The Chant of Savant

Tuesday 12 October 2021

Waraka wa Wazi kwa Watumishi wa Umma

Kwa tuliokulia chini ya mfumo wa chama kimoja enzi za vita baridi kati ya kambi za ubepari na ukomunisti zikingozwa na Marekani dhidi ya uliokuwa umoja wa Kisoshalisti wa Kisovieti wa Urusi, watakumbuka namna serikali za kiafrika zilivyokuwa zikikandamiza uhuru wa vyombo vya habari bila kupigiwa kelele na mabingwa wa demokrasia wa magharibi.  Nchi hizi zilifanya hivyo kulinda maslahi makubwa ya mabwana zao na madogo ya manyampala waliokuwa wemewekwa kwenye mamlaka. Hali ya wakati ule iliruhusu kwa vile kila taifa lilikuwa likilindwa na kutetewa na mabwana zake. Tulikuwa chini ya ukoloni mambo leo ambao haupaswi kurudiwa au kuendelezwa chini ya kisingizio chochote.
Kwa nchi ambayo ilipata uhuru wake miaka sitini iliyopita kuwa na mawazo, mikakati au sheria zinazofungia au kukandamiza vyombo vya habari ni kujidhalilisha na kushindwa kuonyesha si ukomavu tu bali hata hayo matunda ya uhuru. Mojawapo ya matunda ya uhuru ni kuwa na haki ya kutoa na kupokea habari, mawazo na kujieleza bila kizuizi ilmradi asivunje sheria pia kujiamini na kuaminika. Kwa kinachoendelea nchini, hakifanani na nchi huru tena kwa muda mrefu kiasi hiki. Hata siasa za sasa za ushindani na kisasa hazina nafasi ya ukandamizaji wa vyombo vya habari kwa sababu hakuna sababu zozote za msingi za kufanya hivyo. Wala, kama jamii na taifa hatuhitaji kufanya hivyo. Ni aibu mbali na kuwa dhuluma.
        Je tunapaswa kufanya nini kuachana na ukale na mawazo mgando kama haya? Yafuatayo ni mambo ambayo tunapaswa kuyafanya kama jamii, nchi na watu walio huru na wanaojifunza tokana na makosa hata mapungufu yao:
Mosi, tunapaswa kuanza kujenga ustaarabu na utamaduni wa kukubali kukosoana bila kuchukiana, kuhujumia, kutishana wala kuumizana. Kama chombo cha habari kitakosoa jambo, badala ya kukifungia, watendaji wake waitwe na kueleza walichomaanisha au kujua nini walitumia au kuzingatia hadi kufikia hitimisho walilofikia. Kunaweza kukawa na makosa hata nia mbaya. Hata hivyo, kukosea ni sehemu ya ubinadamu.
Pili, kama taifa na jamii ya watu wanaotaka kutenda na kutendewa haki, tupambane na ufisadi, uoza, wizi na ubabaishaji na mengine kama hayo yanayosababisha kuwa chanzo kizuri cha habari ili kuepuka kutoa habari zinazoonekana kuwakwaza baadhi ya wenzetu hadi wakatumia madaraka yao vibaya. Mfano, inapotokea chombo cha habari kikaandika habari ambayo inakionyesha chama fulani au serikali vibaya, badala ya kukimbilia kufungia chombo husika, wahusika wasafishe nyumba yao. Waache kufanya hayo yanayovutia waandishi na wachunguzi kuyafichua. Ukitaka inzi wasikufuatefuate, jitenge na harufu.
Tatu, tunapaswa kujenga utamaduni wa kutenda haki bila kuangaliana usoni au itikadi ya mtu. Tunapaswa kuongozwa na dira moja kuwa wote ni binadamu na ni watanzania wenye haki na stahiki sawa. Maana inapotokea upande mmoja, yaani serikali inayojiita ya wananchi, kuwa na mazoea ya kutumia maguvu dhidi ya wananchi wale wale ambao ni wenye serikali, inakuwa si kutenda haki wala sawa.
        Nne, licha ya kutoa haki, tukubali kuwa kila mtu ana haki na haki hizi zinalingana kwa watanzania na binadamu wote. Hakuna haja ya kuwa na kwa mfano mojawapo ya imani ya mwanachama tawala kuwa binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja lakini serikali yake au watendaji wake–––tokana na sababu zozote–––ziwe mbaya au nzuri–––kutenda na kufanya maamuzi bila kuzingatia msingi huu muhimu ambao ni kiashiria tosha cha ubinadamu na uhuru wa kweli.
    Tano, tukubali kuwa hatujui kila kitu. Na hii ni sifa ya kawaida ya binadamu. Hivyo, inapotekea chombo cha habari kikaandika kitu ambacho hatukijui vizuri, tujipe muda wa kujifunza na kudurusu lau tukijue hicho kitu au nia au mazingira yaliyofanya wenye kukiandika wafikie hitimisho husika na wakajiaona wako sahihi. Wanaweza kuwa sawa au wakakosea sawa sawa na wale wenye mamlaka ya kuwapatiliza. Elimu haina mwisho. 
    Sita, tuondoe woga dhidi ya vyombo vya habari. Kwa nchi zilizoendelea, serikali huwa hazina bifu na vyombo vya habari wala hakuna anayemuongopa mwenzake kwa vile kila mtu anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria kwa lengo la kujenga taifa husika. Kwetu ni tofauti. Vyombo vya habari havipati ushirikiano wa kutosha kutokana na kuogopwa na baadhi ya watendaji wabovu. Hili nalo ni tatizo. Hakuna haja ya kuogopana, kuogopeshana au kufundishana woga.
        Mwisho, kama jamii ya watu walio huru, tunapaswa kujenga ushirikiana na urafiki baina ya serikali na vyombo vya habari. Hakuna haja ya kuwa na uadui wakati wote tunatumikia taifa moja ukiachia mbali kuwa wote ni wananchi wa nchi moja wenye kupaswa kushirikiana kuijenga. Hata hivyo, kama kuna wanaojiona wana haki au mamlaka zaidi ya wengine au kutenda ndivyo sivyo halafu wakataka waachwe na mchezo huu, hapa lazima kutakuwa na uadui baina ya waovu na watetea mema hasa ikizingatiwa kuwa vyombo vya habari ni sauti ya wasio na sauti. Vyombo vya habari licha ya kuwapo kisheria, vinatumwa na wananchi saw ana serikali ingawa havipigiwi kura. Sifa mojawapo ya jamii na taifa huru ni kujiamini, kuaminiana na kuthaminiana na kutendeana haki. Hichi ndicho wenzetu walioendelea wanatuzidi.
Chanzo: Raia Mwema Jana

No comments: