The Chant of Savant

Wednesday 22 December 2021

Kuendelea, tufumue mifumo yetu ya kikoloni na kitapeli

Huwa siachi kujiuliza maswali ambayo si wengi huuliza au kujiuliza. Inakuwaje baadhi ya huduma au kazi kuzifanya au kuzitoa, lazima kusomea wakati nyingine hapaswi kusomea? Je huu si ubaguzi wa kimaarifa na uchochoro wa ubabaishaji, utapeli hata wizi? Kama daktari hawezi kutoa huduma au mwanasheria bila kusomea au dereva au rubani kuendesha chombo bila kusomeea, inakuwaje wengine wanatoa huduma tena kwa maelfu bila kusomea?
            Leo nitaongelea janga linalokabili Afrika tokana na mifumo ya kikoloni/kitapeli tuliyorithi toka kwa wakoloni–––waliyoacha makusudi ili tujicheleweshe kimaendeleo na kuangamizana. Leo nitaongelea nyanja za dini na siasa ambazo ni watoto wa baba na mama mmoja.  Kabla ya kuzama zaidi, inabidi nieleze kuwa dini ilizaa siasa na siasa ikaipindua dini. Ushahidi? Ukisoma, kwa mfano historia ya dini mbili kuu za kikoloni, Ukristo na Uislam, utagundua kuwa zilianza kama himaya za kidini na kisiasa. Himaya ya Roma iliyoanzisha Ukristo wa Kirumi kabla ya kumegeka na kuzaa madhehebu tuliyo nayo leo nayo yakizaa mengine ilikuwa dini dola. Kiongozi wake mkuu Papa, alikuwa kiongozi wa kidini na kisiasa. Ndiyo maana mapapa wengi walivaa kama wafalme na kubeba vyeo vyenye namba kama wafalme. Kuepuka migongano, viongozi wa kanisa walianzisha kitu kilichoitwa oikonomia au uchumi ambapo mapadre walisimamia oikonomia au uchumi kwa niaba ya ufalme. Mfano, katika karne ya 13, mfalme Philip IV wa Ufaransa alimtoza kodi Papa BoniphaceVIII ili kupambana na mfalme Edward I wa Uingereza ambaye pia alilitoza kanisa kodi tofauti na makubaliano kuwa viongozi wa kidini wasilipe kodi. Kadhalika, Uislam ulikuwa dini dola huku Mtume Muhammad akiwa kiongozi wa dola la kwanza la kiislam chini ya dhana ya al-khilafa au ukhalifa ambao ulizua ugomvi baada ya kifo cha Muhammad na kuzaa Usunni na Ushia.
            Kwa vile tumeishagusia chimbuko la dini na siasa, ngoja tuliunganishe na ukoloni hasa ikizingatiwa kuwa, katika Afrika, licha ya kusaidia kueneza ukoloni, dini ni zao la kikoloni au kwa kiingereza the product of cultural imperialism yaani ukoloni wa kimila ambapo mila koloni huwa juu ya mila tawaliwa. Ndiyo maana waswahili wanatumia majina ya kizungu na kiarabu ukiachia mbali kuamini na kuapia miungu ya kikoloni wakitelekeza, kukidharau na kukitukana kila kitu chao. Hata wakati ukoloni ukiingia Afrika, dini na utawala wa kikoloni vilikuwa kwenye kitanda kimoja cha kunajisi waafrika kama ambavyo imeendelea hadi leo ambapo serikali za baada ya uhuru (postcolonial governments) ushirika huu. Ndiyo maana, kwa mfano, taasisi za dini hazilipi kodi wakati hakuna aliyeziomba zifanye zinachofanya zaidi ya maslahi binafsi sawa na wafanyabiashara wengine. Hii ndiyo maana mataifa mengi ya kijamaa yalizipiga marufuku, si kwa sababu ya kodi tu bali hata ile hali ya kuharibu watu wakaacha kuamini katika kufanya kazi na badala yake wakaamini katika maombi, miujiza na utapeli mwingine. Je kwanini serikali huruhusu kadhia hii huku zikiwatoza kodi maskini? Jibu ni kwamba huwatumia watu wa dini kuwapoza au kuwaathiri kiakili kwa makubaliano ya kulindana. Hapa ndipo ukoloni na utapeli ulipoibuka na kuendelea kuengwaengwa kwa maafa ya walio wengi hata taifa.
            Tukirejea kwenye kusomea taaluma, ndiyo maana serikali zetu zimeruhusu watu wasio na elimu wala ujuzi wowote wa dini kujipachika vyeo mbali mbali vya kidini kama uchungaji, uaskofu, utume, ushehe hata uhubiri mihadhara. Kama haitoshi, sasa wameongeza na udaktari feki na uwezo wa kufanya miujiza ambayo si chochote bali kuwaskinisha wafuasi wao wengi katika uhusiano wa matapeli na mbumbumbu. Ukiondoa viongozi wa madhehebu yanayojulikana, mengi yamejaa matapeli wanaotafuta riziki kwa kisingizio cha roho mtakatifu wakati wana roho mtakakitu. Tumekubali kuwa jamii ya hovyo kweli kweli. Sie tunaoishi kwenye nchi za magharibi huwa tunashangaa namna kusivyo na utitiri wa madhehebu wala makanisa na miskiti. Sana sana, asasi hizi zinazidi kupunguzwa tokana na nchi hizi kukumbatia kila aina ya ushenzi chini ya kisingizio cha haki za binadamu.
            Je ni kwanini ukoloni na utapeli huu uliojificha nyuma ya ulimwengu wa kiroho umeendelea kushamiri hata baada ya Afrika kujikomboa kutokana ukoloni kisiasa lakini si kiuchumi na kijamii? Jibu ni rahisi kuwa tulirithi mifumo ya kikoloni na kitapeli ili tuendelee kujichelewesha na kucheleweshana.  Kwa mfano, ifike mahali asasi za kidini zilipishwe kodi kama biashara nyingine huku wanaoziendesha wakilazimishwa kwenda shule ili wapate maarifa vinginevyo tutatengeneza vurugu huko tuendako. Hata hivyo, tumshukuru Hayati Kambarage Nyerere na Pombe Magufuli ambao–––hata kama walitumia mbinu na mifumo tofauti kuzipoza–––walijitahidi kuzibana asasi hizi ima kwa kuzinyima mamlaka au kwa kuziweka karibu nao. Waingereza wanasema weka marafiki zako karibu na maadui zako karibu sana. Hii ndiyo aliyotumia Magufuli.
            Ili kuondoa unyonyaji, utapeli na ukwepaji kodi, tuanze kutoza kodi madhehebu ya kidini huku tukiwalazimisha wanaotaka kuendesha biashara hii ya kiroho wasomee. Pia, mamlaka zianze kuzuia imani za kivivu na kishenzi kama vile kuamini katika kudra na miujiza badala ya kuchapa kazi. Hata hili balaa la PhD mabomu, nyingi zinatolewa na taasisi ambazo zimeshikamana na makanisa huku viongozi wengi wa makanisa wakijipatia shahada hizo kwa njia za mkato japo si wote. Kimsingi, ili tuendelee, lazima tufumue mifumo yetu ya kikoloni na kitapeli.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: