How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 20 October 2021

Waraka kwa Waumini wa Uchama, Udini, Kkabila na Ukanda na Wantanzania.

Maneno ya Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba yalinichoma na kunisikitisha na kunilazimisha kuandika waraka huu kwa watanzania hasa viongozi. Warioba alikaririwa hivi karibuni akisema “ukabila unaanza kuzungumzwa sana, udini unaanza kuzungumzwa sana, ukanda unazungumzwa sana, uchama unazungumzwa.” Ni aibu kweli kweli kwa taifa. Ni hatari sina mfano. Hata hivyo, nakushukuru sana mzee wangu kwa kuliona hili na kulisemea hata kama ni kwa kuchelewa kidogo hasa ikizingatiwa kuwa kurejea kwa ukabila hakukuanza jana. 
Warioba aliongeza kuwa “watanzania wenzangu, tukemee watu wote wanaotaka kuleta mambo ya ukabila, udini, ukanda na uchama, tuwe kitu kimoja, tuilinde amani yetu ambayo Mwalimu Nyerere alituachia.”
 Kwa wanaojua namna ukabila unavyoendelea kuzihangaisha nchi kama Kenya, Afrika ya Kati, Kameruni, Nigeria, Somalia na nyingine, watakubaliana nami kuwa janga la ukabila lina madhara makubwa. Waulize warundi na wanyarwanda hata wakenya ambao walikwishanyongana kisa ukabila. 
Wasomi wengi wanakubaliana kuwa Tanzania ni mwalimu wa kuondosha ukabila. Mwandishi wa makala hii aliandika tasnifu yake juu ya namna nchi za kiafrika zenye ukabila zinavyoweza kuupiga vita na kuushinda kwa kujifunza toka Tanzania. Hivyo, anapoona kansa hii ya kijamii ikirejea, anajisikia si kuaibika tu bali hata kuugua. Kwani, pamoja na umaskini wetu, watanzania tunafika dunia nzima kwa mambo mawili yaani kuwa nchi yenye amani na mshikamano na kutokuwa na ukabila japo tangia miaka ya 90 baada ya kung’atuka baba wa taifa Hayati Mwl Julius K Nyerere, tulianza kushuhudia udini uchwara ukiibuka na kukemewa naye na hatimaye kupungua. 
Nimegusia hapo juu kuwa ukabila ulianza kitambo kidogo hasa baada ya kuanza kuona hisia na tabia za kikabila hata kwa viongozi wetu wa juu. Kwa mfano, kuna baadhi ya teuzi zilifanyika chini ya baadhi ya awamu zilizopita zilizokuwa na sura za kidini, kikabila hata kikanda huku tukishindwa kuzikemea kwa kuogopa wenye madaraka. Nitatoa mifano toka awamu zote. Kwenye awamu ya pili, tulianza kuona kuibuka kwa uholela uliotoa mazalia kwa kansa za udini, ukabila, uchama hata ukanda. Awamu ya tatu ilifisika kwa ubinafsishaji ambao pia ulibeba sura ya ukabila baada ya wenzetu wa kabila fulani kumtumia ndugu yao kwenye nyadhifa za juu kulihujumu taifa letu. Rejea kashfa ya ABSA ambapo ndugu wa mke wa mkubwa fulani walituhumiwa kuihujumu na hatimaye kuia benki ya Biashara (NBC). Awamu nne ilisifika kwa uwekezaji ulioishia kuwa uchukuaji wa ajabu wa mali za umma. Tulianza kuona watu wa rangi fulani wakijitwalia kila kitu wakiwatumia viongozi wetu wajinga na wasioona mbali. Awamu ya tano ilisifika kwa upendeleo wa kikabila pamoja na kufanya makubwa. Pia, uchama ulikua kiasi cha uchaguzi kugeuka kiini macho cha kurejesha utawala wa chama kimoja huku wakubwa wakipendelea maeneo yao kihuduma na kiuchumi kiasi cha kutengeneza hata vimikoa visivyotakiwa kutumikia utashi wa kikabila na kikanda. Wapinzani walihoji na kukemea. Lakini walipuuzwa na kupatilizwa. Awamu ya sita bado changa. Sina cha kusema juu yake japo ushauri wangu ni kwamba ichukue tahadhali isijichafue na kansa hizi kwa sababu zozote. Kwani , siyo siri. Tunaanza kusikia wananchi wakilalamikia kukosekana kwa huduma ukiachia mbali kuanza kujadili miradi ya uwekezaji tuliyoambiwa ni ya kichaa na kipumbavu. Hizi si dalili nzuri wala mwanzo mzuri.
Nikirejea kwenye kansa tajwa, naungana na Jaji Warioba kuwa tunapaswa si kukemea tu bali kuchukizwa na kuzisaka na kuziteketeza. Tuukatae uchama, udini, ukabila na ukanda na uchafu mwigine kama huu. Ni vigumu kujenga ila ni rahisi kubomoa. Tulitumia miaka zaidi ya 30 kujenga taifa lisilo la kikabila, kidini, kikanda japo tangia awamu ya kwanza tulijenga uchama kwa kuwa na chama kimoja kilichoua siasa za ushindani.
Kimsingi, uchama, udini, ukabila na ukanda ni mabaki ya ukoloni. Kabla ya kutawaliwa, waafrika hawakuwa na ukabila zaidi ya utaifa wa kiafrika. Walipokuja wakoloni na mkakati wa gawanya na utawale, walifutilia mbali mataifa asilia na kuigawa Afrika vipande vipande na kuzalisha mataifa dhaifu na ya hovyo ya sasa. Walianzisha makabila mapya ili kupambana na mataifa ya kiafrika yaliyokuwa na nguvu. Mfano, hapa Tanzania, wakoloni walitengeza kabila la wahaya ambalo halikuwapo ili kupambana, kufisha na kufuta himaya ya Karagwe iliyosifika enzi zile. Mifano iko mingi. Kule Afrika Kusini walianzisha Bantustans.
Tukija kwenye uchama na ukanda hata udini, vilianzishwa kwa makusudi kuwaganya waafrika ili kuwatawala. Mfano, vita baridi ilisimika uimla wa chama kimoja kwa mataifa yaliyokuwa ya kijamaa na kisoshalisti huku udini na ukanda ukienezwa kupitia madhehebu ya dini. Mfano, wamisionari walijenga mashule kwenye maeneo walipo waumini wao hasa yenye rutuba walikoanzisha biashara ya mazao ya biashara huku wakoloni wakiwaacha baadhi ya wenzetu mfano waislamu bila elimu ya maana zaidi ya elimu ya kidini wakijua wakiondoka haya matatizo yangeisumbua Afrika huru.
Kansa tajwa hapo juu zilisaidiwa na kuibuka kwa uchoyo, ufisadi na upogo kiasi cha kutishia kuzisambaratisha baadhi ya nchi huku maangamizi haya yakitendwa na wananchi wenyewe badala ya wakoloni kwa faida ya wakoloni. Kwa nchi zenya raslimali lukuki kama Tanzania, kurejea kwa kansa hizi ni adhabu ya kifo ya kujitakia hasa wakati huu ambapo tuna uhaba wa kazi, huduma za kijamii na uwekezaji ambapo kila mwenye mamlaka ataangalia ukoo wake, kabila lake, dini yake hata kanda yake.
Tuhitimishe kwa wosia wa nguli mwingine, Waziri Mkuu Mstaafu Dkt Salim Ahmed Salim alioyotoa mwaka 2015 kuwa “na kamwe tusifikiri kuwa amani na umoja ni vitu ambavyo vipo tu… ukiona kuna amani na umoja ujue kuwa zilifanywa jitihada, tena jitihada za kweli kweli. Tanzania ikipata matatizo hakuna atakayepona. Biashara haiwezekani katika mazingira ambayo nchi haina amani na utulivu; kilimo na ufugaji haviwezekani penye fujo.” Mwenye macho na aone na mwenye masikio asikie huku mwenye akili akitia akilini. Ni ushauri wa bure tu.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: