wapo wanaoendelea na wimbo ule ule wa kutaka uchaguzi uonekane uliibiwa bila kutoa hata chembe ya ushahidi. Kulalamika ni haki ya wahusika; kudanganya na kuzua si haki. Leteni Ushahidi; tuhukumu. Watanzania sio wajinga wala wapumbavu kushindwa kupima ushahidi utakaotolewa. Kwa namna ghilba hizi zinavyofanywa, kuna dhana kuwa kuna maadui wa nje ima wanaowatumia wahusika au wahusika kutafuta watu wa kuwatumia ili kufikisha malengo yao.

            Gazeti hili lina kanuni ya kutotaja majina vinginevyo kuwepo ulazima wa kufanya hivyo. Hivyo, nitatolea mfano wa kiongozi mmoja aliyeshiriki uchaguzi akashindwa na kutimkia nje akidai usalam wake ulikuwa hatarini. Madai yake ya tishio la usalama wake yalitufanya tuulize maswali kadhaa. Mosi, je ni kweli maisha ya kiongozi huyu kweli yalikuwa hatarini? Kwanini iwe baada ya uchaguzi mkuu? Kama serikali haikumhakikisha usalama siku aliyorejea toka ughaibuni ambako alirejea baada ya kushindwa, ilikuwaje akawa salama kwenye kampeni zilizompeleka sehemu mbalimbali tena zisizo na usalama wa uhakika nchini? Je tatizo ni tishio la usalama au ni zaidi? Je alikuwa ametumwa? Je alikuwa anatafuta kiki baada ya kukaa nje ya ulingo wa siasa kwa kitambo kabla ya uchaguzi? Je alikuwa anatafuta urais ili kulipiza kisasi au kujaribu bahati? Je huu si ushahidi kuwa kama angeshinda, angeweza kutumiwa kirahisi na wakoloni na maadui wa taifa kama alivyodhihirisha baada ya kushindwa?  Kwani, alikaririwa na vyombo vya habari kuwa anakwenda nje kuendesha mapambano dhidi ya maovu nchini. Ya kweli haya? Wapo wanaodai kuwa mhusika alikwenda nje kuwapigia magoti wafadhili wake wamsaidie kudhoofisha juhudi za kuijenga Tanzania ambazo haziwapendezeshi kutokana na nchi kuachana na uombaomba na utegemezi? Ukweli au uongo wa madai itategemea wahusika watakavyojitetea? Ama kweli mjenga  na mbomoa nchi ni mwananchi mwenyewe.

            Kinachoendelea–––hata kama kitavikwa kila aina ya sifa za kidemokrasia–––hakilisaidii taifa wala wale walioko nyuma ya mpango huu ambao mwisho wake ni hasara. Wahusika wangeleka madai yao kwenye mamlaka husika. Huko nje hakuna msaada wala jibu la tatizo. Madai ya kuibiwa kwa uchaguzi–––yawe ya msingi au vinginevyo–––si mapya wala si tatizo kwa Tanzania wala Afrika tu. Hivi karibuni, kwenye uchaguzi uliopita nchini Marekani inayojisifia kuwa mwalimu wa demokrasia duniani, yalizuka madai ya kihuni na yasiyo na msingi wala mashiko ambapo rais anayeoondoka alishindwa vibaya. Kwa msingi huo, licha ya kukataa kumpongeza mpinzani wake aliyemshinda kihalali, bado analalamika kuwa aliibiwa ushindi wakati serikali yake ndiyo iliyosimamia uchaguzi husika.

            Kwa wanademokrasia wa kweli, kushida na kushindwa si sababu za kubomoa, kuzushia au kuijengea nchi uhasama kwa kuitangaza vibaya. Kila mtu ana nchi moja aliyopewa na Mungu, yaani alipozaliwa bila kuomba wala kujaza fomu. Wahusika wanaweza kupata uraia nje japo uraia wa karatasi thamani yake ni ndogo ikilinganishwa na ule wa kuzaliwa. Ndiyo maana ukiishi ughaibuni huachi kuonyeshwa kuwa wewe ni wa kuja na huwezi kuwa haki sawa na wazawa kwa vile wanajua una kwenu. Kwa kuzingatia hili, wanaoichafua, kuizushia na wanaoidhalilisha Tanzania wanafanya hivyo ili kupata nini zaidi ya hasara?

            Kitu kinachoshangaza ni ile hali ya wanaotuhumiwa kutoa hata nafasi kwenye kuunda serikali ambayo wahusika walishindwa kuchaguliwa kwenye uchaguzi. Kwa upande wa Zanzibar, umeonyesha mfano wa kuwa kinachogombaniwa si kweli. Kwani, kama wahusika walishindwa na wakakaribishwa kwenye serikali, wanachotafuta cha mno ni nini zaidi ya kuichafua Tanzania bila sababu za msingi?

            Tuhitimishe kwa kushauri watanzania tuwe wazalendo. Tanzania ndiyo nchi yetu pekee. Kwingine hakuna jibu; na kama lipo ni la muda. Wanaoichafua Tanzania wanafanya hivyo kupata nini?

Chanzo: Nipashe Jumapili kesho.

No comments: