The Chant of Savant

Tuesday 12 October 2021

Barua ya Wazi kwa Polisi, Watanzania

Hakuna kitu kinatia aibu na kusikitisha kama taarifa kuwa askari polisi saba wa Tanzania waliingia nchini Malawi kinyume cha sheria tena wakifukuzia magendo ya shilingi 30,000. Hii ni akili au matope? Hata hivyo, tusiwashangae sana wenzetu hawa waliotia aibu kwa taifa, familia zao, kazi ya polisi hata wao wenyewe. Huu ni ushahidi kuwa watu waovu na wabadhirifu hutumia akili vibaya kufikia maangamizi yao hata taifa. Wengi wanajiuliza: ilikuwaje watu wazima saba kujiingiza kwenye aibu, hatari na kadhia kama hii bila kutumia akili. Kwa waliosoma saikolojia watakubaliana nasi kuwa waovu wengi wenye uchu na uchoyo wa kupata, mara nyingi, huwa hawatumii akili; hata wakizitumia, huzitumia vibaya hata kwa maangamizi yao wenye ukiachia mbali wengine.
Ndugu zangu Polisi na Watanzania wengine, hili liwe si onyo tu bali hata somo kuwa dhuluma hailipi. Sina haja ya kuwatetea wafanya magendo waliohusika na kadhia hii. Hata hivyo, nikizingatia makali ya maisha na mabaki ya ukoloni ulioligawa bara letu la Afrika kwenye vipande vya nchi dhaifu, maskini na tegemezi, haiingii akilini kupambana na watu wanaotafuta riziki wakati tunawaendekeza, kuwalinda na kuwatetea majambazi na mafisadi wakubwa ambao madhara ya jinai yao yanaumiza wengi bila sababu ya msingi zaidi ya roho mbaya, uroho na ujinga. Hivi, hawa polisi hawakuona mabaya mengi yanayofanyika? Sishangai hata kidogo. Wangeonaje hili wakati jinai ndiyo umekuwa mtaji wa mafanikio yao kwa madhira ya wengine wengi tena wasio na hatia?
Jukumu na kazi ya polisi ni kuwalinda raia na mali zao. Hata hivyo, kwa nchi nyingi za kiafrika, hali ni kinyume. Tumekuwa mataifa na jamii ya hovyo inayoshabikia kupata bila kuhoji kupata huku kunapatikana au kufikiwa vipi. Tuna wenzetu wengi, mafisadi, majambazi, dhulumati hata wauaji ambao mtaji wao mkubwa ni kutuhujumu na kutuumiza. Polisi aliyekula kiapo kuwalinda wananchi anapojiingiza kwenye hatari na kadhia kama hii, mkono wa Mungu humshukia na kumuadhibu ukiachia mbali kumuaibisha na kumfunua. Je tunao askari na maafisa wengine wengi wa serikali wanaotenda jinai hii? Tunao mahakimu na majaji, watendaji wa seriali kuu na za mitaa wanaoishi kwa jinai hii? Tunao mawaziri wangapi wanaopata cha juu na kuona ni sawa? Tunao wabunge wangapi wanaopitisha sheria za hovyo bila kujali umma? Tunao walimu wangapi wanaovujisha mitihani mbali na madaktari na manesi wanaowatoza rushwa maskini? Tunao maprofesa wangapi wanaomba rushwa iwe ya fedha au ngono kuwasaidia wanafunzi wao? Je tunao waandishi wangapi wanaogundua kashfa hatarishi na kutaka chochote toka kwa mtuhumiwa? Je wapo maafisa biashara na kodi wanaowatoza rushwa wafanyabiashara wakijua wazi wanahujumu taifa? Tumefikia hata kutojali maisha na uhai wa wenzetu kana kwamba hatujui umuhimu wake! Rejea tabibu huko Tanga aliyemfumua mgonjwa nyuzi kwa vile alishindwa kulipa gharama za matibabu. Tuna wengi lukuki tokana na mfumo wetu wa hovyo wa kuumizana na kunyonyana.
Japo waraka huu ni kwa Polisi, kimsingi, ni kwa watanzania wote wapokeaji na watoaji rushwa. Utamkuta askari akiitwa kwenye tukio la uharifu. Badala ya kuangalia madhara, anaangalia atapata nini. Magari mengi ya umma yanatumika kwenye kutengeza fedha kwa wahalifu hawa walioaminiwa na umma kuliko kutoa huduma. Trafiki anapewa rushwa na kuruhusu gari bovu litowe huduma bila kujali madhara yake. Anachojua na kujali ni maslahi finyu na ya hovyo binafsi. Tubadilike. Mwanasiasa anapiga kelele kutetea maslahi binafsi kwa kisingizio cha kutetea umma. Kiongozi wa kiroho mwenye uroho anapiga kelele kuwahimiza wafuasi watoe fedha badala ya kuangalia imani na maslahi yao. Badala ya kukiri kuwa anasukumwa na roho mtakakitu anasingizia roho mtakatifu! Mzazi mpumbavu anamfundisha mtoto wake kuwatumia wenzake kupata bila kuangalia madhara ya mchezo mzima. Mke au mume anamhujumu mwenzake bila kuangalia kuwa naye atahujumiwa na mfanyakazi wa nyumbani. Tajiri anamhujumu maskini bila kujua kuwa naye ana akili. Bosi anahujumu umma bila kujua kuwa mlinzi au shamba boi wake naye atamhujumu. Tuache. Ni hatari kwa jamii na taifa. Tunafanya yote tokana na ujinga na upogo wa kutojua kuwa kila tunalofanya lina madhara au matokeo yawe mabaya au mazuri.
Baba au mama zima linakula kiapo cha uaminifu na kuishia kutenda hujuma. Ukiishi kwa upanga utakufa kwa upanga. Ukipndisha haki au kugeuza haramu kuwa halali–––ni suala la muda tu–––utaumbuka tu. Hii ndiyo tabia ya ukweli na sayansi asilia ya mambo.
Tokana na kadhia hizo hapo juu, je nini kifanyike? Kama jamii na taifa, tukumbuke kuwa tulikuja bila kit una tutaondoka bila kitu. Kwa wale wanaoamini katika maneno ya dini, wasome Muhubiri (1:1-18) anayesema kila kitu chini ya jua ni ubadhilifu mtupu na maonyo mengine mengi. Hebu jikumbushe wale waliohujumu taifa kwa kuingia mikataba mibovu kama IPTL, Air Tanzania, rad ana mengine mengi. Wako wapi? Wengi wameishakufa na wengine wako wanamuomba Mungu awaepushe na kesi na kifo. Je wamepata nini? Mabilionea tuliowafukia wameondoka na nini? Warembo waliotisha wakazeeka au kufa bado wana urembo ‘wao’? wababe waliozeeka na kuishiwa nguvu wana nini? Wasomi waliopotezwa na ujinga na wajinga wana nini?
Tumalize kulishukuru Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua za haraka kuwatimua waharifu hawa haraka. Pia tuwaombe watu wetu kuwa na hekima na ridhiko badala ya kukimbizwa na tamaa na ujinga. Binadamu ni nini na ana nini zaidi ya majuto na udhaifu. Hata ukiwa bilionea, mbabe au msomi wa kutisha, bado u binadamu. Ulizaliwa kama wazaliwavyo wadudu na wanyama na utaondoka kama wao. Uwe mnyenyekevu na mwenye kutenda haki badala ya dhuluma. Hata ujenge ghorofa na kuwa na misururu ya magari, utaondoka mtupu kama ulivyokuja. Wale mliokula viapo basi viheshimuni na kuvishikeni. Mtaondoka wenye amani na furaha. Wanandoa, watendaji wa umma na wengine Heshimu viapo vyenu na nyadhifa mlizopewa na wengine. Ni ushauri tu. Afande jifunzeni kwa wenzenu sawa na wengine wote mlio katika utumishi wa umma hata kuaminiwa na familia na jumuia. Kilichotokea mpakani mwa Malawi na Tanzania ni aibu na somo kwetu sote. 
Chanzo: Raia Mwema Kesho.


No comments: