The Chant of Savant

Monday 18 October 2021

Waraka wa Wazi kwa Watu Wasiojulikana

Wapendwa ‘watu msiojulikana’, Nawasalimu kwa jina tamu la JMT. Msishangae kuona nawaandikia waraka wa wazi tena kwa kuwaita wapendwa. Mimi ni nani niwaite wabaya watu wa Mungu ambao sijui kilichowatuma kujiingiza kwenye jinai ya kuumiza wenzenu? Imeandikwa:Usihukumu ukahukumiwa. Hivyo, nami siwahukumu bali nataka wote tujue ukweli ili utuweke huru. Isitoshe, nanyi mnahitaji msaada tokana na kujiingiza kwenye jinai kama hii.
Kwa wanaokumbuka sakata la kile kilichojulikana kama ‘watu wasiojulikana’ ambapo watu wetu wasio na hatia walitekwa, kupotezwa na kugundulika wamekufa, kupigwa risasi na kuteswa, watakubaliana na safu hii kuwa–––kama taifa–––tuna kiu na sababu ya kuwafichua na kuwajua hawa ‘watu wasiojulikana.’ Kufanya hivyo kuna faida nyingi kwetu kama taifa. Japo tuliambiwa kulikuwa na ‘watu wasiojulikana’ waliokuwa wakiteka na kuua watanzania, je kweli kuna kitu kama hiki––––hasa kwa serikali yenye vyombo vyote taalamizi vya dola? Kama wapo na serikali na vyombo vyake walishindwa kuwabaini na kuwashughulikia vilivyo kisheria, serikali na mamlaka kama hizi zinaongoza na kutawala watu wake vipi n ani za nini? Je serikali na taasisi zinayoshindwa kujua watu waliomo kwenye mipaka yake hadi wanaitwa ‘wasiojulikana’ inaweza kujilinda na kuwalinda watu wake dhidi ya maadui wa nje––––tena wenye mbinu za juu na nguvu kubwa? Je kweli kuna serikali isiyojua watu wote walioko kwenye himaya yake au kuna au kulikuwa na namna–––hasa ikizingatiwa kuwa, pamoja na kuingia awamu ya sita–––‘watu wasiojulikana’ hawakujawa na juhudi za–––achia mbali kuwashughulikia–––hazijafanywa? Kwanini na kunani?
Tokana na unyeti wa suala hili, kuna haja ya serikali na taasisi zake kufanya kila liwezekanalo wahusika wajulikane ili tuondoe kitendawili na myth na kuwapa uhakika wa usalama na amani watu wetu ukiachia mbali kuwashughulikia wahusika mara moja tena vilivyo. Je ni kweli kuwa hawa ‘watu wasiojulikana’hawajulikani? Je hatuwajui? Je nani aliwatuma na kwa nini? Je serikali yetu ina mpango gani wa kufidia hata kuwafuta macho wahanga wa kadhia hii ya ‘watu wasiojulikana’ ambao wengi wameptoza ndugu zao hata walezi wao? Kuna kila sababu ya kuwatendea haki haraka ‘watu wasiojulikana’ na wahanga wa jinai yao. Pia, tusisahau kuwakamata na kuwahoji ili kujua nguvu na sababu vilivyowatuma kutenda maovu waliolitendea taifa letu. Tungependa kujua walipo wahanga kama Ben Saanane, Azory Gwanda na wengine wengi. Tulitendee haki taifa na wahanga hata watanzania wa kawaida ambao maisha yao yalitiwa mikiki na sintofahamu chini ya himaya ya ‘watu wasiojulikana. Kwani, ‘watu wasiojulikana’–––licha ya kuwa aibu ya taifa–––ni tishio kwa amani na usalama wa taifa.
Kama taifa, tunataka kujua ukweli ili utuweke huru licha ya kutenda haki kwetu binafsi kama watu na jamii. Wapo watakaosoma na kuhoji ni kwanini nahoji sasa hivi na si wakati jinai hii ikitendeka. Wana haki ya msingi kuhoji kama ninavyohoji. Lazima nikiri. Kipindi ambacho ‘watu waliojulikana hawakujulikana’ hata kama walijulikana, hakuna gazeti lingechapisha makala kama hii likawa salama. Kwani ‘watu wasiojulikana’ walikuwa na nguvu kiasi cha kuwa kama serikali ndani ya serikali hasa pale serikali iliyokuwapo madarakani kutoonyesha hamasa ya kuwashughulikia kwa sababu ambazo tutazijua tukiwanasa na kuwashughulikia ili liwe somo kwa wengine wenye mawazo ya jinai kama hao. Wote tuligwaya. Tuliwagwaya watu hawa na hata mamlaka zilizowafumbia jicho. Wakubwa waliogopa. Wadogo waliogopa. Kila mmoja–––isipokuwa wao na mabwana wao–––tuliogopa kweli kweli. Wakati ‘watu wasiojulikana’ wakiishika mateka nchi yetu, nilikuwa na hamasa na nia ya kuandika ili kulalamika japo historia ijue kuwa tulichukua hatua. Hata hivyo, hakuna aliyekuwako kwenye mipaka ya Tanzania angeweza kusema au kuaandika haya ‘watu wasiojulikana’ wakamuacha bila kumharakisha kwa Muumba wake.  Nani mpumbavu angeweza kujihukumu kifo hasa akijua kuwa mamlaka zilizokuwa na jukumu la kuzuia asiuawe zilikuwa kimya? Nakumbuka mnano  Aprili 26, 2018, kwenye gazeti la kiingereza la kila siku la the Citizen, niliandika makala kumuonya mmojawapo wa wahanga wa jinai ya ‘watu wasiojulikana’ Tundu Lissu aliyenusurika kuawa nao nikimtaka asikanyage Tanzania. Badala ya kusikiliza ushauri wangu, Lissu aliandika barua ya kusikitisha akinituhumu kuwa Usalama wa Taifa. Aliniita fisi aliyevaa ngozi ya kondoo pamoja na kuandika makala nne mbili kwenye the Citizen na mbili kwenye Tanzania Daima kabla ya kuacha kuwaandikia waliponidhulumu malipo yangu. Niliumia na kumuogopa Lissu kama ukoma pamoja na kumsamehe kuwa huenda hakuwa ametengamaa kiakili.
Hata hivyo, baada ya kuingia awamu mpya, nilijipa moyo na kusema–––wakati ukifika nitakumbushia kadhia hii kama ninavyofanya leo bila woga wala wasi wasi. Hata wakati naandika sikuwa na woga kama wale waliokuwa wakiishi tanazania. Kwani, niko mbali ambapo wahusika wakijaribu kunitoa roho, pamoja na ‘kutojulikana’ watakamatwa na kupewa haki yao kabla ya kunihujumu. Hivyo, kwa wanaohoji ni kwanini sasa, watakuwa wamepata majibu juu ya hatua mujarabu nilizochukua binafsi kupinga jinai hii ambayo hadi sasa, sijui sababu zake za msingi. Pia, ifahamike kuwa baada ya kuandika makala husika kwenye gazeti la the Citizen, nilikatishwa haraka kuandika bila kupewa maelezo ya kufanya hivyo. Kitendo hiki kilifanya hata gazeti dada la the Daily Nation la Kenya kuacha kuchapisha makala zangu. Hata hivyo, baada ya kutaka nielezwe kwanini nilipigwa kibuti bila maelezo, niliamua kuanza kuchangia kwenye gazeti la the Daily Monitor la Uganda ambalo nalichangia hadi sasa. Pia, baada ya hapo, nilianza kuandikia gazeti hili.
Wapendwa ‘watu msiojulikana’, wakati wa kuwafichua umefika. Pia, nimalizie kwa kuomba serikali na vyombo vyake husika watutoe kizani kuhusiana na kadhia hii chafu na katili kwa taifa letu. Nirudie. Tunataka ukweli ili ukweli utuweke huru. Tunataka haki kwa wote bila kujali nani walikuwa nyuma ya kadhia hii ili tuwe salama na kuheshimika kama taifa lililochafuliwa na ‘watu wasiojulikana.’  Mbona tulifanikiwa kuwajua na kuwashughulikia waliokuwa wakiua vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi kwa imani chafu na mfu za kishirikina? Uwezo wa kuwafichua tunao hata sababu bila kusahau nia.
Chanzo: Raia Mwema Oktoba 19, 2021

No comments: