The Chant of Savant

Friday 29 October 2021

Waraka kwa Rais Kuhusu Viongozi Kuendeshwa

Mheshimiwa Rais, 
Mwanzoni mwa mwaka huu niliandika makala ya kuishauri serikali namna ya kuongeza mapato yake bila kuombaomba na kukopa. Sikwenda mbali zaidi ya kuchambua na kudurusu mfumo wetu wa utawala tuliorithi toka kwa wakoloni; tukaulea na kuuendekeza huku tukiishia kuwa ombaomba na tegemezi bila sababu tena bila kuona hata aibu au kuhisi tuna dhambi ya kujitakia! Kabla ya kuandika waraka huu, niliangaza hapa na pale mitaani niishiko hapa Kanada. Nilijiuliza. Inakuwaje mawaziri, majaji, wakuu mbali wazito tu, wabunge na wengine wengi ambao mishahara yao ni mikubwa ukilinganisha na wa kwetu wanavyoweza kuuhudumia umma bila kuwa tegemezi kama ilivyo nyumbani kwa kodi za wananchi. Nilihoji mantiki ya watendaji wetu kuwa na madereva, walinzi hata wasaidizi kana kwamba hawana akili wala mikono. Je huku siyo kuwageuza wanyonyaji kinyemela hata kama tumefanya hivi tangu tupate uhuru?
        Mheshimiwa Rais, kukumbushia, nagusia suala hili tena ili likufikie na kukufikirisha ili ulifanyie kazi kama ambavyo umefanyia kazi baadhi ya ushauri wangu kama vile kumteua mwanamke kuwa Waziri wa Ulinzi na JKT–––kama itakupendeza japo naamini itakupendeza tu. 
    Mheshimiwa Rais, nakukaribisha na kukuomba tufikiri pamoja. Tukiondoa wewe, Makamu wako na Waziri Mkuu, kweli kuna haja ya wasaidizi wako waliobaki nchi nzima kupewa madereva kana kwamba ni watoto, vikongwe au mataahira wasioweza kuendesha magari yao? Je kabla ya kuteuliwa nani alikuwa anawaendesha wakati wengine hawakuwa na hata na baiskeli? Iweje wazito wa huku tena wanaotimiza majukumu yao bila kuiba, kubangaiza, kubebwa wala kujiingiza kwenye ufisadi wajiendeshe pamoja na kuwa na changamoto ya madai yasiyoisha ya wanaowawakilisha ikilinganiswa na wanaowakilisha matumbo yao japo si wote–––wahudumu vizuri tena bila kunyonya umma wao?
        Mheshimiwa Rais, hata suala la baadhi kufunguliwa milango ya magari yao nalo linatia doa uhuru wetu. Pamoja na kukaa huku kwa muda si haba, sijawahi kuona  mfano, Rais wa taifa jirani jeuri kifedha na kivita la Marekani au Waziri wetu Mkuu akifunguliwa kitabu cha hotuba yake au kuwa na mtu anayesimama nyuma yake utadhani mtu huyo ni ukuta ambao unaweza kuzuia asiumizwe wakati ni binadamu wa kawaida na asiye na uhumuhimu wa kuwa hap? Kama mtu hawezi kujifungulia kabrasha lake la hotuba ina maana hata kuisoma hiyo hatuba anapaswa apewe mtu wa kufanya hivyo. Je ni kweli kuwa hamna uwezo wa kufungua makabrasha na kusoma hotuba zenu au ni kwa vile haya mambo ni mazoea mliyorithi kama sehemu ya madaraka wakati siyo bali mabaki ya ukoloni na njia fichi ya kuwafanya muonekane hamjiamini?
        Mbali na kuendeshwa, wakubwa wetu walio wengi wanapenda kulindwa kama watoto wadogo au wafungwa. Je wanamuogopa nani? Ukiachia wewe Mheshimiwa Rais, Makamu wako na Waziri Mkuu, hawa wengine wana tishio gani la usalama wakati wengi wao wanateuliwa tu? Hivi Spika wa Bunge ana adui gani wakati kazi yake ni kutunga sheria tu? Je wanauhitaji huo ulinzi kiasi cha kupoteza kodi za watanzania maskini au ni makandokando na mbwembwe alizoanzisha mkoloni kwa faida yake na hasara kwetu? Kimsingi, wakoloni walioshika vyeo kama hivyo walilindwa kwa sababu walikuwa ni maadui wa wananchi waliowatesa, kuwanyonya na kuwakandamiza. Hawa walistahiki  ulinzi huu tokana na jinai na ujambazi waliokuwa wakitenda. Je hawa wetu wanamtenda jinai gani kiasi cha kupaswa kulindwa dhidi ya watu wanaowatumikia kama kweli wanawatumikia na si kuwatumia?
        Mheshimiwa Rais, kitu kingine ambacho kinalitia hasara taifa ni ile hali ya kuwapangishia nyumba wazito tena wenye marupurupu na mishahara mikubwa huku wengine wakiwekewa walinzi na watunzaji bustani. Je mishahara yao inafanya kazi gani? Je ni haki kwa watu wa viwango vya chini tena wenye mishahara kiduchu kama vile walimu, waganga, na watendaji wengine wadogo kujilipia nyumba wakati wana mishara na marupurupu kidogo? Je serikali ina utajiri gani wa kuwabeba kiasi hiki? Kwanini wapewe mishahara mikubwa na kulala bure ukiachia mbali kutumia hata magari ya umma kwenda na kurudi maofisini kwao wakati watendaji wa kawaida wa chini na wananchi wanasota kwenye usafiri wa umma? Kwanini  watumishi wenye mishahara mikubwa wasikopeshwe magari watumie badala kutumia ya umma wakati wafanyakazi wengine hawana huduma wala haki hiyo? Licha ya kuhujumu na kusikinisha umma, je kuendelea kuwadekeza watendaji wetu wakubwa siyo kuwafanya wasifikirie ukiachia mbali kuwapendelea na kuwapa fursa ya kuhujumu umma kwa kutumia vibaya mali za umma kwa vile hawana uchungu nazo?
        Mheshimiwa Rais, ukipiga mahesabu ya fedha zinazotumika hovyo kuwalaza, kugharimia usafiri na mambo mengine ambayo si muhimu kama kuwapa walinzi na watunza hata bustani kwa idara na taasisi zote za serikali, utakuta ni mabilioni au matrilioni ya fedha ambayo yangefanya mambo ya msingi kama vile kupambana na umaskini kwa kutoa huduma kwa watu wetu na kuwajengea uwezo. Ni jambo la aibu kwa nchi inayochezea fedha kwenye mambo yasiyo ya msingi kwa kundi dogo la walaji huku ikitegemea kuombaomba na kukopakopa badala ya kubana matumizi na kutumia kidogo ilicho nacho vizuri.
        Mheshimiwa Rais naomba nimalizie kwa kushauri yafuatayo:
Mosi, mtindo wa kuwapa watendaji wa umma  upendeleo na huduma wasizostahiki kama nilivyoonyesha hapo juu ukomeshwe mara moja–––tena si kwa utashi wako bali utungiwe sheria ambayo itafanya kazi hata baada ya wewe kuachia madaraka.
Pili, watumishi wa umma waliorodheshwa hapo pamoja na wengine wote wanaoendeshwa, waanze kuendesha magari yao mara moja. Wasiojua wapelekwe kwenye shule za udereva na wengine watakaoteuliwa mojawapo na masharti iwe ni kujua kuendesha gari.
        Mwisho kabisa, Mheshimiwa Rais, kama utafanyia kazi mawazo, haya–––amini nakuambia–––taifa litapaa ndani ya muda mfupi. Licha ya hiyo, utakuwa umeanzisha kitu kipya chenye kutafsiri maana ya uhuru na kujitegemea kama tulivyotarajia kwa kupigania uhuru tukaishia kukopi kila kitu alichofanya mkoloni ima kwa kujua au bila kujua tusijue tunawakomoa watu wetu na kujenga mazingira ya vurugu huko mbele tuendako. Tuache kuwalemaze wakubwa zetu kwa hasara yetu. Kwa leo ni hayo tu.
Chanzo: Raia Mwema leo.


No comments: