The Chant of Savant

Wednesday 20 October 2021

Waraka wa Wazi kwa Mwalimu Nyerere

Mpendwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius K Nyerere Burito,
Shikamoo. Naamini huko uliko bado unaikumbuka na kuiombea Tanzania, nchi uliyoijenga na kuipenda kwa moyo wote. Nadhani bado unakumbuka na kuchukia wale maadui wakuu wanne wa taifa ambao ni ujinga, malazi na umaskini mbali na wale wengine nyemelezi kama vile uchama, udini, ukabila na ukanda. Naamini, pia, kuwa bado unakumbuka siasa ya Ujamaa iliyojenga mshikamano, kuleta amani na maendeleo japo kinadharia.
Mwezi na mwaka huu, unatimiza miaka 22 tangu uondoke. Bado wengi tunakukumbuka na kukulilia japo kifo hakiepukiki. Hivi karibuni tulimpoteza rafiki yako kipenzi Kenneth Kaunda na kijana mwingine machachari ambaye–––hata hivyo–––humjui aitwaye Dkt John Pombe Magufuli aliyechukua urais toka kwa yule jamaa uliyemkatalila ambaye sitaki nimtaje aliyemrithi mwanafunzi wako Benjamin Mkapa ambaye naye alifariki ghafla mwaka jana.  Mkeo, Mama yetu Mama Maria bado anadunda japo kidogo umri unaenda. Wanao wapo ila tulimpoteza binti yako Rosemary Januari mwaka huu. Ni misiba baba. Hata hivyo, ndiyo maisha na ndicho kilimwengu. 
Mwalimu, mwanao Makongoro sasa ni mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara. Aliteuliwa na Rais wa sasa ambaye nitakuja jina lake hapa chini. Na bado anaendelea kuchapa kazi bila kusahau vituko vyake na ucheshi hapa na pale Mwanao mwingine, Madaraka, bado anadunda akisimamia makumbusho yako. Hata hivyo, juzi niliongea naye na kugundua kuwa ameanza kuota mvi. Hata hivyo, anaendelea kulinda urathi wako kweli kweli. Nakumbuka, nilipokuwa nikitafuta habari juu yako na Ujamaa, alinipa ushirikiano mkubwa sana.
Japo uliacha Tanzania ikiwa imeshikamana, mambo yanazidi kubadilika. Udini, uchama, ukabila na ukanda vimerejea japo viongozi wanakemea hivyo hivyo. Hata hivyo, japo hukumfahamu, Hayati Magufuli alileta maendeleo haraka ndani ya muda mfupi pamoja na mapungufu kidogo kama vile kuminya wapinzani ukiachia  mbali kusambaratisha makundi hasimu ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho bado kinatawala. Kitu kimoja kilituchanganya enzi za utawala wa kijana huyu ni kuibuka kwa kundi lililojulikana kama ‘watu wasiojulikana.’ Kundi hili lilitesa na kuua watu wetu bila kushughulikiwa hadi nchi ikageuka kichaka cha woga. Hata hivyo, siku hizi limezama. Halisikiki. Halitesi wala kuua. Tunangojea kuona watawala wa sasa watafanya nini kuuelezea umma nani hawa wasiojulikana na nani alikuwa akiwatuma na kwa nini. Taifa sasa linataka wasiojulikana wajulikane ili ukweli ujulikane na haki itendeke.
Cha mno leo baba ni kwamba sasa Tanzania ina Rais mwanamke wa kwanza. Anaitwa Samia Suluhu Hassan ambaye alichukua ukanda baada ya kifo cha Magufuli ambacho nacho kilitokea ghafla kiasi cha kuibua utata. Huyu kaka alijenga nchi kiasi cha kuishangaza dunia tena bila kuombaomba. Alisifika kwa kupambana na ubabaishaji, utoro kazini, ufisadi, wizi na matumizi mabaya ya fedha na mali za umma. Alijenga barabara, mashule, mahospitali, reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR), alipanua bandari, viwanja vya ndege na cha mno alinunua ndege mpya 11 bila kukopa. Kwa sasa shirika la Ndege la ATCL linafanya kazi japo liko kwenye hatua zake za vidudu. Mambo sim abaya sana Mwalimu japo kuna dalili kuwa ufisadi unaanza kutunyemelea baada ya kufariki Magufuli ambaye alijipambanua kama mfuasi wako wa kweli. Kabla sijasahau, Magufuli alizidi kukumbuka na kukupaisha kwa kuliita daraja la Kigamboni na mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa mto Rufiji Nyerere. Hivyo, ninapoandika kuna Daraja la Nyerere linalounganisha Feri na Kigamboni na mradi wa kuzalisha umeme almaarufu Bwawa la Nyerere. Pia kabla ya kusahau, mtoto wa mrithi wako, Ali Hassan Mwinyi, Dkt Hussein sasa ni Rais wa Zanzibar. Pia mtoto wa swahiba yako Abeid Amani Karume, Aman alikuwa Rais wa Zanzibar. Hivyo, Tanzania inayo sifa ya kuweza kuzalisha Marais wawili watoto wa marais wa zamani. Hata nchi ya jirani inaye Rais Uhuru Kenyatta, mtoto wa mzee Jomo Kenyatta ambaye alikuwa swahiba yako. Kule Uganda, Yoweri Museveni–––yule kijana wako aliyemgeuka Milton Obote anaendelea kutawala akifukuzia miaka 40 ya utawala.
Kitu kingine muhimu kukufahamisha ni kwamba idadi ya mikoa imeongezeka. Kuna mikoa mipya ya Geita ambao pia unataka kugawanywa na kutengeneza kimkoa kingine kidogo cha Chato–––nyumbani kwa Hayati Magufuli, Katavi––kwa Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, Njombe, Simiyu–––kwa Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali Andrew Chenge, Manyara––kwa Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, na Songwe.
Mwalimu, watanzania bado wanakumiss sana. Haupiti mwezi bila kusikia au kusoma habari zako kwenye magazeti,majumbani, vijiwe na kwenye vyombo vya usafiri. Bado legacy yako inatingisha hata kama uling’atuka miaka kibao iliyopita. Kuna vitu vingi ulifanya wengi wamevisahau au kujifanya hawavikumbuki. Kwa mfano, ulitoa elimu bure kuanzia chekechea hadi PhD. Kwa sasa wanavyuo wanasoma kwa kujilipia kupitia mikopo. Wasomi wameongezeka japo ajira hakuna kabisa. Watanzania wamezaana kweli kweli. Wanakaribia kufikia milioni 60. Nadhani hii imechangiwa na huduma bora za afya ulizotoa ambazo zilirejea kidogo wakati wa Hayati Magufuli na kuanza kutoweka baada ya kifo chake. Ndivyo siasa zilivyo.
Mwisho, Mwalimu, naomba nikuage ka kukwambia kuwa urathi wako utazidi kutukuka kila litajwapo jina Tanzania. Muungano wetu unaendelea kulindwa. Amani, umoja na mshikamano vinalindwa japo kuna mambo yakwenda ndiyo siyo. Udini, uchama, ukabila na ukanda vinaendelea kupigwa vita huku wananchi wakionyesha kuchukizwa wazi wazi na ufisadi hata kama upo na baadhi ya wakubwa wakiushiriki na kuufumbia macho. 
Mwalimu, naomba nikuage nikikutakia usingizi mwema wa milele. Inshallah, tutawasiliana mwakani wakati kama huu ambapo taifa litakuwa kwenye mapumziko kukukumbuka kiongozi na baba yake mahiri aliyelipigania, kulikomboa na kulijenga kwa namna ulivyoweza. Lala Salama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Burito (RIP).
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: