The Chant of Savant

Wednesday 6 October 2021

Barua ya Wazi kwa Rais Naomba Nikushauri pia Kukushukuru


Mpendwa Rais, sitaki kukuzeesha kukuita Mama yangu wakati tunakaribia kulingana, nakusalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa rais, najua una majukumu mengi. Haraka haraka najitambulisha. Mie ni mshauri wako wa hiari ambaye juzi tu nilikushauri umteua Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mwanamke na ndani ya siku chache ukafanya hivyo kuonyesha wewe ni Rais anayewasikiliza watu wake.
    Mheshimiwa Rais, naomba uniruhusu nikupe machache yafuatayo:
Kwanza, pokea taarifa kuwa hujasoma ushauri wangu kwa mwezi mzima tokana na gazeti hili kufungiwa kwa sababu na namna za ajabu ajabu. Hivyo, leo nitagusa mambo zaidi ya moja haraka haraka. Gazeti lilifungiwa kutokana na mambo fulani liliandika ambayo wenye madaraka ima hawakupenda, kuelewa au walitafsiri vibaya kiasi cha kulifungia gazeti bila stahiki wala sababu za msingi. Sina ugomvi na maamuzi yao kama yangetenda haki na kufuata kanuni za haki asili au natural justice au kuwa na mantiki hata kwa mtu asiye msomi wala mtaalamu. Mfano, waliofungia gazeti ndiyo walikuwa walalamikaji, waendesha kesi na mahakimu jambo ambalo ni kinyume na natural justice ambapo mwenye kushitaki hapaswi kuwa hakimu, mpelelezi, mwendesha mashtaka au lolote. 
Mheshimiwa Rais, sikushitakii bali kukumbusha na kukushauri. Gazeti hili lilifungiwa kwa siku 30 baada ya kueleza wasi wasi wake kwa kile lilichokiorodhesha kama maumivu 17 na kuandika kuwa yule kijana aliyeua askari polisi alikuwa mwana CCM jambo ambalo si uzushi. Wahusika walisahau kujua kuwa kila jamii au kundi la binadamu lina wema na wabaya. Na hili ni jambo la kawaida. Sijui kusema kuwa Hamza aliyetuhumiwa kuwa gaidi alikuwa mwanachama wa CCM ni kosa sawa na kuwa mwanachama. Hayo tuyaache. Hivi inapokutikana kuwa mtu fulani aliyefanya kosa fulani ni mwanachama fulani ni kukichafua chama wakati siyo kazi ya chama kufuatilia tabia za watu? Kwanini watendaji hawa walishindwa mambo rahisi kama haya kweli kama wana sifa za kushika nyadhifa husika? Je haya siyo matumizi mabaya ya ofisi za umma? Je inakuwaje kazi ya kutoa haki ambayo ni pekee kwa ajili ya mhimili wa mahakama inaanza kuingiliwa?
    Mheshimiwa Rais, nashauri kwenye nafasi nyeti kama hizi wateuliwe watu wenye taalumu za kutosha na siyo watu wanaotia shaka na kuchafua sifa nzuri ya Serikali yako. Hivi hawa wateule wako wanaoanza kuwa na sifa ya kufanya mambo yasiyosaidia taifa wanakusaidia au kukukomoa? Je mtu anapofungia gazeti hajui kuwa––––licha ya kuwanyima wananchi haki ya kutoa na kupokea taarifa––––anaathiri ajira na maisha ya watu wengine wanaofanya kazi kwenye gazeti na kunufaika nalo kama vile wasambazaji, wauzaji na hata wapakia mizigo? Je aliljiuliza kwanza, kuwa wale wanaowategemea kama vile watoto watakula nini au kusomea nini? Je wazazi wao wanaowategemea mnawaweka kundi gani? Je kufungia gazeti ndilo jibu? Inakuwaje hata mafisadi wanafunguliwa huku magazeti yakifungwa? Je watendaji wanaochukua maamuzi haya wanalisaidia taifa kiuchumi na kijamii? Je jibu pale gazeti linapoandika mambo ambayo hayawapendezi wakubwa ni kulifuta? Je hapa wanatoa picha gani ambapo tuliaminishwa kuwa  kuna mageuzi yamefanywa kwenye uendeshaji wa Serikali? Je hawa wanaofanya madudu haya wanatumwa na nani na wanafanya hivyo kwa faida ya nani? Ni hatari kuwa na watendaji wasio waza sawa sawa hasa linapokuja jambon yeti na practical kama hili.
Mheshimiwa Rais, naomba uniruhusu nigusi suala jingine ambalo sikupata nafasi ya kulidurusu baada ya uga wangu kufungwa. Ni kuhusu ukusanyaji wa kodi. Juzi nilisoma kwenye vyombo vya habari mamlaka husika zikijisifu kuwa zimekusanya kodi kwa asilimia 94.3 kwa kipindi cha mwezi uliopita. Hapa kuna la kujisifia au kuona aibu hasa ikizingatiwa kuwa asilimia saba iliyopungua si haba. Je hapa tatizo ni nini? Kuna uzembe katika kukusanya kodi? Je ni kwa sababu ya athari za Ukovi-19 zilizoathiri chumi nyingi duniani? Je kuna ukwepaji katika kulipa kodi hasa baada ya watu kuchezea mashine za kielectroniki? Je kuna misamaha ya kodi isiyopaswa kutolewa? Je walioshindwa kufikia malengo nao mishahara yao imepunguzwa kwa asilimia hiyo hiyo? Nashauri, kuanzia sasa watakaoshindwa kufikia malengo ya serikali wapanguliwe. Sitaki kutumia neno kutumbua maana lilionekana ni la kikatili. Napendekeza panga pangua ili kieleweke.
Katika kufanikisha ukusanyaji kodi, naomba nikushauri urejee kwenye mfumo wa Hayati mtangulizi wako John Pombe Magufuli wa kuhakikisha wateule wako wanaishi kwa tension. Mheshimiwa rais, nakushauri usome kitabu cha Magufulification, New Concept that Will Define Africa’s Future and the Man who Makes Things Happen nilichoandika na mzee Pius Msekwa kinachoeleza kilichomfanya Magufuli awe lulu. Katika mambo ambayo wachambuzi wengi wanakubaliana ni kwamba Magufuli alikuwa mfuatiliaji na asiye na huruma linapokuja suala la kuwajibika na kuchapa kazi. Pia, hakuruhusu watu waridhike na nafasi zao zaidi ya kuwataka watimize matarajio na hayo ndiyo yawape ridhiko na uhakika wa nafasi husika. Ndiyo maana alitumbua tumbua bila kujali nini kitasemwa.
Mheshimiwa Rais, naomba niseme wazi kuwa awamu ya sita siyo ya tano wala ya nne. Hata hivyo, ina mambo mengi ya kujifunza kutoka kwenye awamu ya tano kuliko awamu zote. Kwani, matendo ya awamu ya tano, yataendelea kuwa kipimo kwa utendaji wa mliofuata hasa wewe mheshimiwa Rais.
Mwisho mheshimiwa Rais, naomba nikupongeze kwa hotuba yako safi kwenye kikao cha wakuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) hivi majuzi. Hata hivyo, nina dokezo. Katika baadhi ya watu waliokupongeza ni kampuni moja chafu iliyotuhumiwa kwa ufisadi wa kutisha kiasi cha mahakama kuamua mali za wenye kampuni hiyo kupigwa mnada. Baada ya kifo cha Magufuli, tunaona jamaa huyu mwenye kutia mashaka amerejea kwa nguvu hadi kufikia hata kutaka kushitaki serikali akidai mali zake badala ya kufikishwa korokoroni. Kunani? Hapa hapa, naomba niongezee kushangazwa kwangu kwa kuachiwa hivi karibuni kwa watuhumiwa wa kashfa ya IPTL huku mmoja akiamriwa kulipa pesa kiduchu ikilinganishwa na aliyoiba na mwingine kuachiwa bila kuamriwa kurejesha hata senti moja wakati wote walikuwa wakikabiliwa na mashataka yanayofanana. Je tunaanza kuelekea wapi? Je tujiandae kuona mafisadi wakishika kani?  Haya si maswali yangu. Ni maswali ya umma ambao mali na fedha zake zilibadhiliwa. Ni mshangao wa umma ambao hadi sasa haujui kinachoendelea kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi, uzembe, ubabaishaji, matumizi mabaya ya mali za umma, uzururaji na mengine kama hayo. Naomba niishie hapa kwa leo nikikuombea afya nje, amani na fanaka katika shughuli zako mheshimiwa.
Chanzo: Raia Mwema leo

No comments: