How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 28 December 2021

Rais Samia si Wingu lipitalo

Japo mtifuano na mvivutano tunayoanza kuushuhudia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vinaweza kuchukuliwa kama mambo ya kawaida kisiasa. Hata hivyo, siyo hivyo. Kuna namna. Kuna sababu nyingi hasa wakati huu ambapo chama kimo mikononi mwa mtu ambaye anaonekana kuwa ima mgeni chamani japo si mgeni au hatokani na majina makubwa au ‘wenye chama’ ambaye si mwingine ni Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Je kwanini tunaamini hivi? Yafuatayo yanaweza kutoa majibu:
    Mosi, CCM ilipompitisha Hayati John Magufuli ambaye hakuwa mtu wa ndani ya chama kwa hofu ya kupigwa kumbo baada ya kukumbwa na kashfa kibao na kuona alichofanya, ‘wenye chama’ wana kila sababu ya kuwa na hofu na yeyote asiyetokana na wale waliowategemea au kuwaandaa. Hakuna ubishi. Magufuli alikibadili chama na kuingiza watu ‘wageni’ ambao hawakutegemewa japo nao wameondoka baada ya kuja awamu ya sita kitu ambacho ni cha kawaida. Wanaoshuku warejee zama za ‘magamba’ ambayo CCM ilijaribu kuyavua yakagoma hadi alipojitokeza Magafuli akaiokoa kutokana na uchapakazi na usafi wake. Hivyo, baada ya kuwa na Magufuli, wapo waliojiandaa kufanya kila wawezalo japo kumridhisha lau wamrithi–––kama siyo mkono wa Mungu kuingia. Kwa kundi hili, kuja kwa Samia ilikuwa kama wingu lipitalo ambalo–––inavyoonekana limefika mwake. Kwani, wengi watashangaa kama Samia hatagombea 2025.
    Pili, japo makundi ya kimaslahi yameishagundua kuwa kumbe Samia siyo wingu lipitalo–––ana kila sifa ya kuendelea–––hayawezi kutundika buti bila kujaribu hasa ikizingatiwa kuwa siasa, saa nyingine, ni mchezo nyemelezi. Hivyo, kujaribu siyo sawa na kutojaribu japo wanatwanga maji.
Tatu, ili kufanikisha kujaribu, lazima makundi husika yajenge lau mtafaruko jambo ambalo linaweza kumkwamisha wasiyemtaka au ambaye ni kikwazo kwao kufikia malengo yao hata kama ni kwa kukihujumu wasijue hakuna anayeweza kufurukuta nje ya CCM. Samaki gani aweza’ishi nje ya maji?
        Tatu, kuna wale ninaoweza kuwaita wamagufuli–––walioingizwa kwenye nyadhifa za juu chamani  na Magufuli na siyo sifa wala mchango wala uketereketwa wa chama. Hawa, kimsingi, baada ya kifo cha Magufuli, ulaji wao ima umekufa au kupungua kama siyo kupunguzwa. Hawa wanajulikana. Tena, wengi hawaamini wala kukubali yanayotokea. Wanajitahidi kukosoa hata mema ilmradi ima wajiridhishe au watoe uchungu wao. Mfano, mmoja juzi alisikika akihoji mambo ambayo, alipokuwa kwenye ulaji hakuyahoji. Wengine wamejitokeza kuwa wakosoaji wakati yale wanayokosoa ndiyo walioyaasisi. Hapa ndipo Samia anawapiga bao la kisigino.  Huwezi ukampenda Magufuli ukamchukia Samia ikizingatiwa kuwa ndiyo chanzo cha awamu ya sita.
    Nne, hadhi/maslahi na ushufaa wa Urais na uenyekiti wa CCM si kidogo wala mchezo. Ukishika CCM na urais umeishika nchi pande zote. Na Samia analijua hili fika hata kabla hajawa Rais. Maana, haikuwa kazi rahisi kuhimili mikiki ya Magufuli, kiongozi aliyeonyesha umwamba wa ajabu ukiachia mbali spidi na ukali. Hata mwanzilishi wa taifa na chama, Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, hakuachia nyenzo hizi kwa pamoja kwa kujua namna zilivyo na ushawishi ukiachia kumhakikishia usalama aliyezishika. 
    Tano, wapo wahafidhina wasioamini mwanamke anaweza kumudu madaraka makubwa hivi wasijue alipokuwa Makamu wa Rais, alionyesha busara, uvumilivu na kuona mbali kuliko wanaume wengi. Hivyo, kwao, mwanamke kuwa kwenye nafasi kama hizo ni jambo linalowapa taabu.                         Tushawasikia wengine wakilalamika eti kwanini Mheshimiwa anasema mimi ni Rais mwanamke. Walitaka aseme nini iwapo ujinsia ni nyenzo ambayo wengi wametumia kuwahujumu wanawake? Kwa wanaofahamu kilichotokea nchini Uingereza chama cha Conservative kilipompitisha Iron lady Margret Thatcher au Ujerumani alipotwaa ukanda mutti au mama, Angela Merkel, watakubaliana nami kuwa Samia si wingu la kupita wala mpasha kiti joto. Anaweza kuwa chemi chemi ya uongozi isiyokauka hata atakampomaliza muda wake. Laiti tungeweza kumuuliza mumewe anayemjua kuliko yeyote; Samia ni mtu wa aina gani, wengi wetu tungepata elimu ya bure na kuondoa ndoto za kumhujumu, kumuona kama wingu lipitalo. Waulize waliofanya kazi na kusoma naye; watakwambia ile namba nyingine inapokuja kwenye busara, uvumilivu na mikakati. 
        Hata Daniel arap Moi, aliyetawala Kenya kwa muda mrefu kuliko wote, alionekana hivyo pale bosi wake alipofariki na akaapishwa Rais. Waliomuona kama wingu lipitalo waliishia kuula wa chuya huku wakijilaumu. Inapokuja kwa Mheshimiwa Samia, kufikia kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu na Rais si mchezo jamani. Anayebisha, mtafakari unavyomuona, kumsikia hata kumtathimini. Pia, kwa wanaomjua Magufuli aliyemuamini watakwambia siyo huyu mnayaweza kumrahisisha kwa aibu na hasara yenu. Sisi ni nani kumtilia shaka hadi tumkatae na kumhujumu na ili iweje wakati ameishaonyesha njia?
        Mwisho, lazima wana CCM wakiri na kukubali kuwa wanamhitaji Samia kuliko anavyowahitaji kama watajikumbusha ni kwanini wazee wa CCM walimpitisha Magufuli ambaye alikuwa hajulikani. Sababu ni rahisi; mkicheza makidamakida, mtajikuta kwenye upinzani kirahisi. Nenda mkajifunze Zambia, Malawi hata Kenya. Kimsingi, CCM inamhitaji Samia kuliko anavyoihitaji hasa ikizingatiwa hawajawahi kukamia madaraka. Wanaoona kama Samia hawafai wanapaswa kufanya utafiti japo kidogo kuhusiana na makuzi na malezi yake mbali na ithibati yake kazini pote alikopitia. Ukitaka kujua ukarimu, ukatili, ushenzi au ustaarabu wa mtu, mpe fedha au madaraka. Nadhani wengi wanajua nimaanishacho. 
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: