How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 23 October 2021

Barua kwa Prof Assad, CAG Mstaafu

Kaka, Salamu wa Jina la JMT,
Juzi nilisoma sehemu ukilalamika kuwa unachukia kuitwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG). Kwanza nilishangaa na pia kusikitika kutokana na hoja dhaifu ulizotoa kuhusiana na kutokupenda kuitwa CAG mstaafu, Mussa Assad. Kaka, shukuru huitwi fisadi wala mwizi. Hata hivyo, ngoja niulize. Kaka, hivi unaelewaje dhana nzima ya kustaafu? Kwangu, kustaafu kunatokana na kufikia ukomo wa kufanya kazi fulani ima kwa kutaka au kulazimishwa ima na umri au mamlaka zinazohusika na uteuzi au uajiri au sheria ya ajira. Je wewe imekuwaje siyo CAG mstaafu wakati kama unavyokaririwa ukisema “sipendi sana kusikia neno mstaafu na kwamba neno hilo linaniudhi linapotamkwa mbele yangu” (Mwananchi, Oktoba 6, 2021)? Kwanza, pole sana kaka kwa hili japo unapaswa ujibu swali hilo hapo juu–––tena kwa usahihi. Je wewe imekuwaje ukaitwa CAG mstaafu? Mwandishi aliandika kuwa hupendi kuitwa mstaafu kwa vile hukondolewa kwa kufuata utaratibu na katiba kutosimamiwa bila kutoa ufafanuzi. Je ya kweli haya? Ni utaratibu huu ambao hukuwa tayari kuuelezea wala kuufafanua kwa faida yetu wasomaji pia tusiojua suala zima kitaaluma? Je katiba ilivurugwa vipi na vifungu vipi na nani na kwa nini ili iwe nini? Je kwanini hukupeleka malalamiko haya mbele ya vyombo husika? Je kuna kitu kinafichwa hapa? Je katika kulalamika umeishaona dalili za kupata au kutendewa haki?
Kaka, kitendo chako kina nia njema japo, kwa wengine kinaweza kuonekana kama kitu cha aibu na shaka hasa ikizingatiwa kuwa aliyetengua nafasi yako ni Rais kwa mamlaka yale yale aliyo nayo kukuteua na kutengua uteuzi wako. Hata kama kama uliteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na uteuzi wako kutenguliwa na Rais Hayati Dkt John Magufuli, bado huna hoja kiakili na kisheria kutoa madai unayotoa sasa. Je natoa madai haya tokana na kwamba aliyetengua uteuzi wako hawezi kuja kujieleza au kueleza kwanini alifanya hivyo hata kama sheria hailazimishi hili kufanyika hata kama angekuwa hai?
Kaka, unadai kuwa uliondolewa baada ya kutoelewana na Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai. Je una ushahidi kuwa mgogoro huu na Bunge ndio ulipelekea kutenguliwa uteuzi wako? Je kwa maoni na ujuzi wako, yupi alikuwa sahihi na yupi alikosea? Je kama unao, kwanini usilifikishe Bunge kwenye vyombo vya kutoa haki au kutaka Ndugai awajibishwe kama siyo taasisi anayoongoza? Hivi kaka ulipodai kuwa Bunge ni dhaifu bila kutoa maelezo na ushahidi, ulitaka lifanye nini zaidi ya kuonyesha kuwa siyo dhaifu kwa kukushughulikia–––kama kweli ndilo lililofanya Rais akuteme kama njia ya kukuonyesha kuwa lina nguvu? Unadai ulisema kuwa Bunge likukuwa dhaifu. Je hili lilikuwa sehemu ya kazi yako au ulipitiwa, kughafirika au kuudhika?
Kaka, sina nia ya kukulaumu bali kukushauri. Kwanza, ningekushauri–––kama kweli unahisi umeonewa–––fuata taratibu badala ya kulalamika kwenye majukwaa. Hayawezi kukusaidia. Pili, nashauri ujinyamazie. Kwani, kuendelea kulalamikia maamuzi yaliyopitishwa na Hayati ni kujiweka kwenye kundi la mazandiki na wasaliti wasio na aibu wala utu hadi kuwasaliti hata wafu. Mfano mzuri ni ile hali ya kujitokeza baadhi ya wenzetu waliokuwa karibu na Hayati Magufuli kumgeuka na kumuonyesha kama alikuwa kiongozi asiyefaa wakati walikuwa na mud na nafasi ya kumshauri lakini hawakufanya hivyo tokana na ima woga au unafiki.
Wachumia tumbo, wanafiki na wasaka ngawira hawa, kwa sasa, wanajikomba kwa Rais Samia Suluhu Hassan kiasi cha kusahau kuwa alikuwa Msaidizi mkuu wa yule wanayemtuhumu na kumsaliti. Wanasahau kuwa Rais anajua fika kuwa naye wanaweza kumgeuka na kumsaliti; kama walivyomfanyia aliyemwezesha kufika hapo alipo. Kuna watu waliojifanya maswahiba na wasiri wa Hayati Magufuli ambao sasa wamemgeuka kiasi cha kufanya kila anayewajua kuwadharau na kuwachukia. Wanamponda Magufuli wakijifanya wanapenda Samia. Wapo ambao bado wamo serikalini na waliostaafu wanaomng’ong'a wakati ndiyo walikuwa wakimshangilia kwa kila alichofanya. Nadhani Rais anawajua kiasi cha kuwanyamazia na kuwachukulia tahadhali kwani utapofika ukomo wa mamlaka yake hawatamwacha.
Kaka, nakuheshimu sana kama mwana taaluma mwenzangu. Nisingependa uwe katika  kundi la wachumia tumbo au walalamishi wakati kuna njia za kisheria za kudai haki yako–––kama kweli zilikiukwa. Mfano, huyu Rais aliyepo madarakani alikuwa msaidizi mkuu wa mamlaka iliyotengua uteuzi wako. Hivyo, anajua kila kitu. Na kama kungekuwa na namna, asingengoja uanze kulalamikalalamika kiasi hiki. Isitoshe, wewe kama Prof, bado unaweza kurudi darasani na kupiga chaki na mambo yakaenda. Wewe siyo mwanasiasa ambaye ulaji wake hutegemea hisani ya wapiga kura au wenye kuteua.
Kaka, leo sisemi mengi. Naomba nimalize waraka huu kwa kukuomba ulinde heshima ya taaluma. Nisingependa uwe kama yule mwenzetu aliyeteuliwa uwaziri akachanganyika na kupayuka kuwa alitolewa jalalani wakati aliteuliwa tokana na usomi wake ambao–––kwa ujinga na njaa yake–––alishindwa kuutukuza akaishia kuuita jalala. Hata hivyo, simlaumu sana mwenzetu. Kwani, unaweza kusoma sana bila kuelimika na kuelimika bila kusoma sana. Isitoshe busara haifundishwi darasani bali hutokana na umakini wa mhusika katika kuyachunguza maisha na malimwengu na kujifunza. Nani alijua kuwa Hayati Shehe Abeid Aman Karume angejenga majengo ya Michenzani na kutoa huduma bora vilivyowashinda Madaktari wa Falsafa?
Hivyo, kaka, tulia ule pensheni yako na kuachana na malalamiko ambayo hayawezi kubadili kitu. Ushauri wa mwisho ni kwamba–––kama unaamini katika Mungu–––hakuna aliyedhulumiwa akakoswa kulipwa haki na stahiki yake na yule yule mwenye kujua na na kutoa haki. 
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: