The Chant of Savant

Monday 25 October 2021

Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Kesi za Kubambikiza

Mheshimiwa Rais, kwanza nakusalimu kwa JMT.
Niliwahi kusikia ukiwaasa polisi kuacha kubambikia watu kesi. Nakumbuka ulitoa kauli hii Machi 28, 2021 ulisema “hapa kuna kesi tunazoshindwa na hizi hazikuwa na misingi mizuri au zilikuwa za kubambikizwa yote yapo haya! Kwa hiyo nakuomba Mkurugenzi zile ambazo huna misingi mizito ya kuweza kushinda zifute kabla hujazipeleka huko kila siku kusema kuna kesi tumeshindwa hazina tija kwa Serikali.” Je mfano Kesi inayomkabili Mwanasiasa fulani wa upinzani–––ambaye siwezi kutaja jina lake kwa vile kesi iko mahakamani–––ina maslahi gani kwa taifa? Mwandishi wa makala hii ni msomi na mtaalamu wa masuala ya ugaidi. Kimsingi, kesi nyingi zinazoitwa za ugaidi si za ugaidi bali ukandamizaji wa kukomoa maadui. Rejea namna Marais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein na wa Libya, Muamar Gadaffi walivyozushiwa kesi za ugaidi na mataifa ya magharibi ili kuwakomoa na kuuawa na hatimaye kukutikana kuwa madai yote hayakuwa na ukweli. Kwa tuliosemea ugaidi, hakuna watenda ugaidi wakubwa kama serikali. Mheshimiwa Rais, nisingependa serikali yako iwe mojawapo ya serikali gaidi kama zilivyo serikali nyingi za magharibi.
            Mbali na kesi za kigaidi za kubambikiziwa hapo juu, mfano wa karibu ni wa Rais wa sasa wa Zambia, Mheshimiwa Hichilema Hakainde aliyezushiwa kila aina ya kesi. Sasa ni Rais na wale waliomfanyia unyama huu hawa amani, usingizi wala uhakika wa kesho yao kama atalipiza kisasi. Hawa wanaosingiziwa na kubambikiwa kesi leo wanaweza kuwa Marais wenu. Kwani,  mambo yajayo binadamu hatuyajui. Kwa unyenyekevu nakuomba Mheshimiwa Rais hapa busara itumike.
            Kuambikiana kesi ni jambo hatari si kwa wabambikiwa bali hata taifa hasa ikizingatiwa kuwa linaumiza watu binafsi na taifa bila sababu. Licha ya kuwa jinai ni aina nyingine ya ufisadi wa kimfumo. Hivi familia ya mwanasiasa huyu inajisikiaje kwa mateso inayopata? Kumbuka naye ana mke au mume na watoto na mambo ya kufanya kwake binafsi na taifa kama wewe na mimi. Je hawa waliomfungulia kesi husika walishajiuliza ingekuwa wao wangetaka watendeweje? Je wanayajua ya kesho? Mfano mzuri, nani alijua kuwa wewe Mheshimiwa Rais ungekuwa Rais tena bila kumuumiza yeyote wala kukisumbua chama chako? Je nani anaweza kusimamisha mkono na utashi wa Mungu? Je ni makosa kusema kuwa wewe ni Rais kwa kudra za Mwenyezi Mungu kama ulivyowahi kukiri jambo ambalo laweza kumtokea yeyote hata hawa wanaobambikiziwa kesi za ajabu ajabu? 
        Binafsi si mtetezi wa yeyote hasa ikizingatiwa kuwa niliwahi kuwa mchambuzi wa magazeti ya mmoja wa waathirika wanotuhumiwa ugaidi na kudhulumiwa ujira wangu halali. Hata hivyo, kama binadamu na mtanzania yeyote, anapaswa kutendewa haki sawa na wengine.
        Wenzetu wenye kuchelea ya kesho hutumia njia laini kuwatuliza marafiki zao. Mfano, huwateua wapinzani wao Ubunge. Kwa wale wanaoukataa baada ya kuwasiliana nao ili isiwe aibu baada ya kuwasiliana nao, huwateua wenzao. Wahenga wanasema kuwa hakuna haja kumuua adui yako kwa sumu wakati unaweza kutumia asali. Kuna haja gani ya kumsukuma aliyechutama wakati anakaribia kuanguka? Kuna haja gani kumuogopa mtu au mnyama asiye hatari kwako wakati ukiwakumbatia walio hatari kuliko yeye wanaong’ata na kupuliza kuliko yeye anayelalamika tokana na hasira na kukata tamaa?
        Kuna mambo mengi na hasa kashfa za ufisadi na wizi wa mabilioni ya umma ambazo hazijashughulikiwa. Hata hawa polisi wanaohadaa umma kwa kumfungulia mashtaka hawana ubavu au utashi wa kuwashughulikia mafisadi na mafisi wanaojulikana tokana na waliowawezesha kutenda jinai hii.  Imeishia wapi kesi ya Lugumi? Nini kimetokea kwenye kashfa ya IPTL ambayo walioiasisi wamewahi hata kuwa wakubwa tu?
        Mheshimiwa Rais chunga sana wabaya wasikutumie na kukuchafua kukutumia kuficha, kupuuzia au kusafisha uchafu wao. Una mamlaka na sababu vya kutosha kuwakatilia hata kuwakamata na kuwashughulikia. Mtangulizi wako alikataa–––au tuseme–––aligwaya kufukua makaburi kutokana na alivyojuana nao au kuangalia hatari ambayo wangeusababishia utawala wake. Wewe hukuwa kwenye kundi lao. Mfano, kashfa za uuzaji wa nyumba za umma hukuhusika wala kashfa yoyote. Hivyo, una fursa nzuri ya kupambana na ufisadi na kuendelea kuwavutia watanzania kuwaongoza hata baada ya kumaliza ngwe yako. Nisingependa uwe Rais awa awamu moja. Mtangulizi wako amekuwa Rais wa awamu moja tokana na maamuzi ya Mungu ila si maamuzi ya wananchi. Kwani alikufa akiwa anaanza ngwe ya mwisho ya awamu yake. Una kila kitu cha, nafasi na sifa ya kuwa Rais wa vipindi viwili kama wengine kama utahiari na kuamua kuanza akulifanyia kazi hili kisayansi na si kisiasa tu. You have what it takes and the opportunities to do so.
            Mheshimiwa Rais, naomba niishie hapa kwa kukuomba kuangalia haki ilivyo bila kujali aliyeko upande wa pili. Tumejifunza mengi tokana na baadhi ya dhuluma. Binadamu ana nini ni nani au nini hata angekuwa nani? Licha ya kuwa mama, mke na mwanadamu aliyejaliwa ujuzi na uchungu wa ubinadamu kama mama mwenye kujua uchungu wa uzazi, kama Rais, nakuomba na kukushauri uwe msuluhishi na mwenye kufanya wanyonge wajisikie salama kwako. Hakuna siri iliyomfanya mtangulizi wako kipenzi cha watu cha kweli kama kuwajali wanyonge. Kwa leo sina mengi zaidi ya kukutakia afya njema, amani na ufanisi bila kusahau usikivu katika kazi yako adhimu ya ujenzi na uongozi wa taifa letu.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: